Imethibiti kwamba pamoja na mikakati yote inayotumika kuhakikisha wanavunja hamasa ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), imeshindikana na bado watawala wanaendelea kuuona uthubutu ule ule wa wakaazi wa Soweto dhidi ya makaburu wa Afrika Kusini katika madai ya haki. Kila kukicha ari ya wananchi kuwaonesha wababe wachache – hasa mkoloni – kuwa hana nafasi katika vifua wala vichwa vyao, inadhihirika wazi kwa jinsi muamko mkubwa. Uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Dimani ulichukuliwa na Wazanzibari kwa hamasa ile ile ya uchaguzi mkuu.16174659_10154924366489655_4189704472600029101_n

Ndio maana ukawakuta wale wale waliopita Kipumbwi na Sakura wakiwa na mabwenzi yao kuja kupiga kura na suti zao za Jumapili, wakikimbia hata picha wasionekane. Uchaguzi huu umeionesha waziwazi rangi halisi ya mkoloni na makucha yake dhidi ya Wazanzibari walio wengi wanaoamini katika haki, usawa na heshima katika muendelezo wa Muungano, badala ya maskini kumkalia kifuani fakiri kwa upuuzi wa ati kuogopa kijitaifa chenye asilimia 99 ya Waislamu katika dunia na karne ya leo kama vile upande wake yeye mwenyewe mtawala hakuna Waislamu.

Na Foum Kimara
Na Foum Kimara

Kama kuna chochote kile, basi uchaguzi huu mdogo umetupa nafasi ya kujitathmini wenyewe juu ya namna gani wananchi na machungu yao wameweza kuyapokea maamuzi ya uongozi ya kukabiliana na hili kwa nguvu ya juwa, badala ya upepo utaoezuwa mapaa yetu na kutuwacha katika umasikini mkubwa zaidi na au ukoloni mwengine wa kisingizio cha kulinda amani au kuwa hatuwezi kujitawala wenyewe.

Ukitazama makosa tuliyoyofanya nyuma kama taifa, yakapelekea mtafaruku mkubwa wa 1964, hatuwezi kuyarejea. Tukifikiri matokeo yake yaliyojiri baada ya kukosea kule, tunajuwa kuwa makosa kama hayo yatatusukuma zaidi shimoni, tusitambuane.

Ukweli ni kuwa wananchi hawajakata tamaa na mabadiliko na hili ndilo muhimu katika mapambano yoyote ya kupigania haki. Na hiyo ni faida kubwa kabisa iliyojidhihirisha kwenye ile hamasa ya Wazanzibari kwenye uchaguzi huu.

Uchaguzi wa Dimani na udhaifu wa watawala

Mbali na kuonesha uhai wa dhamira ya Wazanzibari dhidi ya ukoloni, uchaguzi huu wa Dimani umeonesha zaidi udhaifu wa watawala, hasa ukizingatia kuwa jimbo hili lilikuwa ni lao ambalo lisingehitaji nguvu kubwa walizotumia kujihalalishia.

Unapokuta wapigakura wasiolijuwa hata jimbo lao, lafudhi ya sehemu husika na wakiwa na woga nyusoni, basi unafahamu namna gani mtawala alivyokosa hata takwimu za kwake mwenyewe – hajui nani ni wake na nani si wa kwake.

Kinachowasukuma Wazanzibari ni kimoja tu: nazo  ni nguvu za mkoloni mwenye dhamira hasa ya uchochezi kwa lengo lake mwenyewe. Yanayofanyika ni idhara na kumfichua hasa aliyejificha katika taharuki ya Visiwani.

Hebu pitia matokeo katika dunia hii ambayo tunayo mkononi kwa kila kitu, halafu usikiye mtu anashinda bila ya hata kura moja kuharibika! Woga umewazidi hata hesabu wanazoiogopa. Mantiki ya kushinda imewapitia kiasi kwamba khofu ya kutotambua umadhubuti wao, imewafanya kubeba tu nambari ya urahisi kama mtoto mdogo na hesabu vya vijiti.

CUF imepewa kura 1,234. Hawakutaka hata kubahatisha, wakijuwa kabisa nambari haziko upande wao. Mdhulumiwa hana cha kupoteza katika madai ya haki yake, ila dhalimu ndiyo anayeishi na woga kiasi kwamba hataki hata sindano idondoke Zanzibar, ikamtoa.

Na jitihada zote – kuanzia ya Bwana Ruzuku za vigunia, Msajili Chori, vitisho vya Inspekta kumkamata mshindi wetu, ukata wa kutunyima haki yetu ya ruzuku kikatiba, kesi kwa wagombea wetu, kamata kamata mpaka ng’ombe na mbuzi, masoksi, na kila aina ya hamasa na tisha tisha na bado wao katika jimbo lao wenyewe wako taabani na roho zao. Walichokizoea ni hizi furaha za muda sawa na kamba inayofumuka kidogo kidogo, maana hii Unguja yenyewe na jitihada zote za kuwagawa watu, ina dalili zote za kuwatoka.

