Hakuna ushahidi wowote uliothibitisha kwamba waandamanaji walifanya vitendo vyovyote vya utumiaji nguvu. Hata hivyo, namna vyombo vya usalama vilivyojitayarisha kabla ya tarehe 27 Januari, inaonyesha kwamba viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wa vyombo vya usalama walipanga na kuamrisha mashambulizi hayo mapema. Miongoni mwa wahusika walikuwa polisi, jeshi la wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na wanamgambo wa chama tawala. Matokeo haya yalisababisha malalamiko mengi kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali lakini serikali haikufanya uchunguzi wowote wala kuomba radhi kwa matokeo haya. Kwa hakika viongozi wa Tanzania waliwapongeza viongozi wa mauaji hayo. Rais Mkapa pia aliwapongeza askari hadharani kwa kile alichokiita kazi nzuri sana ya kurudisha amani visiwani Zanzibar. – Muhtasari wa Ripoti ya shirika la Human Rights Watch.

Huyu ni majeruhi wa Kinuni mwaka 2005. Miaka saba baadaye, bado Zanzibar inazalisha wahanga wengine kama hawa.

TANZANIA: “RISASI ZILINYESHA KAMA MVUA”

Mashambulizi Dhidi ya Maandamano ya Amani Yaliyofanyika Zanzibar Tarehe 27 Januari Mwaka 2001

 1. MUHTASARI

Katika hatua iliyopokewa kwa furaha mwezi wa Januari mwaka 2002 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin Mkapa alitangaza kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama huko Zanzibar mwaka 2001.

Mwezi wa Januari mwaka 2001 vikosi vya usalama vya serikali ya Tanzania vikiongozwa na jeshi la polisi viliyakandamiza na kuyavunja maandamano ya kisiasa yaliyoitishwa huko Zanzibar kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000. Vikosi vya usalama vya serikali na hasa jeshi la polisi wakisaidiwa na askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) na askari wa usalama wa taifa na pia wakiungwa mkono na wanamgambo wa chama tawala cha CCM, kwa nguvu zilizopita mipaka, waliwakamata, kuwapiga na kuwanajisi wakaazi wa visiwa vya Zanzibar.

Human Rights Watch (HRW) inakisia kwamba, kwa uchache, watu the lathini na watano waliuwawa na wengine wapatao mia sita kujeruhiwa. Wazanzibari wengine elfu mbili (2,000) walikimbilia nchi jirani ya Kenya. Kiwango cha ukiukaji wa haki za banadamu uliofanywa na vikosi vya serikali ya Tanzania na ile ya Zanzibar mwezi Januari mwaka 2001 kilikuwa cha kupita kiasi kwa jinsi unyanyasaji na mateso vilivyoandaliwa dhidi ya maandamano halali ya kisiasa visiwani Zanzibar.

Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa mwaka 1964 kwa muungano kati ya Tanganyika na visiwa vya Unguja na Pemba ambavyo kwa pamoja vinajuilikana kama Zanzibar. Mivutano ya muda mrefu ya kisiasa imeanza kujitokeza wazi wazi baada ya kuanza kwa siasa za vyama vingi hapo mwaka 1992.

Kufuatia matokeo mengi ya udanganyifu katika uchaguzi ambao haukuwa wa huru na wa haki uliofanyika huko Zanzibar mwezi wa Oktoba mwaka 2000, chama kikuu cha upinzani cha Tanzania, Chama cha Wananchi (CUF) kiliitisha maandamano ya nchi nzima hapo tarehe 27 Januari 2001 kupinga matokeo ya uchaguzi huo wa mwaka 2000.

Chama cha CUF pia kilikuwa kinadai mabadiliko ya katiba. Maandamano hayo yaliyoungwa mkono na vyama vyengine vya upinzani na ambayo yalikuwa makubwa kupita yote katika historia ya Tanzania, kwa ujumla yalikuwa ya amani ingawaje kulikuwa na vitendo vichache vya unyanyasaji vilivyofanywa na polisi.

