Mbunge Godbless Lema wa Arusha Mjini, ambaye jana hakupewa nafasi ya kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wa ajali iliyoangamiza watu 35, wengi wao wakiwa wanafunzi, kutokana na kile kinachotajwa kuwa “chuki za kisiasa”, leo ameibukia bungeni ambako amelaani vikali matendo ya utekaji nyara, uvunjwaji wa haki za binaadamu na mateso dhidi ya raia anaosema umeshamiri nchini Tanzania katika siku za hivi karibuni.

 

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI, MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016


1.0 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha za wizara hii kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie fursa hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoa pole na salamu zetu za rambirambi kwa wazazi, familia na uongozi wa shule kwa wanafunzi 32, walimu na dereva wa Shule ya Lucky Vincent waliopoteza maisha mkoani Arusha mnamo tarehe 6 Mei, 2017 katika maeneo ya Rhotia Marera, wakiwa njiani kuelekea wilayani Karatu kwa ajili ya mitihani ya ujirani mwema kujipima uwezo na shule ya wenzao. Msiba huu ni mzito na janga kubwa kwa Taifa kupoteza hazina kubwa ya vijana waliokuwa na ndoto kubwa ya kulitumikia Taifa, ni msiba ambao na umegusa moyo wa kila Mtanzania na watu wote ulimwenguni na hivyo kutuunganisha pamoja kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, nikiwa mwakilishi halali wa wananchi wa Jimbo la Arusha Mjini mahali ambapo msiba ule wa Kitaifa umetokea, nilinyimwa kwa makusudi nafasi ya kutoa salamu za rambirambi pale uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kwa wafiwa, Watanzania wote na wapiga kura wangu kwani siasa za chuki dhidi yangu zilipewa uzito mkubwa kuliko ubinadamu. Hii ni ishara mbaya kwa taifa na ni wazi kwamba tofauti zetu za kisiasa zinaweza kutufikisha pabaya kama taifa.

Hata hivyo nakushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Bunge zima kwa pamoja kwa kuguswa na msiba huu mzito na kuamua kutoa mchango mkubwa wa rambirambi kiasi cha shilingi milioni 100 kwa familia zote za wafiwa wote. Watu wa Arusha kwa pamoja wamenituma nikuletee salamu zao za shukrani na kwa Bunge lako tukufu. Aidha, namshukuru pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa salamu zake kwa wakazi wa Arusha zilizosilishwa na Makamu wetu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu.

Mheshimiwa Spika, Nilikamatwa mwezi wa Kumi mwaka 2016 nje ya Ukumbi wa Bunge Safari yangu ya kupelekwa magereza ilianza kwa matisho makubwa. Nilikamatwa na Askari Polisi wasiopungua watano. Tulianza safari kuelekea Arusha na kuwasili Kondoa majira ya saa 4 usiku ambapo niliwekwa rumande kituo cha Polisi Kondoa mpaka saa 8 usiku na kisha kuchukuliwa mpaka kufikishwa kituo kikuu cha Polisi jijini Arusha; ambapo safari yangu ya mateso na huzuni ilikamilika kwa mimi kukaa jela kwa zaidi ya miezi 4, kwa kosa tu la kuota ndoto na kuona maono niliyopewa na mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Spika, Kwa dhati ya moyo wangu sifa na utukufu, heshima, nazirudisha kama shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na nchi kwa kunijalia afya njema.

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru wale wote walionijali wakati nilipokuwa magereza. Namshukuru Kipekee mke wangu Neema kwa maombi yake na ujasiri wake, watoto wangu Allbless, Brilliant, Terrence na Precious Mawazo. Precious Mawazo ambaye baba yake mzazi Alphonce Mawazo hayupo kwani aliuawa kikatili katika mazingira ya kisiasa kwa kosa la kuwa mfuasi wa siasa za upinzani.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru marafiki zangu wafungwa na mahabusu niliowaacha Gereza Kuu Arusha kwa upendo na uwenyeji wao wenye ukarimu katikati ya mateso mengi, ulionifundisha mengi na kumjua Mungu zaidi. Sijaacha kuwaombea hata siku moja tangu nimetoka gerezani.

Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru viongozi wangu wa chama, Mwenyekiti wetu wa Taifa, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe, viongozi wote wa UKAWA, na wengine wote waliokuja kunisalimu nilipokuwa magereza bila kusahau viongozi wa dini zote, na wanachama wote wa CHADEMA na wanachama na viongozi wa CCM ambao hawakujali kuitwa wasaliti kwa kujali utu, upendo kuliko chuki za kisiasa na utengano. Aidha, niwashukuru viongozi wa CCM waliothubutu kuwaza kuja kuniona lakini wakaogopa, ninaweza nikaelewa hofu yao na inatupa picha Taifa linakwenda wapi. Pia wao nawaombea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa na changamoto nyingi sana, changamoto kubwa ya msingi ni hali ya usalama wa nchi ambayo ni muhimu ikiwezekana hekima zetu zikajikita kwenye mjadala wake na kutafuta ufumbuzi wa haraka.

2.0 HALI YA USALAMA WA NCHI

2.1 Maadili ya Familia na mapambano dhidi ya rushwa

Mheshimiwa Spika, Jambo hili linalohusu maadili nilianza kulisema katika hotuba yangu ya mwaka wa fedha 2016/2017 kuwa ukitaka kuhakikisha hali ya usalama wa Taifa ni sharti jamii na serikali kwa ujumla iwekeze nguvu zake katika malezi yenye maadili bora yatakayojenga Familia zetu ili kuunda Taifa imara kabisa Afrika na duniani kote.

Nilisema hapa mwaka jana na nitanukuu kuwa;

“Taifa lolote Duniani msingi wake ni familia , hivyo njia sahihi ya Taifa kuwa na usalama wa kweli katika Jamii ni muhimu Serikali ikajua kuwa Jamii ni Familia, kuongelea hali ya usalama na amani ya Nchi yetu bila kuongelea maadili ya familia zetu ni kupotosha fikra zetu.”

Na pia “ukweli ni kwamba familia yenye maadili, wajibu na inayomcha Mungu ni jamii bora itakayozalisha Raia wema wenye wajibu na tija kwa Taifa, hatuwezi kuwa na Nchi yenye nidhamu na ustawi pasipo kuwa na familia zenye wajibu katika malezi.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa suala la rushwa ni suala linalohusu zaidi maadili. Hata hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hairidhishwi kabisa na jitihada za Serikali katika kukabiliana na rushwa, kwani viongozi wakuu wa nchi wameonekana wazi wazi wakiwa wanatumia fedha za Serikali nje ya mfumo wa kibajeti unaopangwa na Bunge jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona ni kuwa ni kiashiria cha rushwa kubwa (Grand Corruption).

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni tofauti ya rushwa kubwa na ndogo na msingi huu unajengwa na hoja yetu kuwa rushwa ni suala linalohusu zaidi maadili. Kwani kauli hivi karibuni iliyotolewa na Mkuu wa Serikali hii ya CCM, kuhusu kuwapatia fedha Askari Polisi wa usalama barabarani kuwa Shilingi 5,000 ni jambo dogo tu na la kawaida ni kauli inayochochea matendo ya rushwa, kwa kuwa rushwa kama hizo ndio zimekuwa kichocheo kikubwa cha ajali barabarani. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutotengeneza mazingira yanayochochea uwepo wa rushwa ndogo au kubwa katika nchi yetu.

