Ulikuwa ni mwanzo wa usiku wa siku ya Jumanne ya tarehe 30 Agosti 2016, majira ya saa mbili na nusu, nikiwa nimeketi katika kingo za Bustani ya Forodhani, nikiwaza hili na lile. Mbele yangu kunapita kundi kubwa la watalii wa Ulaya. Nyuma yao nikaona kuna mtoto umri wa kati ya miaka 11-13. Ghafla mtoto yule anapiga ubinja (mlunzi) kumwita mwenzake wa umri wa kati ya miaka 7-8, kisha kwa pamoja wanaanza kulifuata kundi lile la watalii huku wakiwasonga kwa maneno na ishara, kuonesha kuwa wanawaomba vyakula walivyoshika mikononi mwao watalii hao.

Muonekano wa Bustani ya Forodhani kutokea jengo la Beit el-Ajab
Muonekano wa Bustani ya Forodhani kutokea jengo la Beit el-Ajab

Kabla ya jua kuzama, nilishashuhudia tukio jingine la watoto wasiopungua watano, wakimsonga mtalii mwengine kutoka Asia, ambaye alikuwa anatembea huku ameshika dafu anakunywa kwa mrija. Mwisho mama yule akaamua kuwapa lile dafu, watoto wale wakaanza kugombana, huku wakirushiana maneno na kutoweka kwenda kwengine kuendeleza mchezo huo.

Kwa hakika, matukio haya (ambayo lazima niseme ya pekee kujiri) yakaifanya siku yangu kuwa mbaya sana. Taswira ya Zanzibar yangu, mbele ya uso wa Bahari ya Hindi, ikiwa na kizazi kinachoinukia kwenye ombaomba.

Kiswahili kina misamiati miwili inayofanana na kukinzana kwenye dhana hii. Mmoja ni ‘kuomba’, ambao una maana ya kawaida na si tatizo, lakini wa pili ni ‘kuombaomba’, ambao una maana mbaya sana. Muombaji na ombaomba ni watu wawili tafauti, na hili la kuombaomba ndilo  lisilokubalika katika jamii. Na sasa linapokuja suala la kuwa hawa ombaomba wamekuwa watoto wadogo kama hawa niliowaona na kwa jamii ya Kizanzibari niliyokulia na kuijuwa vyema, hapana shaka hapo msumari wa kutokukubalika ndipo unazidi kushindiliwa.

Siku ile wakati nikielekea Forodhani (ama Foro kwa umaarufu wa ufupisho wake), nikiwa katika likizo ya kumaliza kozi yangu ya masomo, sikuwa nimejiandaa kwenda kufanya utafiti ili niandike makala, ama kwenda kukusanya taarifa zinazokirihisha za eneo lile. Nilijiamulia mwenyewe kuwa mtalii wa ndani, lakini nilichokikuta ndicho kilichonifanya niuweke kando utalii wangu wa ndani na kujivika taaluma yangu ya uandishi wa habari.

Na Rashid Abdallah
Na Rashid Abdallah

Maswali yangu yalikuwa mengi: Je, watoto hawa hawana wazazi? Hivi kweli wana umasikini mkubwa mno unaowalazimisha kuja kuomba chakula midomoni mwa watu? Ama ni nini khasa kilichowasibu?

Ndipo nikaamua kuwakabili walinzi wa eneo lile ili wanieleze kinagaubaga juu ya watoto wale. Mmoja wao, kwa jina la Yusuf Yakoub, akiwa na wenzake, alinieleza kuwa wao kama walinzi wamejitahidi kadiri ya uwezo wao kuwadhibiti watoto wale, hadi kuwachapa mikwaju, lakini bado wanaendelea na kazi zao za kuombaomba.

Kinachoumiza, kwa mujibu wa walinzi hao, ni kuwa baadhi ya wazazi wanaunga mkono tabia za watoto wao kuendelea kuombaomba, huku wakinitolela mfano wa mtoto mmoja ambaye walinionesha baba yake ni mkamua miwa na walishamueleza tabia ya mtoto wake, lakini hakuna hata alichofanya.

“Hawa watoto ni wachumaji katika familia zao kwa kazi hii ya kuombaomba watalii, kwani huanza kuomba katika Hoteli ya Tembo wakati wa mchana na kuja kumalizia huku (bustani ya Forodhani) wakati wa usiku”, alinieleza mlinzi mwengine ambaye sikupata jina lake kwa mara moja.

