NIMEKUWA nikilitafuta neno moja la Kiswahili kuielezea hali ya Zanzibar ilivyo na inavyoelekea kuwa endapo mambo yake yataendelea kuwa yayo kwa yayo, tuseme katika kipindi cha miaka kumi au ishirini ijayo.  Kila neno nililolizingatia na kulipima nimehisi kuwa halikidhi haja. Halitoshelezi kuielezea jinsi hali hiyo ilivyo au itavyokuwa katika miaka ijayo. Kwa upande mwingine, kila nikiifikiria hali hiyo, kuna neno moja ambalo hunitwanga na huhisi kuwa hili ndilo, kwamba  hatimaye kisu kimepata mfupa.  Kwa bahati mbaya neno lenyewe ni la Kiingereza.

“Dystopia” ni neno ambalo ni kinyume cha neno jengine la Kiingereza,  “utopia”, lenye maana ya jamii timilifu ya kufikirika. Mtaalamu mmoja wa Kiswahili amenambia kuwa maneno yote hayo mawili hayawezi kufasiriwa kwa tamko moja la Kiswahili.

Ameshauri kwamba badala ya kulitafuta neno moja moja la kulifasiria “dystopia” au “utopia”,  ingekuwa jambo la maana zaidi pangetafutwa mjumuiko wa maneno kulielezea kila moja ya maneno hayo mawili. Alivyosema ni kwamba maneno yote hayo mawili yana ukaidi wa kukataa kufasiriwa kwa neno moja tu pekee. Kwa hivyo, kila moja ya maneno hayo mawili yanahitaji kufasiriwa kwa kishazi cha maneno.

“Dystopia” basi ni jamii ya misukosuko, maafa, maudhi, uchakavu na maradhi.  Huwa ni jamii yenye kutawaliwa kimabavu ambapo mambo yote huwa yanakirihisha.  Hali za maisha huwa ni duni kupita kiasi.

Na Ahmed Rajab

Mazingira ya jamii kama hiyo ni mazingira ya kudhalilisha.  Tunaweza kusema, kwa muhtasari, kwamba kuishi katika “dystopia” ni kuishi katika ulimwengu wa machungu.

Ulimwengu huo wa “dystopia” ni mahala pa kufikirika ambapo watu huwa hawana furaha. Pamoja na kukosa furaha, watu hao aghalabu huwa woga, kwa sababu huwa wanakabiliwa na vitisho vya watawala na wakati huohuo huwa hawatendewi haki.

Kwa kawaida neno hilo hutumika kuelezea riwaya ya kufikirika kuhusu jamii ya miaka mingi ijayo yenye sifa hizo za machungu niliyoyataja.  Lakini nadhani kwa jinsi mambo yalivyo sasa Zanzibar na yanavyoelekea kuwa Tanzania nzima, tunaweza tukalitumia kuielezea Tanzania ya leo.  Tofauti ya riwaya ya “dystopia” na hii “dystopia” iliyo nayo Tanzania ni kwamba hii ya Tanzania ni halisi na taifa linaishi nayo.

Hebu tuiangalie Zanzibar, kwa mfano.  Vitu vyake vingi ni vibovu, vimechakaa. Toka majengo yake ya Mji Mkongwe hata fikira.  Labda ni jina lake tu ambalo limebaki linavutia. Na isipotahadhari miaka isiyo mingi ijayo hata hilo jina lake huenda nalo likaharibika na kugeuka likawa na maana ya makuruhu.

Jambo la kutia moyo ni kwamba wakaazi wake, ingawa wa hoi, bado hawakuchoka kuwa wabunifu wa mbinu za aina kwa aina zinazowapa uwezo wa kuendelea kuishi.

Hali hiyo imefurutu ada Zanzibar ambako wakaazi wake wameizoea. Kinachozidi kuhuzunisha ni kuiona hali kama hiyo siku hizi ikianza kuibuka na kuigubika Tanzania nzima.

Katika Tanzania ya leo, Watanzania wengi wanaishi  hivyohivyo tu. Wanaishi kama hawaishi.  Wanaishi kimasikini katika nchi yenye utajiri mwingi, utajiri ambao wanaufaidi wachache tu katika jamii.

