Hufika muda tunalazimika kukubali matokeo. Inawezekana kuikubali hali hiyo kwa shingo upande au maumivu makali yasiyomithilika. Hata hivyo, maumivu na sononeko hilo haliondowi uhalisia wa mambo. Kwamba la kuvunda halina ubani hata hikima na juhudi kubwa zikitumika.

Prof. Ibrahim Lipumba
Prof. Ibrahim Lipumba

Chanzo cha maumivu na sononeko la wengi huwa ni mapenzi ambayo hupelekea mjengeko wa matumaini yenye kuegemezwa kwa kitu au mtu fulani. Kukosekana kwa kile kilichotarajiwa hupelekea kuibuka mengi, yakiwemo kukata tamaa au hata fikra za kujitowa uhai. Na hata baada ya hayo, hakika jitihada haishindi kudura!

Na mimi pia na nina maumivu – nataka nikiri tangu mwanzo – na maumivu yangu yanarudisha fikra zangu miaka kadhaa nyuma. Namkumbuka mmoja wa waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), Marehemu Mzee Shaaban Khamis Mloo. Namkumbuka mzee huyu siku alipopanda juu ya jukwaa na kumkabidhi chama hiki Profesa Ibrahim Haruna Lipumba pale kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo alimuusia kwa kumwambia: “Ibrahim, nakukabidhi chama, kisimamiye. Ibrahim nakukabidhi wananchi wanyonge walioumizwa na utawala dhalimu, wapiganiye. Ibrahim nakukabidhi umma huu ulio mbele yako, shirikiana nao ili kuiletea nchi hii ukombozi wa kweli baada ya ule wa bendera, ambao umeshindwa kukidhi matarajio yao. Utaweza kulifanya hilo, kama ukiweza kushirikiana na wenzako ndani ya chama chetu cha CUF, ambao wana dhamira ya dhati ya kupigania haki na ustawi wa Watanzania hawa. Mungu akuafikishe.” Huu ndio usia niukumbukao toka kwa Marehemu Mzee Mloo kwenda kwa Lipumba siku akimkabidhi uenyekiti wa CUF.

Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Mapenzi yangu kwa Profesa Lipumba na CUF ni makubwa na yenye ukumbi mpana moyoni mwangu. Naamini, si peke yangu. Tupo kwa malaki kama si mamilioni, walio hai na washaotangulia mbele ya haki. Wengi tumeathiriwa na chama hiki kwa namna moja au nyingine. Wapo waliopoteza maisha, waliopata ulemavu wa kudumu na wapo wengine ambao ndio wengi waliojikuta magerezani kwa mapenzi yao kwa Lipumba na kwa CUF.

Hapa nawakumbuka makumi ya watu waliokatishiwa uhai wao kutokana na mapenzi yao kwa chama hiki kwenye maandamano ya Januari 26 na 27 na yeye Profesa Lipumba na wenzake walioumizwa vibaya. Namkumbuka mzee wangu mmoja ambaye ni mkaazi wa Mbagala ambaye amepata ulemavu wa kudumu na kijana mdogo ambaye alipigwa risasi pale maeneo ya Temeke kwenye harakati za kukisimamisha chama hikii kwenye maeneo mbalimbali. Bado kichwani mwangu zimejaa kumbukumbu za namna vijana walivyojitolea kusafiri kwa malori na mabasi toka Dar es Salaam hadi Tanga, Dodoma mpaka Mwanza kukiimarisha chama hiki kwa gharama zao wenyewe. Bado nakumbuka ibuko la matawi kama vile Chechenya, Bosnia, Ukanda wa Gaza, Hamas na mengine mengi ambayo yaliibuwa hamasa kubwa miongoni mwa vijana. Jee, viongozi wakuu wa CUF, mumeshasahau haya?

