Wanasharia na watetezi wa haki za binaadamu wanatuambia kuwa haki ina misingi yake mikuu, ambayo inapaswa kuhishimiwa ili haki hiyo iitwe kweli ni haki. Mmojawapo ni ukweli kuwa haki na ubinaadamu havitenganishiki.

Maana yake ni kuwa viwili hivi ni sawa na kitu kimoja, na ndio maana kinapoondoshwa kimoja, huwa kimeondoshwa chengine. Inapovunjwa haki fulani ya kibinaadamu, kwa hivyo, ni sawa sawa na kuvunjwa kwa ubinaadamu wa binaadamu huyo.

Msingi huu wa haki unaakisi utukufu wa hali ya juu wa uhai wa binaadamu. Kwamba kila mwanaadamu amezaliwa akiwa na haki ya kuishi kwa usalama, na uhai huo haupaswi kuondolewa, kuharibiwa au kuhatarishwa kwa namna yoyote ile.

Hata hivyo, kuna mazingira ambayo, kwa mujibu wa sharia, mamlaka zilizowekwa kisharia hupewa nguvu za “kuinyang’anya” haki fulani kwa masharti maalum, ambayo pia yameweka na hizo hizo sharia. Ni masharti hayo ndiyo yanayotandika misingi mingine ya kulifanya jengo la haki liitwe kweli haki.

Sharti mojawapo ni kwamba, hata pale inapotokezea mwanaadamu huyo ametuhumiwa kutenda makosa, bado ana hadhi yake ya ubinaadamu kama alivyo mwengine mbele ya sharia na, hivyo, lazima kwanza apewe nafasi ya kusikilizwa na kujitetea, ambapo ndani ya kipindi chote hicho anabakia hana hatia hadi pale mahakama itakapomtia hatiani.

Ndani ya kipindi hicho, ambacho nacho kimewekewa masharti mengine kadhaa ili kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anabakia kuwa mtuhumiwa tu na sio mhalifu na kwamba ubinaadamu wake unadumishwa na sio kudunishwa, sharia inamlazimisha aliyemtuhumu mwanaadamu huyu kuthibitisha tuhuma zake mbele ya mahakama, na sio mtuhumiwa “kujithibitishia” makosa anayotuhumiwa nayo.

Sharti jengine ni kuwa haki lazima itendeke na, kwa hakika, sio tu itendeke, “bali ionekane kuwa imetendeka” ili hasa iweze kuitwa haki. Watetezi wa haki za binaadamu hupenda kutumia msemo wa Kilatini “Fiat justitia ruat cælum” unaomaanisha kuwa “Wacha haki itendeke hata kama mbingu zitaanguka” kusisitiza umuhimu wa sharti hili, ambalo nalo linalazimisha kuwa haki inatakiwa itendeke kwa uharaka na umakini mkubwa, maana kwa msemo wao mwengine ni kuwa “haki inayocheleweshwa huwa ni haki iliyonyimwa!”

Kwa mujibu wa sharia zetu, misingi na masharti haya ya utendaji haki yamekabidhiwa taasisi maalum ambazo zinagharimikiwa kisheria na fedha za walipa kodi – polisi, ofisi za mwendesha mashitaka, ofisi za mawakili, mahakama. Waliomo kwenye taasisi hizi wanabeba jukumu la kuhakikisha misingi na masharti haya ya haki yanadumishwa na sio kudhalilishwa, sharia inatukuzwa na sio kupuuzwa.

Hata hivyo, utendaji kazi wa taasisi hizi unathibitisha kinyume chake katika mifano kadhaa ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mbele yetu pana mifano miwili ya karibuni na hai zaidi inayoonesha namna ambavyo taasisi hizi zinakwenda kusiko panapohusika haki za kibinaadamu za raia. Mmoja ni kadhia ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, na mwengine ni wa viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu na Uamsho visiwani Zanzibar (maarufu kama Uamsho).

Ambapo imechukuwa miezi minne kwa taasisi hizo kudumisha msingi mmoja wa haki ya Lema, yaani “kutokuhisabiwa mkosa hadi hapo mahakama itakapomtia hatiani”, sasa unaingia mwaka wa nne na bado taasisi hizo hizo hazijadumisha msingi huo huo kwa Uamsho, ambao bado wameendelea kuswekwa gerezani hadi makala hii inaandikwa.

