Tu, tu tu! Piga huyu, kamata yule! Kazi inaendelea.Kijiji kimejaa vilio vya watoto wachanga, kimetanda khofu na kimesambaa hewa ya sumu ambayo inapopulizwa kuchukuwa masiku kabla haijesha. Kwa siku kadhaa mahali hapa pamekuwa pa mateso mabaya kwa kina mama, wazee na watoto wadogo ambao maisha yao sasa ni ya kukimbia vibanda vyao na kuhamia maporini. Ni kijiji cha Kangagani, kilicho jimbo la Ole, kaskazini mwa kisiwa cha Pemba. Lakini je, nini sababu ya haya? Je, ni mambo mapya kuwahi kutokea kwenye eneo hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

i9calmg

Hapana. Mateso ya sasa si mageni kama usivyo upinzani wa dhati wa wenyeji wa kisiwa hiki kwa karne kadhaa sasa dhidi ya utawala wowote wanaouchukulia kuwa si halali. Nikiwa nachimbukia kwenye kisiwa hiki, haya nimeyashuhudia kwa macho yangu si mara moja wala mbili, ndani ya umri wangu usiofikia nusu karne. Pemba imekuwa muhanga wa athari mbaya za siasa chafu ambazo zimeasisiwa kwenye msingi wa ung’ang’anizi wa madaraka nyuma ya pazia la ushindani. Historia ya matukio ya mauaji, utesaji na unyanyasaji wenye kusukumwa na utashi wa kisiasa ndio blanketi lilokifunika gubigubi kisiwa hiki.

Baada ya kutumia miongo kadhaa ya maisha yangu kwenye nchi za watu, mwaka jana nilipata fursa adimu ya kurudi na kuishi kisiwani Pemba kwa kipindi cha mwaka mmoja. Naiita kuwa ni fursa, maana kimazowea, wenyeji wengi wa kisiwa hiki, Wapemba, wanaoondoka, huwa hawana tabia ya kurudi na kuishi tena kisiwani kwao baada ya kuondoka. Kutokana na kuhama nikiwa na umri mdogo mno kuweza kupambanua mambo, kurudi kwangu sasa kuliniwesha kuona na kujifunza mengi juu ya maisha halisi waishiyo wenyeji, ambao licha ya udhaifu wao wa nguvu za misuli, wana uimara usiomithilika wa kimsimamo. Msimamo wao huo ndilo chimbuko la mateso na madhila yanayowapata kila uchao kutoka kwa watawala.

Nilifika kisiwani Pemba tarehe 25 Ramadhani ya mwaka 2015 nikiwa na familia yangu, ambayo haikuwa imewahikanyaga kwenye ardhi ya kisiwa hicho. Lengo kubwa lilikuwa kuwaonesha watoto wangu kwamba pamoja na wao kuishi kwenye miji ya watu, wanako. Alhamdulillah, uwepo wetu kwenye ardhi yetu kulitufanya tujisikie huru na wenye furaha muda wote kiasi cha kizazi changu kuwaza mahali hapa muda wote. Hadi sasa ambapo wapo nje ya kisiwa hiki, sehemu pekee iliyojaa fikrani mwao ni kisiwa cha Pemba na hawaishi kupataja kwa wema.

Watoto wangu walizaliwa jijini Dar es Salaam katika wakati ambapo jiji hili limekuwa kwa ukuwaji unaotishia maadili ya kifamilia. Walifumbuwa macho na kukuta watu wenye kutembea nusu uchi, lakini Pemba wakakuta kivazi tafauti – cha kujitanda na kujisitiri. Walizowea kwenda kila mahali wakiwa chini ya ulinzi wa baba au mama, lakini hapa walikuwa huru kupita kiasi. Hapa hawakuona mabasi makubwa ya ghorofa, viwanja maalumu kwa michezo yao ya kitoto, au maeneo makubwa yenye viwanda vya kila aina ambavyo ndio jambo la fakhari kwa ile iitwayo serikali ya watu. Pamoja na wao kuishi shamba jirani na bonde maarufu la Makwararani, hawakupata kuona trekta, bali idadi kubwa ya watu ambao walikuwa wakipita chini ya nyumba yao wakiwa na majembe mabegani mwao na huku wengi wao wakiwa na afya dhaifu ambayo ilichangiwa sana na ugumu wa maisha yao.

Uchaguzi wa Oktoba 2015

Wakati nikifika kisiwani Pemba, vuguvugu la uchaguzi wa mwaka 2015 lilikuwa kali sana. Nilishuhudia shamrashamra za kila aina bila ya umwagaji damu kinyume sana na chaguzi za nyuma ya hapo. Kutokana na kazi yangu, nilibahatika kukitembea kisiwa cha Pemba kwa marefu na mapana yake. Niliweza kujionea hali yenye kufanana sana kiimani na kisiasa. Nilichoona mahali hapa hakikuwa tofauti na kile nilichokuwa nikikisikia nikiwa nje yake.

