Zanzibar imejinamia. Tarehe ya leo imesadifiana na tarehe ya  miaka 16 iliyopita pale vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vilipowafyatulia risasi, kuwauwa, na hata kuwatia vilema raia kadhaa visiwani Zanzibar, kufuatia maandamano ya amani yaliyogeuzwa machinjio na watawala. Kosa lao kubwa ni maandamano hayo yalifanyika katika kupinga matokea ya uchaguzi wa mwaka 2000, kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.mazombi

Tofauti na nchi nyengine ambazo zimepitia mikasa ya mauaji, kama vile Rwanda, na nchi hizo kuoekana kujifunza kutokana na makosa hayo kwa kuchukua hatua madhubuti kuzuiya kutokea kwa mengine, utawala wa Tanzania, kwa ujumla wake, na wa Zanzibar, kwa upande wake, haujawahi kujutia mauaji haya.

Baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Rwanda ilijiundia mahakama zake za ndani maalum kwa lengo la kusaka ukweli na maridhiano, huku jumuiya ya kimataifa nayo ikiunda Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Rwanda (ICTR) yenye makao yake Arusha, kaskazini mwa Tanzania, kwa lengo la kuwashughulikia wauwaji. Ndani ya Rwanda walianzisha mifumo maalum ya kijamii mfano “ndumunyarwanda” yaani ‘mimi ni Mnyarwanda’, lengo likiwa ni kuondoa hisia za kibaguzi na uadui miongoni mwa Wanyarwanda ili kuzuia kutokea kwa matukio ya mauaji yaliyochochewa na chuki.

Na Mohamed Aliy
Na Mohamed Aliy

Baada ya mauaji ya maangamizi dhidi ya Mayahudi nchini Ujerumani na kusambaa kote Ulaya (Holocaust), kulichukuliwa jitihada za makusudi, zikiwemo za kuwasaka na kuwashitaki waliohusika na mauaji hayo, wengi wao wakiwa maafisa wa juu katika utawala wa Adolf Hitler. Lengo la hatua hizo ilikuwa ni kuzuiya kutokea kwa matukio ya mauaji yaliyosababishwa na chuki miongoni mwa raia wa nchi moja kwa kisingizio cha itikadi za kisiasa au hata asili za watu.

Kwa Zanzibar hali imekuwa tofauti. Baada ya miaka 16  kupita, hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria waliohusika na unyama ule.

Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa na umri mdogo, lakini nilikuwa na uwezo wa kufahamu kinachoendelea katka siasa za nchi yangu japo kwa kiwango kidogo. Kulikuwa na watu ambao walifurahia mauaji yale, wakisema kuwa eti ni watu wa aina fulani ndio walioathrika na ilikuwa stahiki yao kukutwa na mkono wa chuma wa dola.

Baada ya kelele za mashirika ya kimataifa na wadau mbalimbali wa haki za binaadamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ndiyo iliyokuwa na jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia, ilijitutumua na kuunda tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Brigedia Mstaafu Hashim Mbita.

Licha ya kuundwa kwa tume hiyo na kufanya kazi kwa mujibu wa muongozo iliyopewa na serikali, matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo yalitofautina kwa kiwango kikubwa na matokeo ya ripoti za tume nyengine za kimataifa. Mfano, ripoti ya shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch likitaja jumla ya watu 35 waliouawa na vyombo vya usalama, Tume ya Mbita ilitaja idadi ndogo mno ya hiyo. Pamoja na mambo mengine, Tume ya Mbita ilifanya kama inawahukumu waliouawa, kubakwa na kujeruhiwa ikisema kuwa maandamano hayo yaliweza kuepukika baada tu ya agizo la polisi la kuyazuia maandamano hayo. Haikuwalaumu polisi kwa kushindwa kuwalinda waandamanaji kutumia haki yao ya kikatiba, na badala yake ikawauwa!

Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo, Omar Mahita, hakuguswa hata unyusi na aliendelea na majukumu yake na hatimaye kustaafu kwa heshima zote – ikiwa mtu ambaye mikono yake imejaa damu anaweza kweli kuambiwa ana heshima. Sambamba na hilo baadhi ya askari walioshiriki katika mauaji ya raia wasio na hatia walipandishwa vyeo, huku wale wachache waliokataa kutii amri ya kuwapiga risasi raia wasio hatia wakifungwa na kisha kufukuzwa kazi. Katika tukio moja la kufedhehesha sana, nilimsikia askari mmoja wa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania akijisifia jinsi aivyoshirki vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake kisiwani Pemba.

Ya 27 Januari yaendelea

Baada miaka 16 kupita, vitendo vile vile vya ubabe wa vyombo vya ulinzi kwa wananchi wasio na hatia vimekuwa vikiendelezwa,  tena kwa sura tofauti na ya kiwango cha juu ambacho kinaashiria kutojifunza kwa wenye mamlaka juu ya yale yaliyotokea Januari 2001. Uchaguzi wa mwaka 2015 uliwashuhudia watu waliopewa jina la mazombi wakiwa wamevaa soksi za kuficha nyuso zao wakipita mitaani na kupiga watu ovyo, kuvunja majengo na biashara na kutisha na kujeruhi.

Walikuwa wanatumia magari ya vikosi vya serekali  na silaha za moto ambazo kiutaratibu wa kisheria ziko chini ya Jamhuri ya Muungano Tanzania. Wazanzibari waliamua kuwapa jina la “mazombi” watendaji wa jinai hizo, kwa kuwa serikali nzima ilijifanya haiwajui.

Mauaji dhidi ya raia wasio na hatia ni suala ambalo viongozi wa chama tawala wamelipuuza muda mrefu huku wakikataa hata kutoa ruhusa kwa Wazanzibari kufanya lolote linaloazimia kuwakumbuka wahanga wa mauaji hayo. Kwa mfano, jeshi la polisi limeizuwia Jumuiya Vijana wa Chama cha Wananchi (JUVICUF) kufanya maandamano ya amani hivi leo kuwakumbuka wahanga hao. Sababu za jeshi hilo kuzuwia maandamano hayo ni za utoto wa kisiasa na zisizioingia akilini, bali zaidi ni za vitisho kwa watu wale wale ambao waliuliwa ndugu zao na jeshi hilo miaka 16 nyuma.

Kwa vyovyote vile, kukosekana kwa hatua madhubuti dhidi ya wahusika wa mauaji hayo, hakuashirii dhamira njema wala mustakabali mzuri sio tu kwa wale waliopotelewa na ndugu na jamaa zao, lakini kama taifa tuna deni kubwa la kuzilipa damu za wahanga wa mauaji yale.

Hata hivyo, ukweli ni mmoja tu: kwamba hata kama serikali zilizopo zitaendelea kuziba masikio na kuacha kuwachukulia hatua stahiki wahusika, hata ipite karne nzima, bado waliopoteza jamaa zao iko siku wataidai haki hii katika mahakama za ndani au nje ya nchi hii na wataipata. Waache watawala na mawakala wao wendelee kutojifunza na waendelee kuwatumia vijana wao kuendeleza na kushabikia vitendo vya uvunjaji wa haki za binaadamu visiwani Zanzibar. Hatimaye hati itapatikana na itasimama, maana dhuluma haidumu milele!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.