2.2 Mifumo wa Kutoa Haki Nchini

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika ijapokuwa ukweli huo unapata vikwazo vingi kwamba haki huzaa amani. Kama Taifa ni muhimu tukajua kwamba wingi wa silaha, ukubwa wa majeshi hauwezi kuwa sababu ya kuwepo kwa amani katika Taifa. Katika Taifa lenye uonevu na ukimya ukatawala kwa sababu ya mabavu ya dola, Taifa hilo lipo kwenye hatari kubwa ya migogoro ya kijamii. Kwani njia pekee ya kutunza amani ni mifumo ya kutoa haki nchini ikajua kwamba haki huzaa amani.

Mheshimiwa Spika, Katika Taifa hili haki ina mgogoro mkubwa katika maeneo mbalimbali ya utoaji haki nchini. Ni muhimu kwamba ukimya huu uliopo sasa ukatazamwa kama uvumilvu unaoweza kufikia ukomo na kukata tamaa. Ukienda Sehemu mbalimbali zinazotoa haki kuanzia Serikalini, Mahakamani, Polisi na sehemu nyingine ambazo kwa asili hutakiwa kutoa haki, utakuta kuna uonevu, unyanyasaji na ukazamizaji wa hali ya juu ambao unakusanya hasira za watu ndani ya mioyo yao.

Mheshimiwa Spika, ni rahisi kuendelea kupuuza maneno kama haya kwa sababu yanatolewa na upande wa pili wa waleta maoni. Lakini ipo siku tutakumbukwa kwa ukweli huu tunaosema ndani ya Bunge hili. Uonevu na ukandamizaji katika Taifa hili imekuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku ya Watanzania. Mimi ni Mfano hai wa uonevu huo, Mhe. Lijualikali ni mfano wa uonevu huo, Mhe. Lissu ni mfano wa uonevu huo, familia ya Marehemu Alphonce Mawazo ni mfano wa uonevu huo. Familia ya Ben Saanane ni mfano wa uonevu huo. Msafiri Mbwambo aliyeuawa kwa kuchinjwa shingo maeneo ya USA River na waliomuua kutoroka wakiwa wamefungwa pingu mbele ya Polisi wanne wenye SMG.

Mheshimiwa Spika, hawa ni wale ambao nimewakumbuka kuwataja lakini ukienda Magerezani, Ukienda Mahabusu, Ukienda Mahakamani, Mahospitalini na makaburini na kila mahali panapotolewa huduma za umma zinazowahusu Watanzania utakutana na vilio na mateso kutoka kwa watu wengi sana wanaodhulumiwa haki zao. Angalau kila familia katika Taifa ukiachilia watawala wa Serikali hii ya CCM hili inaweza ikasimulia huzuni na mateso wanayokutana nayo kila siku katika mifumo ya utoaaji haki.

Mheshimiwa Spika, mateso na huzuni zao haziwafundishi watu hawa kuwa waoga, japokuwa wanaonekana ni waoga, kama hatua za haraka zisipochukuliwa na Serikali kwa kuganga mioyo yao kwa kutenda haki ipo siku Taifa letu litakuwa na historia mbaya kwa kuwa watu hawa wanaandamana ndani ya mioyo yao wakati miguu yao imezuiwa kuandamana kudai haki kutokana na vitisho vya zana za kivita. Ni ajabu mtu anapoandamana kudai maji ya kunywa anakabiliwa na mtutu wa bunduki. Ni jambo la kushangazwa chama cha siasa kinapotaka kudai haki yao ya msingi ya kutaka kuandamana na kufanya mikutano ambayo ni haki yao kikatiba na kisheria wanakamatwa na kufunguliwa kesi zilizobatizwa jina la “Uchochezi”.

Mheshimiwa Spika, Tunaamini mambo haya ni kwa muda tu, haki haijawahi kushindwa na kila mpigania haki ni mpenzi wa Mungu. Ni hakika yetu kuwa kila mtu atavuna anachopanda. Ni maombi yetu kwa nia njema kabisa kwamba Serikali hii ijitahidi kutenda wema ili watoto wenu na wajukuu wenu wakute Taifa lenye misingi ya kuheshimu haki na utu. Kwani huo ndio urithi mnaopaswa kuacha kwa watoto wenu na sio nyumba na magari.

Mheshimiwa Spika, Nilishawahi kusema huko nyuma kwenye moja ya mchango wangu kuwa CCM ikitawala muda wote lakini ikatawala kwa haki, heri na baraka utawala wao unapaswa kuheshimiwa. Lengo Letu kama Wapinzani si tu kuindoa CCM madarakani bali ni kuhakikisha kuwa CCM inatawala kwa haki na heri kwa nyie ndio watawala kwa sasa. Mnapokosea ninyi sio CCM inayopata hasara bali ni taifa ndio linalopata hasara, na sisi na ninyi ni miongoni mwa wananchi wa Taifa hili. Haki Huinua Taifa.

2.3 Ongezeko la Uhalifu unaotakana na uchumi duni

Mheshimiwa Spika, amani ya Taifa hili itategemea pia hali ya uchumi wa Taifa. Kwa hali ilivyo hivi sasa katika mzunguko wa fedha nchini ni ishara kwamba jitihada za ziada zinapaswa kufanyika juu ya uchumi na biashara ili kuongeza tija na maisha bora miongoni mwa Watanzania na kupunguza uhalifu unaosababishwa na njaa na ukosefu wa Kipato halali.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la mzunguko hafifu wa fedha linatokana na kauli za viongozi mbalimbali wa Serikali ambazo zimesababisha mashaka makubwa katika uwekezaji wa biashara maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa ni busara kubana matumizi lakini ni muhimu zaidi ikajulikana kwamba, matumizi ya kila siku ya Serikali na jamii ndio chanzo cha mzunguko wa fedha katika jamii. Hivyo sera za Serikali katika uchumi wa nchi sharti zizingatie hali ya usalama wa maisha ya wananachi wake kwa kuruhusu mzunguko halali wa fedha katika maeneo mbalimbali ya kibiashara, ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ya wazabuni mbalimbali wanaoidai Serikali kwa muda sasa.

2.4 Tishio la Ongezeko la Uhalifu unaotokana na Njaa na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi

Mheshimiwa spika, Ni muhimu Taifa kupitia Wizara hii ya Mambo ya Ndani ikajenga uwezo wake wa kuona picha kubwa katika Taifa ya kuangalia visababishi vinavyotishia hali ya usalama wa ndani ya nchi, ikiwemo na suala la tishio la mabadiliko ya Tabia ya Nchi. Hivyo kazi muhimu sana ya wizara ya mambo ya ndani ni kuzuia kuporomoka kwa amani sasa na katika siku za baadae. Kambi Rasmi ya upinzani bungeni inaona kuwa hali ya mabadiliko ya hali ya nchi duniani na Tanzania kwa ujumla ni moja ya sababu zinazoweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani katika siku za usoni kwa kuwa tabia ya nchi imebadilika sana hivyo kupelekea ongezeko la njaa kutokana na uzalishaji duni wa chakula cha kutosha kupitia kilimo kinachosuasua.

