Ilikuwa tarehe 15 Juni 2016 ambapo katika kijiji cha Kiungoni na maeneo mengine mengi ya ukanda wa mashariki wa kaskazini mwa kisiwa cha Pemba yalifanyiwa  matukio kadhaa ya unyanyasaji na utesaji dhidi ya raia. Kuna ushahidi unaothibitisha kuwa unyama na udhalilishaji huu ulifanywa na kusimamiwa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambavyo kimsingi vina dhima na wajibu wa kulinda usalama wa watu na mali zao.
risasi2
Wakaazi wa kijiji cha Kiungoni, kaskazini Pemba, wakionesha magamba ya risasi zilizotumika wakati kijiji chao kilipovamiwa.

Wakaazi wa ukanda huo wanasimulia namna vikosi hivyo vilipoanza kupita kijiji kwa kijiji kufanya hujuma ya kupiga watu pamoja na kuwaibia mali zao, kama vile baiskeli, fedha taslimu na seti za televisheni.
Haya yalianza kwenye kijiji cha Shengejuu, umbali mdogo kutoka Kiungoni,  ambapo vijana kadhaa waliokuwa wakitoka masomo ya usiku, walisimamishwa, kupigwa na kisha baiskeli zao kuchukuliwa na vikosi hivi. Hadi leo, baadhi ya baiskeli hizo zipo kwenye lango la kuingilia mapokezi ya makao makuu ya Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Wete.
Baada ya kufanya tukio hili kwenye kijiji cha Shengejuu, vikosi hivyo viliingia kwenye kijiji cha Kiungoni, kilikotumia risasi za moto na plastiki sambamba na mabomu ya machozi kuelekea majumba ya wanakijiji, ambamo ndani yake walikuwamo pia wanawake, wazee wasiojiweza na watoto.
Hujuma na wizi kwenye eneo hili la Kiungoni ilitia fora, yumkini kutokana na uhalisia wa eneo hilo lilivyo. Kiungoni ni kijiji-mji unaokuwa kwa kasi kwa biashara. Kina maduka makubwa zaidi ya nguo kupita eneo jingine lolote kwenye barabara ianziayo Meli Tano, Wilaya ya Chake Chake hadi Wingwi, Wilaya ya Micheweni, kupitia Kiuyu na Madenjani, Wilaya ya Wete. Barabara hii inaitwa kwa umaarufu wa “Njia ya Kojifa” na wenyeji wa kaskazini Pemba, au njia mpya na madereva wa madaladala.
Ahmad Juma
Na Ahmad Abu Faris

Wenyeji wa maeneo hayo wanasema ni Kiungoni ndipo vikosi vya SMZ vilipofunga kazi kwa kupiga mabomu, risasi za moto na plastiki, na kisha baada ya taharuki na watu kutawanyika, vikosi viliingia madukani na kuanza kukomba manoti, seti za televisheni na baiskeli zaidi ya sita. Katika “utwaaji huo wa ngawira”, duka moja lilivunjwa na pesa taslimu milioni nne na ushei sambamba na vocha vilichukuliwa na vikosi hivyo.

Tukio hili lilikuwa na ishara zote za uhalifu sawa na ule ufanywao na majambazi watumiao silaha katika maeneo ya Bara – hasa miji ya Dar es Salaam na Arusha. Kwa hivyo, wananchi waliofikwa na kadhia hii waliamua kwenda kufungua malalamiko katika Ofisi za Makao Makuu ya Polisi, Wete, ambako walipatiwa RB yenye namba 1070.
Binafsi nilifika eneo hili siku ya pili yake na kukutana na wazee kadhaa waishio hapo, miongoni mwao ni Bwana Omar Ismail, ambaye nilifanya naye mahojiano kuhusu kadhia hiyo kwa urefu. Bwana huyu mrefu kidogo na mwenye kufuga ndevu nyingi alinisimulia kila kitu kuhusiana na uvamizi wa vikosi kijijini kwao sambamba na wizi ulioacha umasikini kwa baadhi ya watu.
