ASALAAM alaykum wa RahmatuLlah wa Barakatuhu. Nina mawili matatu ninayotaka kusema kabla ya kuiingilia mada yetu. Kwanza, nawashukuruni kujumuika nasi kumkumbuka mwana wa Zanzibar, ambaye licha ya udhaifu wake na pengine makosa ya hapa na pale, ni mmoja wa vigogo wa siasa za Zanzibar. Na ninamshukuru zaidi ndugu yetu Sheikh Muhammad Yusuf na taasisi yake kwa kutupatia nafasi hii ya “kumfufua” Hanga.

Waliokaa kutoka kushoto: Marehemu Abdullah Kassim Hanga na Abeid Karume,
Waliokaa kutoka kushoto: Marehemu Abdullah Kassim Hanga na Abeid Karume,

Pili, nawaomba radhi kwamba siko nanyi tukaweza kumzungumza pamoja Al Marhum Sheikh Abdulla Kassim Hanga. Madhumuni ya mhadhara kama huu yawe si kusikiliza tu mtu kama Hanga amesoma wapi, amefanya nini au amekula mandazi kwa mbazi au kunde, lakini yaweze pia kutupa fursa ya kujifunza mawili matatu kutokana na maisha yake.

Yupo wa kumlaumu kwanini sipo hapa nanyi. Na si mwengine ila Muhammad Yusuf kwa ubakhili wake wa kutoniwezesha kufika.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Mwisho nataka kuwajulisha kwamba mengi nitayoyasema leo nimeyadokoa kutoka kwenye muswada wangu wa maneno yanayokaribia 20,000 (elfu ishirini), muswada ambao bado haujakamilika kuchapishwa na uitwao “The Killing of Hanga” (Mauaji ya Hanga).

Bado muswada huu ungali “work in progress” na kwa hivyo, kutadhihirika mapengo ya hapa na pale katika nitayoyasema leo. Ni matumaini yangu kwamba kutatokea hapa wataoweza kuyajaza mapengo hayo.

Ama baad,

Wiki iliyopita nilihudhuria hafla moja jijini London ambapo mshairi mmoja binti wa Kipalestina, Jehan Bseiso, akisoma baadhi ya mashairi yake.

Kuna kipande cha mshororo wa shairi lake moja kilichonikaa moyoni tangu nikisikie. Chasema: “Hata waliokufa nao huzeeka…”

Lau angelikuwa hai, Abdulla Kassim Hanga leo angelikuwa “Mzee” wa miaka 84. Alipouliwa 1969 alikuwa kijana wa miaka 37 tu.

Sijui kuna siri gani lakini wanaharakati wengi walio vipenzi vya umma huiaga dunia wakiwa katika rika hilo. Frantz Fanon, aliyezaliwa kisiwani Martinique na aliyeyakumbatia Mapinduzi ya Algeria na akawa Mualgeria, alifariki akiwa na miaka 36; kadhalika, Patrice Lumumba wa Congo, naye alikuwa na umri huohuo wa miaka 36; Walter Rodney, mwanahistoria kutoka Guyana aliyewahi kusomesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliuliwa akiwa na umri wa miaka 38. Malcolm X naye aliuliwa miezi mitatu kabla hajatimia miaka 40.

Hanga wa kihistoria hakuwa na bahati. Alionewa kwanza na wenzake alioshirikiana nao kuyaandaa na kuyaongoza mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Wao ndio waliomdhulumu roho yake. Akaonewa tena na historia iliyomnyanyua halafu ikamtupilia mbali, asisikike tena.

Hii leo Hanga, aliyekuwa akivuma zama za kupigania uhuru wa Zanzibar, amesahaulika.

Nimesema “amesahaulika” ingawa sidhani kama “amesahaulika” ni tamko sawa. Hanga hakusahaulika. Amesahauliwa kwa kusudi. Watawala hawataki akumbukwe. Nasema hivi kwa sababu kumkumbuka Hanga ni kuufichua uhaini aliofanyiwa na wapinduzi wenzake pamoja na Mwalimu Julius Nyerere, aliyemleta machinjoni Zanzibar ya siku zile.

Kwa kadhia hiyo tu Nyerere hawezi kusafishika. Na nathubtu kusema kwamba itamyima “utakatifu” (sainthood) ambao wapambe wake wanampigania apewe huko Vatikani, kwenye Makao ya Papa.

Angelikuwa Hanga ameishi nchi nyingine, hii leo tungeshuhudia mengi yakiitwa kwa jina lake: majengo, skuli, viwanja vya mpira, barabara au taasisi mbalimbali. Lakini bahati yake ilikuwa kuzaliwa nchi isiyowathamini watoto wake.

NIMKUMBUKAVYO HANGA UTOTONI MWANGU

Ingawa siasa zikimwenda katika damu yake tangu alipokuwa mwanafunzi Hanga aliangukia kwanza kuwa mwalimu kabla hajawa rasmi mwanasiasa. Alikuwa mwalimu aliyekuwa akipendwa na wanafunzi wake wa kila kabila lakini umaarufu wake aliupata katika medani ya kisiasa, hasa katika siasa za usoshalisti wa kimataifa na katika mapinduzi ya Zanzibar.

