makonda-miti8-961x1024
Ghafla polisi wamevamia kwa mama muuza gongo wakiwa na mabunduki yao. Kufumba na kufumbuwa, risasi zikafyatuliwa hewani. “Wote kaa chini, mukikimbia nitauwa mtu!” Anapaza sauti mmoja wa maaskari ambaye mikononi mwake ameidhibiti barabara bunduki yake aina ya SMG.

Kishindo hichi kinanifanya nisimame si kwa woga, bali kuutazama mchezo wa kisanii na kitoto ambao ulikuwa ukiigizwa na watu wazima waliokuwa wamevalia magwanda ya polisi na wengine wakiwa na mavazi ya kawaida. Nabaki kujiuliza masuali kadhaa ambayo jibu sipati hadi leo hii ambapo ni wiki mbili sasa zimeshapita.
Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Inakuwaje kufyatuwa risasi ya gharama kubwa kwa wanywa gongo ambayo thamani yake haikaribii hata theluthi ya gharama ya risasi moja? Inakuwaje kufyatuwa risasi kwa watu ambao wamelewa chakari na wasio na hata uwezo wa kutembea seuze kukimbia? Inakuwaje kufyatuwa risasi kwenye makaazi dhaifu yaliyojaa vitoto viachiwavyo kuzurura bila mpangilio? Nini kubwa na muhimu la kufyatuwa risasi – jambazi, ugomvi wa watu wenye kushikiana silaha au kitisho kwa lengo la kupewa rushwa kubwa? Jibu sina!

Utaniuliza: je, nawe mwandishi unatetea wanywa gongo? Hapana. Siwatetei walevi wa aina yoyote ile, lakini kwenye mkasa huu nilioushuhudia kwa macho yangu, niliwaona wale maaskari wakitoka ndani ya banda wakiwa na “mateka” kadhaa ambao wamechoka kwa ulevi wa kupindukia wa pombe kali. Sura zao zilijaa mashaka na ishara ya watu waliokwishapoteza matumaini ya maisha. Miongoni mwao ni vijana, lakini kutokana na dhiki za maisha zilizowazonga, wanaonekana kama vizee vya miaka 60 au 70.
Wahalifu walala kitanda kimoja na polisi
Kitu kimoja kilizidi kuniacha hoi. Ni ile hali ya polisi hawa kuanza kurushiana maneno na mama muuza gongo ambaye alisimama kidete kutetea wateja wake. Hata hivyo, kelele zake hazikufuwa dafu na safari ya wateja wake kupelekwa kituoni iliendelea bila mjadala na huku mtaa mzima ukiwa umeshikwa na fadhaa kutokana na nguvu kubwa iliyotumika kuingia eneo lile maarufu kwa uuzwaji na unywaji wa pombe za kienyeji!
Muda mfupi, mama akatoka ndani akiwa na simu yake sikioni huku akiongea na mtu ambaye ni dhahiri kwamba alikuwa ni polisi mwenye cheo na mwenye kula kupitia biashara hii haramu ifanywayo na mama huyu.
“Mkuu mbona vijana wako wananisumbuwa wakati jana tu nimekuletea mzigo wako? Wamevamia ofisini kwangu na mabunduki hadi mtaa mzima umetaharuki na wameondoka na wateja wangu sita. Kwa nini lakini munatufanyia ivi wakati pesa nimeshaleta mkuu!?” Mama muuza gongo alikuwa anazungumza kwa kujiamini. Kufikia nukta hii, nikawa nimebaki mdomo wazi huku nikitafakari namna maisha yetu yalivyozungukwa na uoza mbaya kwenye vyombo muhimu vya kidola.
Lakini dakika chache baadaye nikawaona vijana wale waliochukuliwa chini ya mtutu wa bunduki wanarejea kwa furaha kana kwamba walikuwa kwenye maigizo na si kitu halisia. Mmoja wao akasimama mahali kununuwa samaki wa kukaanga huku akisimulia kilichotokea huko mbele ya safari. “Yule afande wenzake juzi walikuja  na mama akawarushia elfu thelathini kwa Tigo Pesa. Lakini kumbe wenzake wamemuacha kwenye mataa hawakumpa na ndio leo kaja kututingisha tena. Lakini mama kashamtuliza hata kituoni hatukufika. Wametuzururisha tu kisha tulipofika pale Kidarajani wametuachia!”
Hadi hapo kuna nini!? Hizi ndio taasisi zetu za usalama wetu! Ukiambiwa jela kuna watu wamefungwa bila hatia, usibishe kwani hilo ni rahisi sana kwa mnyonge asiye na kitu cha kuhonga wenye kufanya maamuzi!
La Makonda na makandokando yake
Wiki hii imeisha kwa tukio moja kubwa ambalo limewavutia wengi. Ni tukio kutajwa hadharani wanaodaiwa kujihusisha na biashara hatari ya dawa zakulevya. Ni tukio la kihistoria ingawa lina ishara za mashaka ndani yake na hapa nitaeleza kidogo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ndiye aliyeongoza mkutano wa kuwataja watu hao ambao miongoni mwao wamo wasanii na viongozi mashuhuri akiapa kupambana nao hata kwa gharama ya maisha yake.
Kwanza, lazima nitambuwe kwamba uamuzi wa Makonda ni mzito na usiostahili kupuuzwa na kila mwenye mapenzi na taifa letu. Ni uamuzi mzito ambao kwenye dhamira ya kweli utasaidia sana kupunguza maangamizi dhidi ya nguvukazi ya Tanzania ambayo imekuwa ikiuliwa kila uchao na biashara hii chafu.
Sio siri kwamba hali, hasa kwenye majiji makubwa, imefikia kiwango kibaya kwa vijana wengi kutumia dawa za kulevya kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, suala ambalo linaiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi hatari, na sababu ni kukosekana mipango madhubuti ya udhibiti wa dawa hizo. Hivyo, anapojitokeza kiongozi mwenye uthubutu kama wa Makonda, hapaswi kurejeshwa nyuma!
Hata hivyo, uamuzi wa mkuu huyu wa mkoa kijana mwenzetu unaacha masuali mengi zaidi kuliko majibu. Kwamba kama taifa, ipo misingi na taratibu za kumkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria kwa kila mmoja ambaye atajihusisha na mambo yaliyo kinyume chake. Kwamba sheria inatutaka kufikisha mahakamani wahalifu. Lakini sheria hio haitowi mwanya kwa mtu kumtia mwengine hatiani kwa njia za kihisia, bali vidhibiti halisi ambavyo ndiyo njia pekee ya kuthibitisha hisia zetu.
 