Ni yeye aliyekuwa kiongozi aliyeongoza timu ya wananchi kadhaa kwenda kufikisha madai ya wizi huo polisi ya Wete na ni yeye aliyeongoza kundi la wazee wenzake kunionesha maganda kadhaa ya risasi za moto na plastiki kama uthibitisho kwamba walichokifikisha polisi hakikuwa uzushi kama ambavyo jeshi la polisi limekuwa likidai, bali tukio la kweli na lenye ushahidi rasmi. Nilichukuwa maelezo yao kwa kila njia – maandishi, picha na sauti. Ni picha zake na wenzake ambazo nilizituma baadaye kwenye mitandao ya kijamii, naamini kuwa ndizo zilizokuja kumchongea bwana huyu kwa vyombo vya dola kama nitakavyoonesha hapo baadaye.
Nilifanikiwa kufanya mahojiano pia na wahanga wengine kadhaa wakiwemo watoto wadogo na kinamama, na wote walielezea namna walivyokoseshwa amani na vikosi hivi ambavyo vimezowea kupita nyakati za usiku na kupiga raia ovyo. Miongoni mwa niliowahoji ni mtoto mdogo wa miaka 13 aitwaye Ali Said. Huyu nilishamuelezea kwenye makala zangu zilizopita juu ya tatizo lililomsibu baada ya uvamizi wa vikosi hivi muda wa usiku, ambapo hadi leo amejikuta na tatizo la kushindwa kuzuia haja ndogo zisimtoke.
Hadithi ya Ali ilikuwa ya kusikitisha sana, hasa kwa sababu ya umri wake, nami nikaamua  kufunga safari moja kwa moja hadi makao makuu ya jeshi la polisi, Kilimandege, mjini Wete. Niliingia mapokezi na kueleza shida yangu na kupewa kitambulisho maalumu na kisha kuelekea ofisi husika.
Kwa ukubwa wa kadhia yenyewe, nilipaswa kukutana na kamanda wa polisi wa mkoa wa Kaskazini Pemba, ambaye kwa bahati mbaya hakuwepo na nafasi yake kukaimiwa na RCO wake, Bwana Issa Juma. Niliingia ofisini mule na kumkuta Afande Issa amejaa kwenye kiti akitoa maelekezo ya kikazi kwa maofisa wa chini yake. Nililazimika kusubiri kwa dakika kadhaa ili kumpa muda amalizane na maofisa hao, ambapo mara alipomaliza ikawa zamu yangu kueleza kilichonipeleka ofisini mwake.
Mwanzoni, Afande Issa alikuwa mzito mno kufanya mahojiano nami kwa madai kwamba yeye hakuwa msemaji rasmi wa polisi, bali alikuwa anakaimu kwa muda. Nikamueleza kwamba iwapo yeye ndiye kaimu, basi pia alikuwa na wajibu kwa kile anachokikaimu, kwani hakuna wajibu usio mamlaka. Hoja yangu kwake, na ambayo baadaye aliikubali shingo upande, ni kuwa ndani ya ukaimuji wake, umo pia wajibu wa kujibu masuali ya wanahabari juu ya kadhia mbali mbali.
Alijaribu kujikurupusha, lakini sikumpa mwanya na nikaendelea kumtawiza ili auone mstari wa wajibu huo, na hatimaye akakubali na ndipo nikampa mmaelezo ya kile nilichohitaji kumuhoji.
Hapa naye akaanza kunipa ufafanuzi wa kadhia zote anazozifahamu kwa mtazamo wake, likiwemo suala la watu kuvamia na kuharibu shamba la mtu aliyemtaja kwa jina la Dadi Faki Dadi huko kwenye kijiji cha Finya na pia tukio la shamba la migomba kuvamiwa na kukatwa na aliodai watu wasiojulikana huko kwenye kijiji cha Mtambwe.