Matumaini ya sisi wengine yakaaza kupotea juu ya mustakbali mwema wa CUF miaka kadhaa iliopita. Hii ilitokana na mienendo ya baadhi ya viongozi wa chama hichi, ambao walionekana wazi kupigania maslahi binafsi na si yale mapana na yenye manufaa kwa kila mdau wa chama hichi. Wapo miongoni mwao waliowaza na kujaa zaidi tamaa ya vyeo ili kufanikisha ya kwao, huku wakisahau lengo na madhumuni ya kuanzishwa CUF. Lakini wapo pia ambao waliumizwa sana na chama hiki kiasi cha kuamuwa kuachia nafasi zao za kiuongozi kwa lengo la kulinda heshma zao. Hawa walikhiyari wakauze chips mitaani kuliko kusaliti dhamira na malengo ya chama hichi. Jiulize, kwa mfano, nini kilimuondoa Said Miraj Abdullah, kijana shupavu na makini, mtu aliyejitolea hadi kupata ulemavu wa kudumu sababu ya CUF?

Wakati Profesa Lipumba akitangaza kujivuwa wadhifa wa uenyekiti wa chama chake mwezi Agostu 2015, wengi waliumia, kwa vile walikuwa wamejenga imani kwamba ni jambo gumu kuweza kutokea mwingine wa kuvaa viatu vyake au wa kujaa ndani ya kiti chake cha uenyekiti ambacho alikaa na kujaa ndani yake. Waliumizwa pia na wakati wenyewe alioamua kufanya hivyo, kwani ni wakati ambao kwa hakika CUF ilikuwa ikihitaji uongozi wake.

Hata hivyo, waliumia zaidi pale alipotangaza kurudi tena kwenye nafasi ile ile ambayo alishaamuwa kuiwacha. Na hapa waliumizwa kutokana na namna alivyoamuwa kuirejeshea hiyo. Kwamba kwa namna alivyoamuwa kuirudia, kurudi kwake kulibeba masuali mengi vichwani mwa wenye kutafakari.

Kuteleza, kwa hakika, si udhaifu kwa mwanaadamu. Ndilo pambo lake. Wengi waliamini kuwa Profesa Lipumba alikuwa ameteleza kama binaadamu, pale alipoamua kukitelekeza chama chake katika wakati kama ule muhimu kwenye siasa za nchi. Lakini inaonekana alipoamua kurudi kwenye nafasi yake ya uwenyekiti, jambo la kwanza ambalo amelitaka lifunikwe ni kutuaminisha kwamba hakuwa ametenda kosa lolote kuachia wadhifa wake katika hali ile na kisha kukaa nje ya chama kwa zaidi ya miezi kumi, akiwa hakushiriki kazi yoyote ya kichama ndani ya kipindi hicho chote. Anataka tuamini kuwa alikuwa sahihi kukiacha chama muda aliotaka kukiwacha, alikuwa sahihi kutokujishughulisha na chama hiki muda wote ambao hakujishughulisha, na sasa yuko sahihi kurudi kwenye nafasi ya uwenyekiti na kufanya apendavyo!

Kama si hivyo anavyotaka tuamini, basi Profesa Lipumba alikuwa na njia rahisi ya kurudi kutuongoza na ambayo ingelijenga imani kwa wenzake wa karibu ambao amekuwa nao tangu hajawa mwenyekiti mpaka amekuwa, nayo ni ile ya kufata taratibu ambazo zimewekwa kikatiba. Kinyume chake, si jambo jepesi kuamini kwamba pale ambapo mume anadai kumrejea mkewe katika hali ambapo kile kilichomfanya kumpa talaka kwa mara ya kwanza, bado kingalipo.

Kama mtu ambaye ana nafasi kubwa mioyoni mwa wengi na mwenye dhamira ya kututetea kama alivyousiwa siku ile pale Mnazi Mmoja na Mzee Mloo, hivi Profesa Lipumba alishindwa nini kujaza fomu kuomba tena uenyekiti penye dhamira njema juu ya anaowapigania? Kwa nini aliamua kuuwacha njia panda ule umma aliokabidhiwa na Mzee Mloo? Kweli ametawaliwa na ghadhabu kiasi cha kusahau uzito na umuhimu wa kauli ya Mzee wetu huyu?

Kwa hakika, uamuzi wa Profesa Lipumba umewakatisha tamaa wengi ambao walimuimbia na kushangilia kila walipomuona. Umewaumiza wengi ambao walikubali kupigwa na jua, mvua na hata mabomu na risasi za moto kwa ajili yake na CUF yao. Imewauma na kutafishi nafsi zao kwamba hata viongozi wakubwa wenye kuheshimika kiimani kama vile masheikh na mapadri hakutaka kusikia nasaha zao na badala yake akaendeleza msimamo ambao leo umeacha sononeko kubwa miongoni mwao.