Tanzania, kwa hakika, si nchi inayostahili kuitwa nchi masikini au kujiendea kimasikini.  Nchi si masikini lakini watu wake ni masikini kwa sababu ya maswaibu yasiyokwisha yanayowakuta kila uchao.

Kama hawakumbani na ukali wa watawala na vitisho vyao, basi hukumbana na ukali wa maisha usiowaonea huruma. Ulimwengu wao umekuwa ni ulimwengu wa vitisho vya kila aina.

Katika mazingira kama hayo mtu hukaribia kukufuru kwa sababu huuona ulimwengu kuwa kama hauna tena maana kwa sababu hawakioni cha maana.

Watanzania wanafaa washukuru kwamba miongoni mwa wanasiasa wao wamo wenye kufikiri, wamo waliouweka mbele uzalendo badala ya maslahi yao binafsi.  Wanasiasa aina hiyo wanapatikana hata ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), chama kinachotawala.  Wanakosea wenye kudhania kuwa CCM ni chama chenye kufuga wakorofi tu.

Hivi karibuni akizungumza bungeni, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, aliielezea Tanzania nzima kuwa ni nchi yenye watu wasio na furaha. Neno “dystopia” linaisibu hali hiyo aliyoielezea Bashe.

Bashe, ambaye ni mbunge wa CCM, alisema kuwa Tanzania, kwa mujibu wa takwimu za dunia zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, ni moja kati ya nchi 20 za mwisho ambazo raia wake hawana furaha.  Aliendelea kukumbusha kwamba jambo la msingi linalowafanya raia wasiwe na furaha ni kunyimwa haki zao.

“Haki za raia kuheshimiwa ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa nchi unazidi kushamiri,” alisema Bashe.  Hili ni suala muhimu sana ambalo mara nyingi inaonesha watawala ama wanalisahau au wanalipuuza kwa kusudi.

Wao huwa wepesi wa kuzikanyaga, kuzifinyafinya na kuzifikicha haki za kiraia kana kwamba hazina maana.  Hujifanya kuwa hawajui ya kwamba kuheshimiwa kwa haki za kiraia na za kiuchumi ni jambo la msingi katika jamii yoyote iliyoazimia kuwa na maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hakuna taifa linaloweza kustawi bila ya kuhakikisha kwamba wananchi na wakaazi wake wanazo, kwa ukamilifu, haki zao za kiraia na wanao uhuru usiominyika wa kuzitumia haki hizo.  Moja ya haki hizo ni haki ya watoto kupatiwa elimu katika skuli za serikali.

Kila mtoto anahitaji elimu. Kila taifa linahitaji watoto wake waelimishwe na hujitwika lenyewe, kupitia serikali yake, dhima ya kuwaelimisha watoto wake.  Taifa hufanya hivyo kwa sababu linatambua kwamba watoto wake ndio rasilmali yake, ndio fahari yake.

Mwishoni mwa Januari, zilitangazwa shule kumi za sekondari zilizo bora na kumi za mwisho Tanzania.  Ilishtusha kuona kwamba Zanzibar ilikuwa na nyingi ya shule za mwisho kitaifa.

Ikiwa ni sahihi viwango vyenyewe vya elimu ni hivyo, kweli Zanzibar itaweza kuendelea? Ilipotolewa orodha hiyo kila mtu serikalini huko Zanzibar alikauka. Hakuna aliyesema kitu. Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wale wenye kusimamia sekta ya elimu Zanzibar.

Katika nchi zenye kuuenzi uwajibikaji wa wenye madaraka waziri kama hajiwajibishi mwenyewe na akajiuzulu basi huwajibishwa kwa kutimuliwa kazini. Kama si hivyo basi angalau yeye, katibu mkuu wa wizara pamoja na wakurugenzi hutakiwa wajieleze.  Wengine wanaoweza kuingizwa katika kaumu hiyo ni wakuu wa skuli zilizoiaibisha nchi.