Alinieleza kwamba katika tukio la Mtambwe, migomba zaidi ya 140 ilikatwa. Nilijuwa kuwa anatia chumvi, maana mimi nilishafika kwenye shamba hilo na kushuhudia tukio la uharibifu huo siku mbili nyuma na idadi aliyoitaja haikuwa ya kweli. Lakini kwa vile hili la migomba alikuwa amelileta yeye, sikuwa na sababu ya kuimbishana naye.
Nilimsikiza kwa umakini na baada ya ufafanuzi wake, nikamtaka ayaeleze yale kwa njia ya mimi kumrekodi ili jamii anayoitumikia imsikie. Alikubali na kuanza mahojiano,  ambapo alisimamia nukta kwamba yale yanayotokea kwenye vijiji mbalimbali kisiwani Pemba, ni katika jitihahada za polisi kuimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo ili kuzuwia hujuma ambazo alieleza kushika kasi.
Hata hivyo, nilipomuuliza kwa nini uimarishaji huu wa ulinzi hufanyika mitaani waishimo raia na sio maporini kwenye mashamba husika na tena unafanyika kwa njia za watu kuvamiwa na kupigwa huku wengine wakilazimika kukimbilia maporini usiku na watoto, Afande Issa alikanusha hili na nilipomueleza kwamba ninao ushahidi wa hilo kupitia maganda ya risasi zilizopigwa Kiungoni na sauti ya mtoto Ali Said akielezea hilo nililomuuliza, alikuja juu na kudai kwamba nimekwenda ofisini mwake kwa lengo la kutaka kumfukuzisha kazi!
Kutoka hapa akasimama kana kwamba kiti chake kilikuwa na sindano na kusogea hadi nilipokuwa nimekaa akinitaka nifute sauti yake kwenye kinasa sauti changu. “Ahmed tafadhali nakuomba ufute hiyo sauti kabla hujaniingiza kwenye matatizo. Nakuomba kama kaka yako niliye na familia ya watu kumi na saba wanaonitegemea. Tafadhali ifute.” Nataka nikiri kuwa katika umri wangu wote wa kuishi, sikuwahi kumuona afisa wa ngazi za juu wa usalama wa raia na mali zao akionesha sura ya kinyonge kama siku hiyo nilivyoiona kwenye uso wa Afande Issa.
Huruma zikaniingia kwa fadhaa iliyomkumba afande huyu, moyo wa kibinaadamu ukanigonga, hasa aliponitajia kuwa ana familia kubwa inayomtegemea na kwamba mazungumzo yetu yalikuwa yanaihatarisha kazi yake. Nikiri tena kuwa nilifanya kosa la kibinaadamu kwenye kazi yangu. Maana sitakiwi kuwaamini watu kiasi kikubwa kama hicho. Nikakubali kuifuta sauti ile kwa makubaliano ya kurekodi upya bila kuuliza suali ambalo lingemfanya ataharuki.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, mara tu baada ya mimi kuifuta sauti ile, yeye Afande Issa alikataa kufanya tena mahojiano mengine nami na badala yake akaniomba nimpe robo saa ya kuwaulizia watendaji wa chini yake kwa vile yeye hakuwa na taarifa sahihi ya matukio hayo ya watu kuvamiwa na kupigwa nyakati za usiku. Nilikubali na nikampa muda aliouhitaji.
Lakini wakati nikiwa mapokezi kusubiri muda alionipa, ghafla nikamuona akishuka na begi lake mkononi na nilipomuuliza mbona anaondoka bila kunipa maelezo ya kilichonipeleka kwake, Afande Issa alijibu kwa mkato kwamba hawezi kulielezea suala hilo na harakaharaka akajitia garini mwake na gari ikaondoka!
