Nimesikiliza sehemu ya hotuba ya Rais John Magufuli wakati wa sherehe za Siku ya Sheria leo (Alkhamis, 2 Februari 2017). Nimemsikiliza aliposema wanaokamatwa na nyara za serikali au madawa ya kulevya wanastahili kuchukuliwa hatua bila kufuata taratibu za kawaida za kisheria, hasa pale wanapokamatwa ‘red-handed’ (na ushahidi kamili).john-magufuli

Amesema na mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao, nao wanastahili kukamatwa na kuwekwa rumande ili na wao ‘waisome namba’ ili, pengine, waache kuwatetea ‘wakosaji’ hawa.

Wote waliokuwa wanamsikiliza Rais Magufuli, akiwemo Kaimu Jaji Mkuu na majaji wenzake wa Rufaa na wa Mahakama Kuu, mawakili na wageni wengine waliokuwapo pale, waliangua kicheko kikubwa.

Wanafikiri alichokisema ni cha kuchekesha. Lakini, kwa hakika, si cha kufurahisha hata kidogo. Jeshi letu la polisi limekubuhu katika kusingizia watu vitu vya uongo. Kwa polisi wa nchi hii, kuondoka ushahidi, kuwekea watuhumiwa nyara za serikali au madawa au silaha ili wawakamate na kuwafungulia mashtaka mazito ili kuwakamua watoe pesa, ni kitu cha kawaida sana.

Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Tundu Lissu
Na Tundu Lissu

Polisi wetu wamekubuhu katika kuwafanyia watu upekuzi bila ya kuwa na hati za upekuzi na bila kufuata sheria na taratibu za kufanya upekuzi. Hivi ndivyo wanavyopandikiza ushahidi.

Polisi wetu wamekubuhu katika kutesa watuhumiwa ili wakiri makosa ambayo, mara nyingi, hawakuyafanya. Yote haya tunayafahàmu na mawakili, majaji na mahakimu wa nchi hii wanayafahamu sana. Wanakutana nayo kila siku mahakamani.

Kwa hivyo, kauli ya rais wetu kwamba watuhumiwa hawa washughulikiwe mara moja bila kujali taratibu za kisheria zilizopo ni baraka kwa matendo haya machafu ya jeshi letu la polisi. Ni baraka ya rais kwa utendaji mambo kinyume na sheria ndani ya nchi na ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Ndicho kitakachofuatia bila shaka yoyote. Yamekuwa yanatokea muda wote, sasa yataongezeka kwa sababu yana baraka za rais.

Hata hivyo, kilichonishangaza mimi sio alichosema Rais Magufuli – maana huyu tumeshamzoea – bali ni kile kilichonishangaza na waliokuwa wanamsikiliza ambao wanafahamu fika madhara ya kauli hii ya rais.

Kwingineko duniani, mawakili wangetoka nje kupinga kauli hii na rais angeshambuliwa vikali kila mahali kwenye vyombo vya habari, kama tunavyoona yanayomtokea sasa Rais Donald Trump wa Marekani. Lakini sio Tanzania. Kwetu kila mmoja anaona ni kichekesho.

Kuhusu mawakili kukamatwa, miezi kadhaa iliyopita Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi, alitoa kauli ya kuwatisha mawakili wa Zanzibar waliokuwa wanawatetea watuhumiwa wa kesi za kisiasa walizofunguliwa viongozi na wanachama wa Chama cha Wanachokiamini (CUF) visiwani humo. Kamanda Msangi alisema mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao nao watakamatwa na kuwekwa ndani. Kauli hiyo ilishambuliwa vikali, na kwa usahihi kabisa, na Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS) na wenzao wa Tanzania Bara (TLS).

Leo Rais Magufuli ametoa kauli hiyo hiyo na waliokuwa wanamsikiliza wamechekelea badala ya kutoka nje ya ukumbi kupinga!