Huko Zanzibar hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kabisa na ya kutisha. Vikosi vya usalama vya serikali vilipewa amri ya kuyazuia maandamano hayo kwa njia yoyote ile. Vikosi hivyo viliwashambulia kwa kuwapiga risasi waandamanaji katika miji minne ya Wete, Micheweni, Chake Chake na mji wa Zanzibar uliopo katika kisiwa kikuu cha Unguja.

Waandaaji walipanga maandamano ya amani na wakawataka washiriki kufika kwenye maandamano bila silaha na kujifunga vitambaa vyeupe mikononi ili kuashiria amani. Kwa upande wake serikali ya Tanzania, siku nyingi kabla ya tarehe ya maandamano hayo kufika, iliyatangaza maandamano hayo kuwa si halali na ikaanza kuchukua hatua za kuwatisha wananchi waliotarajia kuhudhuria maandamano hayo.

Serikali pia iliwaonya na kuwataka waumini kutawanyika na kuondoka misikitini mara baada ya kumalizika kwa sala ya Ijumaa. Ikiwa kama ni hatua ya kuonyesha utumiaji nguvu utakaofuatia, siku moja kabla ya tarehe iliyopangwa maandamano hayo, askari waliwapiga risasi na kuwauwa watu wawili. Waliouliwa walikuwa kiongozi mmoja wa dini na mfuasi mmoja ambao walipigwa risasi nje ya msikiti huko mjini Zanzibar.

Siku iliyofuata, hapo Januari 27 maelfu ya waandamanaji wasio na silaha waliandamana kwa amani kuelekea sehemu zilizopangwa. Askari katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba waliweka vizuizi barabarani na kuwaamrisha waandamanaji hao kutawanyika. Waandamanaji walishikilia msimamo wao na waliendelea kuandamana kwa amani. Askari polisi na wanajeshi waliwashambulia waandamanaji hao kwa kuwapiga mabomu ya machozi na badaye kwa risasi.

Bila ya kuwaonya, waliwashambulia, kuwafukuza, na kuwafuata watu waliokuwa wakikimbia kutoka katika maeneo ya matokeo. Baadhi ya waaandamanaji walipigwa risasi na askari wenye silaha waliojificha au waliopiga risasi kutoka kwenye helikopta ya polisi iliyokuwa ikizunguka angani. Helikopta hiyo ilizidi kuwatisha waandamanaji waliokuwa wakikimbia huku na huko kutafuta mahali pa kujinusuru.

Wakati waandamanaji wakitawanyika, askari waliwashambulia waandamanaji hao na pia kuwazuia waliojeruhiwa kupata matibabu. Polisi na askari wa usalama wa taifa walidhibiti hospitali na wale waliojeruhiwa na kujaribu kupata huduma katika hospitali walinyimwa matibabu. Mwananchi mmoja aliyeshuhudia matokeo haya alieleza kwamba “risasi zilinyesha kama mvua”. Kufuatia mashambulizi hayo, vikosi vya usalama visiwani Zanzibar wakipita nyumba hadi nyumba waliwanyang’anya watu mali zao, kuwatisha na kuwadhalilisha kijinsia.

Watu waliounga mkono chama cha CUF na hasa watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba ndio waliopata matatizo zaidi. Ofisi nyingi za chama cha CUF zilivamiwa, kuharibiwa na kunyang’anywa vitu vilivyokuwemo. Katika matokeo mengine askari walitoa kauli zenye kukashifu dini ya Kiislamu wakati wakiendelea kuwanyanyasa wakaazi wa Zanzibar ambao wengi wao ni Waislamu.

Mamia ya waandamanaji ambao wengi wao walikuwa wamejeruhiwa vibaya waliwekwa kizuizini kwa siku kadhaa bila kupelekwa mahakamani huku wakiendelea kuteswa. Zaidi ya Wazanzibari elfu mbili (2,000) walikimbilia nchi jirani ya Kenya. Ingawa wakimbizi wengi wamerejea Zanzibar bila ya kupata matatizo kufuatia msamaha uliotangazwa na serikali, kiasi cha watu mia mbili (200) mpaka sasa wanaendelea kubakia katika sehemu za Kenya au Somalia.