Kinachothibitika kwenye kadhia hizi mbili kitu ni kimoja tu – “kunajisiwa kwa tasnia ya haki na sharia” – kwa kutumia kauli ya Jaji Benard Luanda wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania alipokuwa akitoa uamuzi wa kutupilia mbali hoja za upande wa mashitaka kwenye zuio la dhamana dhidi ya Lema: “Taaluma hii (sheria) na ofisi ya DPP (mwendesha mashitaka mkuu wa serikali) mnaitia najisi. Kitu kiko wazi, ila mnafanya kitu cha ajabu, hakipendezi. Kwani mnafanya wanasheria wote tuonekane hatuna akili, mtu ashikiliwe kwa misingi ya sheria. Tumepitia jalada, tunashangaa hivi ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina wanasheria? Kwa nini huyu mtu yuko ndani mpaka leo?”

Najisi hii ambayo inaidhalilisha taaluma ya sharia ina sababu zake kadhaa, lakini kwa mantiki ya makala hii tutazungumzia moja tu, nayo ni “usiasishwaji” wa mfumo wa kusimamia haki ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kadhia zote mbili tunazozingumzia hapa, si jinai iliyopelekwa mbele ya kizimba cha mashitaka, bali ni siasa. Siasa tupu, siasa potofu na siasa mbaya. Siasa ndiyo inayoshitaki na siasa ndiyo inayoshitakiwa, na siasa ndiyo inayotumika kuzuia sharia kuchukuwa mkondo wake, maana mwenye nguvu za maamuzi kwenye siasa hiyo yupo upande wa mshitaki na mnyonge kwenye siasa hizo amesimama upande wa mshitakiwa.

Siasa za Lema za ukosowaji dhidi ya baadhi yale yanayofanywa na utawala ulioko madarakani ndio chimbuko la kesi dhidi yake, kama kwamba kupinga yanayofanywa na utawala ni kosa la jinai. Kumuweka mtu miezi minne gerezani kwa kuwa amesema ameota ndoto inayobashiri kutokea kwa jambo baya ni siasa tupu na siasa potofu.

Lakini wakati Lema amekaa ndani kwa zaidi ya siku 100, Uamsho wako gerezani kwa zaidi ya siku 1,000. Na kwao pia, iliyoko gerezani ni sias, siasa tupu na siasa chafu. Unajuwa kuwa ni siasa, pale unapowasikia viongozi wakuu kwenye serikali ya Zanzibar wakizungumzia kadhia hii kibabe na kwa kiburi kwamba wamewapeleka Uamsho “wakanyelee ndooni katika magereza ya Bara kwa jinai yao.”

Na ipi jinai iliyotendwa na Uamsho? Ni ile ile “jinai” waliyonayo maelfu kwa maelfu ya Wazanzibari wengine, ambayo ni kuamini kuwa mfumo wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar si wa kiadilifu, si sahihi na unapaswa kufanyiwa marakibisho makubwa ili kuipa Zanzibar hadhi inayostahiki kama mshirika mmojawapo mkuu kwenye Muungano huu, na sio kuwa kama mgeni mwalikwa au, baya zaidi, kuwa kama “koloni la Tanganyika!”

Mwengine angeliweza kuhoji kuwa kama ni “jinai ya siasa za Muungano” iliyo Segerea na ikiwa ni kweli jinai hiyo ndiyo waliyonayo maelfu kwa maelfu ya Wazanzibari wengine, ni kwa nini basi Wazanzibari wote hao hawako gerezani hivi sasa na wapo Uamsho pekee?

Majibu yake ni mawili: kwanza, hawa ndio ambao wamethubutu kutamka waziwazi hadharani na kupata ufuasi mkubwa kupitia matamko hayo, na sasa wanatiwa adabu ili iwe ni funzo kwa wengine walioko nje, kwamba “adhabu ya kuukosoa mfumo huu wa Muungano ni kunyelea ndooni!”

Pili, historia inaonesha kuwa wakati viongozi wa kupigania ukombozi barani Afrika wakifungwa jela kwa kuzikosowa tawala za kikoloni, kulikuwa pia na maelfu kwa maelfu ya Waafrika nje ya kuta nne za magereza, lakini nao walikuwa wamefungwa kisaikolojia kama walivyofungwa viongozi wao kimwili na kiakili.

