HISTORIA ni nzito. Tukiingia 2017 tunaiona yetu sisi kuwa ni zigo kubwa la dhambi za watawala wetu pamoja na zetu wenye kuwaachia watawala wafanye wayafanyayo. Jecha Salim Jecha

Tunawaachia wajifanyie watakavyo kwa sababu, kama walivyo watawala na sisi pia, hatuna uadilifu.

Tunayaona makosa yanayotendwa na watawala, tunaona jinsi haki za wananchi zinavyokandamizwa, jinsi uhuru unavyominywa, jinsi viongozi wanavyolihadaa taifa na jinsi taifa linavyoishi likigubikwa na kivuli cha utawala wa kimabavu.

Tunajua kuwa ingawa utawala wa kimabavu unaweza ukaja kwa mpigo mmoja, hata hivyo, ikiwa hautokemewa na kupingwa huenda pia ukanyemelea polepole na ghafla tukashtukia tumekabwa koo na dikteta.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Yote hayo tunayajua lakini tunayafumbia macho. Hatuthubutu kufungua midomo yetu kuyakemea na kuyapinga. Tunafanya hivyo kuyakinga maslahi yetu na kujinusuru watawala wasitudhuru.

Sisi ni wale tujiitao wanaharakati, wachambuzi, wadadisi, waandishi, wanasheria na hata wanasiasa. Wengi tunapenda kujigamba kuwa ni wasomi. Wengi wetu ni watu wenye kuujua ulimwengu na tunayajua yanayojiri nchini. Tunakwenda nayo na unafiki wetu huku tukiibeba historia yetu na tukijikokota nayo.

Migongo inatuuma kwa sababu historia yenyewe, kama nilivyokwishadokeza, ni nzito.

Wengi wetu tunatambua kwamba ni hatari kuwa na mtawala apendaye sifa, anayeamini kuwa kila alitendalo ni sawa na kuwa umma unampenda na unayakubali yote ayafanyayo.

Juu ya kutambua huko hatuthubutu kutahadharisha kuwa mtawala aina hiyo ni hatari kwa demokrasia na ustawi wa jamii.

Kadhalika, inasikitisha kwamba hatuthubutu hata “kukumbusha”. Tunaona ni sawa tukishirikiana na watawala kuyasahau yanayopaswa kukumbushwa mara kwa mara, ingawa tunajua kuwa kusahau ni moja ya mbinu zinazotumiwa na watawala kuidhibiti jamii.

Kwa mfano, watawala wangependa tuyasahau yaliyojiri Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na ule wa bandia, usio wa halali, wa Machi 2016. Baadhi yetu tunaona ni sawa kuyasahau hayo na kwamba ikiwa tunajifanya kuyasahau na umma mzima nao utayasahau.

Lakini ukweli ni kwamba aibu ile haiwezi kusahaulika. Tunajipurukusha tu lakini hatuwezi kwa dhati kuisahau kwa sababu imekwishaingia katika historia na historia hujiandika kwa wino usiofutika.

Leo, kesho, mwakani, miaka 50 ijayo au karne ijayo, mpaka kiyama yaliyojiri katika uchaguzi huo yataendelea kuwa bayana.

Kila siku zikenda ndipo patapozidi kuibuka ushahidi zaidi wa nani miongoni mwa viongozi na vibaraka wao, aliyefanya nini, nani alisema nini, kwa dhamira gani na kwa manufaa ya nani.

Watawala wamefanya uhaini mkubwa kuyabirua matakwa ya wananchi kwa kuufuta uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015. Walichofanya ni kuwapora Wazanzibari waliopiga kura uhuru wao wa kuwachagua wawatakao. Wangeyaheshimu matakwa ya wananchi wangepiga hatua kubwa ya kuimarisha demokrasia nchini.

Walichofanya watawala ni ulaghai na wizi. Kujidai kuwa wanafuata mfumo wa demokrasia ilhali walichokuwa wakifanya hasa ni kuhakikisha kwamba upinzani kwamwe hautoshinda katika uchaguzi huo. Kwa hakika, walichofanya ni sawa na kuuendeleza mfumo wa utawala wa chama kimoja.