Mimi binafsi nilianza kumjua alipokuwa mwalimu na nilipokuwa nasoma skuli ya “primary” ya Darajani katika miaka ya kati ya 1950. Wakati huo Hanga alikuwa anamaliza masomo yake ya ualimu katika Seyyid Khalifa Teachers’ Training College, Beit-el-Ras.

Aliletwa Darajani kufanya mazoezi ya kusomesha (teaching practice). Kwa muda mfupi alinisomesha somo la Kiingereza. Alipohitimu masomo yake ya ualimu, akarudishwa skuli ya Darajani ambako pamoja na kusomesha alikuwa pia akisimamia mambo ya riyadha na kuogolea. Alikuwa “sports Master”.

Miaka hiyo ya 1950 mara kwa mara nikikumbana naye jioni nilipokuwa nikitoka kwetu Vuga kwenda Baraste Kipande kumzuru bibi yangu. Nyumba ya bibi yangu ilikuwa karibu sana na nyumba ya dada yake Hanga. Saa hizo za jioni Hanga akipendelea kwenda Jogoo Club kucheza bao au dhumna.

Jogoo Club ilikuwa kama barza ya Mahizbu, wafuasi wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP). Hanga alikuwa Afro, mfuasi wa Afro-Shirazi Party (ASP), chama kilichokuwa kikipingana vikali na kile cha Hizbu. Jogoo ndiyo iliyokuwa nembo ya chama cha Hizbu. Juu ya yote hayo, Hanga hakuona taabu yoyote kwenda kupiga soga Jogoo Club.

Hanga wa siku hizo alikuwa mtu wa mbwembwe na mikogo. Alikuwa na mwendo wa kuyumbayumba, akipiga hatua huku akitikisa mabega yake. Mtu mwengine angelikuwa anakwenda kama yeye angeonekana kinyago cha kuchekwa. Lakini huo mwendo wa mbwembwe ulimsibu Hanga kwa urefu wake na umbo lake. Ilikuwa kama mwendo huo aliumbiwa nao.

Hanga alifanikiwa kuitia mikogo yake bila ya kuonesha kama akijidai. Na hakuwa mtu wa kujidai wala mwenye majivuno.

Wala Hanga hakuwa na watu waliokuwa wakimfuata na kumuigia lakini walikuwepo watu waliokuwa wakimhusudu kwa namna alivyokuwa akiipenda lugha ya Kiingereza. Walikuwepo wengine waliokuwa wakimdhihaki kwa alivyokuwa akiupenda uzungu; si bure kwamba kuna baadhi ya watu waliokuwa wakimwita “Ba Zungu”.

Alikumbwa na ule ugonjwa aliouelezea Frantz Fanon kwenye kitabu chake Black Skin, White Mask, ugonjwa uliokuwa ukiwafanya Waafrika wadanganyike kimawazo kwamba wakifikia kiwango fulani cha elimu watakubalika kwa watawala na watapewa dhamana katika dola.

Viongozi wengi wa Kiafrika waliokuwa na hamu ya kuwaiga wakoloni Wakizungu waliambukizwa ugonjwa huo, hata kiongozi mfano wa Kwame Nkrumah katika ujana wake. Na walikuwa nao ugonjwa huo mpaka walipotanabahi kwamba nawasome vipi lakini wakoloni Wakizungu hawatowakubali kuwa ni sawa nao. Daima wataendelea kuwa chini yao.

Hanga aliishi na ugonjwa huo mpaka alipoanza kuamka kisiasa. Mwamko wake, hata hivyo, haukuwa wa mara moja. Aliamka pole pole. Akaanza kufuata itikadi nyingine.

Alipoiangalia jamii ya Zanzibar aliiona jamii iliyogawanyika. Licha ya kuwa na dini moja na utamaduni unaoweza kusema kuwa ulikuwa mmoja kwa kiwango kikubwa, hata hivyo kila jamii (kabila) ilikuwa na ya kivyake. Nadhani hichi ndicho alichokiona mwandishi wetu adhimu wa riwaya, Abdulrazak Gurnah.

Katika riwaya yake inayosifika sana na iitwayo Admiring Silence, Gurnah ameandika kwamba miaka hiyo kila kabila la Zanzibar lilikuwa likiishi katika “historical ghettoes” zake. Kila kabila lilikuwa limefungika na ya kwake. Ndiyo tulikuwa na utamaduni mmoja lakini kila kabila lilikuwa na mkondo wake wa kitamaduni uliokuwa umefungika ndani ya kabila hilo.

Lililozidi kumshughulisha Hanga, aliyekua anaanza kuamka kisiasa, ni imani yake kwamba mfumo wa kikabila uliokuwepo ulilinufaisha tabaka fulani la wakaazi wa Zanzibar na kwamba mtu kama yeye, aliyejiona kuwa ni “Mwafrika halisi”, akiangaliwa vingine. Hanga wa ujanani na aliyeanza kuamka kisiasa hakuamini kwamba Wazanzibari walikuwa wakiishi katika jamii moja iliyojaa furaha tupu.

Wacha nisimumunye maneno, Hanga akiamini kwa dhati kwamba wale waitwao “Waarabu” hapa Zanzibar au wale wanaojinasibisha na “Uarabu” ndio waliokua na ulwa, ndio waliokuwa juu katika jamii na Waafrika ndio waliokuwa chini.