Tusubirie tuone kama TLS watadiriki kutoa kauli ya aina waliyoitoa wakati wa sakata la Zanzibar au wakili mwenzao alipokamatwa Loliondo.

Mimi binafsi nina mashaka makubwa kama watadiriki kufungua mdomo. Katiba yetu inatamka wazi kwamba kila mtuhumiwa anahesabika kuwa hana hatia mpaka mahakama zitakapothibitisha vinginevyo. Rais Magufuli haamini hivyo. Kwake kila mtuhumiwa sio tu ana hatia, bali pia hastahili kusikilizwa wala kupata utetezi wa wakili mahakamani. Anachostahili ni adhabu tu, na kila adhabu ikiwa kubwa ndivyo bora kwake.

Katiba yetu inasema kila mtuhumiwa ana haki ya ‘kusikilizwa kwa ukamilifu.’ Haki hii, kama ambavyo mahakama zetu za juu zimesema mara kwa mara, inajumuisha kusikilizwa kupitia kwa wakili. Na juzi Jumanne tumepitisha haraka haraka na kwa mbwembwe nyingi Sheria ya Msaada wa Kisheria. Sheria hiyo inasema kila mtuhumiwa wa kesi ya jinai ana haki ya kupatiwa wakili bila malipo yoyote kama jaji au hakimu akiona inafaa. Mtendaji Mkuu wa Mahakama, mteule wa Rais, amepewa mamlaka ya kuwalipa mawakili watakaowatetea watuhumiwa hawa. Kwa hiyo fedha za umma zitatumika kuwalipa mawakili watakaowatetea watuhumiwa hawa wa makosa ya jinai. Bila shaka Muswada wa Sheria hii ulipitia kwenye Baraza la Mawaziri kama ilivyo kawaida.

Lakini leo Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Baraza hilo la Mawaziri anatamka hadharani kwamba mawakili watakaowatetea watuhumiwa wanaokutwa na nyara za serikali au madawa ya kulevya nao wakamatwe na kutiwa ndani. Waziri ambaye juzi alikuwa anashadidia watuhumiwa hawa wapatiwe msaada wa kisheria bila malipo anachekelea kauli ya Rais. Majaji na mahakimu watakaoamua watuhumiwa hawa wapatiwe msaada wa kisheria nao wanachekelea. Na mawakili ambao wanatakiwa na sheria watoe msaada wa kisheria na ambao watakuwa wahanga wa kauli ya Rais Magufuli nao wanachekelea.

Nafikiria kama lau Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya angetoa kauli ya aina hii, mawakili, wanasiasa, waandishi habari na wananchi wa kawaida wa Kenya wangemfanyaje. Wa kwetu wanachekelea. Haya yanatokea Tanzania tu.

One thought on “Kauli ya Magufuli si ya kichekesho, ni ya kupingwa vikali”

  1. Bwana Breivik kule Norway kwa makusudi kabisa aliripua kwa mabomu jengo la kiongozi mkuu wa serekali lililopo katikati ya jiji la Oslo mwaka 2011. Muda mfupi badae akakimbilia kisiwani ambako aliwafyetulia risasi za moto vijana na watoto kadhaa ambao takriban watu 77 aliwauwa bila kisisi ama huzuma yoyote. Alishitakiwa na kwa vile ni haki yake alipatiwa wakili mahsusi ambaye yeye mwenyewe alimkubali kumuwakilisha. Je leo ikiwa rais ambaye aliapa kuilinda haki ya kila mtu na katiba ya Tz eti anawapa amri majaji wasiwaruhusu hata mawakili kuwawakilisha WATUHUMIWA?!. Lakini vitisho vya namna hii kwa Tz si vigeni, tunakumbuka miezi michache tu Znz tulisikia viongozi wa idara ya usalama wakiwatisha mawakili wanaowawakilisha wafuasi wa CUF mahakamani. Tz inaendeshwa kibabe siku hizi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.