Hakuna malezi mazuri kwa mtoto kama ya wazazi wake wawili na hakuna makuzi mazuri kama mtoto huyo kukuwa akiwaona wazazi wake wiwili wapo pamoja katika ndoa.

Kuna raha na ladha maalum ambayo si rahisi kuelezeka ambayo mtoto huwa nayo pale anapopata fahamu akiwakuta wazazi wake bado wakiwa katika ndoa.

Kinyume chake ni kwamba kuna madhara mengi yanayowapata watoto endapo wazazi wao watakuwa wameachana, hasa hasa wazazi hao wasipokuwa makini katika malezi baada ya talaka. Kuna hata msemo kuwa “yatima afadhali ya mtoto wa talaka!”

Kiwango cha kuvunjika kwa ndoa zisizodumu muda mrefu kimekuwa kikubwa hapa petu siku hizi. Ndoa hizo zinavunjika huku zikiwa na vitoto vidogo visivyofikia hata umri wa baleghe. Wengi wa wazazi wa kisasa husababisha madhara kwa watoto wao, kwa kuachana huku ovyo ovyo kulikoshamiri.

Sisemi kuwa ndoa inapaswa kuendelea kuwapo katika mazingira yoyote yawayo hata yakiwa ya udhalilishanaji na mateso kwa wanandoa, lakini ninachohoji ni kuwa taasisi hii muhimu sana ya kijamii imekumbwa na dafrau visiwani Zanzibar na sasa taifa hili lililowahi kusifika kwa maadili, malezi na misingi, linaporomoka kwa kasi

Talaka nyingi za sasa hutolewa kwa wanandoa kutokuwa waaminifu katika ndoa zao na dunia nayo kukosa staha na heshima za ndoa. Namaanisha kuwa tangu wanandoa wenyewe wamekuwa hawaheshimu ndoa zao, na hata wasio na ndoa nao hawaheshimu ndoa za wenzao.

Hayo hupelekea upande mmoja unapogundua mwenza wake amekosa uaminifu katika ndoa na akapoteza imani hulazimika kumuacha mwenza wake.

Hapa ndipo pale misemo mipya inayoonesha kudumu kwa ndoa kimashaka mashaka huzaliwa, kama vile “ukiona ndoa imedumu basi kuna mmoja kakubali kufanywa bwege”,, ikimaanishwa kwamba hakuna kudumu kwa ndoa zama hizi kwa mapenzi, maadili na misingi. Ni mmoja tu kuamua kujifanya bwege ili maisha yaende hata pale mwenzake anapobobea kwenye usaliti, uchafu na ushenzi.

Lakini ukweli ni kuwa si wengi wanaokubali kuwa mabwege kiasi hicho. Kinyume chake ndicho hicho nilichokisema cha kujazana kwa watalaka mitaani na majumbani mwetu, wengi wao wakiwacha vitoto vyao vikihangaika.

Kimantiki huwezi kuwa muungwana na mwenye akili timamu halafu ukakubali kujibebesha ubwege, maana tafsiri ya ubwege katika ndoa ni pamoja kumuacha mwenza wako afanye mahusiano ya kimapenzi na mtu asiyekuwa wewe halafu wewe ugombe kidogo tu, ikisha ukubali ya she – yaani usiwe na wivu, ukubali matokeo.

Ndoa isiyo na wivu si ndoa tangu hapo awali. Mke ama mume kwenye ndoa hasa huwa na wivu. Asilani hakubali kufanyiwa uadui na kuvunjiwa heshima, utukufu na hadhi yake, kisha akae kimya bila kuchukua hatua yoyote ile seuze awe mwenye kuridhia au mwenye kutabasamu.

Kwa Zanzibar inayoaminika kulelewa kwenye maadili ya Kiislamu, basi wivu ni moja ya misingi muhimu ya ndoa ya Kiislamu. Kwa hivyo, kijana wa Kiislamu haufumbii macho hata kidogo uadui wowote ule, hususan utukufu na heshima ya dini na ndoa yake kuhusiana na mchakato huu, ni mashuhuri kwamba zipo fatwa za wanazuoni zinazoeleza wazi kwamba: “Mwenye kufa hali ya kutokubali udhalili basi mtu huyo ni shahidi.”

Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume (sala llahu Alayhi wasalam) amesema:

“Hakika Mwenyezi Mungu humchukia mtu ambaye huvamiwa nyumbani kwake wala hajihami.”

Na Imepokewa kutoka kwa Mtume amesema:

“Baba yangu Ibrahim alikuwa mtu mwenye wivu, na mimi nina wivu zaidi.  Mwenyezi Mungu aigangamize pua ya asiye na wivu miongoni mwa waumini.”

Yote hayo ni miongoni mwa alama za watu wenye imani, na imekuja katika maandiko kwamba: “Hakika wivu ni katika imani.”

Hivyo wivu ni jambo la lazima na unapokithiri maamuzi ya kuachana ndio hutokea, na hapo ndipo mzazi ambaye aliyefanya mazonge yaliyosababisha ndoa kuvunjika hubeba lawama hata kama hujikausha kutokubali lawama na kudata na kujikausha kifua kuilazimisha jamii aonekane mtukufu, lakini mzazi huyo ambaye hakua muaminifu katika ndoa hulazimika kubeba lawama za mateso, idhlali, manyanyaso, mahangaiko na mabaya yote ambayo watoto watayapata baada ya kuachana kwao.

Wazazi tujirekebishe kwa ajili ya watoto wetu.

Tanbihi: Makala hii imeandikwa na Ali Mohammed. Anapatikana kwa anwani ya msheli@excite.com.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.