Hayo hayafanyiki Zanzibar.  Mambo huenda kombo na viongozi wanang’ang’ania madaraka utadhani hapajatokea kitu. Matokeo yake ni kwamba leo Zanzibar haina lake jambo isipokuwa kujinata na iliyokuwa nayo katika zama zilizopita.

Wakati ilipopata uhuru 1963 Zanzibar ilikuwa imezipita takriban nchi nyingi za Afrika ya Mashariki na ya Kati kwa viwango vyake vya elimu. Ukilinganisha idadi ya wakaazi wake wa wakati huo na idadi ya wahitimu wake wa vyuo vikuu, Zanzibar ilikuwa iko mbele sana.

Kumbukumbu hizo za adhama na fahari zake za kale haziifaidi kitu Zanzibar ya leo, ila labda kutukumbusha tu kwamba Wazanzibari si “mabumla” nikitumia tamko la mitaani.

Wanachokosa vijana wa leo Wakizanzibari ni fursa. Kinachowachongea waikose fursa hiyo ni utawala mbovu uliojikita juu ya maovu kadhaa yakiwa pamoja na udhalimu, ubaguzi na upendeleo, na uendeshaji mbovu wa serikali.

Wanatawaliwa na watawala wenye maradhi ambayo tangu 1964 hadi sasa yanaonesha kuwa ni sugu.  Kila Januari 12 kuanzia 1965, mwaka mmoja baada ya Mapinduzi na miezi kama saba baada ya kuundwa Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa ahadi kwa wananchi na kila mwaka imekuwa ikizivunja ahadi hizo.

Tunayaona hayo wazi tukiviangalia viwango vya afya, elimu na vigezo vingine vya maendeleo.  Vigezo hivyo vimekuwa vikididimia mwaka nenda mwaka rudi.

Kuna mtafaruku na kizaazaa nchini kwa sababu watawala wameshindwa kuongoza. Matokeo yake ni kuzuka kwa mambo ya ajabuajabu tunayoyashuhudia. Kwa ufupi, jamii, kwa jumla, imeumizwa kisaikolojia. Watu wanaishi katika matumaini yenye uzito wa mapovu.

Tatizo kubwa walilo nalo Watanzania ni kutotambua kuwa katika “dystopia” yao wanaishi katika ulimwengu wa viini macho. Kwa hivyo, masimulizi yao ya historia au uchambuzi wao wa matukio ya kihistoria nchini Tanzania unahitaji nahau au sarufi mpya. Watanzania wanahitaji wawe na mizungu mipya ya kuweza kujitambua katika “dystopia” yao.

Watawala wamechoka. Sera zao nazo zimechakaa. Ndio maana unawaona watawala wao wakitawala kwa kupiga kelele, kwa kusema kwa vishindo au kuzungumza kwa ukali. Wanavyofikiri ni kuwa kutawala ni kutisha. Wanawatisha watu na kulifanya taifa liwe linatetemeka au liwe linajichafulia suruali kila wanapofungua mdomo kuzungumza.

 

Tanbihi: Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 8 Machi 2017. Mwandishi anapatikana kwa anwani ya barua pepe: ahmed@ahmedrajab.com

 

One thought on “‘Dystopia’ na machungu ya viongozi wakali”

  1. Bwana Ahmed Rajab makala yako inaakisi hali halisi ya nchi yetu hasa kwa upande wa Zanzibar.Raia tumekuwa wengi wamekuwa na ugonjwa wa kisaikolojia unaotokana na matendo ya vitisho vya watawala.Sasa imekuwa watu wanahisi bora waishi katika dhiki na unyonge ilimradi tu wapate salama ya nafsi zao. Ni wachache sana wenye ujasiri wa kulisemea ovu la watawala na wao huonekana binaadamu wa ajabu pale wanapotumia ujasiri huo kulinda haki zao dhidi ya watawala.

    Panahitajika mabadliko na mahubiri ya nguvu kuwatoa watu katika hii uliyoiitwa “dystopia na kuwaelewesha kuwa hali hii haiwezi kudumu na inaweza kuondoka ikiwa fikrazetu zitabadilika na kuanza fikra mpya za kupigania haki zetu bila ya woga

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.