Mheshimiwa Spika, Ni kweli kabisa wote tunakubaliana kuwa mtu mwenye njaa ni mtu mwenye hasira, hivyo ili kukabiliana na uhalifu unaosababishwa na njaa na tafrani nyingine za kimazingira, ni muhimu sasa Serikali ikaweka malengo muhimu katika utunzaji wa misitu na upandaji miti ili kukabiliana na changamoto hizi kwa siku za usoni , na vile vile serikali ni muhimu sana ikaongeza bajeti katika wizara inayoshugulikia mazingira nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kuliangalia suala la Usalama wa Chakula na Mabadiliko ya tabia ya nchi kama suala la usalama wa raia na mali zao, hivyo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliingize katika Sera na mipango yake kama suala mtambuka la kiusalama. Mathalani jeshi la Magereza kupitia mashamba yake yatumiwe kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo muda wote.

2.5 Mateso na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na mauaji ya raia katika Taifa hili kwa kiwango ambacho hakiwezi kuelezeka , katika Mkoa wa Arusha vijana wengi sana wameuwawa au kuteswa na Jeshi la Polisi kwa kuhusishwa na tuhuma mbali mbali za uhalifu , Jeshi la Polisi linamwaga damu isiyo kuwa na hatia.

Mheshimiwa Spika, Kuna kituo cha Polisi Arusha kinaitwa Guantanamo, kimewauwa vijana wengi sana na kutesa wengi na wengine kuachwa na vilema vya kudumu, Mhe. Waziri Mwakyembe akiwa Waziri wa Katiba na Sheria alipotembelea Gereza Kuu Arusha alielezwa juu ya kituo hicho na ukatili unaofanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Arusha , sina uhakika kama kuna hatua alichukua lakini na uhakika kuwa anaweza kuwa akumbuki ataalichoambiwa na mahabusu pale alipofanya nao mkutano.

Mheshimiwa Spika, matukio ya utekaji , mateso na mauaji yapo kila kona nchini na familia nyingi zina vilio na huzuni kuu kwa kupoteza ndugu zao katika mateso makubwa , nilipopata bahati ya kuwa Magereza kwa kipindi cha miezi minne nilipata simulizi za kutisha na mpaka nikafikiri pengine siko Tanzania. Siwezi kueeleza katika hotuba hii yote niliyoyasikia, ila nimeeleza katika kitabu changu nachoandika, ambacho kitaweza kusaidia zaidi kutoa mwelekeo mpya wa fikra za haki katika Nchi hii hususani katika Wizara hii.

Mheshimiwa spika, kufikiri njia sahihi ya kukabiliana na uhalifu ni kuua , inaondoa dhana nzima ya kuwa na mfumo wa kutoa haki nchini. Hatuwezi kuushinda ubaya kwa ubaya, ndio maana kuna mahakama kama chombo cha kutoa haki. Polisi wameruhusiwa kuuwa Jambazi pindi wanapomkamata, swali ni je ni wangapi wameuwawa kwa makosa yasiyo yao kwa hukumu tu ya mwanzo ya Jeshi la Polisi ? bila kufikishwa mbele za haki ?

Mheshimiwa Spika, Wabunge wanaweza wasielewe ila iko siku watoto wao na wajukuu wao watakapokuwa wanapitia maandiko haya yetu siku za usoni, watatuelewa na kusema wale walioitwa wahuni na wachochezi walikuwa na busara sana na hekima za kutetea haki na ustawi. Hakuna damu itakayomwagwa bila hatia ambayo Mwenyezi Mungu hataipigania. Only time will tell.

2.6 Njia bora za kupambana na ugaidi na ujambazi nchini

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa kumekuwa na viashiria vya wazi kabisa vya matendo ya kigaidi katika Nchi nyetu. Hata hivyo ni uhalifu ambao unahitaji utaalamu wa hali ya juu na hekima katika kukabiliana nao , ni rai yetu kuwa suala la Ugaidi halihitaji tu operation maalumu na muhimu katika kuwasaka magaidi mahali popote walipo lakini pia ni muhimu zaidi ikafamika kwanini sasa sura ya hali hii ya matukio ya kigaidi yanaanza kujitokeza Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia jeshi la Polisi likikabiliana na matukio mbalimbali ya kiuhalifu, mengine yenye sura za ujambazi, na mengine yenye sura za kigaidi. Ni muhimu sasa jeshi la Polisi likajua changamoto wanazopitia za kiusalama ndani ya nchi yetu, haziwezi kutatuliwa kwa wingi wa askari waliopo na wingi wa silaha zilizopo, bali wanahitaji kujenga mahusiano mazuri baina ya Jeshi hilo na raia wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Katika kuonesha kuwa tunajali mahusiano mema baina ya jeshi la Polisi na raia, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na raia wote wa Tanzania kulaani vikali matukio ya mauaji ya Askari Polisi wetu ambayo miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakijirudiarudia na Serikali bado haijatoa taarifa za kina juu ya kujirudia kwa mauaji hayo.

Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa mnamo tarehe 13 Julai, 2015 Kituo cha Polisi cha Sitakishari kilichopo Ukonga jijini Dar es Salaam kilivamiwa na watu ambao walidhaniwa kuwa ni majambazi, wakafanya mauaji ya Polisi na raia wetu na kupora silaha na kutokomea kusikojulikana.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 13 Aprili, 2017 Askari Polisi 8 waliuawa kikatili na ‘watu wasiojulikana’ katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani huku wauaji hao wakipora silaha tisa kati ya hizo SMG sita zikiwa na risasi 30 kila moja na long range tatu.

Mheshimiwa Spika, Mwezi Februari, 2017 Afisa wa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) wa Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, Afisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni Mlinzi/Mgambo wakiuawa kwa kupigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.

Mheshimiwa Spika, Gazeti la Mtanzania la tarehe 15 Aprili, 2017 liliripoti kuwa mwezi Mei, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa kwa risasi. Oktoba, 2016, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho cha Nyambunda Ally Milandu, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne. Novemba, 2016 wenyeviti wawili wa Vitongoji wa Kijiji hicho hicho, waliuawa kwa kupigwa risasi. Mwezi Januari, 2017 watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu waliomuua mfanyabiashara, Oswald Mrope kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake. Februari 3, 2017 watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebaini kuwa wauaji wa Askari Polisi hulenga kupora Silaha na kutokomea nazo kusikojulikana na haijafahamika kwa nini viongozi wa Serikali za Mitaa wengi wameuawa katika maeneo hayo ya ukanda wa kuanzia mkoa wa Pwani mpaka Lindi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua mchango wa Jeshi la Polisi katika kustawisha amani katika maeneo ya ukanda huo na nchi nzima kwa ujumla isipokuwa Jeshi linapokosa zana za kisasa na rasilimali za kutosha kuendesha operesheni za kutokomeza kabisa mauaji hayo ya askari na viongozi wa Serikali za Mitaa basi linashindwa kabisa kumaliza tatizo hilo hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa inapokuja kwenye masuala ya kuzuia vyama vya upinzani visifanye mikusanyiko ya kikatiba, maandamano na mikutano ya hadhara, kwa nyakati mbalimbali Jeshi limekuwa jepesi kutumika kisiasa kuzuia mikusanyiko hiyo kwa kisingizio cha ‘taarifa za kiintelijensia’ kuwa kungeweza kutokea vurugu. Lakini inapokuja katika suala la kuzuia mauaji ya askari hao hao basi uwezo wao wa kunusa taarifa na kuzuia mauaji yasitokee unakuwa duni. Huu ni ushahidi tosha kuwa ‘intelijensia ya jeshi letu la Polisi’ ni dhaifu kwa sababu za kujiingiza katika siasa badala ya kuangalia maslahi mapana ya kitaifa na kuzingatia weledi wa kazi yao.

