Mwandishi Harith Ghassani anakiita kitabu chake Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru, yumkini akimaanisha kile kilichotokea tarehe 10 Disemba 1963 kilikuwa kiini macho cha aina yake ambapo Zanzibar ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Muingereza na baadaye kujikuta baada ya mwezi mmoja ikiingia katika Mpainduzi ambayo baadaye nayo, ndani ya siku 100 tu, yakafuatiwa na kuasisiwa kwa Muungano wa tarehe 26 Aprili 1964. zanzibar_uhuru_63_scaled

Baada ya matukio haya matatu: Uhuru wa tarehe 10 Disemba 1963, Mapinduzi wa tarehe 12 Januari 1964 na Muungano wa tarehe 26 Aprili 1964, Zanzibar ilipotea katika ramani ya dunia.

Lengo la makala yangu sio kuelezea matukio hayo na athari zake za kisiasa na kijamii kwa Zanzibar. La hasha! Ninachotaka kutanabahisha hapa ni jinsi gani Zanzibar ilivyoshindwa kusimama katika ramani ya dunia na kupoteza ushawishi wake iliokuwa nayo kutokana na kupuuzwa kwa historia yake halisi.

Na Mohamed Aliy
Na Mohamed Aliy

Tarehe 10 Disemba 1963 ni siku ambayo Zanzibar ilichukua nafasi yake kama taifa kwa kule kukabidhiwa uhuru wake bila ya kumwaga damu na kuwa na katiba ambayo ilikuwa na ubora pamoja na kuhakikisha ukuwaji wa demokrasia na haki za kibinaadamu kwa kule kutambua kwake rasmi uwepo wa vyama vya upinzani sambamba na serikali ya umoja wa kitaifa.

Wazanzibari wamekosa nini?

Hapo linaweza kuja suala: Sasa Wazanzibari wamekosa nini hata wakashindwa kuiadhimisha siku hii adhimu kwenye historia yao?

Kama ilivyokuwa kwa nchi nyengine za Kiafrika, Tanganyika na Zanzibar zilipokea uhuru wao kwa njia za kikatiba ambapo kwa Tanganyika tarehe 9 Disemba 1961 Waingereza walikubali kuiacha huru lakini kwa sharti kuwa mkuu wa nchi ataendelea kuwa Malkia wa Uingereza na Mwalimu Julius Nyerere kubakia kuwa Waziri Mkuu.

Zanzibar pia ilipitia mkondo huo huo, kwani tarehe 10 Disemba 1963 pale katika Jumba la Mnazi Mmoja pakiitwa Victoria Garden palifurika na hatimyae Zanzibar ikakabidhiwa Uhuru wake chini ya Waziri Mkuu Bwana Mohamed Shamte bin Hamad ambapo pia katiba hiyo ilimtambua Sultani kama kiongozi wa heshima (ceremonial) huku madaraka yote ya kuongoza nchi yakiwa chini ya Waziri Mkuu.

Hapo linaweza kuja suala kwa nini Uhuru wa Zanzibar uitwe wa bandia na ule wa Tanganyika usherehekewe kwa mizinga 21 na gwaride kila mwaka? Je, Wazanzibari tunakosa nini? Je, Wazanzibari tumekosa hamu ya kuitambua na kuithamini historia adhimu ya nchi yetu?

Tafauti na Tanganyika, Zanzibar ilipitia mikondo tofauti katika harakati za kudai uhuru, ambapo chuki na hasama pamoja na vitimbi vya kila namna vilitokea na hilo ni miongoni mwa sababu za kutokea kwa kile kinachoitwa Mapinduzi ya 1964, baada ya walioshindwa kwenye uchaguzi, Chama cha Afro-Shiraz, kuamini kuwa walikuwa wao ndio wenye haki ya kutawala peke yao.

Sitaki kuzungumzia chochote kuhusiana na undani wa Mapinduzi yenyewe, lakini jambo la msingi ni kuwa yalibadilisha upepo wote wa siasa na historia ya Zanzibar na hata ukanda wote wa Afrika ya Mashariki.

Bila ya shaka nchi nyingi zinazopitia katika mkondo wa mapinduzi hukumbwa na chembe chembe ya udikteta, na Zanzibar nayo iliselelea huko. Serikali ya baada ya Mapinduzi iliharamisha kabisa Uhuru wa Disemba 10. Kila aliyedhaniwa kuwa ni mpinzani wa Afro-Shiraz alikiona cha mtema kuni. Vifungo mateso na kila aina ya viteweji viliwakumba Wazanzibari hao.

Ndio maana, tafauti na jirani zetu wa Tangayika ambao siku ya uhuru wao huiadhimisha na kuitikuza kwa kiwango kinachostahili, kwa Zanzibar tarehe 10 Disemba sio tu imesahaulishwa lakini pia imefanywa isionekane umuhimu wake na hata hadithi zake hazisikiki popote pale.

Yumkini ukisikiliza historia ya Zanzibar hakutajwi chochote isipokuwa Mapinduzi ya Zanzibar, utadhani kuwa huko nyuma hakukuwa na lolote lililotokea kabla ya hayo Mapinduzi yenyewe kufanyika.

Uhuru wa Disemba 10 na Mzanzibari wa sasa

Mimi ni kijana wa Kizanzibari niliyezaliwa miaka mingi baada ya Uhuru wa Disemba 10 na Mapinduzi ya Januari 12, lakini bado – licha ya umri wangu mdogo nilionao – naona kuna haja kubwa ya kuifundisha historia yetu kama ilivyo, bila kuweka matakwa ya kisiasa kama ambavyo imekuwa ikifanywa.

Kuifundisha huko historia kunaweza kuchukua sura mpya ikiwa Wazanzibari watawacha tafauti zao na kufungua ukurasa mpya kwa kuiadhimisha siku ya tarehe 10 Disemba na kuitambua rasmi kama siku ya kitaifa, kwani ni tukio ambalo tunapaswa kujivunia na kulisherehekea kwa kila namna kama taifa.

Kuishereheka tarehe 10 Disemba hakuondoi ukweli kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea, ila kunalipa mawanda zaidi tukio hilo kwa kuwaleta pamoja Wazanzibari kwa kuweza kutambua wapi nchi yao imetoka na wapi inaelekea.

Kuisherehekea na kuiadhimisha siku ya Uhuru wa Zanzibar, ambayo wengine wanauita “hhuru wa bandia”, ni kutoa picha kwa ulimwengu kuwa Wazanzibari wanaijua vizuri historia yao na wanajua wapi nchi yao inapaswa kuelekea.

Kwa hivyo, kuna haja kwa Wazanzibari wa rika zote kuiona haja ya kuisoma historia ya nchi yao kwani kufanya hivyo kunaweza kuyaleta pamoja makundi tofauti ndani yao ambayo sasa yamegawanyika kwa misingi ya matukio ya historia na itikadi zao za kisiasa.

Sisi tunaojitambulisha na Uzanzibari wetu hatuna budi kuitambua historia yetu kwani kuna historia ndiyo roho ya taifa lolote lile duniani. Taifa lisiloijuwa na kuienzi historia yake, basi ni taifa mfu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.