Jumatatu ya tarehe 21 Machi 2016, Dk. Ali Mohamed Shein aliamka mapema kisha akasimama mbele ya kioo chake kujiangalia. Ile taswira kwenye kioo ikamuambia: “Wewe ni Ali tu!” Mwangwi wa sauti hiyo ukatoka nje na kumchoma moyoni, naye kwa hasira akajibu: “Hapana. Mimi sio Ali tu. Mimi ni Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, niliyechaguliwa na asilimia 70 ya kura halali.” Alipokiangalia tena kile kioo, ile taswira aliyoiona ikamuambia tena: “Wewe ni Ali tu!”

Ni mwaka mzima sasa tangu hayo kuanza kutokezea na hiyo ndiyo hali ilivyokuwa, ilivyo na itavyokuwa kwake muda wote wa miaka mitano ya awamu hii ya utawala wake. Kila siku, Dk. Shein anajikuta akipaswa kukabiliana na kivuli chake mwenyewe, ambacho kimekuwa kikimsuta kwa kumueleza yeye ni nani hasa, naye kila siku anataka kuthibitisha vile anavyojidhani ndivyo alivyo.

Tafauti na Rais Ali Mohamed Shein wa 2010 hadi 2015, huyu wa 20 Machi 2016 na kuendelea ana miaka migumu mno maishani mwake. Sababu ni kuwa nafsi yake imepasuka baina ya kujijuwa kuwa alipo sipo au aliyepo hapo si yeye. Hata katika kilele cha kujitoa fahamu anachojikuta kuwa nacho, bado kuna kitu ndani yake kinamrejesha kwenye ukweli wa mambo na ukweli huo unamuonesha taswira ya kwenye kioo – Ali tu.

Msikilize kila mara anapoinuka kujibizana na watu wasioutambua uhalali wake wa kushikilia nafasi ya urais wa Zanzibar, ndipo utajuwa kuwa Dk. Shein huyu si yule ambaye alikuwa na fahari ya kuyashikilia madaraka yaliyomuhalalikia. Mara kadhaa amenukuliwa akirajisi malalamiko yaliyochanganyika na vitisho vyenye kibwagizo vya kupambana na kioo: “Mimi ndiye, wewe siye!”

Jamii yako inapokumbwa na matatizo yanayotokana na dhuluma ya mwenye nguvu dhidi ya mnyonge, ile dhana waliyonayo wajiitao wasomi ya “kutokuwa na upande” huwa ni alama ya ujinga wao, kwa sababu huwa wanamsaidia dhalimu kwenye vita vyake dhidi ya mnyonge na kushirikiana moja kwa moja na dhalimu dhidi ya mnyonge huwa ni ukatili.

Namzungumzia myonge wa Zanzibar ambaye tayari alishakuwa taabani kwa kuwa serikali yake iliamua kutumia makundi ya uhalifu wa kisiasa yanayolindwa na vyombo vya dola, yampige, yamtese na yamuharibie mali zake. Vyombo hivyo vya dola, ambavyo kimsingi vilikuwa na wajibu wa kumlinda, tayari vilishamueleza kuwa yeye hasa ndiye muhalifu na hivyo asitazamie ulinzi wowote.

Kinachotokea Zanzibar hadi hivi sasa, ikiwa ni mwaka mzima tangu uhuni wa Machi 20, kinatuhitaji kuchagua upande upi tunasimama kwenye kuielezea hali yenyewe. Hadi wiki chache zilizopita makundi yanayoitwa Mazombi yemeendelea kuwanyanyasa wanyonge.

Kwenye suala la Zanzibar, mimi nimechaguwa upande walio wanyonge hao ambao wana hadithi za kusikitisha kila siku, eti tu kumthibitisha anayekanushwa na kioo chake mwenyewe kuwa ndiye. Ndizo hadithi za kupigwa kwa watu wazima – wanaume na wanawake, kuchomewa moto nyumba zao, ofisi za vyama na vituo vya afya, maeneo ya kukusanyika, na kukamatwa kwa hadi watoto wa miaka 14.

Yote haya yalianza na kile kilichoitwa “Uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016” ambao lengo lake pekee lilikuwa ni kumpatia Dk. Shein jina la urais wa Zanzibar na uwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Baada ya hapo, Zanzibar imeendelea kupiga hatua za kurudi nyuma, kuzidi kupasuka, ikiselelea kwenye giza la hasira na chuki.

Mimi nimechaguwa upande na wala sitakaa nikasema ninajipumbaza kusaka mizania ya mambo kwenye hili, kwa sababu si jambo lenye mizania. Amri ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli, ya kuwashughulikia waleta fyokofyoko visiwani Zanzibar haiwezi kutiwa kwenye mizania na kauli za viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliolalamikia kuwa wamekuwa wakiteswa, kuadhibiwa na kudhalilishwa na sasa wamechoka. Kuchoka kwao hakuwezi kuwekwa sawa na kuzidi kuumizwa kwa wananchi visiwani Zanzibar.

Mimi nimechaguwa upande wa wale ambao hali yao ya maisha imezidi kuwa mbaya kwa sababu ya kutawaliwa na mfumo wa utawala usio ridhaa ya wananchi na ambao, kwa kulazimishwa kutawaliwa huko kumeidamirisha nchi.

Mimi nimechaguwa upande wa kumuambia Dk. Shein kwamba ikiwa gharama za yeye kuitwa rais ni hizi tunazozishuhudia sasa, basi kioo chake kitaendelea kumkumbusha kuwa yeye ni Ali tu. Ni kweli anaendelea kupigiwa ving’ora. Anaendelea kufungwa nyuzi za viatu. Anaendelea kupigiwa saluti. Anaendelea kwenda na kurudi Ikulu. Lakini yote hayo hayatakuwa na maana ya kumfanya kweli kiongozi anayezitawala nafsi za wale anaodhani kuwa wako chini ya utawala wake. Kwao wao, yeye anabakia kuwa ni Ali tu kama anavyoonekana na kioo chake.

Nimechaguwa upande wa mnyonge aliyepanga foleni siku ya tarehe 25 Oktoba 2015 kutoka Bungi Miembe Mingi hadi Msuka Mtongani na akapaza sauti yake ya nani awe nani kwenye nafasi za uongozi wa nchi yake kwa miaka mitano hii. Nilimuona. Nilimsikia. Na hadi sasa nikifunga macho usiku gizani, naweza kuuhisi uwepo wake ndani yangu. Alikuwa sahihi wakati ule na yuko sahihi leo hii.

Niko upande wa mnyonge huyu pale anaposema kuwa kwake uchaguzi ulishafanyika na kumalizika Jumapili ile ya Oktoba 25 na hautambui mwengine kabla ya mwaka 2020. Ikiwa leo hii anaadhibiwa kwa msimamo wake huo, basi mimi niko pamoja naye.

Inawezekana, kuwa kwa sote wawili – mimi na yeye – tu wanyonge, basi kuwa kwangu pamoja naye kusipunguze chochote kwenye maumivu anayoelemezewa na utawala ambao hautaki kusikia neno “HAPANA” kutoka kwake. Lakini angalau nakumpe moyo kuwa hayuko peke yake, na kamwe hatokuwa.

Tanbihi: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 28 Machi 2017.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.