Ule ukarimu, ustaarabu wa Waswahili wa Pwani ulifutika kisha ukungu wa damu za wengi wasio na hatia ndio uliofunika mitaa, fukwe, viambaza na chochoro za visiwa vya Zanzibar, hasa Unguja. Siku ya tarehe 12 Januari 1964 ilikuwa ni siku ya safisha safisha ambayo haikuwahi kutokea kabla, katika historia ya Pwani ya Afrika Mashariki. Harufu ya moshi wa bunduki na roho zilizojaa hofu na suintofahamu ndiyo ambayo yalitamalaki.revo

Niweke wazi jambo moja, mimi sitojadili uhalali au uharamu wa Mapinduzi. Kwa maneno mengine sitojadili ikiwa kulikuwa na ulazima wa Mapinduzi kufanyika au la. Ninalolijadili ni kuwa, hakukuwa na uhalali wala ulazima wa kuuwa raia wasiokuwa na hata bunduki, kwa sababu tu ya misimamo ya vyama vyao au rangi za ngozi.

Sababu yoyote iwayo ikiwa utaitumia kuhalalisha au kuharamisha Mapinduzi, lakini ukweli hautofutika kuwa hakukuwa na uhalali wa kuuwa mamia ya watu wakati lengo la wapinduaji lilikuwa limeshatimia ndani ya masaa machache tu.

Kilicho wazi ni kuwa mauaji hayo yaliwalenga zaidi raia wa kawaida, kwani vifo vya askari wa kiserikali na wale wa kimapinduzi ilikuwa ni ndogo mno. Sehemu kubwa kabisa ya waliouawa ni raia ambao hawakuwa na hata silaha.

Na Rashid Abdallah
Na Rashid Abdallah

Watu wengi waliuwawa na wengine kuchukuliwa mateka. Mauaji ya mateka ambao walikuwa wafungwa lilikuwa ni jambo la kawaida tu kama kuuwa nzi. Wengi wao walikufa baadaye kutokana na mateso mabaya gerezani au katika kambi mpya za wafungwa zilizofunguliwa baada ya kiu ya damu kwisha.

Wapo walioponzwa na rangi ngozi zao, misimamo yao ya kisiasa na wengine bahati zao tu kuwa mbaya, kwani hawakuwa katika kundi lolote kati ya hayo mawili.

Ila na wao wakaishia kwenye mikono ya chinjachinja wasio na chembe ya huruma, wengine wakibaki na majeraha ya milele ikiwa ni kuondokewa au kudhalilishwa.

Picha adimu za kipekee za mauaji ya kutisha zilipigwa na mpigapicha wa Kitaliano zikionesha watu wakikimbia kupitia pwani, maiti zilizozagaa ufukweni, mauaji ya mateka na makaburi ya halaiki.

Picha nyengine zikionesha  dakika za mwisho za mistari ya wafungwa wakipelekwa katika kaburi la pamoja kisha wanapigwa risasi na kuuwawa, vijiji vinaharibiwa, na  malori ya maiti yakienda kufukia maiti katika makaburi ya pamoja.

Masuali ya muhimu ya kujiuliza ni haya: Kulikuwa na haja gani ya kubaka watoto wa kike wakati Mfalme Jamshid bin Abdullah alishakimbia kama kweli utawala wake yeye ndio uliolengwa? Kulikuwa na haja gani ya kuuwa mamia kama si maelfu ya watu kwa sababu ya kumpindua kiongozi aliyekwishakimbia? Kulikuwa na haja gani ya kutesa na kudhalilisha, wakati utawala uliopinduliwa haukuwa tena madarakani na wala haukuleta upinzani wowote? Haja ya kutesa wafungwa hadi wakafa ilikuwa ni ipi?

Haya yote hayakuwa na haja, isipokuwa tu ni ukatili wa wale wenye kiu ya damu ya binaadamu wenzao, kuchoma watu wazima, kuharibu nyumba zao ni unyama tu ambao haukuwa na sababu hata moja.

Mwandishi Chris Oke anapoyachambua mapinduzi ya Zanzibar katika makala yake chini ya anuani; ‘The forgotten genocide of the Zanzibar revolution’ anaweka mstari muhimu sana anaposema: “Siku ya maadhimisho ya mapinduzi ya Zanzibar inasherehekewa kwa mbwembwe nyingi, lakini lile ambalo linadharauliwa na kukaliwa kimya ni maelfu ya maisha ya watu yaliyopotea”.

Na hili ndilo ambalo nalizungumza hapa: la msingi si nani aliuwawa ama mtu wa kabila ama rangi fulani, kilicho wazi ni kuwa Wazanzibari waliuwawa si kwa sababu tu ya kuondoa utawala fulani madarakani, bali lazima palikuwa na sababu nyengine, maana kama nilivyosema: Mapinduzi mazima yalichukuwa robo siku tu kukamilika, lakini mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yakaendelea muda mrefu sana baadaye.

