Annan amesema tabia ya Trump ya kuchupiachupia na “kutoa kauli za kukurupuka zinafanya iwe tabu kwa mataifa yanayohitaji uongozi kutoka Marekani.”

Akiwa ameambatana na viongozi watatu wa “Kundi la Wazee wa Busara”, Annan aliwatwisha jukumu viongozi wakuu wa Magharibi na kwengineko duniani kupambana na ongezeko la siasa kali za mrengo wa kulia.

Alisema haoni faida ya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini, akihoji kwamba yataongeza tu kitisho cha vita vya nyuklia, huku pia akimuonya Rais Trump dhidi ya kuiondoa Marekani kutoka makubaliano ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Annan alimuelezea Trump kama “aina ya kiongozi anayekuja mjini na kuingia madarakani akiamini kuwa ana majibu ya kila jambo,” kwa kutumia visingizio vya Mexico au China kwenye matatizo makubwa ya kimfumo na ya muda mrefu, huku akiweka kando jitihada za kimataifa za kukabiliana na changamoto za uhamaji.

“Punde kidogo wanakwenda kwenye chumba cha ukweli na wanang’amua kuwa kumbe si rahisi kama walivyodhani,” alisema Annan kwenye mazungumzo hayo na bodi ya wahariri ya AP, akiwa amezungukwa na rais wa zamani wa Ireland, Mary Robinson, waziri mkuu wa zamani wa Norway, Gro Harlem Brundtland na mpatanishi wa amani wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa, Lakhdar Brahimi. “Ama watapaswa kubadilika kutokana na mazingira…au wabakie na mitazamo yao na washindwe moja kwa moja na waondoshwe kabisa mjini.”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.