Wakati naanza kutaka kuandika kumbukumbu hizi mwili umenisimka mara kadhaa maana katika akili yangu tukio lile halitafutka. Si kwa kuwa niliona chochote kile kwa macho yangu, la hasha, lakini nimeona zaidi kwa akili yangu.cuf

Kwa sababu ya maumbile yangu kila inapofika kuripoti matukio makubwa kama hili la Januari 26 na 27 au kuzingirwa kwa Mtendeni, au kuzama kwa MV Spice Islander, mfumo wangu wa utendaji huwa zaidi kukaa mbali na kukusanya taarifa na kuzituma, na kutoka mara moja kwa mahojiano ya kimkakati.

Sikuwa naamini kuwa Serikali ingechukua hatua za kuua wananchi wake waliosema na kuweka dhamira kwa sababu ya kuandamana kwa suala la haki. Suala hilo wengi wetu tutalisimamia hadi mwisho wa uhai wetu, na baadhi yetu maandishi yetu yataendelea kupaza sauti zetu hata tukiwa katika makaburi yetu na mifupa yetu imeshakuwa mchanga nalo ni kuwa: CUF iliibiwa uchaguzi mwaka 2000 kama ilivyoibiwa 1995.

By Ally Saleh
Na Ally Saleh

Na pia tutasimamia ukweli kuwa CUF pia wameibiwa uchaguzi 2005,2010 na wazi kabisa 2015 na ndio maana kumbukumbu ya mauaji ya Janurari 26=27 itaendelea kuwepo kwa sababu dhulma dhidi ya umma, CUF na Maalim Seif itaendelea.

Utawambiaje kwa mfano wa South Africa wapuuze au waisahau kumbukumbu ya Sharpvile ambao watoto wasio na hatia waliuuwa huko Soweto? Hivi itafutika vipi jambo kama hilo? Utakuwaje binaadamu ukilifuta hilo? Na wengine wengi katika mataifa yao wanayo mambo kama hayo.

Asubuhi ya Januari 26 haikuwa siku ya kawaida maana tuliamka na ukimya mkubwa sana kama ishara kuwa mauaji makubwa yatafanywa kwa sababu ya kulinda madaraka ya mtu aliyepata ushindi usio halali na kupewa nguvu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Nikiwa nyumbani asubuhi na mapema nilisikia risasi ya kwanza ikilia kwa kutokea upande wa Darajani mimi nikiwa Hurumzi. Watoto wangu abdul-razak shau na Dorid Alberto wakaamua kutoka kiwenda kushiriki maandamano angalau kwa maneno yao wakarushe mawe na mimi sikuwazuia.

Siku hiyo mbali na kuishia barabarani askari waliojihami kwa silaha za kila aina waliingia mpaka vichochoroni ambako milango yetu mingi iitishiwa kuvunjwa.

Basi jinsi nilivyokuwa nimejipanga nilikuwa nikipata ripoti kila baada ya dakika tano,na kwa kuwa mbali na BBC nilikuwa naandikia pia Reuters, basi kila nikipata ripoti mpya nilifanya filing ama ya kuhojiwa upya au ya kuandika new piece.

Niliandika au nilihojiwa mara nyengine huku nalia. Baada kama nilivyosema sikushuhudia kitu lakini ripoti nilizopata zllikuwa so graphic hata kwa kuhadithiwa utaweza kuona kila kitu. Waliopigwa njiani, waliopigwa msituni, walioingiliwa nakunajisiwa majumbani, waliokimbia wakiacha watoto au kuwafungia.

Hata hivi leo hasa Pemba,watu waliokuwa watu wazima au watoto wana hadithi za maumivu makubwa ya kuona, kuhisi,kusikia na yaliowakuta wenyewe

Mara baada ya tukio hllo nilihojiwa na mashirika kadhaa ya haki za binaadamu na watafiti lakini niliitwa kutoa lecture Chuo Kikuu cha Dar es slaama,ambako nililia mara kadhaa huku nikielezea yaliojiri siku mbili ambapo “mvua ya risasi ilinyesha”

Na bado nikaendelea kupata maumivu ya kisaikolojia wakati kupitia mfuko mmoja wa Kimarekani ulipotupa fedha mimi na Salma Said kupitia Zanzibar Journalists Association kwenda kuwashawishi wanawake wa Pemba wajitokeze kutoa ushuhuda wao juu yaliotokea kwenye Tume ya Uchunguzi ya Hashim Mbita.

Na ubabe wangu wote ambao najidai ninao wallahi siwezi kurudia tulioabiwa na wahanga hao, itosehe tu nikikwambieni kuwa “it was horrible experience.”

Wanawake hao walikwenda kwenye Tume hiyo kama walivyokwenda wengine wengi wa Unguja na Pemba. Cha kusikitisha hakuna chochote Tume ilichokiona kwa maana ya nani wakuwajibishwa na kwa hivyo Serikali haikutoa onyo,karipio,haikushtaki mtu yeyote kuanzia askari mkubwa wala mdogo na kabisa kuhusu wanasiasa ambao ndio waliofanya maamuzi ya kuzima maandamano hayo.

Kwa maana kuwa hata baada ya watu 31 kufariki kwa hesabu ya Serikali, watu kwa makundi kujeruhiwa na wengine wakipata vilema na watu 4,000 kukimbilia ukimbizini Shimoni na Somalia hakuna alieguswa hadi hii leo, kama kwamba hawakufa binaadamu, hapakujeruhiwa mtu.

Hii ndio kumbukumbu yangu ya Januari 26 na 27, 2001 na ndio maana mara nyingi hupenda kuisema ili wengine wajue jambo hili kubwa lilopita katika nchi yetu kwa sababu ya uamuzi wa uhuru wa kuchagua.

Na miaka kadhaa mbele bado uhuru wa kuchagua haupo na ndio maana CUF hawaoni sababu ya kutoendelea kutafuta mamlaka kupitia kisanduku cha kura na wanashika ule msemo kuwa kama yaliowafika hayo kwa kutaka sauti ya kura basi sasa “They have got nothing to lose but their chains” yaani hawana tena cha kupoteza zaidi ya minyororo yao.

Na ndio sababu kwamba CUF ina wanachama imara,waadilifu na wasioyumba kwa sababu wanabakia na jukuma la kusimamia matakwa ya waliojitoa muhanga, mbali ya wengi kwa maelfu tulioshitakiwa kwa maelfu,tunaopigwa majumbani na kwenye baraza zetu hata leo.

Eti kuna watu hujitia upofu wa kusema ” kila kitu wao , kila siku wao” kama kwamba hawajui yote yaliowafka watu bila ya kosa zaidi tu kuwa mwanachama au shabiki wa CUF.

Kama kupandwa mbegu ya CUF kudai haki yao ya kutawala kupitia kisanduku cha kura basi ilipandwa Januari 26-27 na dalili za kufika dhamira hiyo zimeanza kujitokeza Oktoba 25, 2015 na kutujenga imani wengi kuwa sasa siku zinahesabika.

2 thoughts on “Baada ya tarehe 27 Januari, Wazanzibari hawakuwa tena na cha kupoteza ila minyororo yao”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.