Chaguzi za wabunge wanaotakiwa kuingia kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) zimefanyika, ingawa hatuwezi kuhoji kuwa zimemalizika, angalau kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako makandokando ya kisiasa yalitumika kuigeuza sheria kutumikia siasa ya mtawala.

Ila hilo silo shughiliko kuu la makala hii. Badala yake, tujikite kwenye kuuangalia mustakabali wa kanda hii nzima mikononi mwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo imo kwenye safari yake ndefu kutoka taasisi ya kibiashara na kijamii kuelekea kuwa taasisi kubwa ya kiuchumi na kisiasa.

Unapoizingatia kauli mbiu yake ya ‘One People, One Destiny’, ni jambo la mantiki kuiona taswira iliyomo kwenye akili za wale wanaoiamini, ambayo ni Afrika Mashariki moja yenye sarafu moja (na kwa hivyo uchumi mmoja mkubwa wa pamoja), paspoti moja (na kwa hivyo uraia mmoja na yanayoambatana nayo) na, hapana shaka, serikali moja kubwa ya pamoja yenye siasa moja ya ndani na ile ya nje.

Kihistoria, dhana nzima ya jumuiya hii imejengwa juu ya wazo la shirikisho, ambalo linasemwa kuwa walikuwa nalo viongozi wa kwanza wa baada ya uhuru kwenye mataifa ya Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar.

Bahati mbaya ni kuwa hisabati za hapa na pale za kisiasa kwenye mataifa hayo machanga zikawa zinawapelekesha sivyo viongozi hao, na ndipo wakaangukia kwenye masalia ya bodi waliyoirithi kutoka kwa Muingereza na kuiwekea nyenzo mpya ili uwe mwanzo kuelekea kwenye shirikisho siku zijazo.

Kwa hivyo, tangu hapo awali, EAC ina kesho yake – dhamira ya kuliona eneo hili tajiri kabisa kwa kila maana ya neno, likiwa imara na kuutumia utajiri huo kusonga mbele kama dola kubwa kabisa lenye nguvu sio tu ndani ya bara la Afrika, bali pia ulimwenguni.

Na hilo linawezekana, hasa ukichukuwa historia ya madola kabla ya majilio ya wakoloni wa Kizungu kwenye eneo letu. Hata kabla Wazungu hawajajinasibu kuwa Dola ya Kirumi, kwetu kulishakuwa na Dola ya Azania iliyolitawala eneo lote la mashariki na kusini mwa Afrika, zikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kenya za leo, kisha kukaja Dola ya Zanzibar iliyotapakaa eneo zima la pwani na ndani ya Afrika Mashariki na Kati.

Ndiyo kusema kuwa na shirikisho au hata dola moja kubwa la Afrika Mashariki si ndoto tu ya waasisi wa dhana yenyewe, bali ni muakisiko wa ukweli ambao watu wa eneo hili wana uzoefu nao kihistoria – ukweli waliowahi kuiishi.

Lakini lazima tukiri pia kuwa kuna mapungufu makubwa yaliyomo kwenye Afrika Mashariki ya leo, ambayo yanaifanya dhamira hii kuwa ngumu kutekelezeka. Mojawapo ni siasa za karibuni za ndani ya madola yanayounda jumuiya hii kwa sasa, iwe kwa waasisi watatu wakongwe – Kenya, Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – na hata kwa waliojiunga baadaye – Rwanda, Burundi na dola changa na mwanachama mpya kabisa, Sudan Kusini.

Wakati Afrika Mashariki ikipigania kuiishi ndoto yake hiyo, changamoto za kisiasa za ndani na za nje ya eneo letu zinabadilika na kugeuka kwa kasi. Hapa tuzungumzie moja tu, nayo ni mfumo unaokuja juu kwa kasi wa chama dola ndani ya kile kinachoelezwa kuwa ni mfumo wa vyama vingii vya kisiasa.

Takribani nchi zote tano ambazo sasa zinaunda EAC zinaongozwa na mfumo huu, ambapo vyama vinavyojinasibisha na ukombozi (uwe wa kutoka kwa wakoloni au wa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe) ndivyo hivyo hivyo vilivyojigeuza kuwa vyama tawala na vya kudumu kwenye madaraka. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina CCM tangu 1977 (kabla ya hapo watangulizi wake TANU tangu 1961 kwa Tanganyika na ASP tangu 1964 kwa Zanzibar), Uganda ina NRM tangu 1986, Rwanda ina RPF tangu 1994, Burundi ina CNDD-FNDD, Sudan Kusini kuna SPLM na Kenya kuna Jubilee ambacho kwa hakika ni mtoto wa KANU kama ilivyo CCM mtoto wa TANU na ASP.

Kuwa na uongozi imara wa mtu mmoja ama chama kimoja ilikuwa nyenzo muhimu sana kwenye kuileta Afrika Mashariki siku hizo mataifa ya awali yakipata uhuru wake kutoka kwa Muingereza, lakini siku zimebadilika sana ndani ya kipindi hiki cha miaka 50.

Sasa, sio tena umadhubuti wa mtu mmoja ama chama kimoja unaoweza kuifikisha ajenda kubwa ya umma mahala fulani, bali ni umadhubuti wa taasisi za uwakilishi wa umma ndani ya mataifa husika. Huu ni wakati wa maamuzi yote makubwa ya umma kuchukuliwa na umma wenyewe na ushirikishwaji wa kiwango kikubwa wa wananchi.

Mwenendo wa kisiasa ndani ya mataifa yanayounda jumuiya hii kwa sasa unaonesha kukuwa kwa kasi kwa tabia ya mfumo wa chama kimoja ndani ya udanganyifu wa vyama vingi. Watu wale wale wanaobadilisha majina ya vyama kusalia madarakani milele kama ilivyo kwa Kenya ama vyama vile vile vinavyocheza na sheria na katiba vitakavyo kama ilivyo kwa Tanzania, Uganda na Rwanda, si nyenzo inayofaa kwenye kuijenga kesho ya Afrika Mashariki.

Hasara iliyopo ni kuwa wazo zuri kama la ‘One People, One Destiny’ – watu wamoja, jaala moja – imemilikishwa kwenye mikono ya wachache, watawala na vyama vyao na, katika baadhi ya mifano, hata watawala na familia zao binafsi. Angalia, mathalani, nani wanatumwa kwenye Bunge la Afrika Mashariki kutoka kwenye mataifa wanachama!

Shirikisho imara na lenye nguvu la Afrika Mashariki, kwa hakika, limo kwenye dhana nzima ya kuwashirikisha wana wa Afrika Mashariki wenyewe kwenye utekelezaji wake, na sio kwenye kuugeuza kuwa mradi wa watawala na aila zao.

Hilo linawezekana kwa kuimarisha taasisi za ndani zinazosimamia ushirikishwaji huo, vikiwemo vyama vya kisiasa, mifumo ya haki na sheria, na utunzaji wa dhati haki za binaadamu na demokrasia. Na sio kuzivunja taasisi hizo kama ambavyo inaonekana ndiyo jukumu kubwa la sasa la watawala walioko madarakani kote Afrika Mashariki.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 19 Aprili 2017

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.