Kimaumbile hatua za makuzi ya mwanadamu yamejengwa kwenye msingi w akutegemeana. Chimbuko lake huanzia mgongoni, tumboni na kisha duniani. Azaliwaye huitwa mwana, aliyembeba miezi tisa ndani ya tumbo lake huitwa mama na yule aliyepandikiza mbegu kutoka kwenye tindi za mgongo wake akaitwa baba. Haya ndio mapitio na mnasaba baina yetu. Ni mnasaba huu umfanyao mama kumnyonyesha kiumbe huyu kwa miezi kadhaa pasi naye huyo kiumbe kula kitu chochote zaidi ya majimaji hayo yatokayo kwenye kifua cha mama. Hula maji hayo akashiba na kiu ikakatika sambamba na afya yake kuimarika.

Ili aweze kuhimili vishindo vya dunia hii iliyojaa kila aina ya vurugu, kiumbe huyu aitwaye mtoto lazima apitie mkondo fulani wa kufanyiwa kila ikhsani. Hujichafua akasafishwa, huhisi njaa akalishwa, pamoja na kufanyiwa kila jambo kutokana na madhaifu yake ya kutoweza kujihudumia. Hali hii ndani yake humfanya ajenge ukaribu sambamba na mapenzi na huruma kwa wale waliomzunguka. Haya ndio maumbile na makuzi yetu.

Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Kwa kiasi kikubwa makuzi ya mtoto huathiriwa na mila, silka na desturi ya wazazi na jamii iliyomzunguka. Kutoka hapa mtoto hubeba nakurithi vile vyote avionavyo vikitendwa au kupendelewa na walio karibu yake na ambao huwa sehemu ya maisha yake. Kwamba iwapo jamii iliyomzunguka mtoto ni yenye kupenda, kuenzi na kuthamini wazee, mtoto naye hujengeka hivyo. Kama wazazi na jamii iliyomzunguka mtoto ni ile ipendayo ushirikina, ulevi, umalaya na mabalaa mengine, mtoto naye huselemeya nakuzama kwenye khulka hio. Pia kama mtoto akizaliwa nakukulia kwenye mazingira ya wazazi au jamii yenye kuthamini elimu au amali nyingine zilokuwa njema, huyu naye atabeba bendera hio. Jee, sisi tumerithi nini?

Zipo jamii ambazo baadhi ya maumbile ni laana isiyostahili kuonekana kwa jamii hiyo. Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia kupitia runinga jinsi walemavu wa ngozi wanavyokatwa viungo na kuuwawa kinyama kwa imani za kishirikina. Tumekuwa pia tukiona vikongwe wanavyokatwa mapanga kwa kuhisiwa uchawi. Jambo moja ambalo sikuwahi kuliona ni matukio ya unyama kama huu yakifanyika kwenye visiwa vyetu vya Unguja na Pemba. Haya sikuwahi kuyashuhudia wala kuyasikia. Kwenye jamii yetu mzee alikuwa mtu wa kuheshimiwa na kuenziwa.
Pengine tukumbushane kwamba huwi kikongwe kama hujapitia utoto, ujana, na utu uzima. Kwamba kikongwe wa leo ndio mtoto wa juzi na kijana wa jana aliyetumia muda na nguvu zake nyingi kulitumikia taifa hili ambalo leo linamwita mwanga au mchawi wa kobwe! Huu ni unyama kupita unyama!
Katika makuzi yangu nimebahatika kuishi na kuona wazee wengi wa jamii yangu na jamii nyingine. Nimebahatika kuona namna uzee ujavyo na kumvaa mwanadamu kiasi cha kumrudisha utotoni. Nimeshuhudia wazee
wakijiendea haja bila kuweza kuzizuwia kama walivyokuwa watoto. Wanakaa bila nguo kama walivyokaa kwenye utoto. Wanapakatwa na kulishwa kama walivyolishwa wakiwa watoto! Jee, mimi na wewe tunaujuwa mwisho wetu?