CUF inabakia kuwa taasisi

Jambo jengine ambalo limejidhihirisha kwa uchaguzi huu wa Dimani ni ithibati kuwa CUF ni taasisi. Tunaposema chama hiki ni taasisi, ni kwa sababu ya umma kujipanga pamoja na kuwa na malengo marefu ya kudumu, badala msukumo wa kututia katika zahama zitakazotufanya sio tu kuikimbia tu nchi yetu tukaishia kama Syria na Libya lakini pia nasi hatimaye tukaikuta haipo hata ndotoni mwetu.

Wakati si kitu kwa asiyekuwa na malengo, bali ndio msingi kwa mwenye malengo makubwa na ya kudumu. Bora uumie moyo kwa sababu ya kusimama na haki kuliko kuumia moyo kwa sababu ya majuto, ukijuwa kabisa majuto ni mjukuu.

Watu wengi wanajiuliza CUF wamekosea wapi katika uchaguzi huu? Jibu ni kwa hakuna walipokosea. Wameshiriki kikamilifu na kuweza kupata jukwaa la kuwaeleza wananchi na kuwakumbusha ahadi za Dubai mwaka tu walizopewa na hali walipo. Wamewakumbusha kuwa haya ni mapambano ya mkoloni dhidi yao na si suala la kisiasa kama tunavyotakiwa kuamini. Wameuambia umma kuwa ushindi wa mkoloni ni pale wanaotawaliwa wanapokata tamaa ya kudai mabadiliko katika nchi yao kwa sababu ya vifaru na roketi alizonazo mkoloni huyo.

Ni nchi chache mno zilizoweza kushindana na mkoloni kwa kutumia mabavu na zikashinda. Inahitaji akili na zaidi uthubutu wa hali ya juu, umoja na ari ya moyoni kabisa ya kuhakikisha tunakabiliana naye kwa nguvu za joto badala ya upepo utakaowageuza wahanga wawili kuwa mahasimu wa milele kwa sababu tu ya sera za chama kilichobeba ukoloni moyoni.

Si unawasikia kwa tashtiti ati Zanzibar shwari kama maji ya mtungi. Hii ni kwa kuwa lengo la mauaji ya wananchi halikutimia. Wameweza kuzusha zahma na fungafunga na dhuluma kwa waliowakataa. Yanayofanyika yote ni kutusukuma huko ili tuendelee kunyosheana vidole kwa sababu ya rangi zetu, asili zetu na aila zetu.

Lengo ni kuhakikisha utengano unazidi baina yetu, ili tutoke katika umoja wa kudai mabadiliko kwa maslahi ya nchi na tubaki katika malalamiko ya ubaguzi baina yetu, ili dunia isahau ustaarabu wetu kutokana na chuki za kujaliza za mkoloni anayefikiri atatuamulia nani wa kutungoza milele.

Uchaguzi wa kutufunguwa macho

Mwisho na la muhimu kuliko yote ni kuwa uchaguzi huu wa Dimani umetufumbua macho zaidi na kutupa nguvu ya kuhakikisha tunasonga mbele na mikakati mikubwa zaidi ya kukabiliana sasa na mama kuku badala ya vifaranga visivyoona chochote zaidi ya mlo ulio mbele yao na kufikiri ubabe wao kwa wengine ni kwa sababu ya nguvu walizonazo.

Kama ni sisi wenyewe tu, mbona zamani tungelishamalizana tena kwa urahisi kabisa bila ya kumwagana damu wala kuumizana? Nafikiri kubwa tungelinuniana tu na kukunjiana nyuso, lakini mauaji hayapo katika nyoyo zetu! Tulipokosea nyuma ni kuvaa joho la uadui wa kupaliliwa kwa waliobeba maslahi makubwa dhidi ya uwepo wa taifa hili dogo lenye historia kubwa barani Afrika.

Yaliyofanyika Oktoba 2015 yalikuwa kielelezo tosha kabisa kuwa kuna kuku mama aliye juu na analinda maslahi yake kwa kutumia tu vifaranga ili wapigane na kuumizana wenyewe huku akiwagawa baina yao, akifurahia njaa na maendeleo duni yao na kwa kuzidi kuhasimiana kwao, vifaranga hao wanasahau kabisa msingi hasa wa hasama zao.

Tunakwenda mbele, haturudi nyuma. Miaka 53 ya Mapinduzi leo wapo wanaokiri kabisa makosa ya kila pande tukafika tulipofika, na tukaweza kwa nia thabiti kabisa kusimamisha maelewano yaliyorejesha matumaini ya walio wengi na ile ndoto ya zabibu na matufaha tena kwa umoja, ihsani na wema.

Hatuwezi kurudi nyuma kwa sababu tu ya fitina ya mkoloni anayechezea watu akili na kuwagawa kwa ukubwa wa matumbo yao.

Tunakwenda mbele na tutafika tu, biidhnilah.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.