Kwa kutumia ghiliba ya mtazamo hasi wa kihistoria, kundi la wanasiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) waliikaba pumzi dhana nzima ya umoja wa kitaifa na maridhiano ya Wazanzibari. Hawa walikuwa hawakuyaridhia maridhiano haya tangu kwenye siku zake za awali pale Novemba 2009 yalipoasisiwa na aliyekuwa kiongozi wa Zanzibar na wa chama chao kwa wakati huo, Rais Mstaafu Amani Karume.

Walifanya kila waliloweza kuyavunja kwenye hatua zake za awali, lakini kwa kuwa mwenyewe Rais Karume alikuwa amesimama imara kuyalinda na kuyaongoza, hawakufanikiwa pakubwa.

Bahati mbaya ni kwamba mfuatizi wake, Dk. Ali Mohamed Shein, ama alikosa imani na maridhiano ya Wazanzibari au hakuwa na ujasiri aliokuwa nao Rais Karume na hivyo haraka mno kundi lililokuwa dhidi yake likamshinda nguvu na kuyashinda nguvu maridhiano yenyewe.

Matokeo yake, kwa maslahi ya matumbo yao, wanasiasa hao waliweza kuyachafuwa hata bado pakiwa na kile kilichoitwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wakayasusuika hadharani na kuyatia nuhusi kila walipopata fursa ya kufanya hivyo. Rejea nukuu mbalimbali za wanasiasa wa kundi hilo kama vile Marehemu Awadh Salmin, Haji Omar Kheri, Vuai Ali Vuai na wenzao.

Kwa bahati mbaya sana ni kuwa walikuwa wakifanikiwa kwa kila hatua waliyopiga ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kilele cha mafanikio yao, hata hivyo, kikawa ni kuuvuruga uchaguzi  wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwenye hatua zake za mwisho, hapana shaka kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kimsingi ilijihisi kutengwa kando na Maridhiano hayo na hatua zilizoambatana nazo, kama yale Mabadiliko ya Katiba yaliyoitambua Zanzibar kuwa nchi na kuanzisha mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Sasa ni mwaka wa pili bila ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, mwaka wa pili bila ya Maridhiano ya Wazanzibari, na swali kubwa ambalo unaweza kuwauliza walioyakaba pumzi maridhiano hayo ni je, Zanzibar imefaidika nini ndani ya kipindi hiki?

Kijuujuu, wanasiasa hawa wanaotumia ghiliba kudumisha maslahi yao wanahoji kwamba serikali ya umoja wa kitaifa haikuwa na nafasi ya kuishi kwa kuwa inakinzana na historia ya Zanzibar. Wanasema kuwa CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), kama vyama viwili vikubwa na pekee vinavyoongoza siasa za Zanzibar, haviwezi kuridhiana na kushirikiana kuongoza nchi hii kutokana na kuchimbukia katika asili zinazokinzana.

Kwao wao, wana-CCM ni watoto wa Afro-Shiraz Party (ASP) na CUF ni watoto wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP). CCM ya Waafrika weusi na CUF ya Waarabu na machotara. Kwa hivyo, wawili hawa hawaivi chungu kimoja.

Mbali ya kuwa kwake hoja ya kipuuzi sana katika zama zetu hizi, bado ndiyo wanayoitumilia licha ya kuwa wenyewe hawaiamini. Kwa maslahi ya wale wanaowapotosha, leo nataka nifafanuwe mapungufu makubwa mno yaliyomo kwenye hoja yenyewe.

Kwanza, msukumo wa kihistoria, ambao ndio unaozaa mjengeko wa kijamii na kitamaduni, unazungumza hadithi tafauti kwa upande wa Zanzibar. Kwamba Wazanzibari ni watu mchanganyiko na kwamba kupitia mchanganyiko huo ndipo maisha yao yanapokwenda mbele katika kila nyanja – kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Pande zote mbili ya kisiasa kabla ya Uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964 visiwani Zanzibar zilikuwa na wafuasi wenye mchanganyiko huo. Wazanzibari wenye asili ya ndani ya Bara la Afrika walikuwemo kwenye ZNP na ZPPP kama ambavyo Wazanzibari wenye asili ya nje ya bara la Afrika walikuwemo kwenye ASP. Na katikati yao palikuwa na waliochanganya damu vizazi kwa vizazi.

Kila mara, mwenendo wa siasa za Zanzibar ulipodharau au kukandamiza dhati hii ya mchanganyiko, basi mustakabali wa visiwa hivi ulitiwa rehani na kuingizwa katika majaribu makubwa. Ndivyo ulivyo ukweli wa sasa, miaka miwili baada ya kuvunjwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Nchi imerudi nyuma kwa hatua nyingi.

Pili, hata kwa kutumia hayo hayo mapokezi ya kihistoria wanayosema wanayaamini wauwaji hawa wa maridhiano, bado historia hiyo si sehemu salama kwao kujifichia, maana ni gofu lililojaa woga, kujishuku na kutokujiamini.

