Nakumbuka, wakati nakuwa kisiwani Pemba, nilikulia miembeni, sio tu kwa kuwa nilizungukwa na miembe nyumbani petu, bali pia kwa kuwa familia yangu ilikuwa ya maembe. Baba yangu alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa maembe, ambaye mbali ya kuuza maembe kutoka mashamba yetu ya Weyani na Kisitu Ubale, alikuwa zaidi akikodi kuanzia petu Mchangani, Penya, Tunda, Kijuki, Masipa, Pembeni mpaka Wingwi na hata mbali ya hapo.

Nikiwa mtoto pekee wa kiume, nilikuwa msaidizi  mkubwa wa biashara hiyo, nikifuatanishwa na wachumaji wetu – akina Tajiri wa Mtemani na Mzee Iddi – na kisha kukusanya, kuhesabu, na kuzipakia kwenye magari ya ng’ombe kurudi nazo nyumbani kwa ajili ya kuzivumbika. Nilifunzwa mbinu za uvumbishaji na upakiaji kwenye masusu na magari.

Wakati huo nikizijuwa aina zaidi ya 40 za maembe, kutoka yale makubwa kabisa yaitwayo Boribo Maji hadi madogo kabisa yaitwayo Kiviringo. Kuna yenye majina ya watu kama vile Said bin Seif na Kiameri (Ameir mdogo) na yale yaliyopewa majina kwa mujibu wa ladha yake kama vile Kisukari (matamu sana) au yanayopewa majina kwa mujibu wa uliwaji wake kama vile Kinyonyo (ambalo hunyonywa). Kuna maembe ya biashara kama vile Dodo, Boribo Ndogo, Kisamli na Viringe na kuna maembe mwitu kama vile Kindema, Kajirambe, Embe Maji, Keche na Bware. Alimradi Pemba ina utajiri wa maembe, na maembe yalikuwa maisha yangu ya kila siku.

Embe nililonunuwa kwa Euro 3

Lakini  hasara kubwa sana ilikuwa ni kwamba msimu wa maembe huwa unakuja na kumalizika ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili, ambapo ndani ya siku hizo chache embe linakuwa ndio taswira ya Pemba. Huenea kila mahala. Wenyewe wana msemo “Kuna embe la kupigia mbwa!” wakimaanisha namna maembe yalivyo mengi. Lakini bahati mbaya ni kuwa huwa halidumu. Ndani ya miezi michache huwa limepotea. Wafanyabiashara, kama alivyokuwa baba yangu, hupatiliza mbio mbio kupata faida ndani ya siku chache, baada ya hapo huwa hasara na embe huwaozea. Miezi miwili baada ya msimu wa embe, wenyewe huwa wanasema “Waweza zinga la uganga usilipate!”

Karibuni, nililalamika hapa kwenye mitandao juu ya ukweli huu, baada ya kwenda sokoni nikanunuwa embe moja bichi kwa Euro 3, sawasawa na shilingi 7,000 za Kitanzania, wakati natokea eneo ambalo kwa pesa hiyo hiyo unapata susu nzima ya maembe. Embe lenyewe nililonunuwa hata halilimwi hapa nilipo, Ujerumani, bali linaingizwa kutoka mataifa ya Amerika Kusini na Asia. Nikasema hilo linawezekana kufanywa pia kwetu lau kuwa tuna mifumo inayoliruhusu, ambayo hadi wakati huo sikuwa nikijuwa kuwa ipo.

Leo nimetumiwa embe lililosarifiwa kwa kukaushwa kutoka kisiwani Pemba, kutoka shamba letu wenyewe la Weyani. Nimeambiwa kuwa limekaushwa kwa viungo vya pilipili manga na kutandaziwa ubuyu wa rangi nyekundu. Ukilila ladha ya embe iko juu, lakini unahisi utamu zaidi kwa sababu ya viungo vilivyotumika kulisarifu. Kaka yangu anayeishi Dubai amelisafirisha moja kwa moja kutoka Pemba na kunitumia kwa kifurushi hadi hapa Ujerumani. Sikwambii furaha niliyonayo.

Naamini kuwa kuanzia sasa, embe halitawachwa tena likaoza kisiwani Pemba na Zanzibar nzima kwa ujumla. Na wanunuzi huku nje wako wengi sana. Muhimu ni namna ya kulisarifu na kulifunga ili livutie wanunuwaji. Waingereza husema: “Eyes feast first”, yaani macho hula mwanzo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.