Kwa hivyo, Uamsho wanabeba mateso yote wanayobeba na familia zao huku nje zinachukuwa machungu yote zinazoyachukuwa, kwa sababu ya “kufundishwa” wengine. Maelfu kwa maelfu ya Wazanzibari wana jinai kama ya Uamsho na wao, kisaikolojia, wako Segerea wakiteseka mateso ambayo Uamsho wanayapata kimwili na kiakili. Mfumo wa haki, kwa hakika, “umesiasishwa!”

Sasa ni upi mwelekeo wangu kwenye hili? Kwanza, kama ilivyotangulia kuelezwa hapo juu kwenye misingi na masharti ya haki, haki lazima itendeke na ionekane kuwa imetedeka. Haki haikutendeka kwa Lema, hata kama ameachiwa kwa dhamana, na haki haijatendeka hadi leo kwa Uamsho, ambao wanaendelea “kuozeana” gerezani.

Hata kama tuhuma dhidi yao zingelikuwa na mashiko (ingawa hazina na ndio maana mwenye kutuhumu ameshindwa kujenga angalau msingi wa awali wa tuhuma zake hadi leo), basi bado wangelibakia kuwa watuhumiwa hadi pale mahakama itakapowatia hatiani. Muakisiko wa sauti za watawala kuhusiana na kadhia yao ni kuwa tayari hawa wana hatia ya kisiasa na hivyo chochote wanachotendewa, wanatendewa kwa kuwa ni wakosa kwa siasa hiyo ya watawala. Hili si sahihi hata kidogo.

Pili, saa moja ya kuchukuliwa haki ya kuwa huru ni nyingi sana, sembuse siku 100 za Lema au 1,000 za Uamsho. Dola ambayo inachukulia kuwa na maoni tafauti nayo kuhusu jambo fulani ni jinai, haiwezi kuwa dola ambayo inatambuwa wajibu wake kwenye ulinzi wa misingi ya haki. Uamsho wameshateseka sana, wameshaumizwa sana. Wameshaonewa sana. Dola inapaswa kuacha siasa zake kwenye haki za raia wake.

Badala ya kujificha nyuma ya sharia za makosa ya jinai “kuihalifisha” misimamo ya kisiasa isiyoipenda, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ina njia rahisi zaidi ya kupita kuliko hii ya kuitia najisi taaluma ya sharia. CCM, yenye siasa ya serikali mbili kimaneno na moja kivitendo, inao wingi wa kutosha bungeni kuweza kutunga sharia ambayo inatamka wazi kuwa ni kosa la jinai kwa raia yoyote kuikosoa siasa hiyo na ikaweka adhabu inayotaka yenyewe kwa anayethibitika kutenda kosa hilo. Lakini kabla ya kufanya hivyo, itende haki kwa Uamsho.

Tatu, na mwisho, ni kwa mahakama na wanasheria wetu. Ikiwa tangu awali mulishaona kuwa serikali inatumia siasa kwenye kesi ya Lema na hivyo kuinajisi taaluma yenu munayopenda kuiita tukufu, kwa nini mukae kimya kiasi hiki na muache miezi minne ipite ndipo muzinduke kuwa taaluma yenu inanajisiwa, kama ulivyokuwa uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kwa kesi ya Lema?

Wenzenu madaktari katika taaluma yao, huwa hawasubiri kuitwa panapotokea dharura ya kuokoa maisha ya watu. Huingia kuokoa uhai kuwa kuwa huo ndio wajibu wao. Sisi kwenye taaluma ya habari huwa pia hatusubiri kuitwa panapotokezea dharura inayohatarisha ustawi wa jamii yetu, maana tuna wajibu wa kijamii wa kuripoti na kusambaza habari kuhusu dharura hiyo.

Nanyi, muliovishwa majoho ya uanasheria, hamupaswi kusubiri kuitwa munapoona haki za raia zinavunjwa. Ni wajibu wenu kuokoa haki hizo. Munajuwa kuwa kama lilivyokuwa la Lema, la Uamsho pia ni najisi mbaya zaidi ya kisiasa dhidi ya taaluma yenu. Munajuwa pia kuwa siasa huwa zinabadilika, ila haki za binaadamu zipo pale pale, nanyi muna wajibu wa kuipigania haki itendeke na ionekane kweli imetendeka, tena bila kucheleweshwa, hata kama mbingu na ardhi zitatikisika.

Tanbihi: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 7 Februari 2017.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.