Vijana wajifanyao machizi

Wakati tukiwa katika mazungumzo hayo, mara tukamshuhudia kijana aliyechafuka mchafukoge kutoka ukucha mpaka utosi – hafahamiki nguo, hafahamiki nywele – akichakua kwenye debe la taka pembeni pakiwa na mtalii wa kiume aliyebeba mtoto wake.

Walinzi walinieleza kuwa wanaamini kuwa kijana yule alikuwa na akili zake timamu. Nilipotaka ufafanuzi, wakanichukuwa kunizungusha katika Bustani ya Forodhani kuoneshwa vijana kadhaa ambao wakiingia Forodhani wanakuwa ni wagonjwa wa akili kwa kila jambo walifanyalo pale, lakini mitaani wanakuwa wazima wa akili.

Walinzi hao na mmoja wa wenyeji wa maeneo yale walineleza kuwa wanaamini katika Bustani ya Forodhani wagonjwa wa akili wapo wawili tu, lakini kila siku wanaonekana zaidi ya hao “na inapofika siku ya Jumamosi na Jumapili ndio huongezeka.”

“Wengi sio wagonjwa wa akili. Ni maisha ya kutafuta tu. Wakitoka hapa, wapo vizuri tu. Wagonjwa wa akili hawafiki watatu”, alinieleza mfanyabiashara mmoja, mara baada ya kumuuliza kuhusu kijana aliyekuja kununuliwa chakula na mtalii, alipomzuia kuchakua debe la taka.

Jingine nililoelezwa kuhusu hawa vijana wanaojiingiza katika maisha ya ugonjwa wa akili ni kuwa wengine wanatumia madawa ya kulevya. Sasa ili kupata chakula na pesa, ni lazima waigize maisha hayo, waonewe huruma na kupewa chochote.

Kula makombo ya watalii

Siku ya tatu yake nikarudi Forodhani kwenda kuwatafuta watoto omb omba, kujua khasa kinachowasibu kutoka katika vinywa vyao na kufikia khatua hiyo ya ‘kushika mashati watalii’. Kwa makusudi, nikajiweka pembeni mwa watalii wawili waliokuwa na chakula. Ghafla mtoto mmoja alikuja naye akajiweka upande wa pili, pembeni yao kwa ukaribu sana, akawaambia: “Hi!”

Lakini baada ya kuwasalimu hivyo, nikamuwahi kabla hajaendelea na chengine chochote. Nikaamua kumwita. Akanieleza jina lake (hapa nalihifadhi) na umri wake ni miaka 11, anasoma darasa la tatu, alinieleza kuwa hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza kuja na alikuja kuomba pesa kwa watalii ili akatumie. “Marafiki zangu wanakuja kuomba pesa na vyakula kwa watalii,” alinisimulia.

Wakati naendelea na mazungumzo na mtoto huyo, umbali wa mita saba kutoka nilipokuwa nikaona kundi kubwa la watoto likiwa limemzunguka mzee wa Kizungu ambaye alikuwa anakula. Kwa kutumia uzoefu wangu wa juzi yake na hadithi ambazo nimezipata juzi na leo hii, nikaamua kuwafuata.

Niliwakusanya kiurafiki kisha nikazungumza nao. Maswali yangu yalikuwa yale yale ya juzi yake: Je, watoto hawa hawana wazazi? Hivi kweli wana umasikini mkubwa mno unaowalazimisha kuja kuomba chakula midomoni mwa watu? Ama ni nini khasa kilichowasibu?

Mmoja wao, aliyeniambia ana miaka 14 na mkaazi wa Hamamni, alinieleza kuwa yeye anapenda tu kuja kuomba pesa na chakula kwa watalii, lakini familia yake haijui na wala sio kwamba hapewi chakula kwao.

Mwengine mwenye umri wa muiak 13, alisema anaishi Nyarugusu na wazazi wake, anasoma Darasa la 5 na baba yake ni mwalimu. “Ukweli kwa siku hizi kinachonileta hapa ni kutafuta chupa, lakini mwanzo nilikuwa nakuja kula makombo ya chakula kinachoachwa na Wazungu,” aliniambia akiwa hana wasiwasi wowote, akisisitiza kuwa “wapo watoto ambao wanakuja kwa kuomba pesa watalii, kuomba chakula na kula makombo.”