Najua kuna wengi wanaoipinga dhana hii na kuna hoja nyingi ambazo mtu anaweza kuzitoa kuonesha kwamba dhana hiyo ni potovu. Juu ya hayo, hatuwezi kuipuuza kwasababu hisia za waliokuwa wakiiamini dhana hiyo ndizo zilizochangia pakazuka mapinduzi na chuki zinazoenezwa na watawala ingawa si na wananchi.

Isitoshe, kwa sababu ya kuwepo kwa hisia hizo Sheikh Abeid Karume, kiongozi wa ASP, aliweza kuwashawishi zaidi ya nusu ya wakaazi wa Zanzibar kwamba “ukabila” na “upendeleo wa kikabila” yalikuwa mambo ya hakika. Walimuunga mkono kwa sababu walimuona kuwa yeye ndiye sura ya uananchi wa Kiafrika. Wapinzani wake, kwa upande mwingine, walikuwa na hakika kwamba alikuwa sura ya uovu.

Hivyo ndivyo jamii ya Zanzibar ilivyokuwa imegawika siku hizo. Kuiangalia Zanzibar hivyo ni kuitathmini kijuujuu kwa sababu si Waarabu wote waliokuwa katika tabaka la mabwanyenye (bourgeois class), wengi wakiishi maisha ya chini sawa na hao waliokuwa wakiitwa “Waafrika”. Lakini tusiyaingilie hayo kwa sasa asije Hanga akatupotea.

HANGA NA SIASA ZA KIKABILA

Hanga wa ujanani mwake alikuwa akizifuata siasa za kikabila zilizokuwa zikihubiriwa na chama chake cha ASP, kilichokuwa kikiupinga, kile chama hicho ilichokiita “ubwana wa Waarabu”. Hanga akavuka mpaka. Akaanza kuupinga na ufalme, usultani. Kulikuwa gazeti lililokuwa likiitwa MWIBA, ufupisho wa “More Work Illustrate Better Africa”, lililokuwa likimilikiwa na kuhaririwa na Marehemu Jamal Ramadhan Nasib.

Gazeti hilo liliporipoti matamshi ya Hanga ya kuupinga usultani, Jamal Nasib alilazimishwa kumuomba radhi sultani kupitia redio ya Sauti ya Unguja na pia kwenye gazeti la serikali lililokuwa likiitwa Maarifa.

Hanga aliupinga usultani licha ya kwamba dadake, yule aliyekuwa akiishi Baraste Kipande alikuwa mke wa pili wa jamaa wa aila ya Kifalme, Seyyid Farid. Huyu alikuwa mwana wa Sultan Seyyid Ali bin Hamoud, ambaye 1911 baada ya kwenda London kuhudhuria sherehe ya kutawazwa Mfalme George V (wa tano) alilazimishwa na Waingereza ajiuzulu. Ufalme akapewa shemeji yake Seyyid Khalifa bin Haroub, babu yake Sayyid Jamshid bin Abdulla, mfalme wa mwisho wa Zanzibar.

Mama yake Seyyid Ali alikuwa Mnyasa. Alipokuwa mdogo alipelekwa Uingereza kusoma katika skuli ya Harrow na alikuwa mfalme pekee wa Zanzibar ambaye baadhi ya nyakati akiacha kuvaa majokho na akipiga suti na tai. Baada ya kupokonywa ufalme aliishi Paris, Ufaransa, ambako alifariki Desemba 20, 1918.

Kama nilivyokwishasema mwanawe, Seyyid Farid, alikuwa shemeji yake Hanga. Alizaa watoto kadhaa na dadake Hanga.

Kwa vile akiupenda usomi na akizipenda siasa Hanga aliwavutia viongozi wa jumuiya ya African Association ambayo ilikuwa dhaifu. Jumuiya hiyo iliasisiwa 1934 na wafanyakazi Wakiafrika, wengi wao wakiwa wahamiaji Wakikristo kutoka Tanganyika na hadi Malawi.

Haikuchukua muda Hanga akawa kipenzi cha jumuiya hiyo kabla haijaungana na jumuiya ya Washirazi, Shirazi Association, kuunda chama cha siasa cha Afro-Shirazi Party (ASP). Jumuiya hiyo ilimpenda Hanga kwa sababu alikuwa na ujasiri wa kuyatamka yale ambayo yakiogopwa kutamkwa na viongozi wa Jumuiya hiyo waliokuwa wamesoma na waliokuwa wakiogopa wasivitie vitumbua vyao mchanga kwa vile walikuwa watumishi wa serikali ya kikoloni.

Miongoni mwa viongozi hao walikuwa Maalim Aboud Jumbe, aliyekuwa mwalimu wa skuli ya serikali ya sekondari , na Sheikh Ali Khamis, mtumishi wa serikali aliyesomea Uingereza. Watu kama hao waliliacha jukumu lao la kihistoria la kuwatetea Waafrika wenzao.

HANGA AELEKEA ULAYA

Nadhani ilikuwa 1957 baada ya kuasisiwa ASP Hanga alipoondoka Zanzibar kwenda London akifadhiliwa na chama hicho. Marafiki zake wanakumbuka kwamba alikodi chumba katika nyumba ya bibi mmoja wa Kizungu katika mtaa wa Clapham Common, kusini mwa London. Wanakumbuka pia kwamba chumba chake kilikuwa nadhifu sana.