Katika waliotajwa kwenye orodha yake, wapo ambao wametii na kufika kituo kikuu cha polisi huku mamia ya Watanzania wakishuhudia jambo hilo. Lakini si kila mmoja anaamini kwamba Watanzania wana shida ya kuona watajwa wakifika kituoni, bali kubwa na muhimu kwao ni kuona ushahidi wa kile ambacho watu hao wameelezwa kujihusisha nacho.
Nalisema hili kwa vile siamini kwamba chombo chenye mamlaka ya kusimamia haki yaani mahkama kwamba kitafanya kazi yake pasipo na uthibitisho wa kile ambacho Makonda anapambana nacho. Siamini kwamba watu hawa watapelekwa jela kwa vile Makonda kawatuhumu. Pia siamini kwamba mapambano haya yatakuwa na mafanikio kwa njia hizi, bali ninachokiona mbeleni ni Makonda kuingia kwenye utata wa kisheria ambao utakuja kuligharimu taifa fedha nyingi za fidia iwapo watu hawa mashuhuri wakiamuwa kutunishiana naye misuli.
 
Vizuri tuelewe kwamba mbele ya sheria watu wote ni sawa. Pamoja na cheo kikubwa alichonacho Makonda, haikuwa sahihi kuwataja watu alio na mashaka nao mbele ya vyombo vya habari. Kufanya hivi ni kuchafuwa jina la mtu ambapo iwapo akiamuwa kuipigania haki yake mahkamani, hautokuwepo uchochoro wa kutokea, vyenginevyo mahkama isimame kama mkono wa tawi la utawala na sio tawi la kugawa haki.
Hakupaswa kuweka wazi majina yao, kwani kufanya vile kumepelekea kuporomosha hadhi za watu hao na hilo si jambo lisilokubalika. Hili linaweza kufanyika sasa kwa njia za mashinikizo lakini kutokana na kutokuwa kwake na vithibitisho vya kisayansi, vinaweza kuja kuwa jinamizi baya kwa Makonda miaka mingi mbeleni, kwani mifano ya hili ipo duniani kote na hapa ndio chanzo cha kusisitizwa utawala wa sheria. Kwamba hatupaswi kuhukumu kwa hisia bali uthibitisho jadidi, yaani kwa suala kama hili.
Kwa mara nyengine utaniuliza ikiwa nawatetea wavuta unga na wauzaji wa uchafu huu unaoligharimu taifa, na tena jibu langu litakuwa ni hapana. Siwaungi mkono na nataka sana biashara hii iangamizwe, lakini nataka hilo lifanyike kwa kutumia njia za kisheria tulizojiwekea kama taifa. Serikali iliyo madarakani ni ya chama tawala cha CCM tangu uhuru, hivyo yenyewe ni sehemu ya janga la madawa ya kulevya, maana iliwalea na kuwaendeleza wauzaji na walaji kwa faida yake. Makonda anapopambana na dubwasha ambalo limeumbwa na chama chake kwa gharama ya taifa letu, asitugharimu misingi ya kisheria ambayo nchi hii imejiwekea, maana kitakuwa kigezo kibaya kwa mengine.
 
Wakati nikiwa kwenye mjadala wa hili na sahibu yangu mmoja aliye mtaalamu wa sheria, alinieleza kwamba: “Hapa hakuna mapambano, bali usimikaji wa mifumo mipya ya kuvuna kutoka kwa wauza unga kutokana na ile ya zamani kutoaminika na waliopo sasa.”
Unaweza usikubaliane na shutuma za swahibu wangu huyu, lakini hoja yake ni kwamba kinachofanyika sasa ni kuwaondowa kwenye mfumo wale wote waliowekwa na utawala uliopita ili kutengeneza mifumo mipya ambayo itakuwa tiifu na yenye kuaminiwa na wateule wapya. Kalisema hili akiamini kwamba mapambano haya yametawaliwa zaidi na hisia na sio sayansi ya kupambana na uhalifu huu mkongwe ambao unafanywa vigogo wenye ukwasi wa kutisha duniani.
Mungu ibariki Afrika!
Mungu ibariki Tanzania!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.