Tundu Lissu
Tundu Lissu

Mutakuwa mumesoma hapa na pale maelezo ya kilichotokea Mahkama ya Kisutu Jana (14 Februari 2016), wakati kesi ya jinai Na. 208/2016 ilipoanza kutolewa ushahidi. Upande wa Mashtaka (Jamhuri) ulimleta shahidi wa kwanza, anaitwa SALUM MOHAMED HAMDUNI, ambaye ni Assistant Commissioner of Police (ACP) mwenye wadhifa wa RPC Mkoa wa kipolisi wa Ilala. Wakati wanaanzisha kesi, Salum alikuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi wa Jinai Kanda Maalum – Asst CID Zonal, Dar es Salaam.

Washitakiwa katika kesi hii ni (1) JABIR IDRISSA YUNUS (mm), niliyeandika habari, (2) SIMON MKINA, Mhariri wa MAWIO, (3) ISMAIL MEHBOOB, mfanyakazi wa Jamana Printing Plant, na (4) TUNDU LISSU, aliyenukuliwa maelezo yake ktk stori iliyochapishwa Toleo Na. 182 la Jan 14-20, 2016, chini ya kichwa cha maneno “MACHAFUKO YAJA Z’BAR.”

Na Jabir Idrissa
Na Jabir Idrissa

Maudhui ya habari kwa mtizamo wangu ni kutoa tahadhari kwamba mgogoro usiposhughulikiwa unaweza kuzaa machafuko. Lissu amemshauri Rais Magufuli aingilie kati kuchukua hatua za kuondoa mgogoro ili kuepusha machafuko Zanzibar.  Maelezo ya Lissu ambayo kwa kweli ni maoni yake (na mnajua kila raia wa Jamhuri ana haki ya kutoa maoni kulingana na Ibara 18 ya Katiba ya Muungano ya 1977), kwamba kufutwa kwa uchaguzi tarehe 28 October 2015 na Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ni haramu kisheria na panahitajika Rais kuchukua hatua kuepusha machafuko. Na huyu ni rais ambaye mwenyewe aliliambia bunge atashughulikia mgogoro huo akisaidiana na makamu wake, Bi Samia.

Sasa, mmesoma kuwa kesi imekwama. Ilitarajiwa kupatiwa uamuzi leo. Haikuwa kwa sababu Mhe. THOMAS SIMBA, hakimu anayeisikiliza, ametuambia hakukamilisha kuandika uamuzi mdogo kuhusu ubishi wa kisheria uliotokea. Baada ya mashauriano, imeteuliwa tarehe 23 Februari kutoa uamuzi.

Hivi ni nini hasa kilichokwamisha kesi? Ndio swali muhimu hapa. Kulijibu ni muhimu kwanza nieleze moja ya mashtaka MATANO yanayotukabili kuhusu kesi hii. Shitaka la Pili ni kuchapisha habari zilizolenga kuchochea wananchi wa Zanzibar kuleta chuki dhidi ya MAMLAKA HALALI ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Hapa panahusu kile ambacho Jamhuri inakiita “mamlaka halali ya SMZ” na hivyo basi,  kwa maoni yangu, katika kulidhoofisha shitaka hili ili tusipatwe na hatia, tuna wajibu wa kupigania ionekane kuwa hiyo wanayoita mamlaka halali si halali kwa vile iliingia kupitia kufutwa kwa uchaguzi halali wa 25 Oktoba 2015, na kuitishwa alichoita “Uchaguzi wa Marudio” tarehe 20 Machi 2016. Kupigania hapa tunajenga utetezi tusionekane na kosa. Na hiyo ndio haki yetu washitakiwa KUJITETEA tusifungwe.

Jamhuri imegoma. Haitaki Lissu ambaye ameruhusiwa na Mahkama kujiongoza mwenyewe kama wakili, akiuliza swali linalohusu kama mamlaka ya SMZ ni halali au si halali. Swali husika hasa lililozua mabishano ni: “Ieleze mahkama maoni yako, eleza opinion yako wewe shahidi ambaye unajua Katiba ya Zanzibar na unajua kama uchaguzi ulifutwa… huu uchaguzi wa Zanzibar ambao umeshaieleza mahkama kuwa ni uchaguzi wa wananchi sio uchaguzi wa serikali, kuhusu  kufutwa kwa uchaguzi huu wa wananchi wa Zanzibar, unavyoona ni halali?”

Ni hapo Wakili wa Serikali, PAUL KADUSHI aliingilia na kutaka SHAHIDI asijibu swali hilo. Akaibua hoja za kisheria. Zikajibiwa. Wakili wa utetezi Kibatala akaeleza si sahihi shahidi kuzuiwa kujibu swali, ni swali la msingi. Wakili 2 wa Utetezi, MTOBESYA, akaeleza swali lijibiwe ni la msingi. Lissu akaeleza kuwa swali hilo linahusika hasa kwa sbb SHITAKA 2 linasema washitakiwa wamechochea wananchi wa Zanzibar kujenga chuki dhidi ya MAMLAKA HALALI ya SMZ. Hili ni shitaka wamelileta wenyewe hapa mahakamani, tuna haki ya kujitetea kusema hakuna mamlaka halali. Swali lijibiwe mheshimiwa Hakimu. Akatoa vifungu vya sheria kutoka CPA (Criminal Procedure Act, sheria ya mwendo wa jinai).

Na ikumbukwe wakati swali hilo linaulizwa, tayari SHAHIDI alishaulizwa na kujibu maswali: “Unajua Katiba ya Zanzibar, unajua ipo sheria ya uchaguzi ya Zanzibar; unajua Zbar walifanya uchaguzi 25 Okt 2015; ni sahihi nikisema uchaguzi huu ulifanywa kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar; unajua ni kweli uchaguzi ulifutwa, na ulifutwa na Jecha wa Tume ya Uchaguzi; sasa ikumbushe mahakama, hivi ulisema uchaguzi ni mali ya wananchi, sawa si sawa? Kwa hivyo uchaguzi wa wananchi ulifutwa sawasawa?” Ndipo likaja swali hilo ambalo wakili wa Serikali amemkatalia shahidi kujibu.

Maoni yangu ni kuwa hofu ya Serikali ni kwamba jibu linaweza kuwa ufunguo wa kuieleza mahakama pia iende mbali kutamka kuwa mamlaka ya SMZ si halali kwa sbb haikupatikana kwa uchaguzi wa wananchi, ule si ulifutwa? Na itabidi paletwe maelezo na Jamhuri kuthibitisha mamlaka ni halali, wataleta maelezo yepi wakati Jecha hakuwa na hana mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi?

Tukifika hapo unaweza kuona hali ya nchi itakuaje. Wanaogopa kufika hapa, kwa hivyo wafanyeje? Wamtie hakimu kwenye mtihani. Atajibu vipi siku ya kutoa uamuzi mdogo khs mkwamo huu? Lakini wamesahau, pengine kwa makusudi, kwamba ni hakimu huyohuyo, baada ya Wakili wa Serikali kujenga hoja kuwa mahkama hiyo ina uwezo wa kusikiliza masuala yanayohusu mamlaka ya serikali Zanzibar na kwamba hata haya ya uchaguzi yanajadilika.

Uamuzi mdogo wa suala hili tunausubiri kwa hamu kubwa.

TANBIHI: Mwandishi wa waraka huu ni Jabir Idrissa, ambaye ni mmoja wa washitakiwa kwenye kesi hii.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.