Alipofika alikuwa akisomea masomo ya GCE “A” levels katika skuli ya Westminster College ili aweze kuingia chuo kikuu. Ilisadifu kwamba mwishoni mwishoni mwa 1964 nami nilijiunga na skuli hiyohiyo, iliyokuwa eneo la Westminster karibu na Victoria, kwa madhumuni hayo hayo.

Hanga alikuwa na hamu akimaliza ajiunge na London School of Economics And Political Science (LSE), ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha London. Huko ndiko alikosoma Jomo Kenyatta, Rais wa mwanzo wa Kenya, na ndipo aliposoma Salim Rashid, katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar.

Bado sikujua kwa nini lakini mambo yalimwendea vingine Hanga. Alipewa msaada wa masomo (scholarship), na akaukubali, wa kwenda Moscow kusomea mambo ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Lumumba.

Kuna jambo jengine lililomtokea London na bado sikuupata undani wake wa namna lililovyoanza. Na jambo lenyewe ni usuhuba mkubwa aliokuwa nao na Oscar Kambona, mwanafunzi wa sheria aliyetokea Tanganyika. Kambona hakumaliza masomo yake kwa sababu Nyerere alimwita arudi Tanganyika kwenda kusaidia harakati za kupigania uhuru.

Hadithi ya Kambona ni ndefu na hapa sipo mahala pake. Naitoshe tu tukikumbusha kwamba Hanga alikuwa na usuhuba naye na kwamba usuhuba huo ulichangia baadaye kuyaponza maisha yake.

HANGA AKIWA MOSCOW

Huko Moscow, Hanga alimuona, akampenda na hatimaye akamuoa mwanamke wa Kirussi, Lily Golden. Lily alikuwa Mrussi mweusi. Babake alikuwa Mmarekani mweusi, John Oliver Golden na mamake, Bertha Bialek, alikuwa Yahudi aliyezaliwa Poland.

Baba mkwe wa Hanga alikuwa mtaalamu wa kilimo na Mkomunisti maarufu kutoka Mississippi. Alikuwa rafiki wa wanaharakati wengine Wamarekani weusi waliokuwa pia maarufu. Miongoni mwao walikuwa mwimbaji Paul Robeson, mshairi wa Harlem na mwandishi Langston Hughes, mshairi mwengine na mwandishi wa riwaya Claude McKay na kiongozi wa wafanyakazi George Padmore.

Nina mengi kuhusu wakwe zake Hanga ambao wote wawili walikuwa Wakomunisti. Hapa nitayafupisha maelezo yao. Kwa ufupi, walihamia Urussi katika miaka ya 1930 ambako binti yao Lily alizaliwa.

Hanga hakumuona babamkwe wake kwa sababu alifariki 1940. Lakini alimuona mama mkwe wake aliyefariki 1985. Binti yao Lily alisomea historia katika Chuo Kikuu cha Moscow State University na baadaye akawa profesa katika Taasisi ya Mitaala ya Kiafrika, Moscow. Aliwahi pia kuuwakilisha Muungano wa Sovieti katika mashindano ya mchezo wa tenis. Alifariki Desemba 2010 akiwa na miaka 76.

Mara ya mwanzo Hanga kumuona Lily ilikuwa 1957 alipohudhuria Tamasha la Kimataifa la Vijana, jijini Moscow. Kuna Wazanzibari wenzake waliomuona mwanzo na wakamhadithia Hanga. Sikuwajua walikuwa akina nani ingawa nadhani Ali Sultan Issa alihudhuria tamasha hilo.

Siku moja saa za usiku 1958 Hanga alipiga hodi kwa Lily, akamlilia hali akitaka kumuoa. Alikuwa ameolewa kwa muda wa miezi michache tu na mpiga piano na mumewe akafa katika ajali ya gari. Huyo mumewe alikua mtoto wa watu, wa familia ya wasomi Wakirussi waliokuwa wakiheshimika.

Lily mwanzo akisitasita kumkubali Hanga lakini mamake akimshikilia amkubali. Ilipita miaka miwili kabla ya Lily kukubali kuolewa na Hanga na ndoa yao ilifungwa 1960. Walijaaliwa binti mmoja, Yelena Khanga.

Nilikutana na Yelena alipopita London akiwa njiani kuja Zanzibar kuwatafuta jamaa zake. Nililetewa na mjombake Hanga, Marehemu Mohamed Ibrahim aliyekuwa baharia aliyeishi London kwa maka mingi. Sadfa nyingine ni kwamba huyu bwana ndiye aliyenipokea London 1964 na akanikaribisha kukaa kwake. Alipomleta Yelena ofisini kwangu akitaka nikamjulishe na Abdulrahman Babu, ambaye siku hizo akiishi London. Ukimuangalia Yelena ni kama Hanga aliyejizaa, sema yeye ni mwanamke.

Yelena anatafahari kuwa yeye ni Mrusi mweusi na Mmarekani. Ni maarufu Urussi kwa vile alikuwa akiendesha vipindi vya televisheni vyenye kuvutia. Yeye na mama yake wote wameandika vitabu. Chake kinaitwa Soul to Soul na cha mama yake kinaitwa My Long Journey Home. Alikiandika baada ya kuhamia Marekani 1988. Mwaka 1993 akisomesha Chuo Kikuu cha Chicago State University.

