Siku hizi ni kawaida kuwasikia watu – hasa wasomi na wataalamu waliobobea kwenye fani zao hapa Zanzibar  – wakisema “kwa tatizo hili bora pawepo mtaala maalum unaofundishwa maskulini ili kuliondosha’. Swali linakuja: je, tutabadilisha mitaala mingapi na kwa haja gani li kukidhi matatizo ya kijamii yanayoibuka kila leo, ambapo mengi yao ni kutokana na kukosa maadili? Hebu tuyaangalieni maradhi sugu ambayo jamii yetu ya Zanzibar inauguwa kisha tujuwe hasa namna ya kujitibu.Schooling in Zanzibar

Madawa ya kulevya

Tuanze na la maadawa ya kulevya, ambalo sio tu kuwa tatizo sugu lakini pia ni maarufu na mashuhuri sana kiasi cha kwamba linajulikana na kila mtu. Suluhisho lake pia linajulikana na sote, lakini ukweli lazima tuambiane kuwa hatujakuwa tayari kulitatua. Mimi naamini kuwa kama serikali itataka leo, basi kesho hakuna tena tatizo hili.

Na Ali Sultan
Na Ali Sultan

Hapahitajiki mtaala wa skuli wala wa chuo kulimaliza hili.

Tunapajuwa madawa yanapoingilia, tunajuwa sote yanapopitia, tunamujuwa yanamotumiwa, lakini kama serikali na kama jamii hatutaki kuyazuwia. Kisha tunalalamika kuwa watoto wetu wanaangamia, na kumbe tunawaangamiza kwa ugoigogi wetu.

Kuwanajisi watoto wadogo

Ukiwacha la madawa ya kulevya, hapa petu Zanzibar tuna tatizo jengine baya zaidi la ubakaji na kuwanajisi watoto wadogo. Liwati na udhalilishaji mwengine kama huo wa vitoto umekuwa kama sehemu ya khulka ya jamii yetu sasa.

Tatizo limezidi kupindukia hivi sasa kama kwamba Zanzibar haina watu wenye imani ya dini yoyote ile, maana mtu mweye kuamini imani yoyote iwayo, kamwe hawezi kufanya kama haya yanayofanyika hapa. Ofisi za serikali – kutoka za masheha, wakuu wa wilaya na mikoa, mawizara hadi polisi – zimejaa ripoti za matukio hayo, hivyo kila mmoja anajua ukubwa wa tatizo hili sasa.

Hapahitajiki mtaala mpya maskulini kuwafundisha watoto wetu kuwa wanabakwa na wanadhalilishwa, panahitajika sisi kama walinzi wa jamii hii, sisi raia na serikali, kuamua kulikomesha na likatokomea au angalau kupungua.

Lakini hii nchi yetu inaonekana kuwa na hadithi ya samaki, anayeambiwa kuwa pindi akitaka oza huwa anaanzia kichwani. Vyombo vya kutoa haki na kusimamia sheria vinahusika sana kwenye mfano huu. Polisi, mahkama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, hospitali, na mwenginemo mote mumejaa danadana. Mara watakuambia hawana mashine ya kupimia vinasaba (DNA), mara wakuambie uongo kuwa wananchi hawataki kushirikiana na polisi kwa upelelezi, na mara hili ama lile.

Hivi kweli inaingia akilini umnyime mtu haki yake kwa sababu tu eti ‘shahidi au wananchi hawakutaka kushirikiana na wapelelezi? Daktari anayemchunguza muathirika, anajua kabisa kama binti au mvulana huyu amehujumiwa kwa kubakwa, lakini anaweza kubadilisha ushahidi na ukweli wote kwa sababu tu ya rushwa au ukorofi tu.

Tumeganda kwenye kutoa visingizio hivi na vile kuikandamiza au kuichelewesha haki ya mtoto wetu mwenyewe, ambaye keshokutwa ndiye atakayekuwa mtu mzima wa taifa hili. Tunatarajia nini?

Ufisadi serikalini

Zanzibar inakabiliwa pia na tatizo la ufisadi, ingawa kwa bahati mbaya sana hauripotiwi na vyombo vya habari kama ulivyo ufisadi wa Tanzania Bara, labda kwa sababu hatuna vyombo vya habari huru na pia hatuna wanasiasa na wanaharakati machachari wenye kuchimba mambo kama walivyo nao upande wa pili wa Muungano. Lakini ukweli ni kuwa ufisadi wa Zanzibar  ni wa kutisha na unatendeka bila ya wasiwasi wala hofu ya kuchukuliwa hatua.

Mwanzo, kilio kilikuwa ni kutokuwa na mamlaka ya kuzuia rushwa na kuundwa sheria zake. Sasa ipo. Sasa kilio ni kuwa eti sheria haina meno. Kisha linakuja jengine kama lile la kwenye kesi za ubakaji na kuharibu watoto, eti wananchi hawataki kushirikiana na mamlaka hiyo.

Hivi kweli inahitajika ushirikiano gani wakati ambapo ufisadi wetu upo wazi wazi kabisa? Kila mmoja anauona na kwa hakika hapahitajiki hata ushahidi wala utaaalmu huo. Hatutaki kukiri kwamba kama jamii na kama serikali hatuko makini kwenye vita hivi. Na hili halitaki mtaala wala somo maalumu maskulini, linataka utekelezwaji wa maadili ya ndani ambayo tumeyapuuza.

Dawa ni ulinzi wa maadili

Matatizo yanayoikumba jamii yetu hayana haja ya kuundiwa mitaala mipya maskulini kuyatatua. Tayari masomo ambayo wanafundishwa watoto wetu ni mengi na karibuni kwenye kila somo, maadili mema yanapandikizwa humo humo kwa njia moja ama nyengine. Hivyo, Zanzibar haina upungufu wa kuyatambua matatizo haya kupitia mitaala yake, bali upungufu umo kwenye kuyaacha maadili yake ya kijamii, ambayo ndiyo msingi mkubwa wa kuyashinda matatizo haya.

Kama kuna lolote, basi Wazanzibari tujiangalieni ndani yetu, ndani ya nyumba zetu, ndani ya mitaa yetu, ndani ya serikali yetu. Humo ndimo mwenye uozo na chanzo cha haya yanayotuumizia nchi na watoto wetu.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.