Katika kundi lile pia kulikuwa na mwigine mwenye miaka 14, yeye anaishi Mwembeladu, anasoma Kidato cha Kwanza. Huyu mwenyewe akiniambia kuwa huja Forodhani kuomba chakula na pesa kwa watalii. “Naishi na bibi yangu, lakini hajui kuwa nakuja Forodhani kufanya hivi!”

Alikuwepo pia wa miaka 13, naye akakiri kuwa yeye na wenzake wengi tu wanakuja kwa kuomba watalii chakula la pesa.

Baada ya dakika chache nilipomaliza kuzungumza na kundi hilo la watoto, niliamua kutembea kidogo, ila nilipofika karibu na mgahawa wa The Floating Restaurant, pembeni yangu katika kingo za bustani kulikuwa na watoto watatu wamekaa mbele ya watu wawili ambao walikuwa wanakula.

Baada ya dakika chache kupita, nikaamua kurudi na kukuta kile chakula ambacho walikuwa wanakula wale watu- kwa sasa wanacho wale watoto wanakila, niliposogea na kuwauliza wale watu kwa kuwanong’oneza: “Vipi mumewaomba hicho chakula?” Jibu lao, lilikuwa “Ndio!”

Siri ya Fododhani

Siri iliyojificha katika Bustani ya Forodhani, ambayo mamlaka zimekuwa zikijitahidi kupadumisha kuwa kituo na kivutio cha utalii wa ndani na wa wageni, ni kuwa panageuzwa kuwa chaka lenye machafu mengi. Mbali ya mengine ya madawa ya kulevya na uzinzi unaosukwa hapo pengine kwa siri na umakini mkubwa, kuna hili ambalo kalamu yangu imeliona kwa safarii zangu mara mbili tu hapo.

Kuna kundi kubwa la watoto, ambao wanaondoka majumbani mwao na wengi bila ya wazazi wao kujua kuwa wanakwenda Forodhani na kisha kufanya kazi ya kuombaomba. Pia kuna vijana wanakwepa kujituma na wanaishia kujidhalilisha mbele ya mamia ya watu.

La muhimu ni wazazi kuwa macho na watoto wao, inasikitisha kuwa kuna watoto wanapata chakula nyumbani ila wanadiriki kwenda kusimama na kuomba, huku familia zikiwa hazijui. Na kwa wazazi wanaojuwa kuwa watoto wao wanafanya haya na kisha wakapuuzia, hawa ni wa kutiwa adabu na mkono mrefu wa serikali.

Nililoligundua ni kuwa jitihada za kukabiliana na matatizo haya ni ndogo sana, sio tu kutoka kwa wazazi wanaowaacha watoto wao ovyoovyo pasina kuwafuatilia wanapokwenda na wanachokifanya, bali pia kwa uongozi wa Mji wa Zanzibar, jimboo la Mji Mkongwe (ambako bustani hii ipo) na jamii husika. Hakuna jitihada za kutosha za kuwadhibiti hawa watoto.

Wakati bustani hii ya Forodhani ikitanuliwa ukubwa wake, ni bahati mbaya sana kwamba kuna ongezeko la watoto ombaomba, wala makombo waongezeke na wenye akili zao lakini wanaojitia ugonjwa. Hili halikubaliki wala halivumiliki hata kidogo kwa Zanzibar yetu.

Ikumbukwe kuwa Mji Mkongwe ndicho kitovu na uso wa Zanzibar nzima. Hivyo ni jukumu la familia, jamii na serekali kudhibiti hali hii, kwani ni aibu kwa jamii iliyostaarabika kuwa na watoto ombaomba kwa starehe tu na vijana wasiotaka kujituma.

One thought on “Foro: Chaka la watoto wala makombo, vijana wajifanyao machizi”

  1. a.alaikum
    Zamani ilikuwa ukiwa na tafrani kichwani Foro palikuwa sehemu muafaka ya kutuliza fikra.lakini leo ukiacha hao wageni wanaosumbuliwa lakini hata sisi wenyeji inabidi kuikimbia bustani hii kwa vituko vyake.
    Kweli hii ni aibu kwa Zanzibar.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.