Huu ni mfano wa jinsi watawala walivyozifanya siasa za Zanzibar ziwe za uoza. Misingi iliyoanza kujengwa 1992 ya kurejesha mfumo wa siasa za vyama vingi ilizidi kubomolewa 2015. Kurejeshwa ushindani wa vyama vya siasa kulikuwa hatua ya kwanza ya kusimamisha demokrasia nchini lakini watawala wameichimba na hawajali kuwa walichofanya ni kitendo cha kigaidi.

Baadhi yetu hatuyaoni hayo. Au kama tunayaona basi hatutaki kukiri kuwa katika sayansi ya kisiasa tunaweza kuuelezea utawala wa sasa wa Zanzibar kuwa ni mfano wa utawala wa kigaidi. Kuna ushahidi wa kutosha wa kuithibitisha hoja hiyo.

Mtawala kamwe asihadaike akiwaona raia zake wakichanja kuni na kupika vitumbua vyao yaani wakiendesha maisha yao kama kawaida juu ya dhiki walizo nazo. Pamoja na kufukuta kwenye majivu ya moto wa vitumbua, aghalabu huwa kunafukuta pia katika jamii.

Watawala wetu watakuwa wanajidanganya wakidhania kwamba umma uliokaa kimya, juu ya dhulma walioufanyia, ni umma ulioridhika nao. Tumeshuhudia kwingineko Afrika kuwa umma hukaa kimya kwa muda kwa sababu unakuwa unaogopa. Unaziogopa zile ziitwazo nguvu za dola. Lakini hufika wakati umma unakuwa sugu na hapo ndipo mambo yanapolipuka.

Ijapokuwa jumuiya ya kimataifa imesema wazi kwamba uchaguzi halali wa Zanzibar ulikuwa ule uliofanywa Oktoba 2015 na si ule wa Machi 2016, watu bado wanashikilia kuwa utawala huu ni halali.

Juu ya hayo, ile iitwayo “lugha ya mwili” ya baadhi yao inaonyesha kuwa hata viungo vyao wenyewe vya mwili vinawasuta. Haviyaamini yanayowatoka kinywani kuhusu kadhia hiyo.

Lau wangekuwa na uungwana na ujasiri wangelijitenga na mfumo uliowazonga wakajitokeza kusimama upande wa haki. Nina hakika umma ungesimama pamoja nao. Wangeheshimika duniani na kwao badala ya kuwa hivi walivyo sasa kuwa ni watu wanaolaaniwa na kuapizwa.

Kwa bahati mbaya hawawezi kuwa na ujasiri wa aina hiyo. Hawawezi kwa sababu mfumo uliopo unawatisha hata wao wenyewe. Wanawajua watawala wenzao, ndio wao kwa wao, wanakijua chama chao kuwa ndicho kile kile kilichoishika nchi miaka yote hii na wanayaelewa malezi yao ya kisiasa kuwa ni yaleyale ya kutishana.

Pamoja na suala la udhibiti wa chama kutoka Dodoma pia kuna suala la Muungano na namna unavyoweza kuyaingilia mamlaka ya Zanzibar.

Ijapokuwa umri wa Muungano umepindukia nusu karne hoja zenye kuuponda, kwa muundo wake ulivyo, zinazidi kuwa na nguvu. Kadhalika, idadi ya wenye kuziunga mkono hoja hizo inazidi kuongezeka.

Badala ya kuwa chapwa, kufifia au hata kufa kabisa hoja hizo zinazidi kuungwa mkono na watu wengi zaidi. Na hapa ndipo watawala, pamoja nasi tujiitao wasomi, tunapohitaji kujiuliza: kwa nini?

Kwa nini baada ya muda wote huu bado suala hili li hai, kwa nini vizazi vipya vya Wazanzibari visivyoyaonja maisha kabla ya Muungano vikawa miongoni mwa walio safu ya mbele ya wenye kuhoji uhalali wake miaka 52 baada ya kuundwa?

Kwa muda mrefu watawala wamekuwa wakijidanganya kuhusu hali halisi ya Muungano huu. Uzoefu umeonyesha kuwa kila miaka ikisonga mbele mamlaka ya Zanzibar yamekuwa yakizidi kumomonyoka na kuhaulishwa kwenye Serikali ya Muungano.