Mheshimiwa Spika, ili kuzuia matukio hayo yasitokee na kutokomeza kabisa vikundi hatarishi vya usalama wa nchi, huu ndio wakati ambao Idara ya Usalama wa Taifa pamoja na intelijensia ya Jeshi letu la Polisi ingetumika ipasavyo kubaini matukio hayo na kuyazuia kabla hayajatokea, lakini hali imekuwa tofauti.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuacha mara moja kuitumia Idara ya usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi kwa maslahi ya kisiasa na ijielekeze katika matumuzi ya vyombo hivyo kuzuia matukio ya mauaji ya askari na viongozi wa Serikali za Mitaa kama ilivyojitokeza katika Wilaya ya Kibiti.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulipatia Jeshi la Polisi zana za kisasa za kupambana na makundi ya kigaidi, kijambazi na makundi yote ya kihalifu yenye mrengo wa uporaji wa silaha na mauaji ya askari wetu.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kitengo cha Upelelezi takribani miaka 20 iliyopita, hakujawahi kufanyika mafunzo maalumu ya Upelelezi (CID Course). Hivyo Basi ndio sababu katika matukio yanayohitaji uweledi wa Intelijensia Jeshi la Polisi limekuwa likijitokeza kama Kikundi cha Mapambano (Operation Force).

Mheshimiwa Spika, Aidha, Jeshi la Polisi badala ya kutengewa bajeti ya kununua magari ya washawasha na kuwamwagia maji hayo raia wasiokuwa na silaha, basi ilipatie Jeshi hilo fedha za kutosha kununua zana za kisasa za Kiuchunguzi, na Kutenga fedha maalumu kwenye Mfuko wa fedha za Upelelezi ambao uko kishera (Criminal Investigation Fund) ili kutoa nguvu na uwezo wa upelelezi kufanyika kwa kina hasa kipindi hiki ambapo ulimwengu unakabiliwa na uhalifu wa aina mbalimbali unaozidi zana na ujuzi uliopo. Ni aibu kwa Taifa kwamba Serikali imekuwa haitoi fedha hizo ambazo zipo kwa mujibu wa sheria na hivyo kufanya shughuli za upelelezi kuwa ngumu sana.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu upelelezi wa washitakiwa wa makosa haya ukaendeshwa kwa haraka iwezekanavyo ili kuepuka kukaa na mahabusu wengi magerezani wenye hatia za makosa ya mbali mbali na kumbe hawakufanya makosa wanayotuhumiwa nayo; kwani unapochanganya watu wema na wabaya ni rahisi watu wema wakawa wabaya. Kwa hiyo namna pekee ya kuwatenganisha ni upelelezi kukamilika haraka na haki kutolewa mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, Katika Magereza yote Nchini watuhumiwa wengi wa Ugaidi ni pamoja na viongozi wa dini, unaposhindwa kukamilisha upelelezi haraka wa kesi hizi, unaweza ukaleta mgogoro mkubwa ma kimatabaka ya dini kwa wasio na hatia kuona kwamba kuna mkakati wa dhati wakuoneana na kudhalilishana na maneno haya yanasemwa na ili yasisemwe ni bora mmakamilisha upelelezi haraka ili kila mtu avune alichopanda kwa haki na sio hila na ulaghai.

Mheshimiwa Spika, katika magereza mbalimbali nchini kuna watuhumiwa wa kesi za ugaidi walioshikiliwa kwa muda sasa. Katika Gereza kuu la Arusha Mahabusu wa Kesi za Ugaidi wanaanza kuhesabu mwaka wa nne wakiwa mahabusu bila upelelezi wa kesi zao kukamilika. Wakati wa kukamatwa kwao , wengine waliuwawa na wengine wameachwa na vilema vya kudumu (kukatwa miguu )

Mheshimiwa Spika, swali la kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inalouliza ni je kwanini upelelezi wa mashauri yao mpaka leo unachukua muda mrefu? kwa matendo yote yale ya kuwakata miguu, kuwatesa na kuua baadhi ilikuwa ni wazi kuwa Polisi angalau wanaushaidi asilimia tisini (90) lakini mpaka leo kesi zao bado zinatajwa tu , ni tafsiri mbaya katika haki, haki inapochelewa kuamuliwa ni wazi kuwa visasi na chuki inaweza kujengwa kwa ufasaha zaidi. Ni muhimu sasa upelelezi wa makosa haya na mengine mengi ukakamilika mapema ili haki ionekane imetendeka , lakini kuwaweka watu rumande wasio na hatia na wenye hatia kwa muda mrefu ni ugaidi dhidi ya haki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ikamilishe upelelezi haraka iwezekanavyo ili anayestahili adhabu apate adhabu na asiyestahili aachiliwe akaungane na familia yake.

2.7 Haki za Wafungwa, Mahabusu na Watuhumiwa wa Makosa Mbalimbali nchini

Mheshimiwa spika, Kama ambavyo jamii iliyoko uraiani ina haki zake ndivyo ilivyo kwa mahabusu na wafungwa. Sio lugha rahisi sana kueleweka kwa watu ambao hawajawahi kuwa magereza na ndio sababu nilipotoka magereza nilimuomba Mungu angalau kila Mbunge apite jela kwa miezi isiyopungua miwili na bado ni maombi yangu tena yenye msisitizo kwa Mungu.

Mheshimiwa Spika, kukosa uhuru ni adhabu kubwa sana Duniani na aneyeijua ni yule anayekuwa hana uhuru, moja ya huzuni kubwa waliyo nayo watuhumiwa katika Taifa hili ni ucheleweshwaji wa kesi , ni kawaida sana mtuhumiwa kujikuta yuko magereza kwa muda mrefu wakati mwingine zaidi hata ya miaka 6 akisuburi kesi au upelelezi kukamilika , haya ni mateso makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu sasa Bunge lako tukufu likatunga sheria ya kuwepo na kikomo cha upelelezi katika makosa yote ya jinai tofauti na sasa ambapo baadhi ya makosa mengi ya jinai hayana kikomo cha upelelezi na hivyo kuwafanya watuhumiwa kukaa ndani muda mrefu bila mashauri yao kusikilizwa na kuongeza taabu na huzuni katika maisha yao na msongamano wa mahabusu magerezani unaolipelekea pia Taifa kupata hasara kubwa ya kuwatunza.