Kwa mfano, mara kadhaa tumewasikia wakisema “Zanzibar inapaswa kusahau yaliyopita“ (wakikusudia uhuni wao wa tarehe 28 Oktoba 2015 walipouvuruga uchaguzi halali). Lakini ni kosa kubwa kudhani kuwa kusahau yaliyopita kunamaanisha kufuta sehemu fulani ya taarifa zilizomo kwenye kumbukumbu ya mtu. Kwamba Wazanzibari wasahau kuwa tarehe 25 Oktoba 2015 walishuka vituoni mapema asubuhi na kushinda huko jua na mvua kufanya maamuzi yao ya nani awe kiongozi wao kwa miaka mitano inayofuatia.

Hapana, hilo si sahihi! Usahihi ni kwamba, kupita kwa jambo hakumaanishi kusahauliwa kwake, na hata kusahau kwenyewe hakumaanishi kuwa taarifa za jambo hilo zimetupwa katika debe la takataka, ambako haziwezi kupatikana tena. Oktoba 25 ipo vichwani mwa walioshuka vituoni siku hiyo kama vile ndio kwanza ilikuwa jana.

Tatu, kadiri wauwaji hawa wa Maridhiano ya Wazanzibari wanavyotumia historia kuhalalisha ukaidi wao kwa Umoja wa Kitaifa, kwa upande mmoja, huku wakisema yaliyopita yasahauliwe, ndivyo wanavyoirejesha wenyewe Zanzibar kwenye kile watumiaji wa mitandao wanachokiita ‚’mashine ya kusaka taarifa’ (search engine) na huko wanabonyeza programu ya kufichua kumbukumbu. Hilo, kwa hakika, haliwasaidii kujenga hoja yao.

Miongoni mwa njia za kufichua kumbukumbu kutoka kwenye akili ni kuyarejearejea maneno muhimu ya taarifa yenyewe (kama kauli yao maarufu kuwa nchi iliyopatikana kwa mapanga haitachukuliwa kwa vikaratasi), kupata taarifa zinazofanana nayo (kama kuendelea kuyatumia makundi ya kihalifu kupiga na kujeruhi watu hadi sasa) na au kufuatana kwa taarifa zenyewe (kama kuuharibu kwa makusudi uchaguzi wa 2015 kwenye hatua zake za mwisho za kutangazwa matokeo).

Sasa ni upi muelekeo wangu kwa leo? Kwa kuwa hiyo ndiyo historia ya Zanzibar na hayo ndiyo makovu yake, na kwa kuwa jitihada yoyote ya kuendelea kujifungia kwenye gofu hili la historia ni kujihalalishia vitisho, woga na kutokujiamini, basi yeyote mwenye akili timamu na dhamira njema kwa nchi hii, hataupa mgongo mlango wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, maana ndio pekee ‘utakaomtoa’ yeye na kuitoa Zanzibar yetu.

Mwenye akili timamu Zanzibar, hasa akiwa kwenye nafasi ya uongozi na kundi la wafuasi, anapaswa kutafuta njia muafaka ya kuifanya historia imsaidie kupiga hatua mbele kama kiongozi wa watu anayejiamini.

Hapaswi hata kidogo kuutumia mtazamo wa kihistoria kuzalisha wauwaji wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, maana busara yake inasema kitu tafauti na ung’ang’anizi wa mambo. Busara ya mtazamo huo inasema kuwa kujuwa tukuendako ni kwa kujuwa tutokako na kupaelewa tulipo. Na ili hilo lifanyike, ni lazima tukumbuke na tujifunze kwa kukumbuka huko. Kwamba ikiwa kuna mabaya yoyote yaliyotutokezea, basi tupate somo la kujifunza yasijirudie tena.

Historia ya Zanzibar ni shuhuda wa ubaguzi na matokeo yake mabaya, kukiwemo kudidimia kiuchumi, kielimu na kisiasa. Ukaidi hausaidii kitu, maana hata macho ya kawaida yanaona kwamba wenzetu wengi ulimwenguni, waliokuwa kama sisi, wameendelea kusonga mbele sana kwa sababu kile kinachotukuzwa Zanzibar – yaani upotofu wa ubaguzi – kinadharauliwa huko.

Kama kweli wanaamini kwenye mtazamo wa kihistoria, basi nawawe wa kwanza kupingana na ubaguzi, kuheshimu matakwa ya wananchi na kuyarejesha Maridhiano na Umoja wa Kitaifa wa Wazanzibari.

Zanzibar inataka kukwamuka kutoka mkwamo huu iliotiwa na ambao hauna manufaa yoyote kwa yeyote – hata kwa hao wanasiasa wanaodhani matumbo yao yanashibishwa na mpasuko uliopo!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.