Kiwango cha utumiaji nguvu na jinsi utekelezaji wa zoezi zima ulivyoendeshwa na serikali inaonesha wazi namna gani mambo haya yalivyotayarishwa ili kuukandamiza upinzani hasa katika zile sehemu ambazo unaungwa mkono sana na wananchi, yaani Zanzibar.

Hakuna ushahidi wowote uliothibitisha kwamba waandamanaji walifanya vitendo vyovyote vya utumiaji nguvu. Hata hivyo, namna vyombo vya usalama vilivyojitayarisha kabla ya tarehe 27 Januari, inaonyesha kwamba viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wa vyombo vya usalama walipanga na kuamrisha mashambulizi hayo mapema.

Miongoni mwa wahusika walikuwa polisi, jeshi la wananchi, viongozi wa serikali za mitaa na wanamgambo wa chama tawala. Matokeo haya yalisababisha malalamiko mengi kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali lakini serikali haikufanya uchunguzi wowote wala kuomba radhi kwa matokeo haya. Kwa hakika viongozi wa Tanzania waliwapongeza viongozi wa mauaji hayo. Rais Mkapa pia aliwapongeza askari hadharani kwa kile alichokiita kazi nzuri sana ya kurudisha amani visiwani Zanzibar.

Matokeo ya uchunguzi wa HRW yanatofautiana na maelezo ya serikali. Viongozi wa serikali ya Tanzania katika taarifa zao rasmi wanadai kwamba waandamanaji walijaribu kuteka vituo vya polisi na kuanzisha maasi ya kutumia silaha. Viongozi wa serikali walidai kwamba idadi ya watu waliokufa ilikuwa ishirini na watatu (akiwemo askari polisi mmoja). Walidai pia kwamba askari waliotumia silaha walifanya hivyo bila ya amri ya viongozi wao wa juu na kwamba vifo vilivyotokea vilisababishwa na mafunzo duni pamoja na bahati mbaya.

Matokeo ya uchunguzi wa HRW, hata hivyo, yanaonyesha kwamba idadi ya waliokufa na waliojeruhiwa kutokana na vitendo hivyo vya serikali inazidi ile idadi rasmi ya serikali.Inaonyesha pia kwamba kwa kiasi kikubwa haya ni matokeo ya vitendo vilivyopangwa vya kuyakandamiza malalamiko ya upinzani.

Tarehe 10 Oktoba mwaka 2001, katika hatua muhimu, chama kinachotawala Tanzania – Chama cha Mapinduzi (CCM) kilifikia makubaliano na chama cha CUF juu ya kufanya mabadiliko ya kisiasa. Sehemu muhimu ya makubaliano yaliyopendekezwa ni kutenganisha vyombo vya kiutendaji baina ya vile vya serikali na vile vya chama tawala. Iwapo yatatekelezwa, makubaliano hayo yatahusu mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, na Mahakama ya Zanzibar.

Muafaka huo pia unataka kuanzishwa kwa orodha ya kudumu ya wapiga kura, kubadilishwa kwa sheria na taratibu za kuendesha uchaguzi, na kutolewa huduma sawa kwa vyama vya upinzani katika vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya Zanzibar. Muafaka huo pia unatoa nafasi ya kuundwa kwa Tume huru ya uchunguzi kuchunguza vurugu lililotokea Zanzibar hapo tarehe 27 Januari 2001.

Tarehe 16 Januari mwaka 2002, tume ya watu wanane iliteuliwa na Rais wa Tanzania kuchunguza mauaji ya Januari mwaka 2001 na kutoa mapendekezo serikalini juu ya hatua ambazo zichukuliwe kurekebisha hali hiyo na kuepusha kurejewa kwa matokeo kama hayo. Tume hiyo inatakiwa kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake pamoja na mapendekezo ifikapo Julai mwaka 2002.