Mheshimiwa Spika, nimekutana na vijana wengi nilipokuwa mahabusu, nilitumia muda mwingi kuongea nao na hivi ndivyo walivyosema “Mhe. Mbunge ili kuzuia rushwa na uonevu unafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na ofisi ya DPP ni muhimu Wabunge wakaondoa vikwazo vya dhamana kwenye makosa yote ya jinai kama ilivyo Kenya na Uganda, kwani ubambikiwaji wa kesi unafanywa kwenye makosa yasiokuwa na dhamana ili watuhumiwa waweze kufikiria kutoa rushwa kubwa “

Mheshimiwa Spika, nakubaliana nao kwa asilimia zote , Kenya makosa yote yana dhamana isipokuwa uhaini , Uganda makosa yote yana dhamana ikiwemo uhaini , Tanzania orodha ya makosa yasiokuwa na dhamana ni mengi , lakini hata yenye dhamana siku hizi pia yanaweza kuzuiliwa dhamama kwa kitu kinachoitwa “ HATI YA MWENDESHA MASHITAKA” (Certificate of DDP). Japokuwa kuna hukumu ya hivi karibuni ya mahakama kuu iliyoitangaza hati ya DPP kuwa ipo kinyume cha Katiba kwa kuzuia dhamana kwa watuhumiwa, lakini ofisi ya DPP imeendelea kuidharau hukumu hiyo ya Mahakama na endapo DPP akijisikia kukuwekea hati hiyo maana yake ujue kwamba unaanza kesi ya kupigania dhamana yako kwenye mashitaka hata yenye nafasi ya dhamana kisheria, jambo limesababisha mateso mengi na kuongeza msongamano wa watuhumiwa magerezani.

Mheshimiwa Spika, Wakili Median Mwale anaanza mwaka wa saba magereza bila shauri lake kukamilika, bado ni mahabusu na aliniambia maneno haya “Mheshimiwa Mbunge nimekaa sana magereza, nimechoka sana mwili wangu na roho yangu, nimezuiwa hata kuzaa, na sijui kesi yangu itaisha lini, ningetamani shauri hili liishe, kwani hata kama ningekutwa na hatia katika shauri hili ningekuwa nimeshafungwa na kumaliza kifungo changu, nashukuru umekuja magereza na pengine Christmas utaweza kuwa nasi na ukitoka nenda ukawatetee Mahubusu , wafungwa na Askari jela”

Mheshimiwa Spika, Wakili Mwale, aliendelea kuniambia kuwa;
“Bunge linapotunga sheria linapaswa kuwa makini, kwa mfano; kesi inayonikabili mimi ya Money Laundery inamkabili pia kijana mmoja anaitwa Masawe yupo humu ndani, anakabiliwa na shitaka la Money Laundery la dola 1,900 lakini amekaa jela zaidi ya miezi 15 kwa sababu shitaka hili halina dhamana na adhabu yake ukikutwa na hatia ni kati ya miaka 4 na 7, wakati huo huo mtu anayetuhumiwa kunajisi au kubaka kosa ambalo adhabu yake ni miaka 30 jela au kifungo cha maisha, anapewa dhamana akisubiri shauri lake kukamilika, wabunge mnapoletewe miswada ya sheria na Serikali, mnapimaje haya mambo? Sheria za nchi zinahitaji rehema ili kujenga dhana ya urekebishaji na sio mateso yasiyolenga dhana ya urekebishaji”

Mheshimiwa Spika,inaweza kuoneka jambo rahisi mtu kukaa jela miaka saba bila kesi yake na upelelezi kukamilika, waheshimiwa Wabunge nawaomba tena niko chini ya miguu yenu vaeni utu na viatu vya hawa watu na familia zao , ni mateso na huzuni sana , Mimi najua , kila siku ninawaombea kwa Mungu. Hivyo chanzo muhimu kinachosababisha msongamano na mateso magerezani ni ofisi ya DPP, Sheria mbovu zisizozingatia utu, na ucheleweshwaji wa upelelezi kutoka Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP) tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali zenye nia ovu ya kuitumia mahakama ndivyo sivyo [DPP abuse of Courts] kupindisha haki kwa makusudi katika kesi mbalimbali, hususani kuzuia haki ya dhamana kwa watuhumiwa ambao hawajatiwa hatiani na mahakama; DPP akiiwakilisha Serikali hudiriki kufanya hivyo hata katika makosa ambayo kisheria watuhumiwa wana haki ya kupata dhamana..

Mheshimiwa Spika, akisoma hukumu kukemea tabia ya Serikali kupitia DPP kuitumia mahakama kupindisha haki, hukumu ambayo nimeambatanisha katika hii hotuba, katika ukurasa wake wa tisa (9), Mhe. Jaji S.M Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, katika iliyokuwa Kesi ya Rufani ya Jinai Na. 135 ya mwaka 2016 tarehe 3 Machi, 2017 alisema na nitanukuu;

“It is after the bail conditions have been set that in the eyes of the laws, we can lawful conclude that the respondent was actually granted bail and should have only been detained thereafter he failed to fulfill the bail conditions so set. The right of appeal of the aggrieved party would have hence accrued AFTER the bail conditions were set and NOT before that has argued by the appealant”

Jaji Maghimbi aliendelea kusema kuwa;

“The records are that after the objection to bail was overruled, instead of proceeding to set the bail conditions as required by the law, the trial magistrate erroneously the appealant herein to enterfere with the court process by prematurely lodging the purpoted notice to appeal”

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia DPP walikuwa wanaufahamu ukweli uliotolewa na hukumu ya Mhe. Jaji Maghimbi, lakini waliamua kwa makusudi kuipigisha Mahakama Sarakasi haramu ambazo hazipo kisheria ili kuendelea kumweka Mtuhumiwa mahabusu kwa muda wa miezi minne.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuacha mara moja kuitumia ofisi ya DPP kuingilia utaratibu wa kimahakama kutoa dhamana kwa watuhumiwa mbalimbali. Aidha, kwa sababu Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma ni mtumishi wa umma na analipwa msharaha na Watanzania ambao yeye anaitumia ofisi yake kupindisha haki za wananchi, basi achukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufutwa kazi, na kufunguliwa mashitaka mahakamani kwa kosa la kuidhalilisha Serikali yetu katika kesi hii ambayo dhamana ilikuwa wazi kama alivyohukumu Jaji Maghimbi katika hitimisho lake akisema, nitanukuu;