Kitu kimoja kipo wazi: nacho ni kuwa yaliyomfanya akiwache chama na kumsuta dhamira, bado yapo. Ushirikiano wa CUF na vyama vingine chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) bado upo. Edward Lowassa wa CHADEMA, ambaye eti Profesa Lipumba anataka iaminike kuwa ndiye kisa cha yeye kuiwacha CUF mkondoni, bado yupo na bado ana dhamira ya kugombea tena urais mwaka 2020, na huenda UKAWA ikamuunga tena mkono. Lakini Lowassa huyu alimleta yeye mwenyewe kwenye UKAWA, na si mwengine.

Binafsi siamini kwamba kama kweli Profesa Lipumaba ana dhamira ya kuiondowa CCM madarakani, kwani uzoefu wa miaka 25 ya chaguzi za vyama vingi umetuonesha kuwa sisi wapinzani hatuwezi kuiondoa CCM kama hatukusimama pamoja. Inavyoonekana ni kuwa Profesa Lipumba anataka CCM iendelee kubakia madarakani, naye anapendezewa kuitwa mpinzani wa kudumu.

Pamoja na hayo, lazima tukiri kwamba ongezeko kubwa la wabunge wa upinzani kwenye bunge letu limetokana na juhudi za akina Profesa Lipumba na wenzake, ambayo waliwekeza kwa muda mrefu kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara. Ni kutokana na kazi hiyo, ndiyo maana ikawa rahisi kwa upinzani kuachiana maeneo na kisha kuungana mkono kwenye baadhi ya majimbi, jambo lililopelekea mafanikiyo haya ya sasa. Lakini leo kuwa na mwenyekiti wa chama ambaye jukumu lake kuu alilojipa ni kukiondoa chama hiki kwenye umoja uliouasisi mwenyewe na ambao umeleta faida maradufu kwa chama chake hicho, kunataka upumbavu wa kiwango cha juu kumkubali, acha mbali kumuamini?

Ni muda mrefu Watanzania wamekuwa wakisisitiza na kulilia vyama kuungana ili kuleta tija na changamoto kwenye bunge letu, jambo ambalo hatimaye limewezekana. Huu ulikuwa mwanzo mzuri wa kuanza safari ya kukiondowa chama tawala madarakani. Ila safari hii ingefanikiwa iwapo viongozi wangetanguliza mbele harakati na mipango ya kufanikisha hilo, huku wakisahau suala la nani awe raisi na ile falsafa ya kwamba kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wakudumu. Viongozi hawakupaswa kugawana fito na badala yake wangeshikamana na kuimarisha jengo ambalo lingewasitiri wote.

Jitihada haishindi kudura, nimetangulia kusema. Mengi yalifanyika ili hali hii ya sasa isijitokeze, lakini ikashindikana, na sasa CUF inaonekana kugawika vipande vipande. Kwa njia nyepesi, CCM imesaidiwa kumaliza kazi ambayo iliipigania kwa miongo mitatu.

Huu ni usaliti na ubaya usiomithilika. Kila aliyehusika na anayeendelea kuhusika, akumbuke kwamba bendera ya mwanzo kupandishwa mlingotini baada ya kuasisiwa kwa chama hiki kule kwenye kijiji cha Shumba ya Mjini kisiwani Pemba, ilimwaga damu na kuondoka na roho ya mpandishaji wa bendera hiyo. Alipigwa risasi na kufariki papo hapo.

Wallah thumma Wallah, Mungu hatomuacha msaliti yeyote. Wakati wakipapurana na kukifikisha chama ambacho wengi wamekijengea matumaini hapa kilipo, kuna watoto ni mayatima na mama zao ni vizuka. Bado pana kumbukumbu ya vijana wabichi waliotolewa roho kwenye maandamano ya Januari 26 na 27.

Labda hawa wanaokisongoa roho chama hiki wamewasahau wahanga hao na ndio chimbuko la kukigawa chama mapande kwa maslahi binafsi. Juhudi kubwa zilifanywa kuwarudisha kwenye msitari lakini wakashindwa kutanabahi. Na sasa hakuna jinsi ila kutafunwa na  ubaya wa dhambi hii.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.