Ajabu kubwa ni kuwa furaha inatamalaki zaidi siku hii ngumu kwa watu wengi, na hakuna aulizaye au kukumbusha kosa la kihistoria lililofanywa na wanamapinduzi, kuteketeza roho zilizotulia majumbani.

Maisha ya watu wengi waliopotea hufunikwa kwa zile Oke aziitazo “mbwembwe”, labda nami niziite mbwembwe za wambwebwekaji katika majukwaa na viwanja.

Nilizaliwa takriban miongo mitatu baada ya Mapinduzi, lakini hata nikifunua vitabu na kusikiliza wana historia, hakuna hoja inayoelezwa ambayo tunaweza kuitumia kuhalalisha huu upotevu wa hizi roho.

Ni mauaji ya kibaguzi, chuki, husuda, ukatili, roho mbaya, uchu, na ugaidi mtupu. Kumwandama mtu nyumbani kwake, kupita nyumba hadi nyumba unatafuta mtu fulani umpige risasi au umkate kwa panga, kama huu si ugaidi ni nini`?

Kisha watu wakapeta na maisha hakuna aliyeulizwa. Ni kana kwamba kulikuwa na mbu tu ambao walikuwa wanakera mtaani, wakapigwa dawa ya IT. Sasa tunafunzwa utukufu wa mapinduzi usiokuwepo na kuachishwa ya maana ili tukeshe kukata viuno na kufanya laana.

Maana akili zimetufikisha ambapo tunu ya kweli hatuijui tena, mauaji na mateso ya wasio na hatia ndio imekuwa tunu adhimu, huku vifijo na nderemo eti ndio vinaponza majeraha kwa waliobaki.

Hakuna haja ya kufukua makaburi, lakini kukiri kosa lilifanywa na radhi ikaombwa ni jambo kubwa mno, kuliko kuzidisha vidonda kwa magwaride na matarumbeta, kana kwamba ni harusi lakini ukweli ulikuwa ni msiba.

Kimya cha usiku na mchana, jua litokapo na usiku ufunikapo visiwa vyetu si ishara ya kusahaulika kilichotokea, wala mkusanyiko wa hutuba refu za kila mwaka hazipo kuwaombea msamaha waliotenda dhambi.

Mungu Ibariki Zanzibar na utupe mioyo ya kukumbuka uzito wa tunakoenda, ili akili zing’amue kuwa kuenzi ukatili, huenda kirama n’ katibiin wakaweka maandishi yao, kuwa nawe ulikuwa miongoni mwao makatili na wauwaji wale.

Na huenda ikawa ndio sababu chinjachinja imeendelea kubakia mpaka leo visiwani Zanzibar na jamii inanyamazia kimya, kwa kuwa mifupa ya walionchinjwa hapo miaka 53 iliyopita na kisha isisemewe, inaviandama visiwa vyetu.

2 thoughts on “Mapinduzi yalifanyika robo siku, chinjachinja ikaendelea milele”

 1. Baada ya kusoma mengi kutoka kwa wafafanuzi mbali mbali kuhusu kilichotokea Zanzibar huo mwaka 1964, baada ya kuyaita mapinduzi, tunaweza kuyaita mauwaji.
  Walio uliwa katika tukio lile ni zaidi ya Wazanzibar 13 elfu (13,000). Nnathubutu kusema kinywa kipana, kuwa wengi wa hao wanaosimama majukwaani na kauli za “mapinduzi daima” hawaelewi chanzo na malengo yaliokusudiwa na hao watayarishaji wa hayo mauwaji.

 2. Haya kuwa Mapinduzi kama wengi wanavyofikiria, bali ilikuwa ni Uvamizi wa nchi yetu.
  Mapinduzi ni lazma yafanywe na wananchi au wazalendo wa nchi ile kuuondoa utawala wasio
  utaka.
  Haya yalifanywa na wageni wengi kwa kushirikiana na wananchi wachache, hivyo ni Uvamizi.
  Kwa mfano, John Okello ni Mganda, Engeni ni Mkenya, Mfaranyaki, Seif Bakari,
  Mohd Mfaume pamoja na Wamakonde wengi kutoka
  Tanganyika na Mohd Kaujore na Wamakonde
  wenzake kutoka Msumbiji.
  Ni Hamid Ameir, Ramadhani Haji, Said Iddi Bavuai etc ndio WaZanzibari.
  Kwahivyo ni Mavamizi.

  Mipango ya kuivamia
  Zanzibar ilipangwa Dar na Nyerere ndio Mastermind.

  Hawa wageni ndio waliofanya mauaji makubwa sana na ya kinyama.

  Kama WaZanzibari
  wangefanya Mapinduzi wao
  wenyewe tu bila
  kushirikisha wageni,
  yasingetokea mauaji ya
  halaiki naya kinyama kama
  yaliyotokea.

  Siku ya tarehe 12 /01 / 1964 ni siku ya Nakama kwa Zanzibar, ndio siku Serekali halali iliyokuwa huru ilipovamiwa na kuondolewa madarakani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.