Hisia ni kitu ambacho kila kiumbehai anacho kutegemea na hukionesha kulingana na mazingira husika. Tafsiri ya hisia hizo ni za aina mbili – chanya na hasi – kama vile ambavyo kinachozipelekea hisia kililivyo. Hisia chanya ni zile ambazo mtu akiwa nazo huonekana hali ya bashasha, furaha, tabasamu na hata kicheko; na hisia hasi hujidhihirisha kwa hali ya hasira, chuki, mikunjo ya uso na hata kilio.

Hisia ni sehemu ya maumbile yetu na mtu anapokuwa nazo – ziwe hasi ama chanya – huwa hajakiuka ubinaadamu wake, isipokuwa kila mtu anavyozidhibiti hisia zake chanya huonekana na wengine kwamba amejiweza zaidi. Hapa nazungumzia kitendo cha Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kukataa kuinua mkono wake kuupokea mkono wa Makamu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, siku ya maziko ya aliyekuwa rais wa pili wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Ninachosema ni kuwa hisia za Maalim Seif ni maamuzi ya nafsi yake juu ya kuficha hisia zake na kiwango cha kuzificha na kuzifichua ni hukumu yetu sisi tulioziona. Lakini ikiwa tunafahamu kuwa Maalim Seif anaamini kwamba Dk. Shein ni hasimu wake kwa kuwa amemdhulumu haki yake, basi hatuna budi pia kukufahamu kule kuonyesha kwake hisia zake.

Tusiwe wasahaulifu kwa matukio ya watu mashuhuri kama yeye au zaidi yake, Maalim Seif. Kiongozi huyu mwenye ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar si mtu wa kwanza kuonyesha hisia zake za hasira kwa mtu anayemchukulia kuwa na sifa (au tuseme ila) alizonazo. Kinyume chake, naweza kusema, Maalim Seif ni wa mwisho hadi kufikia siku ya maziko ya Marehemu Mzee Jumbe kwa watu mashuhuri kukataa kutoa mikono kwa mahasimu wao.

Kwa kuwa tuko katika masiku saba ya maombolezo ya kifo cha Mzee wetu Jumbe Mwinyi, basi nitakuonyesha matukio saba ya watu walionyesha hisia zao kwa kukataa kuwapa mikono mahasimu wao au wasiowapenda, miongoni mwao wakiwemo marais wa nchi kubwa duniani hadi wanariadha na wachezaji mpira mashuhuri.

George W. Bush mwaka 2008

Mnamo tarehe 22 Novemba 2008, mitandao mbalimbali duniani iliripoti tukio la mkutano wa wakuu wa nchi za mataifa 20 yenye nguvu za kiuchumi, G20, ambapo Rais George W. Bush wa Marekani aliwawapita wakuu wenzake wa nchi bila kuwapa mikono na hata hao wakuu wenzake wa nchi hawakunyoosha mikono kumpa Bush.

Wine Bridge mwaka 2010

Mnamo tarehe 28 Machi 2010, iliripotiwa katka gazeti la Daily Mail la Uingereza kwamba mchezaji wa Manchester United alikataa kumpa mkono rafiki yake na mchezaji mwenzake waliocheza pamoja katika timu ya Chelsea ya Uingereza, John Terry. Sababu ya kuonyesha hisia zake hizo na kushindwa kumpa mkono Terry zinaelezwa ni kwamba ni pale ilipogundulika kwamba John Terry alikuwa anatoka kimapenzi na mpenzi wa zamani wa Wine Bridge.

Luis Suarez mwaka 2012

Mnamo tarehe 12 Februari 2016 wakati timu mbili hasimu yaani Manchester United na Liverpool zilipokutana kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ya uingereza Luis Suarez alikataa kumpa mkono Patrice Evra wa Manchester United kwa kuwa alikuwa hampendi kutokana na weusi wake, hivyo alishindwa kuzuiya hisia zake na kukataa kumpa mkono.

Antony Ferdinand  mwaka 2012

Mnamo tarehe 16 Septemba 2012 mchezaji mpira wa QPR alikataa kupeana mkono na nahodha wa timu ya Chelsea John Terry wakati timu hizo zilipokutana kwa ajili ya mchezo wao ligi kuu ya uingereza, ambapo sababu iliyoelezwa ni kwamba John Terry alifanyia ubaguzi wa rangi Antony Ferdinand ndipo na yeye akaonyesha hisia zake za kuchukizwa.

Robert Mugabe mwaka 2015

Tarehe 28 Aprili 2015 rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alikataa kupokea mkono na kiongozi/mfalme wa Wazulu wa Afrika ya Kusini, kwa kitendo cha mfalme huyo kuhamasisha ubaguzi na mauaji dhidi ya wageni wanaoishi Afrika ya Kusini.

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa na polisi mwaka 2016

Tarehe 17/06/2016 imeripotiwa kwamba, ofisa wa polisi wa ngazi ya juu wa Ufaransa alikataa kumpa mkono Rais Francoise Hollande wakati wa ghafla ya kuwapa pole maaskari hao baada ya wenzao wawili kuuawa na shambulio la Dola la Kiislam (ISIS). Na baadae polisi huyo alipohojiwa na kituo cha utangazaji cha BBC alisema hakutaka kumpa mkono kwa sababu kuna matatizo mengi wanayokabiliana nayo ndani ya jeshi la polisi.

Islam El Shehaby wa Misri

Katika michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, imeripotiwa kwamba mcheza Judo wa Misri alikataa kumpa mkono mchezaji mwenzake wa Israel kwa kuonyesha hisia zake kitaifa juu ya ugomvi uliopo baina ya Waarabu na Waisrael katika Mashariki ya Kati.

Matukio kama haya ya kuonyesha hisia yapo mengi sana katika jamii kama kweli tutaamua kuyafatilia. Sasa na hili la Maalim Seif kutokumpa mkono Dk. Shein si kioja. Ni jumla ya kuonesha kile anachokiamini kwamba hakiko sawa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.