“Given the leghth of time that the respondent was so detained in remand custody, I further find it just that I step in the shoes of the trial court and proceed to finalize the grant of bail to the respondent by setting the conditions hereinunder” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu mara kadhaa ofisi hii imekuwa ikiarifu Mahakama kuwa hawana nia ya kuendelea na shauri la jinai ambalo lipo Mahakamani, lakini mara ya mtuhumiwa kuachiwa huru na Mahakama Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata tena watuhumiwa na kuwaweka kizuini na baadae kurudia makosa yaleyale ambayo upande wa Jamhuri umeiarifu Mahakama kuwa hawana nia ya kuendelea na shauri lililpo Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, hata pale shauri linapofutwa au Jamhuri kueleza kuwa hawana nia ya kuendelea na shauri husika bado wanawakamata watuhumiwa kwa makosa yaleyale. Ni kweli kuwa kifungu cha 225 (5) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kinaeleza kuwa kuachiwa na Mahakama haitawazuia Jamhuri kumkamata mtuhumiwa, lakini mamlaka haya yametumika vibaya kama kigezo cha kuwakomoa wananchi waliowengi ambao wanaachiwa na Mahakama.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kuleta Bungeni haraka iwezekanavyo marekebisho ya Sheria Mbalimbali kandamizi kuhusu mienendo ya makosa ya jinai ili sheria zote katika mwenendo wa makosa ya jinai iakisi utu na urekebishaji ili kupunguza mateso kwa binadamu. Aidha, tunaitaka Serikali kuhakikisha kuwa kitengo cha Upelelezi cha Jeshi la Polisi, na Bajeti ya Mahakama ya Tanzania inakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi, wepesi, uharaka, weledi wa hali ya juu, uzingatiaji wa maadili, haki na utu wa binadamu bila kuwa na njaa na tamaa ya rushwa na ucheleweshaji wa mashauri mahakamani unaotokana na ufinyu wa bajeti kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa maslahi ya Waendesha Mashitaka ya Serikali, Watumishi wote wa Mahakama na Askari Polisi wote yanazingatiwa vizuri ili kuwapa utulivu katika kazi ya kutenda haki na sio vinginevyo.

3.0 UHARAMIA DHIDI YA SIASA NA DEMOKRASIA NCHINI

3.1 Siasa safi na Demokrasia ya kukuza amani nchini

Mheshimiwa Spika, Msingi ya amani katika Taifa inategemea siasa safi na demokrasia huru. Ushindani wetu wa kisiasa unapokosa siasa safi na demokrasia huru ni dhahiri kwamba Taifa halitaweza kuepuka uvunjifu wa amani unaopunguza kasi ya Maendeleo na mshikamano katika Taifa.

Mheshimiwa Spika, katazo la mikutano ya hadhara na kazi za siasa katika nchi sio tu ni hatari kwa vyama vya siasa vinavyozuiwa kufanya kazi zake za siasa na chama dola bali ni hatari kwa demokrasia ya chama dola hicho pia kinachozuia kazi za siasa kwa vyama vingine.

Mheshimiwa Spika, uwepo wa vyama vya siasa vinavyowakilisha maoni ya aina mbalimbali ni nguzo muhimu ya usalama wa Taifa hili. Kitendo cha Serikali ya CCM kupuuza nguzo hiyo ni kuamua kwa makusudi kuliingiza Taifa katika majanga ya chuki yanayoweza kuliingiza Taifa katika migogoro isiyoisha. Ni wajibu wa chama kilichopo madarakani kuhakikisha ukuaji wa demokrasia kuwa ni silaha muhimu ya amani katika nchi na sio kupuuza demokrasia, kudhalilisha vyama vingine visiyokuwa na dola kama CCM inavyofurahia kufanya sasa kule visiwani Zanzibar na hapa Tanzania bara.

Mheshimiwa Spika, wingi wa CCM ndani ya Bunge, unaweza kutumika kupuuza hata maoni haya muhimu, Mwandishi Voltaire aliyeishi kati ya mwaka 1694 na 1778 katika moja ya maandiko yake aliwahi kusema kuwa “It is dangerous to be right when the government is wrong” akimaanisha kuwa “ni hatari kuwa sahihi wakati Serikali haipo sahihi” Hiki ndicho kinachowakuta raia wote wa Tanzania leo hii. Katika Serikali ya awamu hii ya tano tumeona na kuthibitisha namna ambavyo demokrasia na wanademokrasia wanavyopita katika wakati mgumu katika maisha yao ya siasa ya kila siku. Dhambi ya kuua demokrasia hapa nchini msidhani kuwa itaishia kuangamiza upinzani, bali italitafuna Taifa, na itaingia hadi ndani ya chama chenu CCM na wakati huo ukiwadia hakuna kati yenu au watoto wenu atakayesalimika. Only Time will Tell.

Mheshimiwa Spika, ni hatari leo hii kwa Mtanzania kuthubutu kuwa na maoni tofauti na yale ya Serikali. Kusikiliza mawazo yasiyofanana na mtazamo wako na usiyoyapenda ni busara na pia ni dhahabu.

Mheshimiwa Spika, wote ni mashahidi dhidi ya mateso wanayopitia viongozi mbalimbali wa kisiasa katika Taifa hili kwa kuwa na mitizamo tofauti na ya wale waliokalia viti vya utawala kwa wakati huu.

Mheshimiwa Spika, wapo wengi waliopotezwa, kuteswa, kudhalilishwa, kutwezwa utu wao, na wengine kuuawa kutokana tu na kitendo cha kuwa na maoni tofauti na yale ya waliopo katika viti vya madaraka, na mmoja wapo ni pamoja na Ben Saanane.

Mheshimiwa Spika, alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mhe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (Mb), alizua tafrani kwenye familia ya Ben Saanane baada ya kusikika maneno kama “huyu mwenzetu aliyetangulia mbele za haki”

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa Kauli, endapo maneno haya yalikuwa ni ya bahati mbaya kutamkwa au kwa kuwa Waziri Mkuu alitumia hekima na busara zake kufikisha ujumbe kuwa Ben Saanane amekwisha fariki?

Mheshimiwa Spika, Wakati Serikali imetumia gharama kubwa sana kumtafuta faru John, Serikali hiyo hiyo haionekani kufikia ukomo katika juhudi za kutoa taarifa za hatma ya suala hili la Ben Saanane. Na taarifa tulizonazo ni kuwa hata kikundi cha Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), ambacho Ben Saanane alikuwa ni Katibu wake, walipoanza kufuatilia miili ya watu 7 iliyozikwa kando ya Mto Ruvu, walibaini kuwa miili ile imefukuliwa na kupelekwa kusikojulikana haswa mara baada ya kupaza sauti ya kutaka kufanyike vipimo vya DNA ya miili ile 7 ya mto Ruvu.

Mheshimiwa Spika, kuna mtu kapotea, na kuna faru alipotea, faru alipewa kipaumbele kuliko binadamu. Hata kama sisi tunaopiga kelele hatuna nguvu wala uwezo, tunaamini Mungu aliyetupa macho sio kipofu hata asione. Kwa namna yoyote ile au vinginevyo kama wapo viongozi wakuu wa Serikali imehusika kumwaga damu isiyo na hatia ya Ben Saanane, damu hiyo haitanyamaza, itaendelea kulia, na kila aliyehusika atalipa hapa hapa duniani, haijalishi cheo chake, wala uwezo wa majeshi yanayomzunguka.

Mheshimiwa Spika, Louis Farrakhan, mwanaharakati wa Amerika, alisema maneno yafuatayo; “There really can be no peace without justice. There can be no justice without truth. And there can be no truth, unless someone rises up to tell you the truth.” Na sisi, Kambi ya Upinzani Bungeni, kuhusu suala hili la Ben Saanane, tunawaambia kuwa muda ndio hakimu wa haki. Only time will tell.

