Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipanga ratiba ya kutolewa kwa elimu ya uraia kwa miezi 18 ndipo tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi. Hii nadhani ingesaidia kuondoa maafa na dosari nyingi zinazojitokeza katika nchi yetu, lakini inasemekana wakubwa wetu wakakataa bila kutoa sababu za msingi zinazoweza kuzipinga na zile alizozitoa Jaji Nyalali zikiwemo kuutambuwa vyema mfumo wa kiutawala wa vyama vingi kutoka ule wa chama kimoja, kujuwa hasa kazi na majukumu ya Mbunge awapo Bungeni na Jimboni, wajibu wa raia na mambo mengine mengi mazuri ambapo ingelikubalika kufanya hivyo, nadhani taifa letu lingeshapiga hatua kubwa na kufika mbali zaidi.
Kwa kukataa kwetu ndio sasa nchi imekuwa inaongozwa kwa mfumo wa kubahatisha, lakini pamoja na kubahatisha kwetu pia hatufikii mafanikio hasa ya hicho tunachokibahatisha kwa kuendekeza woga, aidha huwa woga wa kuogopa kuitwa msaliti, ndumilakuwili na majina mengine yaudhio na kukera huku tukiliacha taifa katika giza na mkwamo wa matopeni.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Maelezo yangu hayo ya awali yamekuja baada ya kukerwa mno na taarifa ambayo imechapishwa na gazeti la Nipashe la siku ya Jumapili (9 Julai 2016) na ikisha kupewa kichwa cha habari kisemacho, “Waziri wa JK amuangukia Magufuli”. Ukisoma gazeti hilo utagundua kwamba mbunge huyo ameacha kufanya kazi yake wakati alipotakiwa kufanya badala yake anatoa maoni yake katika magazeti.
Cha kushangaza wakati bajeti ya mwaka 2016/17 tangu inaanza kusomwa na hadi kupitishwa, Mahmoud Hassan Mgimwa – ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini – hakuwa miongozi mwa wabunge waliotoka kwa kutoridhia kilichokuwa kinaendelea bungeni ambapo baadhi ya wabunge waliamua kutoka ili kupingana nacho na wala hakutolewa bungeni kwa kukiuka kanuni na sheria za bunge, kwa lugha nyepesi yeye alikuwa shuhuda wa hicho anachokipinga sasa kupitia waandishi wa habari na magazeti.
Katika Serikali iliyopita ya awamu ya nne iliyoongozwa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mh. Mgimwa yeye alikuwa ni Naibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo katika Bajeti hiyo ya mwaka 2016/17 eneo analolipinga na kumuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliangalie upya ni hilo eneo la tozo na kodi mbali mabli zinazohusiana na utalii ambazo zitatozwa ili kuengezea mapato serikali.
Bajeti hiyo ilipitishwa mnamo tarehe 20 Juni 2016, ambapo ni ya kwanza kwa Serikali ya Rais Magufuli, ilipitishwa kwa kishindo kikubwa kwa kuwa ndani ya ukumbi huo wa Bunge ni wabunge wa Chama tawala (CCM) pekee ndio waliokuwemo bungeni humo baada ya wale waupinzani kutoka bungeni kwa kutokuridhishwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Arkson anavyoliendesha bunge, hivyo hatua hiyo ya kupitisha Bajeti hiyo hakukuwa hata mbunge mmoja aliyepinga kwa waliokuwa barazani humo akiwemo yeye Mh. Mgimwa.
Katiba eneo analolalamikia na kuanisha kwamba ni khatari kwa serikali ni pamoja na kutoza VAT katika shughuli zote za kiutalii, ikiwemo kuangalia ndege, wanyama pori, kupanda vilima (Kilimanjaro, Mara n.k), usafirishaji watalii, uongozaji watalii na kadhalika.
Mgimwa alielezea hofu yake juu ya tozo hiyo ya VAT katika utalii kwa kupigia mfano nchi ya Kenya kwa kusema kuwa, “Kimiundombinu washindani wetu Kenya wamepiga hatua zaidi. Tulichopaswa kufanya ni kujitengenezea utaratibu wa kuhakikisha tunawazidi katika eneo hilo, rasilimali tulizonazo zinavutia zaidi kuliko za kwako (Kenya), ndio maana tunasema utalii wetu unazingatia quality na sio quantity, ndio maana tuliingiza watalii wachache waliolipa fedha nyingi.”
“Lengo letu sio kushindana na Kenya bali ni kuhakikisha Sekta ya utalii inakuwa kwa kiasi kikubwa na pia kufanya utalii wa ndani rahisi”

Mgimwa amezungumza maneno mengi yaliyo mazuri lakini wazungu husema “right message at the wrong place” ni sawa na kwenda kutoa mawaidha katika kilabu cha pombe, kwani ameacha kufanya kazi anazotakiwa kufanya kama Mbunge, ambapo angesimama bungeni kabla ya kupitishwa akatoa ufafanuzi huo wa kitaalamu, ikizingatiwa yeye amehudumu katika sekta hiyo ya utalii katika serikali ya awamu ya nne akiwa ni Naibu waziri, ukizingatia yeye pia ni Mbunge wa CCM ambacho ndicho chama kinachoongoza Serikali naamini angefahamika na hoja yake kukubalika, lakini alibakia kimya tangu wakati wa majadiliono ya bajeti mpaka kupitishwa kwake, sijui ni ule woga, hofu ya kuitwa msaliti na ndumila kuwili kitu kilichopelekea na yeye mwenye kukubali kuingia katika “Hansard” za bunge kwamba ameshiriki katika kupitisha bajeti yenye kasoro anazoziainisha sasa kupitia vyombo vya habari na magazeti.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.