Harakati ziliendelea kupamba moto kadri siku ya uchaguzi ilivyozidi kukaribia. Madoido na mashamushamu yalishika kasi kiasi huku kukiwa na dalili za wazi za kukosekana kwa mbabe wa kupambana na nguvu ya upinzani ambao uliziteka nyoyo ya wakaazi wengi wenyeji wa kisiwa hiki. Hapa chama tawala kilikosa mvuto kiasi cha wafuasi wake kushindwa kujifakharisha na kujidai kwa vazi la chama hicho. Wengi miongoni mwa wafuasi wa chama hicho walikuwa wakivuwa mavazi ya chama chao mara wanapoteremka magari kutoka kwenye kampeni kukwepa fedheha ya kuzomewa na wapinzani wao wanaporejea makwao.

Hatimaye siku ilifika na kile kilichokusudiwa kikafanyika kwa amani kupita uchaguzi mwingine wowote uliopita kwenye mfumo huu wa vyama vingi. Hata hivyo, kilicho tokea baada ya hapo sina sababu kukielezea kwani kimeerejesha nyuma Zanzibar ambako ilishaondoka.

Kushindwa kwetu kuheshimu masuala yaliyokubaliwa kwa misingi ya kisheria na kikatiba, ndilo chimbuko la vurugu zisizokwisha visiwani Zanzibar. Tumechaguwa kulazimisha na kuendesha mambo kwa mtutu wa bunduki bila kujali athari ambazo zinajengeka kwenye vichwa vya watu. Watawala wanaamini matumizi ya nguvu ndio njia pekee ya kuzima harakati na nguvu za upinzani.

Hapana, hilo si sahihi. Hilo si sawa bali ni njia iliyotokana na udhaifu na yenye kuamsha zaidi ari ya mapambano, ambayo hatimaye mshindi ni umma. Nalisema hili nikiamini kwamba hakuna mahali historia inaonesha ushindi kwa mtawala aliyekataliwa na watu wake.

Matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu visiwani Zanzibar ni mengi na hayatowi ishara na mustakbali mwema kwa Zanzibar na Wazanzibari. Hii ni fedheha kubwa kwa jamii yenye kuzungumza lugha moja na kuamini dini moja. Ni ubaya ulioje mtu kupingana na ukweli kwa risasi za moto au mabomu ya machozi. Kulikuwa na haja gani kufika huko kwa kuporomowa msingi muhimu wa kuendesha nchi kwa maridhiano? Kwa nini tumeshindwa kutanguliza mbele maslahi ya nchi na kutumbukiza kwenye ulevi wa madaraka, kiasi cha kuona matumizi ya nguvu ndio suluhisho? Hii sio sahihi na ni dhulma yenye kuasisi misingi mibaya.

Matukio ya kupangwa na dola

Miongoni mwa mambo yenye kunihuzunisha sana moyo wangu ni pamoja na matukio ya kupangwa ili ipatikane sababu ya kutia watu kwenye madhila. Matukio ya aina hii ndio yaliyopelekea nipokwe kibali cha kufanya kazi zangu kisiwani Pemba. Nilisimama kuhoji juu ya ukweli wa matukio yale nikijuwa madhara yake. Nilijuwa madhara ya kuhoji mambo ambayo yanafumbiwa macho na dola. Nilijuwa kwamba mustakbali wa kazi yangu na hata maisha yangu vingekuwa tabuni kutokana na kufichuwa vilivyofanywa siri kwa lengo la kukandamiza watu wasiweze kuhoji na wasiwe na sauti kwa yote wasiyokubaliana nayo.

Matukio ya hujuma za kupangwa kisiwani Pemba yana chimbuko na asili yake kwenye chama tawala. Wakati ikisemwa hakuna aliye juu ya sheria, wanaopita usiku wakihujumu raia hawafikishwi kwenye vyombo vya kisheria. Suala la ulinzi na usalama ni dhamana ya jeshi la polisi na tulitarajia jeshi hilo lingetueleza ni hatuwa gani limechukuwa kukomesha hali hii Unguja na Pemba. Lakini kinyume chake tumekuwa tukishuhudia udhalilishaji na mateso dhidi ya wazee wetu wanyonge vikizidishwa. Tukio la hivi makaribuni alilofanyiwa mzee mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 Taveta, Unguja, si jambo la kawaida kwa wenye kutafakari. Damu ya wazee kama wale ambao tulipaswa kuwalinda pamoja na watoto wadogo vinaweza kuwa laana ya kuisambaratisha nchi.