5.0 UCHAMBUZI WA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017 NA MWELEKEO WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018

5.1 Njia bora za kuzuia Ukatili wa Vyombo vya Dola nchini

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka 2016 ya ‘Mtazamo wa hali ya haki za kiraia na kisiasa Tanzania 2016’ iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, asilimia 81 ya Mikoa yote nchini imepata alama mbaya kabisa za ukiukwaji wa haki ya kuishi. Ripoti hiyo inasema kuwa, ninanukuu; “..Alama hizi za chini zimesababishwa na mambo muhimu kadhaa, kama vile matukio ya polisi kufanya ukatili na kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa kukamata watu wanaohisiwa kufanya uhalifu, muda mwingine kusababisha kifo,….haki ya kuishi inaonekana kuhatarishwa na mauaji na ukatili mikononi mwa vyombo vya dola….”

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Jeshi la Polisi likituhumiwa kufanya mauaji haliwezi kujichunguza lenyewe na kutoa maamuzi lenyewe; basi sharti kuwe na chombo huru kitakacholisimamia Jeshi la Polisi. Kwa muktadha huo wa kulifanya Jeshi letu la Polisi kuzingatia sheria ya Jeshi hilo, Sheria nyingine na Katiba ya nchi yetu na kuachana kabisa na kujirudia kwa makosa ya uadilifu wa Jeshi la Polisi katika kusababisha mauaji na ukatili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuzingatia ushauri uliotolewa na wadau wa Haki za Binadamu kwa kuleta muswada wa Sheria katika Bunge lako tuko utakaounda chombo maalumu cha kuangalia utendaji kazi wa haki ndani ya Jeshi la Polisi, chombo ambacho kitafanya uchunguzi na kuwawajibisha maafisa wa polisi ambao wamejihusisha na mauaji, utesaji au ukatili.

Mheshimiwa Spika, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarejea ushauri ambao tumekuwa tukiutoa mara kwa mara kwa Serikali ambao haujawahi kufanyiwa kazi juu ya kuundwa kwa Mahakama ya Korona (Corners Court) kwa mujibu wa Sheria inayotoa mamlaka ya kuchunguza vifo vyenye utata (Inquest Act) kuchunguza vifo vyenye utata kama kile cha Marehemu Alphonce Mawazo, ambapo mpaka sasa hakuna taarifa mahususi juu ya kifo hicho ambazo zimetolewa na mamlaka za serikali huku ikijulikana wazi kuwa Mawazo aliuwawa mchana kweupe huko Busanda Mkoani Geita.

5.2 Jinsi za Kuzuia Uhalifu nchini kwa Njia ya Bajeti ya Jeshi La Polisi

Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Bunge liliidhinisha kiasi cha shilingi 5,370,041,105 kama Bajeti ya Maendeleo kwa ajili ya Jeshi la Polisi. Kwa mujibu wa randama ya Wizara, Fungu 28 Jeshi la Polisi, hadi kufikia mwezi Februari, 2017 fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Serikali ilikuwa ni jumla ya Shilingi milioni 40 sawa na asilimia 1 tu ya bajeti yote ya maendeleo iliyotengwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, Kwa nyakati tofauti Askari Polisi wanapotekeleza wajibu wao hupiga, hutesa na hata kuteka nyara wananchi na wakati mwingine kusababisha ulemavu hata kifo kutokana na kukosa mafunzo ya kushughulika na ulinzi wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachelea kusema kuwa hali hii inaweza kutokana na bajeti finyu ya maendeleo ambayo ingetumika kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Askari hao. Kitendo cha Serikali kutopeleka fedha za maendeleo kwa ajili ya Jeshi la Polisi kinapunguza weledi wa jeshi hilo kutokana na kukosa mafunzo muhimu ya kuendesha kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kulieleza Bunge lako tukufu sababu za kushindwa kupeleka fedha za maendeleo kwa Jeshi hili ili kuendelea na majukumu yake mahususi ya ulinzi wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kitendo cha kushindwa kupeleka fedha za maendeleo kinalifanya Jeshi Polisi kushindwa kuwekeza kwenye intelgenisia pamoja na mafunzo ya kuimarisha weledi na hivyo kuzuia matukiko kama yale ya kuuawa kwa Askari wa Jeshi hilo Wilayani Kibiti.
5.3 Kuimarisha usalama wa Barabarani

Mheshimiwa Spika, Wakati Wizara ya Mambo ya Ndani inawasilisha makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Taifa limepatwa na Mshituko mkubwa sana juu ya Ajali mbaya sana iliyotokea huko Karatu Mkoani Arusha na kusababisha vifo vya watoto wa shule ya Msingi Lucky Vicent ya jijini Arusha ambapo walimu wawili na dereva wagari na wanafunzi 32 wote walipoteza maisha papo hapo.

Mheshimiwa Spika, sio muhimu tena kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuja na takwimu za idadi ya vifo na ulemavu unaotokana na ajali za barabarani. Takwimu ziko wazi kwamba watu wanapoteza maisha kila uchwao. Pamoja na Sheria kali za usalama wa Barabarani kutungwa, ni muhimu sasa masuala yanayohusu usalama barabarani yakaanza kufundishwa kuanzia shule za msingi mpaka katika vyuo vya elimu ya juu. Kwani usalama wa barabarani hauhusu gari peke yake bali inahusu pia namna sahihi ya matumizi ya barabara kwa kila mmoja wetu na watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayo taarifa kwamba, fedha na mafunzo ya Askari wa Usalama barabarani (Traffic) hayajafanyika kwa muda mrefu na hivyo Askari wengi wa barabarani wanafanya kazi kwa mazoea badala ya utaalamu. Hii ndio sababu kazi yao imekuwa ni ya kuvizia hadi kufikia kupanda juu ya miti na kamera za tochi huku wakiamini kuwa kosa la barabarani ni mwendo kasi peke yake. Hawana uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina hata juu ya matatizo ya mifumo ya magari kwa undani.

Mheshimiwa Spika, Leo hii kitengo hicho cha traffic kinatumika kukusanya mapato kazi ya TRA badala ya kutumika kuelimisha jamii juu ya usalama barabarani jambo ambalo ndio dhima ya uanzishwaji wa kitengo hicho.

Mheshimiwa Spika, Serikali inayojivunia mapato yatokanayo na makosa ya barabarani, inakosa uhalali wa kutuma salamu za rambirambi pindi ajali na vifo vinapotokea, kwa kuwa haitumii fedha hizo kupunguza ajali za barabrani. Imekuwa ni jambo la kawaida badala ya kutoa taarifa za kupungua kwa matukio ya ajali za barabrani, Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, linajigamba kukusanya mapato ya makosa ya barabarani jambo ambalo linawavutia askari wa kikosi hicho kusahau kuwa wajibu wao sio kukusanya fedha bali wajibu wao ni kuhakisha usalama barabarani na kuzuia matukio ya ajali yasiongezeke.

Mheshimiwa Spika, Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaasa wananchi wawe makini katika chaguzi zinazokuja, kwani vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani ni sehemu ya majanga mengi yanayotokana na Serikali hii ya awamu ya tano kushindwa kusimamia ustawi wa Taifa.