Masomo ya Hanga Moscow yalikuwa ya muda wa miaka mitano lakini Lily ameandika kwamba alimaliza masomo hayo kwa muda wa mwaka tu. Vipi Hanga aliweza kufanya hivyo sijui.

Hata hivyo, baada ya kumaliza masomo alibaki kwa muda Moscow na akisafirisafiri kwenda Zanzibar na London ambako akishiriki katika mazungumzo kuhusu katiba mpya ya kuipatia uhuru Zanzibar.

Alipokuwa Moscow, Hanga alikuwa akidekezwa na kuengwaengwa na Warussi. Maisha yake na mkewe yalikuwa ya raha. Walipewa fleti nzuri iliyokuwa na vitu vya anasa. Ilikuwa fleti waliyowekewa waheshimiwa kutoka nchi za nje. Lily amesema kwamba alikuwa akipata mambo asiyowahi kuyapata kabla. Walikuwa na watumishi waliokuwa wakiwahudumia. Wakiletewa matunda na nyama. Na waliekewa sinema yao ya kuangalia michezo kwenye chumba chao cha kulala.

Kuna mambo aliyoyasema Lily ambayo yamenivunja moyo. Kwa mfano, ameeleza kuwa japokuwa Hanga alikuwa mfuasi wa Marx na hivyo mtu wa kimaendeleo, moyoni mwake khasa alikuwa mtu wa ujinsia, yaani akipendelea mfumodume. Akaongeza kuwa Hanga alikuwa kama mchukia wanawake (misogynist) kwa sababu alipozaliwa Yelena, alivunjika moyo kwamba hakujaaliwa mtoto wa kiume.

Si hayo tu lakini Lily pia alieleza kwamba Hanga alikuwa na wivu kupita kiasi. Alikuwa hamruhusu mkewe achanganyike na wanaume, hata wenzake kazini au marafiki zake yeye Hanga. Kila Lily alipotaka kutoka ilimbidi kwanza amuombe ruhusa Hanga. Wakiwakaribisha wageni wa kiume nyumbani, Hanga alimlazimisha mkewe akae kimya, asifungue mdomo. Pia alimzuia asende kazini alipokuwa Hanga yuko mjini Moscow.

Hanga alikuwa na wake wengine wawili: mmoja Mguinea na mwengine Mzanzibari, Marehemu Bimkubwa Said “Maghee” aliyekuwa mwalimu wa skuli na aliyefariki dunia Dar es Salaam miaka michache iliyopita.

HANGA NA BABU

Hatuwezi kumzungumza Hanga bila ya kumgusa Abdulrahman Mohamed Babu kwa sababu baada ya Mapinduzi ya 1964, nchi za Magharibi zikiwaona kuwa ndio wakorofi wa Zanzibar waliokuwa na nia ya kuueneza ukomunisti Afrika ya Mashariki nzima.

Babu na Hanga walikuwa waumini wa itikadi ya Kimarx. Lakini Zanzibar walikuwa wafuasi wa vyama tofauti. Babu alikuwa katibu mkuu wa zamani wa ZNP (Hizbu) na baadaye Mwenyekiti wa Umma Party. Hanga alikuwa mmoja wa vigogo vya ASP na aliporudi Zanzibar baada ya kumaliza masomo Moscow aliteuliwa msaidizi wa katibu mkuu.

Hata Ukomunisti wa kimataifa ulipogawika na kuwa na mapande mawili la Sovieti na la China, Babu na Hanga nao pia waligawika. Babu akiwaunga mkono Machina na Hanga Wasovieti. Mapambano ya pande hizo mbili yalikuwa makali.

Hanga na Babu wakitafautiana kwa mengine pia. Kwanza walipita njia tafauti kuufikia Umarx. Hanga aliufikia kwa kupitia tarika ya uananchi wa Kiafrika. Babu, ingawa alikuwa muumini wa umajumui Wakiafrika (pan-Africanism) aliufikia Umarx kwa mtazamo wa kimataifa (cosmopolitan outlook) ingawa siasa zake za awali zilikua zikielemea falsafa ya “anarchism”, ya mfumo wa utawala huria usio na serikali.

Ingawa wote walikuwa na haiba lakini khulka zao zikitafautiana. Hanga akionekana kama saa zote akisononeka, akiwa katika mafikra. Babu lilikuwa jitu la raha, akipenda kustarehe na alikuwa mcheshi na mtu wa mizaha.

Ntatoa mfano wa nämna walivyokua wakiangalia sinema. Wakati Babu akionekana kama mgaagaa na njia (Bohemian) akenda sinema ili kujifurahisha, Hanga, kwa mujibu wa mkewe Lily, alikuwa hendi sinema kwa kujipumbaza tu. Alikuwa akenda sinema alipokuwa akijua tu kwamba atajifunza kitu cha kisiasa, kitachoitanua elimu yake ya kisiasa.

Lily amesema kwamba baada ya kufunga ndoa, Hanga alimwambia amuandikie orodha ya filamu za Kisovieti zitazoweza kumuendeleza kisiasa. Akampa mifano ya filamu bubu Battleship Potemkin na October (maarufu kwa jina la Siku Kumi Zilizoutikisa Ulimwengu). Filamu zote mbili zilifanywa na mwananadharia wa filamu za kimapinduzi Sergei Eisenstein.