Katika kipindi cha kuanzia Januari mwaka 2001 kumekuweko na kiwango kidogo cha shinikizo kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa la kuitaka serikali ya Tanzania kuwaadhibu wale waliohusika na ukiukwaji wa haki za binaadamu wa Januari mwaka 2001 au kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kidemokrasia.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Kimataifa hapo kabla, iliamrisha kuchukuliwa hatua dhidi ya Zanzibar. Mbali na kulaani ukiukwaji wa haki za binaadamu, nchi wafadhili zilikuwa tayari zimeshazuia misaada yao kwa serikali ya Zanzibar kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi wa miaka ya 1995 na 2000.

Hata hivyo, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikisita kuchukua msimamo mkali kama huo dhidi ya serikali ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Tanzania imekuwa ikiendelea kupokea misaada kutoka nje. Tanzania pia hivi karibuni ilifanikiwa kupata msaada wa kupunguziwa madeni kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) chini ya mpango wa kutoa nafuu kwa nchi zenye madeni makubwa duniani (HIPC).

Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaziunganisha nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar inayaweka masuala ya ulinzi na usalama chini ya jukumu la Serikali ya Muungano. Kwa hivyo, inashangaza kuona kwamba Jumuiya ya kimataifa imeamua kulishughulikia suala la ukiukwaji wa haki za binaadamu unaofanywa Zanzibar kwa kuvikatia misaada visiwa vya Zanzibar pekee. Hatua zaidi za kimataifa zinazohusiana na utawala wa sheria katika Zanzibar ni lazima zielekezwe katika serikali ya Muungano wa Tanzania kama ilivyofanywa kwa serikali ya Zanzibar ili kuhakikisha haki za binaadamu zinaheshimiwa.

HRW inakaribisha kwa furaha uundwaji wa tume huru ya uchunguzi kama hatua ya kwanza ya kurudisha utawala wa sheria Zanzibar lakini inatahadharisha kwamba hatua hii ni lazima ifuatiwe na uchunguzi wa kina na kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi huo. Serikali pia ni lazima ichukue hatua kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote waliohusika katika ukiukwaji wa haki za binaadamu uliofanyika Zanzibar mwaka 2001.

Kwa hakika, ni aibu kuona kwamba hadi sasa hakuna afisa yeyote wa serikali aliyeshitakiwa au kuadhibiwa kwa kuhusika katika ukiukwaji huo wa haki za binaadamu. Kinyume chake, maafisa mbali mbali wa vyeo vya juu katika jeshi la polisi walipandishwa vyeo muda mfupi baada ya maandamano. Zaidi ya hayo, kwa uchache maofisa wanane wa polisi waliokataa kushiriki katika ukiukaji wa haki za binaadamu walikamatwa na baadaye kufukuzwa kazi kwa kutokuonyesha hamu ya kushiriki katika uvunjaji huo wa sheria.

Matokeo ya uchunguzi wa HRW yanonyesha kwamba viongozi wa vyombo vya usalama na dola walishiriki katika uvunjaji wa sheria za nchi na zile za kimatifa. Vyombo vya usalama vilishiriki katika mauaji yaliyofanywa kinyume na sheria pamoja na matumizi ya nguvu za ziada yaliyopelekea kwenye mauaji na kujeruhiwa kwa raia wasio na silaha, wakiwemo wale waliokuwa wanawasaidia waliojeruhiwa.

Uvunjaji mwengine wa haki za binaadamu ni pamoja na mashambulio dhidi ya majeruhi pamoja na kuwanyima matibabu majeruhi hao, mateso, ikiwa ni pamoja na kuwanajisi na kuwadhalilisha kijinsia wanawake, kukamatwa na kuwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani, unyang’anyi wa mali za watu, kunyimwa kwa haki ya kujieleza, haki ya kukusanyika na haki ya kujiunga na jumuiya na kuzuia kufanyika kwa maandamano ya amani. Ripoti hii inatokana na ushahidi uliokusanywa na kitengo cha Afrika cha HRW huko Zanzibar na Dar-es-salaam katika mwezi wa Julai na Agosti mwaka 2001.

