Mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya pwani za Bahari ya Hindi zimetuletea gharika nchini Zanzibar, ambako makaazi ya watu, miundombinu ya usafiri na majengo ya umma yameathiriwa vibaya.

Mamlaka zinasema kwa uchache nyumba 900 zimeathiriwa kote Unguja na Pemba, takribani nusu yake zikiwa zimeharibiwa kabisa kiasi cha kutokalika tena na, kwa hivyo, familia kadhaa hivi sasa hazina mahala pa kukaa zaidi ya kuhifadhiwa na jamaa zao.

Mabwawa, maziwa, mito na njia za maji zimepasuka, barabara na madaraja yanavunjika, na mashamba kadhaa “yameliwa” na maji.

Jambo la kushukuru ni kwamba hadi sasa hakujakuwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na mvua hizi, na tuzidi kumuomba Mungu kwamba zisije zikaondoka na roho mbichi za watu wetu.

Ingawa mvua za mara hii zinatajwa kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni, madhara kama haya si ya kwanza kutupata. Huwa yanajirejea takribani kila mwaka – mara nyingi mwahala mule mule mulimoathirika mwaka jana, huwa ndimo humo humo munamoathirika mwaka huu.

Uzoefu wa mara zote ni huu huu mmoja – mvua kubwa za masika zinakuja, majanga na madhara yake yanatutokezea, tunapoteza vya kupoteza, tunaumia vya kuumia. Kisha viongozi wakuu wa serikali wanakuja kuwalaumu wananchi kwa kujenga mabondeni ama kwenye njia na vyanzo vya maji. Hadithi inaishia hapo, hadi mwakani inarejea tena vile vile!

Uzoefu huo unaonesha kuwa ni baada ya mvua hizi kumalizika, ndipo hasa yale machungu yake yanapoanza kuonekana waziwazi kwetu kuliko hata wakati mvua zinapoendelea, lakini mafunzo ya machungu hayo huwa yanaingia sikio moja na kutokea jengine kwetu sote, kama raia na kama serikali.

Baada ya mvua kumalizika, ndipo hapo familia zilizokumbwa na dafrau lake zinakapojikuta mikono mitupu, mbele yao pakiwa na viwanja vitupu au magofu ya nyumba zao, mabondeni kukiwa na alama za vipando vyao, na nyoyoni mukiwa rundo la hisia kali za ufukara. Maana kamili ya umasikini

Wingu likishachicha, ndipo maradhi ya kuambukiza yanayotokana na kusambaa kwa uchafu, kama vile kipindupindu, yanapoanza kuwaandama watu wetu. Vifo vingi vya watoto wetu hutokezea kwa maradhi kama hayo baada ya mvua kumalizika kuliko wakati ule mvua zikiendelea. Vifo vinavyotokana na umasikini wetu.

Miundombinu iliyoharibiwa kwa mvua za mwaka huu huvungwavungwa kwenye ujenzi wake na hadi mvua za mwakani zikija zikamalizia kile kilichobakishwa na mvua za mwaka jana. Ishara nyengine ya umasikini uliotitia kwenye mfumo.

Ya mwaka huu pia ni yayo. Mvua kubwa zinaendelea kunyesha. Zinawavunjia watu majumba na miundombinu yao. Zinawazibia njia na kuyazamisha mashamba yao. Kama mwaka jana, mwaka huu pia wanalia na kuomboleza na kuomba.

Kama za mwaka jana, InshaAllah nazo hizi pia zitapita, zikiwaachia ufukara kuliko ule ambao ziliwakuta nao. Lakini haitakuwa mara ya mwanzo na wala haitakuwa ya mwisho.

Kama mwaka jana, serikali itawalaumu wananchi kuwa wamejitakia kwa kutokufuata ushauri wa kutojenga maeneo hatari. Husemi kwamba hapo walipokuwa wakijenga, serikali hiyo haikuwepo ikawazuwia na ilhali mamlaka zake ndizo ambazo hutoa vibali vyote vya ujenzi, tena kwa fedha nyingi, sio bure.

Kama mwaka jana, wananchi nao watambebesha Mungu dhamana na jukumu la yote haya, wakiamini kuwa sio tu mvua na jua ni qadari yake, bali hata athari za viwili hivyo pia kwao ni andiko la Mungu.

Alimradi ya mwaka jana ndiyo ya mwaka huu. Yale yale ndiyo yafanyikayo. Mule mule ndimo taifa lizungukamo. Kwenye mduara wa papo kwa papo wa umasikini. Umasikini wa mali unaozalishwa na umasikini wa hali, nao ukazalishwa na umasikini wa fikira, na kisha kila kimoja kikarejea kukizalisha mwenziwe. Mumo umo, tusemavyo kwa lahaja ya Kipemba.

Mduara huu wa umasikini kwa Zanzibar ni wa kutengenezwa na mfumo unaovitawala visiwa vyetu na ambao ungekuwa rahisi kujiondoa kwenye mduara wenyewe, endapo tu ingekuwa na uongozi unaofikiri nje ya mfumo uliouunda umasikini wenyewe.