Umasikini si kitu kizuri na pindi tuwapo na nguvu za kutafuta, tutafute kwa nguvu zetu zote na tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali muda na pesa, kwani sehemu kubwa ya udhalili wanaofanyiwa wazee kwenye jamii hutokana na umasikini wao na kukosekana kwa sera maalumu zenye kuwajali. Wengi wa wazee wenye kukumbwa na matukio ya kudhalilishwa ni wale waliokulia kwenye mazingira ya umasikini na kuzeekea humo humo. Hawa ni wale ambao hawakubahatika kupata elimu za kuwawezesha kuingia kwenye tabaka la juu au la kati, bali walikuwa na kuishi kwa kilimo cha jembe la mkono au ukwezi. Hawa ndio wale waliobebeshwa jembe na nyundo kisha vikawaumiza wenyewe! Hawa ndio wale ambao kutokana na kuishi sehemu kubwa ya maisha yao kwenye mazingira ya shida na dhiki, uzee huwajia kwenye hali ya kushambuliwa mfumo wao wa akili na kuanza kufanya mambo ambayo wenye akili huwaona wanga au wachawi!
Sehemu kubwa ya wazee waitwao wanga au wachawi ni wale ambao wanakosa huduma muhimu na hivyo hulazimika kuingia mitaani kunusuru maisha yao. Wanalazimika kufanya hivyo huku wakiwa tayari akili zao haziko sawa kiasi cha wengi kushindwa kurudi makwao kutokana na kupoteza kumbukumbu za kule walikotoka. Hawa wengi hawapati huduma ambazo kwa uzee wao walistahili kupatiwa na matokeo yake hulazimika kupita mitaani ambamo sisi tuliostahili kuwastiri tunawadhalilisha kwa kuwavua nguo na kisha kuwaita wanga! Hii nini kama sio laana!
Wiki hii nimeshuhudia tukio la kushituwa kwenye mitandao ya kijamii. Ni tukio ambalo limeelezwa kutokea hapa kisiwani Pemba kwenye kijiji kiitwacho Kipangani. Kijiji hiki kipo Konde, wilaya ya Micheweni, mkoa wa kaskazini Pemba. Ilikuwa ni vidio iliyomuonesha bibi kizee mmoja akiwa uchi baada ya kuvuliwa nguo huku mashuhuda wakipiga picha za vidio na kudai kwamba ni mwanga aliyedondoka eneo hilo. Nilisikia mashuhuda wakimsusuika kwa maneno bibi huyo kwamba kama alikuwa haijuwi Kipangani, ndio ile na ina wenyewe!
“Anajidai sijuwi mke wa nani nani, kama ulikuwa huijuwi Kipange basi ndio hii, ina wenyewe.” Inasikika sauti ya mwanamke ambaye anaonesha kila dalili ya kukosa malezi kiasi cha kutojuwa umuhimu wa kumsitiri mwanamke mwenziwe!
Hili ni jipya kwa kisiwa cha Pemba, kisiwa ambacho hakina mila na utamaduni wa kudhalilisha wazee kama inavyoonekana kwenye vidio hii, ambayo kibibi kisichopungua miaka 80 kinadhalilishwa mbele ya midume na mijike isiyojitambua na iliyojaa ujinga usio na kifani. Mama huyu ni miongoni mwa wazee wa jamii yetu wenye kurukwa na akili kwenye umri wa uzeeni. Ni mzee anayeishi kijiji cha Kiuyu Kiungani.