Hanga alikuwa kama mtu aliyepandwa na pepo wa kisiasa, aliyehitaji kupungwa. Alikua kama akichukua hatua zake zote kwa sababu za kisiasa, tena siasa kali.

HANGA NA MAPINDUZI

Sitozungumzia jinsi Hanga alivyoshiriki katika Mapinduzi. Dk. Harith Ghassany ameyaeleza mengi kwenye kitabu chakeKwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.

Labda niseme tu kwamba juu ya tafauti zao zote, Babu na Hanga walikuwa na lengo moja wakati wa mapinduzi ya Zanzibar. Hata kabla ya mapinduzi, Babu na wafuasi wake wa Umma Party wakishirikiana na viongozi wa mrengo wa kushoto wa ASP, wakiwemo Hanga, Hassan Nassor Moyo, Abdul Aziz Ali Twala na Saleh Saadalla.

Umma Party haikuyapanga mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 ingawa makada wake walishiriki baada ya serikali ya Shamte ilipokuwa imekwishaangushwa.

Mpangilio wa Serikali ya kwanza ya Mapinduzi ulimuorodhesha Sheikh Karume awe Rais, Hanga waziri mkuu na Babu, waziri wa mambo ya nje.

Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi ulikuwa na vituko vyake. Karume aliwashangaza wote waliohudhuria kwa namna alivyonuna na alivyoukataa urais. Hakutafuna maneno.

“Sitaki kuvishwa kilemba cha ukoka,” aliwafokea wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Hanga alishtuka. Akaanza kubabaika. Karume alisema aliyoyasema kwa sababu akijua kwamba madaraka halisi alikuwa nayo Hanga aliyekuwa waziri mkuu mwenye nguvu za utendaji (executive powers). Cheo cha urais alichopewa Karume kilikuwa kama cha kumfutia machozi.

Hanga alikuwa dhaifu mbele ya Karume na akasema hakuwa akiyataka madaraka aliyopewa. Babu alinieleza mara kadhaa kuhusu kisa hicho na kila mara akinambia kwamba akimvuta suruali yake Hanga chini ya meza ili asiyaachie madaraka lakini Hanga alikuwa amekwishamridhia Karume.

Kisa hiki niliwahi kuhadithiwa pia na Salim Rashid, aliyekuwa katibu wa Baraza hilo, pamoja na nikikumbuka na Khamis Abdalla Ameir, aliyekuwa mjumbe wa Baraza. Kama Sheikh Khamis yupo hapa leo labda atatueleza zaidi. Sisemi kama Hanga alikuwa hajui kuzicheza siasa sawasawa lakini labda ilikuwa moyo wake safi na utiifu wake kwa Karume uliomponza.

Hamna shaka yoyote kwamba lau Hanga asingetetereka basi Zanzibar ingeufuata mkondo mwingine. Kwa hivyo, kuanguka kisiasa kwa Hanga na hata kuuliwa kwake ni mambo aliyojichongea mwenyewe kwa kuridhia kuuacha uwaziri mkuu.

Wadhifa wa uwaziri mkuu ukafutwa na Hanga akateuliwa Makamu wa Rais.

Muungano ulipoundwa miezi mine baadaye Karume akaongezewa cheo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania. Hanga pamoja na Babu wakahamishiwa Dar es Salaam na wakateuliwa mawaziri.

Hanga alijichongea pia kwa kumshikilia Karume aukubali Muungano. Kwa mujibu wa Sheikh Aboud Jumbe katika kitabu chake The Partner-ship Nyerere alimpelekea Karume wajumbe wawili, Oscar Kambona na Bi Titi Mohamed, kumshawishi akubali kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika. Hakufanikiwa.

Nyerere alifanikiwa pale tu alipomtumia Hanga na Saleh Saadalla wamshawishi Karume. Ilikuwa kama Hanga alijichimbia kaburi mwenyewe, kwani usuhuba wake na Kambona baadaye ulimghadhibisha Nyerere na lazima ulichangia katika uamuzi wake wa kumpeleka Hanga Zanzibar alikotakiwa na Karume na alikouliwa.

Tangu mapinduzi nchi za Magharibi zilitishika na Zanzibar. Na zilizidi kutishika mwezi mmoja kabla ya Muungano kuundwa pale Salim Rashid, mmoja wa viongozi wa Umma Party, alipolisoma uwanja wa Mnazi Mmoja lile liitwalo “Tangazo la Machi 8”. Tangazo hilo liliainisha sera za Serikali ya Mapinduzi. Kwa hakika, tangazo zima lilikuwa ilani ya Umma Party. Ndipo nchi za Magharibi zilipoanza kuiita Zanzibar kuwa ni “Cuba ya Afrika”, hasa baada ya kuimarisha mahusiano yake na nchi za Ulaya ya Mashariki, zikiwa pamoja na Ujerumani ya Mashariki ya wakati huo.

Mwezi uliofuatia Julius Nyerere alimshawishi Sheikh Karume, kwa msaada wa Hanga, kwamba Tanganyika na Zanzibar ziungane. Nyaraka za siri za Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) zinaonyesha kwamba Nyerere alichukua hatua hiyo kwa kuhimizwa na Marekani pamoja na Uingereza.