Vilio vya Wazanzibari vya kutaka usawa katika Muungano huu vimekuwa vikipuuzwa na serikali ya Muungano. Kuna mtu karibuni hivi alinitanabahisha kuwa awamu hii ya tano ya Rais John Magufuli ndiyo yenye kuonyesha dharau ya kupindukia juu ya Zanzibar, kwani hata waziri wa mambo ya Muungano na naibu wake wote wametoka Tanganyika.

Lakini siamini kuwa ni Magufuli peke yake mwenye kufanya uonevu na udhalilishaji huu. Kwa hakika tunasikia kuwa hivi karibuni Magufuli alipotaka ushauri wa viongozi wenzake wa Zanzibar nini aijibu Jumuiya ya Ulaya (EU) kuhusu malalamiko yake juu ya Zanzibar, kiongozi mmoja mstaafu alimshauri Rais aiambie Jumuiya hiyo iwavumilie hadi uchaguzi wa 2020.

Ukimuangalia mstaafu huyo utadhani kuwa ni mtu wa kuheshimika kumbe ndani ya nafsi yake hana uadilifu.

Huo ushauri wake, na kimya chetu, ndivyo vinavyozidi kumkanganya Magufuli asiweze kulipatia ufumbuzi tatizo la uhalali wa utawala uliopo sasa Zanzibar.

Ile kaulimbiu ya mwenyekiti Mao ZeDong, kiongozi wa zamani wa China, kwamba nchi zinataka uhuru, mataifa yanataka ukombozi na watu (umma) wanataka mapinduzi ni kaulimbiu yenye kuisibu Zanzibar ya leo. Na hii ni kwa sababu Zanzibar inayatamani matakwa yote hayo matatu kwa pamoja na kwa wakati mmoja.

Inataka uhuru kwa sababu inahisi inatawaliwa kikoloni. Wenye kutoa hoja hii wanasema kwamba ukoloni ni ukoloni tu hata uvalishwe majoho ya aina gani. Inataka ukombozi kwa sababu muundo wa Muungano umeibana na haiwezi kujiamulia mambo yake yenyewe na watu wake wanataka mapinduzi ya sera ili waweze kujipatia maendeleo.

Hatutii chumvi tukisema kuwa ishara zilizopo Tanzania nzima zinaonyesha kuwa nchi inaelekea kutawaliwa kimabavu. Tayari tumekwishaanza kushuhudia mifano au ishara za hayo.

Mfano mmoja mzuri ni jinsi Tundu Lissu alivyoingizwa kundini na kuchezeshwa sarakasi. Ni wazi kwa kila mwenye macho na akili kuwa Lissu anachukuliwa hatua anazochukuliwa ili kumkomoa yeye binafsi na kuwaonya wengine wataothubutu kutumia haki yao ya kufikiri, kujieleza na kuisaili serikali.

Mfano mwingine ni mvutano baina ya Chama cha Wananchi (CUF) na aliyekuwa mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba. Hapo pia kila mwenye macho anaona wazi jinsi mkono wa watawala ulivyojiingiza katika sakata hilo.

Watawala hawatupi nafasi ya kuwachambua vilivyo wapinzani kwa sababu kila saa wanatushtua kwa vituko vyao na namna wanavyowadhulumu na kuwaonea hao wapinzani. Na sisi tunaotarajiwa tuwe sauti ya wanyonge tunakaa kimya au tunajipendekeza kwa watawala kwa kutamka yanayowaburudisha.

Huu ni wakati wetu wenye kuweza kusema kuzipaza sauti zetu ili tutetee haki na uadilifu katika jamii. Historia haina haraka, haina papara. Kama si leo, kesho. Hatuna njia ya kuikimbia. Lazima itatushika.

Kama si mwakani, miaka kumi ijayo. Kuna siku itatupandisha kizimbani, ituhukumu na kutulaani kwa kimya chetu au upotovu wetu wa kuwaunga mkono watawala wasio waadilifu.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema kwenye toleo lake la tarehe 5 Januari 2017. Mwandishi wake, Ahmed Rajab, anapatikana kwa baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com. 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.