Kuna haja gani kukimbilia kuumiza watu kwa mambo madogo madogo ambayo yanahitaji zaidi matumizi ya busara? Kuna haja gani kudekeza watu ambao hujihujumu wenyewe kwa lengo la kukomowa wengine wasiokubaliana nao? Kweli tukio la la kule Kangagani ambako inadaiwa msikiti kuchomwa na waumini kutokana na Imamu wa msikiti huo kumtaja Dk. Ali Mohamed Shein kwenye hotuba ya Sala ya Ijumaa linaingia akilini? Hapana, tunapelekeshwa kutokana na uvivu wetu wa kutafakari.

Kama kuna mahali ambapo panaheshimiwa sana na jamii ya Kipemba ni eneo liitwalo Msikiti. Hii si jamii ya watu wa ovyo kama picha ambayo watu wajinga wanajaribu kuitengeneza. Upo uwezekano wa waumini kuhama msikiti iwapo kama imamu wa msikiti huo anaingiza ukada kwenye masuala ya ibada. Upo uwezekano wa waumini kususa kumsalia maiti iwapo imamu anayeswalisha ni kada wa chama tawala. Upo uwezekano wa mtu kususiwa maiti iwapo atamtanguliza mbele kada wa chama tawala kuwa kiongozi kwenye mazishi. Upo uwezekano wa maiti mmoja kuwekewa matanga mawili ndani ya uwanja mmoja, yaani CUF kwao na CCM kwao. Lakini je, kama tulishindwa kusimamia misingi ya haki, tulitarajia mafungamano mazuri miongoni mwetu?

Umuhimu wa Tume ya Kitaalamu

Mara kadhaa nimekuwa nikiliandika hili na leo narudia tena. Kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuunda tume ya kitaalamu ambayo itashirikisha watu mashuhuri na wenye kuheshimika mbele ya jamii ili ijuilikane ni nani mfadhili wa hujuma hizi ambazo zimejaa ishara ya kupangwa ili watu wenye mrengo fulani wa kisiasa watiwe adabu. Iundwe tume ikutane na wanaodaiwa kuhujumiwa. Naamini jibu watalipata kirahisi na ukweli wa matukio haya utajuulikana.

Tufahamu kwamba jamii imechoshwa na ujinga kama huu wa msikiti kuchomwa kisha ikaunguwa kanzu na mabusati tu, tena usiku mkubwa au shamba lenye walinzi pamoja na mbwa, kuvamiwa usiku na miti ikakatwa. Huku ni kufanyana watoto na kibaya tukishuhudia wazee na watoto wakiteseka kwa mabomu ya machozi, vipigo na udhalilishwaji mwingine.

Pamoja na ubaya wake, bado kwa Mpemba msikiti ni mahali patakatifu ambapo anajuwa umuhimu wake. Naamini wale waliozaa wazo la kuchoma kanzu na mabusati ya msikiti,  wana lao moyoni. Nimetumia neno “wale” nikiamini kwamba kuna wafinyazi wa hili na wala si mtu mmoja. Lipo lile kundi la chama kile ambalo limejipajika jina la “kamati ya maafa” huku kazi yake kubwa ikiwa kupanga na kuandaa hujuma kwa lengo la kutengeneza picha itakayoonesha wafuasi wa chama fulani ndio wanaohujumu mashamba na majengo ya wafuasi wa chama kile!

Huu si mchezo mpya kwa wenye kumbukumbu. Umepata kuchezwa sana ukijumuisha matukio ya kutia vinyesi kwenye visima pamoja na kupakaza kwenye kuta za maskuli. Ni mchezo ambao umekuwa ukijirudia sana hasa kisiwani Pemba. Ni mchezo ambao kuna siku mratibu mmoja ilibidi aumbuke mbele ya wanahabari baada ya muhujumiwa mmoja kuropoka kinyume na maelekezo ya kamati. Tukio hili la kuropoka lilipelekea kamati kuwataka waandishi wasiandike maelezo ya mama yule na, kwa vile wote walikuwa kutoka vyombo vya serikali, walilazimika kufumba midomo yao kulinda mkate wao.

Narudia tena, kwamba pamoja na ukorofi wa Wazanzibari, bado hawajafikia kiwango cha kuhujumu miskiti kama picha hii inavyotengenezwa. Lakini ili kuujuwa ukweli wa hili, polisi wasipoteze mabomu yao, bali wamkamate imamu wamuhoji kisayansi na sio kikereketwa au kufunika kombe.

Naamini hapo – kama watataka – wataiona kweli iliyochanganyika na fedheha, kwani wale wanaolia kupigwa, ni wanafiki wanaojipiga wenyewe.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii ni Ahmad Abu Faris. Anapatikana kwa simu nambari +255 774 581 264.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.