Baada ya siku kadhaa za kukesha bila kulala kutokana na kazi ya kumlinda mama huyu usiku na mchana, watoto wa bibi huyu walipitiwa na usingizi kiasi cha yeye kufungua milango usiku mkubwa bila watoto wake kustuka. Ndipo baada ya kuzurura usiku kwa muda mrefu, huku watoto wake wakimtafuta, bibi huyu alipatwa na bahati mbaya ya kuingia kwenye kijiji hiki cha Kipangani ambako ni dhahiri kwamba aliingia kwenye mikono ya watu wasiojuwa heshima ya uzee na wakaanza kumdhalilisha huku akiwa hana nguo. Imesadifu kwamba bibi huyu hapendi nguo kiasi cha kupelekea kufungiwa chumbani muda wote. Hili hufanyika kwa lengo la kumuweka salama na kumuepusha na udhalilishwaji wa watu wasio busara kama hawa aliokutana nao.
Tukio hili si zuri kushuhudiwa kwenye jamii ya kistaarabu kama hii ya Kipemba, ambayo mimi nilizaliwa na kukulia kisha nikahamia  Dar es Salaam. Hili ni tukio baya la udhalilishaji ambalo linafaa kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria. Ni tukio ambalo limemdhalilisha bibi huyu na familia yake pamoja na jamii nzima iliyomzunguka. Hivyo ili kukomesha udhalilishaji wa aina hii usizidi kushamiri, ipo haja kwa mrushaji wa picha hizi pamoja na mtandao uliohusika kumdhalilisha bibi huyu kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nalisema hili kwani bibi huyu si mwanga wala mchawi kama tulivyoaminishwa, bali ni mgonjwa ambaye hata polisi alikopelekwa wamelithibitisha hilo na wanamjuwa matatizo yake!
Kama kuna mambo ambayo kama jamii tunapaswa kuyakemea kwa nguvu zetu zote ni matukio ya aina hii. Haya ni matukio ambayo yanazalisha utamaduni mpya wenye ishara za laana. Kwamba wale wazee wetu ambao walitubeba matumboni mwao na kuvumilia kila aina ya usumbufu wetu, leo twawavua nguo hadharani na kuanza kuwapiga picha za vidio na kurusha mitandaoni!
Tumeshindwa kuwastiri na kuwahudumia kama walivyotufanyia wakati tukiwa vifunza na leo twawalipa malipo ya kuwasusuika maneno machafu kwa ugonjwa wa uzee ambao wengi tutaupitia! Hivi vijana wa Kipemba kweli tumekosa adabu na malezi kiasi kama hiki au ndio tumelewa usasa kila kitu kirushwe kwenye WhatsApp na Facebook!
Tuache ujinga huu kwani si aina ya ustaarabu unaoendana na mila, silka na desturi zetu. Heshima ya mzee kwenye jamii yetu ilikuwa kubwa mno. Hata kwa umri wangu wa miaka isiyozidi arubaini, ilikuwa si rahisi kumpita mzee mwenye mzigo bila ya kumpokea mzigo huo sambamba na kuufikisha kule anakokwenda pasi na kujali umbali au uzito wa mzigo huo.
Tuliwaheshimu na kuwaenzi wazee hata kama si mama au baba aliyekuzaa. Ule utamaduni adhimu wa “mzazi wa mwenzio ni mzazi wako” ulitufanya tuwe salama na tuheshimike. Tulikuwa salama kwa vile hatukujitoa fahamu na utu kama wafanyavyo vijana wengi wa sasa.
Leo kafanyiwa bibi huyu ambaye ni mama au bibi wa mwingine, tunachekelea na kurushiana picha mitandaoni,  lakini tukumbuke kwamba “kama tadinu tudani”. Kama leo umeshindwa kuchukua hatua kukemea fedheha na udhalilishaji huu aliofanyiwa bibi wa mwenzio, kesho itakuwa zamu ya bibi yangu au wako ambaye anastahili heshima na stara zetu. Au itakuwa zamu yetu sisi wenyewe tukishakuwa wazee na vikongwe.
Nimetimiza wajibu wangu kwa jamii yangu. Kazi kwenu!
TANBIHI: Makala ya Ahmad Abu Faris. Anapatikana kwa simu nambari 0774581264.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.