Waswahili hutumia misemo na methali nyingi na kwa mengi katika maisha yao ya siku kwa siku. Miongoni mwa matumizi ya utanzu huu wa fasihi ni kutoa tahadhari juu ya jambo fulani lililowahi kutokea katika jamii ili kuwa ndio sababu jambo lile lisitokee tena.

Mifano ya misemo hiyo ni huu “Ukikataa ya Musa, utapata ya Firauni”. Kisa cha msemo huu kimo kwenye hadithi ya Nabii Musa na mtawala wa Misri ya kale aliyefika umbali wa kujiita Mungu, Fir’aun. Nabii Musa alinasihi wana wa Izrael wamfuate yeye kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Mungu na kwamba Fir‘aun hakuwa Mungu wa kweli. Baadhi walimfuata na baadhi wakakataa maneno ya Musa kutokana na udhaifu sababu mbalimbali, ikiwemo ya udhaifu wa Musa na nguvu za Fir’au. Hatimaye gharika ilipotokea, wale wafuasi wa Musa wakaokoka na wale wafuasi wa Fir‘aun wakazama pamoja na Fir‘aun wao waliyekuwa wakimuamini kuwa ndiye Mungu wao.

Sasa ni mwezi wa tisa tangu uanze utawala wa awamu ya tano wa Rais John Pombe Magufuli na tayari msemo huu umesadifu  kwa Watanzania. Bahati mbaya ni kuwa, kwa Watanzania, yanawapata wote – walioamua kumfuata Mussa na walioamua kumfuata Fir’aun, maana hakuna aliyetoka akaenda kwenye nchi ya ahadi. Sote tumebanana humu humu.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Kutaka kuthibitisha hayo, sikiliza jinsi wananchi wananvyolalamikia vitendo vya unyanyasaji vinavyowakuta katika awamu hii ya Raisi Magufuli! Majuzi ilionekana picha wakati wa mahojiano baina ya mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) na wananchi juu ya hali ya maisha katika serikali hii mpya ya awamu ya tano. Ndipo wakajitokeza wafanya biashara ndogo ndogo wakaeleza ya moyoni pamoja na majuto yao juu ya kumchagua Rais Magufuli kutokana na machungu wanayoyapata na wanayomeza kupitia kwa watendaji wa serikali ya awamu hii ya tano.

Akinamama hao hawakusita kusema kwamba waliamua kumchagua Rais Magufuli kutokana na ahadi zake kwa akina mama kwamba watakuwa huru kufanya biashara zao, sitaki niwalaumu saana akina mama hao na wengineo kwa kufanya hivyo, kwa sababu kila kitu kina taratibu zake. Hivyo niseme utaratibu wa kupata viongozi wa ngazi mbali mbali nchini kwetu kwa sasa ni kwa njia ya mfumo wa vyama vingi ambapo kila baada miaka mitano tunafanya uchaguzi, moja ya njia sinazofanya uuchaguzi ni kuepo wagombea tofauti kutoka vyama tofauti ambao wanawasilisha sera na ahadi zao kwa wananchi, hivyo mwananchi kupitia sera na ahadi za wagombea ndipo hufanywa maamuzi ingawa kwa hapa kwetu na figisu za wizi wa kura pia hutumika japo kuwa wanaofanya hivyo wanajua yakini kwamba kitendo hicho ni kharam mutlak.

Hivyo kwa hatua hizo ndipo akina mama hao wakaeleza kwamba kupitia sera za Chama cha Mapinduzi – CCM pamoja na ahadi binafsi kutoka mdomoni mwa Rais Magufuli, hawakuwa na budi bali ni kumchagua Rais Magufuli kwa kuamini yale waliokuwa yakiwapata wakati wa utawala uliomalizika wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete yasingetokea kwa utawala wa Rais Magufuli. “Alituahidi akina mama, wafanya biashara ndogo ndogo, wote mtakuwa huru mtafanya biashara zenu kwa raha (sawa), na alihidi kusema yeye wamachinga wake, wafanya biashara ndogo ndogo wake, wauza matunda wake, hicho ndio kigezo kilichonifanya nimchague Rais Magufuli kwa kujua huenda ikawa ikasaidia. “Lakini leo hoo sioni raha, hao site (Municipal Police) aliosema watafute kazi ya kufanya, leo wapo FFU. Tunakamatwa na FFU, matunda yetu yanachukuliwa. Sasa leo zile ahadi alizotuahidi akina mama mbona mpaka saa hii bado tunanyanyasika, na wafanyabiashara ndogo ndogo hatuna raha hapa mjini. Tunauza matunda, sijui kama tunauza kitu gani yaani, kiasi kwamba kama tunauza sumu.

“Nambaya zaidi haya matunda wanaochukuwa , wanapotupa mbona sisi hatujui? Toka wameanza kuchukua hatujaona dampo wanalomwaga matunda yetu. Wanaenda kula.” Alisema mama huyo, ambaye muda wote huo amejitwika beseni lake kichwani kuashiria kuogopa kuchukuliwa beseni lake hilo na askari wa FFU, beseni ambalo lina biashara yake ambayo ndio sababu ya kukidhi maisha yake na familia yake.

Kiukweli hayo ni maneno makali sana na ya kusikitisha yaliyotolewa na mama huyo kupitia televisheni ya VoA, ambapo yamemlenga moja kwa moja Rais Magufuli pamoja serikali yake. Maneno hayo ni ishara ya kukata tamaa kwa wananchi hao juu ya serikali na viongozi wao.

Endapo Rais Magufuli akidharau kauli kama hizi za wananchi wakata tamaa na akaamini kwamba ameshafika, basi akumbuke siku hazigandi bali husogea. Miaka mitano si kipindi kirefu cha mtu kujitia sahau, juzi na jana ilikuwa Novemba 3, 2015, leo mwaka mmoja unaelekea kunamalizika kama plastiki iliyoyushwa kwenye moto.

Watanzania wa leo tafauti na wa miaka ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwaka 2020 ni sawa na siku 1,440 tu zilizobakia. Hivyo ikiwa Rais magufuli hatowajibika itakiwavyo kwa wananchi hao wanaolalamika na wanaomeza machungu ya yanayofanywa na serikali yake, basi ule msemo wa “Ukikataa ya Mussa Utapata ua Firaun” utasadifu kwa yeye kubeba lawama ya kukiua Chama cha Mapinduzi – CCM.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.