Kitendo alichokifanya Afande Issa siku hiyo kilikuwa na maana na tafsiri kadhaa kwangu kama mwandishi ambazo nisingependa kuzianika. Hata hivyo, jambo moja napenda lieleweke kwamba huyu ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa masuala yote yahusuyo upelelezi katika mkoa wa Kaskazini Pemba. Kuniambia kuwa hakuwa na uwezo wa kunieleza kinachotokea kwenye eneo lake la kikazi kulimaanisha kuwa ama ni afisa wa usalama anayeficha ukweli au ni mtendaji asiyekuwa makini kwenye kazi zake.
Kilichotokea baada ya siku hiyo, ni taarifa za Bwana Omar Ismail wa Kiungoni kuvamiwa nyumbani kwake usiku wa manane, ambapo alichukuliwa na watekaji nyara wake hadi viwanja vya Mnazi Mmoja, Wete, ambako alipigwa kukaribia kupoteza maisha na kisha kwenda kutupwa kwenye ofisi za makao makuu ya polisi, Wete, jengo lile lile ambalo siku nne nyuma alikuwa amekwenda kufungua malalamiko ya kijiji chao kuvamiwa, kushambuliwa kwa risasi na kuibiwa mali zao, akiwa na ushahidi wa maganda ya risasi.
Bwana Omar, ambaye wakati naandika makala hii yumo mikononi mwa jeshi la Magereza kisiwani Unguja, licha ya kupewa dhamana na mahakama inayosikiliza kesi yake aliyofunguliwa na polisi ya kumzomea Sheha wa Shehia ya Pandani, Bwana Said Hamad Shehe (Mshihiri). Kisa cha kufika Unguja ni kwamba kile kipigo alichopigwa na watekaji nyara wake, kilimpelekea maumivu makali ambayo hata Hospitali ya Wete ilishindwa kumtibu, ikaamua apelekwe ya Mkoani, nako ikaonekana hakuna uwezo wa kumtibu na hivyo kuhamishiwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kisiwani Unguja, akiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Nilipata bahati ya kumtembelea akiwa hospitali ya Mnazi Mmoja, na ndipo nilipojuwa kuwa yuko mikononi mwa askari wa magereza. Nilishangaa Omar tayari alishapata dhamana ya mahkama ili aende akatibiwe. Dhamana hii ilifikishwa kwa Idara ya Magereza Pemba ambako Omar alipelekwa, lakini hadi naandika makala hii, Idara ya Magereza Unguja inadai haijapata taarifa ya dhamana hiyo kwa njia rasmi za maandishi na badala yake wamepata simu tu kutoka idara hio kwa upande wa Pemba, na kwa mantiki hiyo hawawezi kumuachia.
Hiki ni kituko cha makusudi na dharau kwa mahakama, ambacho hata hivyo kinaelezea nini hasa kinachoendelea visiwani Zanzibar hivi sasa, ambako katiba, sheria, na kanuni za utawala wa sheria zimewekwa kando. Suala la mawasiliano ya ndani ya idara hii ya magereza halimuhusu Bwana Omar, bali ni suala la kiutendaji wa ndani yao, lakini kilichopo ni ukiukwaji mwingine wa haki zake za msingi na kumuuwa mgonjwa huyu kisaikolojia.
Binafsi naliweka jukumu la suala zima la Kiungoni na la Bwana Omar na yule mtoto Ali Said kwenye mabega ya Afande Issa, RCO wa Kaskazini Pemba, ambaye mule mwenye ofisi yake siku ile alinilalamikia nisiyaripoti mazungumzo baina yangu naye kwa kuwa yangemchongea kazini kwake, naye ni baba mwenye familia ya watu 17 wanaomuangalia. Kwa msisitizo huo huo, nataka Afande Issa ajuwe kuwa Bwana Omar naye ni baba, na mtoto Ali Said naye ni mtoto kama walivyo watoto wake.
Afande huyu na wenzake waelewe kwamba dunia inayafuatilia yanayotokea kisiwani Pemba hata kama yeye akikataa kutoa ushirikiano kwa wanahabari kwa lengo la kuyaficha. Aelewe kwamba yaliyomkuta hayatopita hivi hivi tu, yataendelea kutangazwa, kusomwa na kusikilizwa kila mahala tena na tena, bila khofu wala woga. Dhulma aliyofanyiwa Bwana Omar ni kubwa kiasi ambacho kuna hatari ya kupooza mwili kutokana na kipigo alichopigwa na wateka nyara wake.
