Historia ya Zanzibar itamkumbuka Amani Abeid Karume kama mmoja wa viongozi waliopigania maridhiano, umoja na demokrasia visiwani humo.

Mizinga ya Forodhani

Katika kitabu chake Conversation with Myself (Mazungumzo na Nafsi Yangu), aliyekuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Marehemu Mzee Nelson Mandela, anaandika:

“Is not our diversity which divides us, it is not our ethnicity or religion or culture that divides us- since we have achieved our freedom – there can only be one division among us: between those who cherish democracy and those who do not.”

Tafsiri isiyo ya moja kwa moja ni kuwa “si mchanganyiko wetu wa rangi unaotugawa, si kabila au dini au utamaduni wetu unaotugawa – tangu tupate uhuru – kunaweza kuwepo mgawanyiko mmoja tu baina yetu: ni kati ya wale wanaoitukuza demokrasia na wale wasiofanya hivyo.”

Katika juhudi za kujenga umoja na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari, viongozi wa vyama viwili vikubwa visiwani humo – Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) walifikia muafaka uliosainiwa na Philip Mangula (wakatui huo Katibu Mkuu wa CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu wa CUF) hapo tarehe 10 Oktoba 2001.

Na Hafidh Ally
Na Hafidh Ally

Huu uliitwa Muafaka wa Pili, kwani miaka miwili kabla ya hapo, wakati Salmin Amour Juma akiwa Rais wa Zanzibar, kulikuwa kumefikiwa Muafaka wa Kwanza baina ya vyama hivyo hivyo chini ya uangalizi wa Jumuiya ya Madola, ambao bahati mbaya ulikufa hata haukutumia mwaka.

Kama ulivyokuwa Muafaka wa Kwanza kuchimbukia kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Muafaka wa Pili nao ulitokana na majeraha ya uchaguzi mkuu wa 2000. CUF ilikataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo na maandamano yake ya mwezi Januari 2001 yakajibiwa kwa mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola.

Wakati huo huo, Karume alikuwa ndiye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kwa kile kinachoweza kutafsirika kuwa nia njema na moyo wa uzalendo, serikali yake ikapitisha Sheria Namba 10 ya Mwaka 2001, ambayo iliunda Kamati ya Pamoja ya Rais ya Kusimamia Utekelezaji wa Mwafaka wa Pili.

Kutokana na mapendekezo ya Kamati hiyo, Katiba ya Zanzibar ilifanyiwa marekebisho kupitia sheria inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Nane ya Katiba ya Zanzibar Namba 2 ya Mwaka 2002, ambayo baadaye ilitiwa saini na Rais Karume tarehe 7 Mei 2002.

Kwa marekebisho hayo, Kifungu cha 66 cha Katiba ya Zanzibar kilifanyiwa marekebisho kwa kuongezwa maneno yafuatayo:

“Isipokuwa kwamba wajumbe wasiopunguwa wawili watateuliwa na Rais kwa kushaurizana na kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakikishi.”

Mabadiliko haya yalipitishwa katika Baraza la Mapinduzi lililoundwa na CCM watupu na hatimaye yalipitishwa katika Baraza la Wawakilishi lililosheheni pia wawakilishi wa CCM.

Moyo wa Mabadiliko ya Nane ya Katiba ya Zanzibar ulikuwa ni kugawana madaraka kwa lengo la kujenga kuaminiana na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari.

Juzi, tarehe 29 Septemba 2016, likisheheni tena wajumbe kutoka CCM, Baraza la Wawakilishi lilifanya Mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Zanzibar na kukifanyia marekebisho Kifungu hicho hicho cha 66, ambapo sasa Rais wa Zanzibar halazimiki tena kuwachaguwa “angalau wawakilishi wa wawili kutoka chama cha upinzani.”

Kwa uzoefu wa siasa za utengano zinazochezwa visiwani Zanzibar, mtu huweza kujiuliza ikiwa kulikuwa na umuhimu na ulazima kwa wakati huu kukifanyia marejebisho Kifungu hicho cha 66, wakati CCM imehodhi viti vyote 54 vya uwakilishi, jambo linalowapa uwezo kufanya maamuzi yoyote ndani ya Baraza! Kipi wanachokihofia?

Ukiyaangalia mabadiliko haya kwa undani, utapata jawabu kuwa sio tu wanajaribu kuuvunja msingi wa maridhiano, bali pia kuyaangamiza matunda ya Muafaka wa Pili. Na kama inavyofahamika kuwa kuna Muafaka mwengine wa Tatu wa tarehe 5 Novemba 2009, ambao Wazanzibari wanauiita Maridhiano.

Kwa hivyo, hapana tone la shaka kwamba sio tafauti zetu za kisiasa, kikabila au kidini zinazotugawanya hapa Zanzibar – tangu tulipofikia Maridhiano tarehe 5 Novemba 2009 na kisha kuanzisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Agosti 2010 – bali kuna mgawanyiko mmoja tu baina yetu: nao ni kati ya wale wanaoyatukuza maridhiano, umoja na demokrasia na wale ambao wanayapiga vita hayo.

CCM Zanzibar imejipambanua kuwa mpiganaji vita dhidi ya hayo.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.