Ripoti hii pia inajumuisha taarifa zilizopatikana kutokana na mahojiano yaliyofanywa na wakimbizi waliokimbilia Shimoni, Kenya, mahojiano ambayo yalifanywa mwezi wa Februari mwaka 2001. Ushahidi huo unatokana na mahojiano 160 yaliyofanywa na watu walioathirika na wale walioshuhudia matokeo hayo na pia maofisa wa serikali (wakiwemo polisi), wafanyakazi wa vyombo vya misaada, wanachama wa chama tawala na wa vyama vya upinzani.

HRW pia imepata mikanda ya video yenye urefu wa dakika kadhaa inayoonyesha polisi wakipiga risasi katika kundi la watu na pia wakipiga raia wasio na silaha katika mji wa Wete. Watu walioshuhudia wamethibitisha kwamba matokeo hayo ni yale yaliyotokea tarehe 27 Januari mwaka 2001. Zaidi ya hayo mahali ambapo matokeo hayo yametokea pamethibitishwa kwamba ni mji wa Wete ambao haujawahi kufikwa na matokeo kama hayo kabla ya siku hiyo ya tarehe 27 Januari 2001.

Majina ya wengi kati ya waliohojiwa na baadhi ya sehemu ya mahojiano yalipofanyika yanahifadhiwa kwa sababu za usalama wa wahusika. Mwezi wa Januari mwaka 2002 HRW ilirudi Tanzania kwa ajili ya kukutana na viongozi wa serikali na kujadili matokeo na mapendekezo uchunguzi kabla ya kuchapishwa kwa ripoti hii.

HR ilionana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Bw. Bernard Mchomvu pamoja na Msaidizi Kamishna Muandamizi wa Polisi, Bwana Shafi na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Bwana Kingwai. Viongozi wa Wizara ya Ulinzi ya Tanzania walikataa kuonana na wawakilishi wa HRW.

Idadi halisi ya waliouliwa na waliojeruhiwa katika matokeo hayo bado haijulikani na idadi iliyotolewa na serikali na ile ya upinzani zinatofautiana. Serikali inadai kwamba watu ishirini na watatu walikufa na themanini na wawili walijeruhiwa (wakiwemo polisi kumi) na 352 walikamatwa.

CUF, kwa upande wake, inadai kwamba watu sitini na saba waliuliwa. HRW iliweza kuthibitisha watu wasiopungua thalathini na watano waliokufa na zaidi ya watu mia sita (600) waliojeruhiwa. Tarakimu zilizotumiwa na HRW katika ripoti hii ni makisio yanayotokana na hesabu za serikali na vyombo vya habari kama kianzio na baadaye kuthibitishwa kwa mahojiano na watu walioshuhudia matokeo hayo.

 1. MAPENDEKEZO

Kwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zanzibar:

 • Heshimuni uhuru wa maoni, wa kujiunga na vyama, na wa kukusanyika kwa wanachama wa vyama halali vya kisiasa katika Zanzibar na pia kwa raia wote na wakaazi wa Tanzania. Hakikisheni kwamba wanachama wa vyama vya upinzani hawakamatwi na kuwekwa ndani ovyo, kudha lilishwa na kufanyiwa vitisho.
 • Hakikisheni kwamba tume iliyoundwa kuchunguza mauaji ya tarehe 27 Januari huko Zanzibar inafanya kazi zake kwa uhuru kamili na inapatiwa mahitaji yote muhimu wakiwemo wafanyakazi na vifaa vinavyohitajika kuendesha uchunguzi wa kina na usiopendelea upande wowote. Hakikisheni kwamba wajumbe wa tume hiyo wanapata mafunzo ya kutosha na yale yanayohusu haki za kimataifa za binaadamu, namna ya uendeshaji wa mahojiano (hasa kwa wale walioathirika kutokana na kubakwa) na namna ya kuhakikisha usalama wa mashahidi. Uchunguzi ni lazima uhakikishe usalama wa watu wote watakaotoa habari, vielelezo au ushahidi. Tume ni lazima itangaze hadharani na kwa ukamilifu matokeo ya uchunguzi pamoja na mapendekezo yake.
 • Chunguzeni, chukueni hatua za kinidhamu na fungueni mashitaka dhidi ya wanajeshi, polisi na wanamgambo pale ushahidi wa kutosha utakapopatikana kwamba wanahusika na uvunjaji wa sheria ikiwa ni pamoja na mauaji kinyume cha sheria na matumizi ya ziada ya nguvu, mateso, unyanyasaji (vikiwemo ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia) uwekaji ndani wa watu kinyume cha sheria, unyang’anyi na uharibifu wa mali uliofanyika Zanzibar tarehe 27 January 2001.
 • Hakikisheni kwamba vikosi vya usalama vya Tanzania vinapokabiliana na waandamanaji wa kiraia vinafuata sheria za kimataifa zinazohusu mwenendo wa askari kama zilivyo katika sheria za Umoja wa Mataifa zilizomo katika Kanuni za Msingi Juu ya Utumiaji Nguvu na Silaha Unaoendeshwa na Vyombo vya Sheria na Kanuni za Umoja wa Mataifa kwa Wafanyakazi wa Vyombo vya Sheria.
 • Hakikisheni haki sawa ya kupata matibabu katika vituo vya afya vya serikali kwa watu wote waliojeruhiwa bila kujali misimamo yao katika siasa au mambo mengine. Ni muhimu kuhakikisha kwamba kibali cha polisi (Form PF3) hakitumiwi vibaya kuwanyima huduma za afya au kuwasumbua majeruhi wanaodhaniwa kuwa ni wapinzani. Fomu ya PF3 inahitajika kupatikana kutoka kituo cha polisi kabla ya mwananchi kupata matibabu ya majeraha yatokanayo na kuchubuka, kujikata, majeraha ya risasi na majeraha mengine.

Kwa Serikali za Nchi Wafadhili na Wanachama wa Jumuiya ya Madola:

 • Wekeni shinikizo zikiwemo njia za kidiplomasia kwa serikali ya Tanzania kuhakikisha haki za binaadamu zinaheshimiwa Zanzibar. Utekelezaji wa muafaka uliofikiwa mwezi wa Oktoba mwaka 2001 ni lazima utumike kama kipimo cha utekelezaji wa haki za binadamu Zanzibar na utawala wa sheria na pia katika kuamua misaada itolewayo kwa serikali ya Tanzania. Kushindwa kutekeleza vipengele vya makubaliano hayo vipelekee kuzuiwa kwa mauzo ya vifaa vya kijeshi au misaada katika vikosi vya ulinzi na usalama misaada ambayo inaweza kutumiwa katika uvunjaji wa haki za binaadamu. Maendeleo hayo ya utekelezaji pia yatumike kama kigezo cha kuamua iwapo misaada 6 iliyosimamishwa kwa serikali ya Zanzibar baada ya udanganyifu katika uchaguzi wa mwaka 1995, irudishwe au la.
 • Toeni msaada wa vifaa na fedha kwa ajili ya utekelezaji wa muafaka wa Oktoba mwaka 2001, na hasa kwa tume ya kuchunguza machafuko ya Januari mwaka 2001 huko Zanzibar. Tumieni diplomasia kuishinikiza serikali kuhakikisha kwamba tume ya uchunguzi inapewa nguvu na vifaa vinavyohitajika kufanya uchunguzi wa kweli na ulio huru na kuhakikisha kwamba matokeo yake yanatangazwa.
 • Endelezeni shinikizo kwa serikali ya Tanzania ifungue mashitaka dhidi ya wale waliohusika na mauaji kinyume na sheria, matumizi ya nguvu kupita kiasi, mashambulizi, utesaji (pamoja na ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia), uwekaji ndani wa watu kinyume na sheria, unyang’anyi na uharibifu wa mali uliotokea katika machafuko ya tarehe 27 Januari mwaka 2001.

Kwa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank):

 • Angalieni kwa makini msaada unaotolewa kwa serikali ya Tanzania chini ya Mpango wa Kupunguza Umasikini na Mpango wa Upunguzaji wa Madeni kwa Nchi Masikini Sana Duniani ili kuhakikisha kwamba mipango hii inachangia moja kwa moja kujenga utawala bora, na kuheshimiwa kwa utawala wa sheria katika Tanzania.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.