5.4 Masilahi duni ya askari Polisi na Magereza

Mheshimiwa Spika, askari wetu wanahitaji mazingira bora na masilahi bora wawapo kazini. Nguzo ya kwanza ya ulinzi kwa askari ni yeye kuwa na amani, askari wasiokuwa na maslahi bora ni hatari kwa usalama wa taifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuacha kucheza na masilahi ya askari wetu na kuanza kuwalipa mishahara vizuri pamoja na posho zote zilizoko kisheria kama ambavyo wanafanya kwa watumishi wengine wa umma kama Wabunge na Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikipokea mara kwa mara taarifa za manyanyaso yanayotokana na urasimu na uonevu unaofanywa dhidi ya askari wetu. Hivi karibuni Askari magereza Anjela Masawe alishushwa cheo kazini na kuhamishwa kituo chake cha kazi kwa sababu ya kumuuliza waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mwigulu Nchemba habari za posho zao (package), Askari huyu ambaye kituo chake cha kazi ilikuwa ni gereza kuu Arusha, sasa amehamishiwa gereza la Mang’ola kama adhabu.

5.5 Kuzuia Msongamano Mahabusu na Wafungwa Na Bajeti Ya Maendeleo – Jeshi La Magereza

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepitia randama ya Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo Fungu 29 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na kubaini kuwa bajeti ya maendeleo iliyopelekwa katika Jeshi la Magereza na Serikali mpaka mwezi Februari, 2017 ni asilimia 6 tu ya bajeti yote ya Fedha za Maendeleo kwa ajili ya Jeshi hilo ambazo zilizoidhinishiwa na Bunge ilikuwa ni shilingi 3,053,380,000 na ambapo fedha zilizotolewa ni shilingi 190,000,000 pekee.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza nchini limenukuliwa likitoa lawama kwa Serikali kutokana na kuruhusu msongamano magerezani bila kuwa na juhudi zozote za kutatua shida hiyo. Ikumbukwe kuwa Magereza nchini yana uwezo wa kuhifadhi wahalifu 29,552 kwa siku lakini yanapokea wastani wa wahalifu kati ya 35,000 hadi 38,000. Katika Randama ya fungu 29 Jeshi la Magereza limeitupia Serikali lawama likisema kuwa “Msongamano huu unatufanya tusiweze kutoa huduma ipasavyo kutokana na fedha kidogo zinazotolewa na Serikali”

Mheshimiwa Spika, Ufinyu wa Bajeti kama unavyosomeka kwenye randama limesababisha kutofanikiwa kwa masuala mbalimbali ya kimaendeleo ya Jeshi hilo kama ifuatavyo;
1. Ukosefu wa Nyumba za Maafisa na Askari
2. Upungufu wa vyombo vya usafiri
3. Upungufu wa watumishi
4. Madeni ya watumishi (Sh bilioni 23.03 na Wazabuni Sh billion 44.92)
5. Ukosefu wa Ofisi stahiki za wakuu wa Magereza wa Mikoa
6. Uhaba wa madawa na vifaa tiba
7. Uhaba wa vitendea kazi

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza kwa mwaka wa fedha 2017/2018 limeomba fedha za bajeti ya maendeleo Shilingi 7,254,742,000 sawa na ongezeko la asilimia 58 la bajeti iliyoidhinishwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaihoji Serikali, inawezaje kuleta hapa ongezeko la bajeti ya maendeleo kwa asilimia 58 zaidi kuliko ile bajeti ya mwaka wa fedha unaoenda kuisha, kama sio kulihadaa jeshi la magereza kuwa watapatiwa bajeti kubwa wakati uwezo wa Serikali kutoa fedha zote haupo?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza vyema Sheria ya Parole, na utekelezaji wake uzingatie kuwaachia huru wafungwa ambao wameshatumikia vifungo virefu gerezani badala ya wale ambao wamehukumiwa miaka michache na wanaachiwa na Parole kila mara. Uzoefu unaonyesha kuwa wafungwa wa vifungo vidogo wanaochiliwa kwa parole ni wafungwa wanaorudiarudia makosa kulikoni wale ambao tayari wameshakaa magereza muda mrefu na hutamani uhuru kwa shauku kubwa. Endapo jambo hili litafanyika kila mara na kwa wakati litapunguza msongamano magerezani hasa wale wa vifungo virefu ambao kimsingi huwa tayari wamejifunza na kujirekebisha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa bodi ya Parole, ifike mahali iwaachilie wafungwa wote waliofungwa wakati wa Nyerere na Wakati wa Mwinyi na hata wakati wa Mkapa ambao wana zaidi ya miaka 10 mpaka 15 magereza. Kwani ni imani ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa watu hao wameshajifunza kiasi cha kutosha. mtu amekaa jela miaka 25, na ana miaka zaidi ya 65 akipata msamaha kisha akawa huru, kweli mtu huyo anawezaje kuwa mhalifu tena?

Mheshimiwa Spika, lakini pia haki nyingine za mahabusu ni pamoja na maisha yao ya ndani ya kila siku, ni maisha ya huzuni kwao pamoja na wafungwa. Chakula sio kizuri , malazi ni ya shida kubwa , selo yenye uwezo wakuchukua watu 35 wanaweza kulala hata watu 80 , mawasiliano yao na ndugu zao ni tabu kwani mpaka leo Magereza Tanzania wanatumia kanuni zilizoachwa na mkoloni kuendesha masuala ya magereza.

Mheshimiwa Spika, kuna unyanyasaji wa aina mbalimbali ambao maneno hayawezi kutosha kuyaelezea katika hotuba hii unaotokana na tabia za askari na mfumo mbovu wa kanuni za uendeshaji magereza. Kwa mfano; wafungwa na mahabusu huvuliwa nguo zote na kupanuliwa makalio yao kwa ajili ya kupekuliwa mara watokapo na kuingia magerezani wakati hasa wakati wanakwenda mahakamani na wakati wa kurudi ikiwa ni pamoja na kutoka kwenye shughuli nyingine mbalimbali ambao mar azote wanakuwa chini ya ulinzi wa askari. Vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Magereza hapa nchini kuwavua nguo mahabusu na wafungwa sio cha kibinadamu ni utekelezaji wa mikakati ya kishetani. Ni tendo la aibu sana kwa Wazee na Vijana wanapokusanyika kufanyiwa hivi hadharani, hata Askari wanaofanya kazi hii na wao wanatiwa huzuni bila sababu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa Jeshi la Magereza kuacha mara moja udhalilishaji dhidi ya utu wa binadamu, na pia Serikali kutenga fedha za vifaa vya kisasa kwa ajili ya upekuzi wa mahabusu na wafunguwa katika magereza yote nchini kwa kutumia mbinu za kisasa ambazo hazitwezi utu wa binadamu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni pia imetambua ugumu wa mawasiliano uliopo ndani ya Mahabusu na Magereza. Hivyo tunaitaka Serikali kuweka ‘Simu Maalumu’ (Call Box) ili kurahisisha mawasiliano baina ya ndugu, mawakili na mahabusu na wafungwa walioko magerezani. Mawasiliano jela kutoka kwa mahabusu au wafungwa kwenda kwa ndugu au jamaa ni magumu sana , Wakati wenzetu wa Kenya wamefikia mahali hata wafungwa na mahabusu kuruhusiwa kuonana na watoto wao, Kenya wameunda sehemu maalumu (Childrens corner)ambapo mahabusu au wafungwa hukutana na familia zao na kupanga mikakati ya maisha. Hapa kwetu Tanzania hata simu kupiga kuijulia hali familia ni jambo ambalo ni marufuku kubwa. Huu sio utu bali ni unyama uliopitiliza.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.