WASIA ALIONIPA HANGA

Mara yangu ya mwisho kukutana na Hanga ilikuwa London. Siku moja mtangazaji mwenzangu wa BBC, Emmanuel Vivian Kassembe, alininong’oneza kwamba Hanga akitaka kuniona pamoja na Wazanzibari wengine wawili: Salim Hamdan, ambaye siku hizi anaishi Maskati, Oman, na Khamis Nura, ambaye sasa ni marehemu.

Salim aliwahi kuwa mhandisi wa Sauti ya Unguja na alikuwa Uingereza akisomea teknolojia ya elektroni. Nura alikuwa mwanasheria wa kimataifa aliyesomea Moscow. Siku hizo akiogopa kurudi nyumbani na akifanya kazi ya ukarani serikalini London. Mimi nilikuwa kijana wa miaka 23 niliyekwishafanya kazi miaka mine BBC na nilikuwa karibu namaliza masomo yangu ya shahada ya falsafa katika Chuo Kikuu cha London.

Kati ya sisi watatu, Nura ndiye aliyekuwa karibu sana kisiasa na Hanga. Na ni Hanga aliyemkuta London akampatia msaada wa kwenda kusoma Moscow.

Lakini siku ya miadi yetu na Hanga ilipowadia, Nura hatukumuona. Kassembe akatuchukua miye na Salim kutupeleka alikokuwako Hanga. Ilikuwa nyumbani kwa Oscar Kambona karibu na stesheni ya treni ya Belsize Park, kaskazini mwa London.

Kambona alitufungulia mlango na kutukaribisha. Kulikuwa vyumba viwili chini ndani ya nyumba hiyo. Kambona alikuwa katika chumba cha mwanzo na mtu mwengine na baadaye Kassembe.

Kambona akatuonyesha mimi na Salim chumba cha pili akisema: “Maalim yuko humo”.

Mara tukamuona Hanga ametoka chumbani akitabasamu na akatukaribisha ndani.

Yeye na Salim wakikaa vitini na mimi nikajipachika kitandani.

“Nimekwiteni kukuhakikishieni kwamba mimi sina matatizo yoyote na Mzee (akiwa na maana ya Karume). Sina matatizo naye lakini anahisi mimi ni kitisho kwake, kwa jinsi ninavyopendwa na watu,” alisema.

Halafu Hanga akatueleza maisha yake alipokuwa waziri Zanzibar na Dar es Salaam. Alitueleza jinsi alivyokuwa akipenda kwenda kwa miguu badala ya kuendeshwa katika gari la waziri na pia kwamba alikuwa akimsikiliza kila mtu aliyetaka msaada wake.

Baada ya hapo akawa kama akitoa mawaidha marefu kupinga ukabila. Alianza kwa kutwambia kwamba alifanya makosa alipokuwa na siasa za kikabila na akatuasa “kama viongozi wa siku za mbele” tuepukane na siasa kama hizo.

Alisema aliwakasirisha baadhi ya viongozi wa ASP alipowasaidia waalimu Wakizanzibari wenye asili ya Kiarabu wapatiwe kazi Bara. Aliwataja baadhi ya waalimu aliosema aliwasaidia wakiwa pamoja na Maalim Salim Sanura na Maalim Shaaban Saleh Farsy. Waalimu wote hao wazuri waliokuwa na ujuzi walifukuzwa kazi na serikali ya Mapinduzi bila ya sababu yoyote ya maana na walikuwa wakizurura tu mjini Zanzibar.

“Nilipowasaidia waje kufanya kazi Bara sikuwaona kuwa wao ni Waarabu. Niliwaona kuwa ni Wazanzibari tu,” alisema Hanga.

Akaanza kunukuu aya za Qur’ani khasa mkasa wa Nabii Musa na Bahari ya Shamu kama ulivyoelezwa humo. Nikimsikiliza lakini nilikuwa na hamu ya kujua fikra zake juu ya Babu na Karume akimuonaje Babu.

“Akiwa Marxist mwenzangu namtakia kheri,” alisema na halafu akaongeza: “Yuko salama kwa sababu si kitisho kwa Karume kama nilivyo mimi.”

Alitwambia kwamba Karume akimuogopa yeye lakini khofu hiyo haikuwa na msingi kwa sababu hakuwa na nia mbaya dhidi ya Karume.

Nilipomuuliza kuhusu mipango yake na atafanya nini, alinijibu hivi:

“Kama ujuavyo nina mke Guinea na amejifungua mtoto wa kiume. Kwa hivyo ntakwenda huo nimpe jina mwanangu kabla sikurudi Zanzibar.”

Alipotutajia kwamba atarudi nyumbani, mimi niliruka nikionyesha wasiwasi wangu na nikamuuliza haogopi?

Hanga alikuwa mtulivu, alimgeukia Salim na akamwambia: “Mtizame kijana huyu. Kwa nini niogope? Sikufanya makosa yoyote. Sikuua wala sikuiba kitu.”

Alitushangaza alipotupa jicho na kukonyeza upande wa ukuta wa chumba alichokuwa Kambona akisema: “Angalau huyo [Kambona] ameiba pesa za TANU.”