Kwa eneo lake la kijografia, Zanzibar haina upungufu wa rasilimali za kujenga makaazi ya kudumu kwenye maeneo ambayo ni salama wakati wa mvua kubwa za masika kama hizi. Inawezekana kuwa haina mtaji mkononi mwake wakati huu kama taifa, lakini inazo rasilimali za kutosha za kuupata mtaji huo.

Utajiri wa nafasi adhimu ambayo Zanzibar ipo kidunia, unatosha pekee kuikwamuwa kwenye mduara huu wa papo kwa papo wa umasikini.

Kwa mjengeko wake wa kijamii na kitamaduni, Zanzibar haina pia upungufu wa rasilimali watu, kwa maana ya nguvu-kazi na nguvu-akili, wa kuiondoa ilipo kwenye dimbwi la ufukara na kuiweka kwenye nafasi ya kiuchumi waliyonayo visiwa vya Seychelles na Mauritius kwa mfano wa karibu, ambavyo navyo vinaelea pia kwenye Bahari ya Hindi.

Rasilimali watu ya Zanzibar imo ndani ya visiwa hivyo na nyengine imetapakaa kote ulimwenguni ikitoa mchango mkubwa kwenye ujenzi wa mataifa mengine.

Kwa nafasi yake ya kihistoria, Zanzibar haina pia upungufu wa uzoefu wala vigezo vya kujikwamuwa kutoka umasikini huu wa kujitakia ambao umekuwa sehemu ya maisha ya watu wake kwa miaka nenda miaka rudi sasa.

Ilichonacho Zanzibar hasa ni ombwe la kiuongozi ambalo linaakisika kwenye huu umasikini wa visiwa vyetu. Uongozi ambao unaweza hasa kuiondoa Zanzibar kutoka kwenye mduara wa umasikini ilimotiwa haujapatikana hadi sasa, zaidi ya nusu karne tangu tuambiwe tuko huru kama taifa na kama nchi.

Badala yake, uongozi uliopo Zanzibar ni uongozi ulioundwa, kukuzwa na kulelewa na mfumo wa kuimasikinisha Zanzibar na, kwa hakika, umetayarishwa kwenye misingi ile ile ya umasikinishaji wa visiwa vyetu. Ni shida, kwa hakika haiwezekani kabisa, kwa uongozi huu kuikwamuwa Zanzibar ilipo kwa kuwa wenyewe ni sehemu ya mkwamo huo.

Ule mduara wa papo kwa papo wa umasikini uliotajwa hapo juu unaashiria kiwango cha mkwamo ambacho Zanzibar yetu imekwama. Tuna umasikini wa mali kwa kuwa tunalelewa na kukuzwa kwenye hali za kimasikini kuanzia ngazi za awali kabisa.

Tuna umasikini wa hali kwa kuwa fikra kuu inayotawala nchi ni fikra ya kimasikini, ya kuulea na kuusambaza umasikini na kuuvumilia na kuutukuza umasikini huo, kwa kisingizio cha kuwa wengine pia wako hivi hivi – masikini kama siye!

Ndio maana kigezo kikubwa cha maendeleo kwa watawala waliopo madarakani Zanzibar ni kipi kinatokea kwa mtawala aliyeko Tanganyika. Madhali, kwa mfano, Tanganyika ina kituo kimoja cha afya kwa kila kilomita 45, basi Zanzibar inapokuwa na kituo kimoja cha afya kwa kila kilomita 20, inakuwa imeendelea pakubwa sana. Yaani ukomo wa fikra za mtawala visiwani Zanzibar ni umasikini wa mtawala Tanganyika.

Mduara huu wa papo kwa papo wa umasikini ambao Zanzibar imeingizwa, unapaswa kuvunjwa ikiwa kweli tunataka kuzifaidi neema kubwa alizozishusha Mungu kwenye visiwa hivi – neema ya nafasi yetu kijiografia, neema ya mjengeko wetu wa kijamii na kiutamaduni, na neema ya uzoefu wetu wa kihistoria.

Kuuvunja mduara wenyewe kunaanzia na kubadilisha uongozi sio tu kwa maana ya watu wanaoongoza, bali pia kwa fikra inayowaongoza viongozi wenyewe. Waswahili husema samaki akioza huanzia kichwani. Tunapouchukulia umasikini wa Zanzibar kama ni ugonjwa, basi huu ni ugonjwa uliomo kichwani, na kichwa cha taifa ni uongozi wake.

Wakati mvua hizi kubwa za masika zikiendelea kumwagika, mitaa yetu ikizidi kujaa maji, majumba yetu yakititia ardhini, watoto wetu wakitaabika, barabara zikikatika na madaraja kuvunjika na mashamba kughariki, Wazanzibari tunapaswa kuliona kila tone la mvua linalomiminika kwenye ardhi yetu kuwa sehemu ya mageuzi makubwa yanayohitajika sasa. Tusiwe wa kusaga meno kila mwaka. Tunastahiki kikubwa na bora zaidi ya hiki kitupatacho kwa kuwa nchi yetu ni bora zaidi ya hivi ilivyo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.