Ikijibu kitisho cha karibuni kabisa kwamba Saudi Arabia itauhamishia mgogoro wake ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, serikali mjini Tehran imeapa kwamba haitakibakisha chochote kimesimama nchini Saudia zaidi ya miji miwili mitukufu ya Makka na Madina, pindipo Saudia itafanya jambo lolote la “kijinga!”

“Tunawaonya wasije wakafanya lolote la kijinga, hatutawacha chochote isipokuwa Makka na Madina,” Waziri wa Ulinzi wa Iran, Hossein Dehghan, alikiambia kituo cha televisheni ya Kiarabu cha Al Manar kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

“Wanadhani wanaweza kufanya lolote kwa kuwa tu wana kikosi cha jeshi la anga,” aliongeza akimaanisha operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen dhidi ya wanamgambo wa Kihouthi wanaoaminika kuungwa mkono na Iran.

Kauli hii ya Dehghan inafuatia matamshi yaliyotolewa na Naibu Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ambaye Jumanne iliyopita alisema vita vyovyote vya kuwania ushawishi kati ya nchi hizo mbili “vitapiganwa ndani ya ardhi ya Iran na sio Saudia.”

Katika mahojiano ya nadra sana na vituo kadhaa vya nchini mwake, mwanamfalme huyo mwenye umri wa miaka 31 na aliyetangazwa mrithi na baba yake, Mfalme Salman, mwaka 2015, alielezea mtazamo wake kuhusiana na Iran ya leo, akirejelea tuhuma za muda mrefu za mataifa ya Sunni ya Ghuba kwamba Iran inataka “kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu” na kusambaza Ushia, kwa mujibu wa shirika la habari la AP.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.