Akiwa kama mkuu wa upelelezi kwenye mkoa wake, anahusika na nani anakamatwa, nani anashitakiwa. Na kwa moyo huo, ndio maana ninamtaka aeleze nini hasa kosa la Bwana Omar hata ikabidi kuchukuliwa nyumbani kwake usiku wa manane, tena baada ya nyumba yake kuvunjwa milango, na kwenda kupigwa hadi akapotea fahamu na kisha kubwagwa kituo cha polisi? Je, ndio ni kwa sababu ya hilo kosa la kumzomea sheha au ni ule ushujaa wake wa kusimama na kuionesha dunia dhulma wafanyiwazo wanyonge wa Pemba kwa kumuonyesha mwandishi wa habari maganda ya risasi zilizotumiwa?
Toka hadharani Afande Issa Juma uieleze dunia kutohusika kwenu polisi iwapo maganda ya risasi yamekamatwa na kesi imefunguliwa? Wako wapi waliohusika kama hamuwalindi na kuwafadhili kwakuwapatia silaha ambazo zilipaswa kuwa kwenye dhamana yenu? Njoo hadharani usijifiche, utueleze ni kina nani waliomtesa Bwana Omar kama sio polisi walio chini yako?
Nimalizie kwa kusema kuwa kwa hakika Zanzibar ipo njiapanda na sasa ni wazi kwamba panahitajika maamuzi ya kiutashi kuinusuru nchi isitumbukie kwenye dimbwi la machafuko na umwagaji wa damu zaidi ya huu ambao hadi sasa unafanywa na upande mmoja tu wa wenye madaraka dhidi ya wanyonge wa Mungu wasio mbele wala nyuma.
Ni wazi kwamba ipo haja kwa wanaharakati wa haki za binadamu kujitokeza hadharani kuipinga hali inayoendelea sasa Unguja na Pemba. Umefika muda sasa wa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria – viwe vya ndani au vya kimataifa – wale wote wanaoshiriki moja kwa moja au wanaoshiriki kwa kuruhusu au kuachia na kushabikia mateso dhidi ya raia. Wanasheria, wanaharakati na waandishi wasimame kidete kuhakikisha wale wote wanaorundika watu kwenye polisi bila kuwafikisha mahkamani kama ilivyo utaratibu, wanapandishwa kizimbani ili wajielewe kwamba nchi ina sheria na vyeo vyao ni dhamana tu ambayo haiwafanyi kuwa juu ya sheria.
Sambamba na hili la mateso dhidi ya raia ambao wengi walengwa wake ni wale wenye mrengo wa upinzani lazima likemewe na likomeshwe. Ipo pia haja kubwa kuyafanyia uchunguzi wa kisayansi haya matukio ya kubuni ya uchomaji mashamba na majengo, ambayo mara nyingi yamesadifu kumilikiwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee. Upo ushahidi kwamba matukio haya ni ya kupangwa kwa lengo la kuwakomoa wanaodaiwa wapinzani kwa vipigo na mateso.

Sasa ili kuondoa fitna hii, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iunde haraka sana jopo la wataalamu, ambalo litapita na kuwahoji wote waliodai kuhujumiwa mali zao, sambamba na wale wanaodaiwa kuhujumu.

Natoa wito kwa taasisi hizo ulisaidie jeshi la polisi, kwani mpaka sasa jeshi hilo limejigeuza kuwa tawi la kisiasa la CCM na hivyo haliwezi kuitekeleza kazi ya kulinda raia na mali zao bila kushirikisha utashi wake wa kisiasa.

TANBIHI: Makala ya Ahmad Abu Faris. Anapaatikana kwa simu Na.  0774581264.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.