Katika moja ya hotuba zake alizozitoa mwaka 1961, mtu anayetajwa na ‘historia rasmi’ kuwa muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, anasimulia kisa cha mama mmoja mwanachama wa Afro Shiraz Party (ASP) aliyehoji ni uhuru gani ambao vyama vya ukombozi hasa ASP vilikuwa vikiupigania? Katika majibu yake, Mzee Karume alisema: “…kwamba uhuru huondoa unyonge, huondoa dhulma, huondoa shida, huondoa kuogopana, na mengineyo mengi…”. 

AFRICA,ZANZIBAR - Portrait of Sheikh Abeid Karume. Hewas the first President of Zanzibar. He lead the Zanzibar revolution against the last sultan of Zanzibar in January 1964. He was assassinated in 1972 by four gunmen. (Photo by: Africa 24 Media /  Camerapix/ Mohamed Amin)ALL RIGHTS RESERVED
                                                                                                                                                         Picha  kwa hisani ya Mohamed Amin.

Hakuna shaka yoyote kuwa ASP na vyama vyengine vilivyokuwemo katika vuguvugu la kudai uhuru vilikuwa na dhamira ya kuleta mabadiliko na uhuru wa kweli miongoni mwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba, ndio maana wakati Zanzibar inaadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi, wananchi wa Zanzibar wana jukumu la kutathmini hali zao za kimaisha zilivyo na kujiuliza kama kweli na ni kwa kiasi gani Wazanzibari wamepata uhuru ambao Marehemu Karume na wapigania uhuru wengine walibeba dhima ya kuutafuta na hata kufikia kutokea kwa tukio la Mapinduzi ya mwaka 1964.

Kuna mengi yanayosemwa kuhusu tukio hilo, huku wengine wakihoji uhalali wa Mapinduzi hayo ambayo yalikuja kuiondoa serikali iliyokabidhiwa Uhuru wa tarehe 10 Disemba 1963 ambao uliifanya Zanzibar itambulike kimataifa kwa kuwa na uwakilishi rasmi ndani ya Umoja wa Mataifa.

Na Mohamed Aliy
Na Mohamed Aliy

Licha ya kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ni suala linalozungumzwa kwa namna tofauti kulingana na anayeyazungumzia na hata itikadi yake, ukweli utabakia kuwa Mapinduzi hayo ni sehemu ya historia ya nchi yetu na hakuna anayeweza kurudi nyuma akabadili kile kilichotokea.

Kwa mintarafu hiyo makala hii haitajadili uhalali wa Mapinduzi ya Zanzibar kisiasa au kitabaka kwa mnasaba wa mtiririko matukio ya kihistoria, bali kutathmini tu miaka 53 ambayo bila ya shaka kwa kiumbe aliyefikia umri huu wa kuishi anatarajiwa kupata kiwango fulani cha mafanikio kama vile kuwa na familia, kuwa na shughuli ya kujiongezea kipato na hata kukuwa na kuongezeka kwa kizazi yaani kupata wajukuu na vitukuu.

Na kwa Wazanzibari, Mapinduzi ya 1964 sio mtoto tena, ni kiumbe kilichopevuka, hivyo wana haja ya kipekee na haki ya kuhoji na hata kutathmini Mapinduzi hayo na mafaniko yake katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni.

Mara baada ya Mapinduzi, serikali iiyoongozwa na ASP ilichukua jitihada mbalimbali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake kwa kuwapatia huduma za kijamii kama vile makaazi, elimu, afya na nyenginezo. Hali imekuwa tofauti kwani kila miaka ilivyokwenda mbele huduma za kijamii zimeendelea kushuka hadhi na hata baadaye kubadilika kwa mfumo wa utowaji huduma hizo kutoka ule wa “bila ya malipo” hadi mfumo wa “kuchangia”, jina linalotumika kuficha ukweli kuwa huduma hizo sasa zinalipiwa. Hata hivyo, suala la kulipia huduma sio jambo gani kwa dunia tunayokwenda nayo, mradi huduma inayotolewa inakuwa na ubora na ni yenye kuridhisha.

Kwa kuzingatia hisabu ya Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2012, ambayo inasema Zanzibar ilikuwa na wakaazi 1,303,569, basi sasa yawezekana kuwa wamefikia 1,500,000. Lakini kwa kuangalia kiwango cha ukuwaji wa uchumi hata kwa mtu mmoja mmoja, Wazanzibari kwa sasa wanaishi zaidi ya chini ya dola moja kwa siku. Hili linatupa taswira kuwa Zanzibar imezidi kudidimia baada ya miaka 53 ya Mapinduzi. Je ni kipi serikali iliyopo inaweza kujivunia?