Tulimuombea kheri tukaagana naye. Miaka kadhaa baadaye Kambona alinambia kwamba hata yeye alimsihi asirudi Tanzania lakini Hanga hakumsikiliza. Pia alinieleza kwamba Hanga alipofika Conakry alikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na Kwame Nkrumah, aliyekuwa akiishi huko uhamishoni. Nkrumah naye alimbembeleza asirudi, akimwambia kwamba hamuamini Nyerere.

Kambona pia alinambia kwamba hata kabla ya Hanga kwenda Conakry, Nkrumah alimwandikia barua alipokuwa London akimtaka asirudi Tanzania. Lakini Hanga alishikilia lazima arudi. Aliiamini ahadi aliyopewa Rais Ahmed Sekou Toure wa Guinea na Nyerere kwamba Hanga akirudi hatodhuriwa.

Baada ya kuwa na familia yake ya Guinea kwa muda Hanga akafunga safari ya kurudi Tanzania kwa kupitia Cairo. Huko alikaa kwa mwenziwe Ahmed Diria Hassan aliyekuwa balozi wa Tanzania. Sijui walizungumza nini Hanga alipokuwa kwa Diria. Lakini katika miaka ya 1980, balozi mmoja mstaafu wa Tanzania alinieleza kwamba aliambiwa na rafiki yake ya kuwa aliiona barua ambayo Diria alimwandikia Karume akimuelezea kuhusu kukaa kwake Hanga jijini Cairo.

Inasemekana kwamba barua hiyo ilieleza kwamba pale Diria alipomsindikiza Hanga uwanja wa ndege wa Cairo, alimuona Hanga akikumbana na Mohamed Fayek, ambaye wakati wa Rais Gamal Abdel Nasser alikuwa waziri wake wa mambo ya Afrika.

Kwa mujibu wa barua aliyopelekewa Karume, Hanga alikumbatiana na Fayek na halafu wakasimama wakizungumza kwa muda. Pakazuka dhana kwamba Hanga akitaka msaada wa Misri kumpindua Karume.

Nakumbuka 1984, Diria alipokuwa balozi Bonn, Ujerumani, alinialika kwake kwa chakula cha usiku. Nilimuuliza kuhusu hiyo barua anayosemekana kumuandikia Karume. Alikanusha.

Hanga alirudi Dar es Salaam na baadaye alikamatwa kwa amri ya Nyerere na kupelekwa Zanzibar alikotakiwa na Karume. Kabla ya hapo, Nyerere alimuadhir Hanga hadharani katika uwanja wa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Mkutano ulifanywa karibu na Arnaoutoglou Hall. Nyerere alimwita Hanga “baradhuli”.

“Huyu ni baradhuli,” alisema Nyerere. “Mnajua maana ya baradhuli nyinyi? Haijambo liji-Babu [yaani Abdulrahman Babu] linachapa kazi. Lakini huyu baradhuli.”

Alipofika Unguja, Hanga aliuliwa kwa kupigwa risasi. Inasemekana maiti yake ilifunganishwa na mawe mazito halafu ikazamishwa baharini. Mkewe wa Kirussi, Lily, alijaribu kuulizia yaliyomfika mumewe. Alijaribu hata kumuomba Svetlana Yosefna, binti wa dikteta Josef Stalin, amsaidie.

Hakufanikiwa hadi ulipoporomoka Muungano wa Sovieti. Nyaraka za siri za Shirika la Ujasusi la Kisovieti (KGB) zimeeleza vingine kidogo. Nyaraka hizo zinasema kwamba baada ya Hanga kupigwa risasi maiti yake ilikatwa vipande vipande, ikatiwa kwenye gunia lililozamishwa baharini. Hakuna mwanadamu anayestahili kifo kama hicho.

Nina na “version” nyingine, maelezo mbadala, ya jinsi alivyouawa lakini bado ningali nikiyafanyia utafiti. Hanga, aliyekuwa mtiifu kwa Karume, hakustahiki kuuliwa. Si yeye, si Othman Sharif, si Saleh Saadalla, wala si Abdulaziz Ali Twala. Wote walionewa. Waliliwa na mapinduzi.

Hakuna serikalini aliyetwambia walikuwa na hatia gani au kulikuwa na ushahidi gani wa kuwaingiza hatiani au walihukumiwa na nani. Na huyo aliyewahukumu, au hao waliowahukumu, walikuwa na haki gani ya kuwahukumu? Ni sheria gani iliyowapa madaraka ya kuwa majaji?

Serikali ina dhima si kwa familia zao tu lakini kwa jamii nzima ya Wazanzibari itwambie kwanini viongozi hao waliuliwa na maiti zao ziko wapi.

Tumkumbuke Hanga kama mzalendo Wakizanzibari aliyekuwa mfano wa mwanasiasa aliyeteleza kwa kufuata siasa za kikabila lakini ambaye baadaye alitanabahi kuwa alikosea na akiwataka Wazanzibari waungane, wawe kitu kimoja.

Magharibi ya Aprili 7, 1972 ilipothibitika kwamba Sheikh Karume aliuawa, kuna bibi mmoja kizee aliyetoka nje ya nyumba bila ya kujistiri sawasawa. Alikuwa akirukaruka nje akishangilia mauaji ya Karume. Bibi huyo akiitwa Mashavu binti Hassan. Alikuwa mamake Hanga.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.