Kwa upande wa miundombinu mara baada ya mwaka 1964, Zanzibar ilkuwa na miradi mbali mbali ya kijamii kama vile makaazi ya nyumba za maendeleo za Michenzani, Makunduchi na Mkoani. Leo hii baada ya nusu karne hakuna miradi ya kimaendeleo kama hiyo iliyolenga kuwapa raia unafuu wa maisha. Wazanzibari wanaishi katika makazi duni yaliyokosa kuratibiwa kwa kukosa mvuto hata kusababisha madhara kwa wakaazi wa maeneo hayo yanapotokea majanga kama vile moto na hata miripuko ya maradhi.

Kama hilo halitoshi hata yale majumba ya kimaendeleo yaiyojengwa mara tu baada ya Mapinduzi, leo hii yamepoteza haiba na mvuto na kibaya zaidi hata ukarabati wa majumba hayo sasa umeshindwa kuwa endelevu. Unaweza kupita jumba Nambari 7 ghorofa ya kwanza kumepakwa rangi ya kijivu jivu, upande wa pili rangi ya chokaa, almuradi hakuna kinachoeleweka.

Hata huduma za kijamii kama vile maji katika majumba hayo yamekuwa ya mashaka sana, na kila pembe ya majumba hayo kumezagaa matenki ya maji ambapo wakaazi wa nyumba hizo za maendeleo wameamua kuyatumia ili kukidhi haja zao za kupata maji safi na salama.

Kwa upande wa elimu, Zanzibar ya kabla na baada ya Mapiduzi ya 1964 ilikuwa na mfumo mzuri wa elimu, ambapo pamoja na uchache majengo ya skuli, kiwango cha elimu na hata ubora wa wahitimu wa wakati huo ulikuwa mzuri, ambapo mhitimu wa kiwango cha stashahada alikuwa na uwezo wa kushindana na mihitmu wa nchi kama Uingereza na kwingineko.

 

Kwa Zanzibar hali ya kiwango cha elimu imeendelea kuporomoka siku hadi siku na Zanzibar imepoteza sifa ya kuwa kitovu cha elimu iliyokuwa nayo kabla ya Mapinduzi ambapo watu kutoka nchi tofauti walikuja Zanzibar kujifunza elimu ya dini pamoja na fani nyengine za kielimu.

Kwa upande wa suala la ulinzi wa haki za binaadamu na demokrasia, Zanzibar imeendelea kutajwa katika ripoti mbali mbali za mashirika ya ndani na ya nje ya nchi kuwa na rikodi ya matukio mengi ya uhalifu wa kidola na uvujwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Mfano ripoti ya shirika la kimataifa la Human Rights Watch imetaja vifo vya watu 35 vilivyotokana na matukio ya polisi kutumia nguvu kubwa dhidi ya raia katia maandamno ya amani yaliyofanyika mwaka 2001. Haya yanatokea baada ya miaka mingi ya kupigania uhuru ambao wengi wetu tuliamini ungeondosha madhila mbalimbali pamoja na khofu miongoni mwa Wazanzibari yangeweza kuondoka.

Hapa ndipo inapokuja hoja ya kujiuliza: je, Mapinduzi ya Zanzibar yamewapa Wazanzibari uhuru wa kutosha wa kufanya mambo yao? Na je kuna lolote la kujivunia tunapoadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi haya?

Kisiasa, Zanzibar bado inasuasua katika kujenga demokrasia ya kweli na uvumilivu, kwani tokea kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao ulitoa mwanya kwa watu kuwa huru kujiunga na vyama wanavyovitaka, bado mfumo huo haujakita mizizi na wananchi kujisikia furaha kuwa wafuasi wa vyama vyengine mbali ya chama kinachotawala.

Zanzibar imeshafanya chaguzi tano tangu mwaka 1995, lakini chaguzi zote hizo zimekumbwa na ukosowaji mkubwa kutoka ndani na nje ya nchi kwa ukiukwaji wa sheria pamoja na uingiliaji unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika kushindikiza na kulazimisha vyama vya upinzani visipate nafasi ya kushika dola.

Chaguzi hizi zote tano ni ushahidi mkubwa kuwa lengo la kujitawala wenyewe kama Wazanizbri bado halijafikiwa, pamoja na ukweli kwamba kihistoria Zanzibar imepitia mkondo mikali ya maji moto na baridi. Kilele cha ishara ya wazi kuwa Zanzibar haiijawa huru lilionekana kinagaubaga katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 ambapo waangalizi wote kutoka jumuiya za ndani  na za nje walisema uchaguzi huo kuwa huru wa haki, lakini kwa kuwa ulionesha ushindi kwa chama ambacho kinafikiriwa kupingana na mfumo wa kuitawala Zanzibar uliopo, basi wasimamizi wa mfumo huo wakaufuta.

2 thoughts on “Miaka 53 ya Mapinduzi: Baina ya uhuru wa kweli na uhalisia”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.