Mimi siamini lakini nafarijika kwamba hata yale makundi ambayo hupanga na kuratibu uigizaji unaoendelea kwenye vijiji mbalimbali visiwani Unguja na Pemba, nayo pia hayakubali. Hayakubali kwa maana kukubali ni kule kutenda jambo pasi na nafsi kujuta au kujawa na huzuni baada ya mtu kutenda jambo lenyewe. 
Nimebahatika kuona matukio kadhaa ya kusikitisha yakifanyika dhidi ya jamii niliyomo ndani yake. Na huja kuujuwa ukweli wake
pindi tu nionapo tukio husika, maana ukweli na maigizo hubeba taswira zisizoweza kufichika hata zikifichwa. Daima ya viwili hivi ni ardhi na mbingu saba.
Siku moja ya hivi karibuni nilifika eneo liitwalo Pembeni – kijiji kilichopo baina ya vijiji vya Pandani na Shengejuu, katika wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba. Kilichonipeleka huko ni kadhia ya watu kukamatwa kwa madai ya uchomaji moto nyumba moja ya mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa jina anafahamika kama Ali Hamad Basha. Nilikutana na Bwana Ali akiwa njiani kujipatia mahitaji dukani, lakini baada ya kujitambulisha kwake akaridhia kuongozana nami hadi nyumbani kwake ambako tulipokelewa na mkewe, Bi Raya Seif, ambaye kwa ukarimu mkubwa aliniwekea busati jipya ili mgeni wao nikaliye!
Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Hapo nikataka kujuwa undani wa kadhia yao ya kuchomewa nyumba moto, ambapo Bwana Ali alianza kunielezea hadithi yenyewe kwa kadiri alivyoifahamu, lakini ghafla mkewe, Bi Raya, akaingilia kati, kwa madai kuwa mumewe hakuwa akikumbuka kila kitu. “Ntu wenyiwe ulikuwa kun’lala wakoroma amba pono, watakakumbukani?” Alisema mama huyo, ambaye ana ufasaha na umahiri mkuwa zaidi kwenye kukielezea kile kilichopangwa.

Kwa simuizi za Bi Raya, moto uliwashwa na watu wasiojuilikana lakini akanitaka nifahamu kuwa watu hao ni wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao ni majirani zao. Kila alivyokuwa akinieleza, hata hivyo, alikuwa anawacha wazi maeneo yanayojaa alama za kuuliza, nami nilipomuuliza alionekana dhahiri kukosa majibu yake kiasi cha kuonesha ubabaifu wa wazi na kupoteza ule ufasaha na umahiri wake wa kuzungumza.
Kwa mfano, nilitaka kujuwa kutoka kwa wote wawili ilikuwaje wakaugundua moto ukiwa tayari unawaka paani na kisha wakaweza kuokoa vitu vyao vyote vya thamani, kabla ya msaada wa majirani, ambao walisema walikuja haraka kuwasaidia, na hawakuwa na jawabu.
Kwa kuwa kwenye masimulizi yao walitajwa majirani, ama kwa wema au kwa ubaya, nikafuata maadili ya kazi yangu ya uandishi wa habari wa kupata upande wa hadithi hiyo kutoka kwa majirani wenyewe. Nao walinieleza wazi kwamba ni kweli walishuhudia nyumba ikiwaka usiku baada ya kusikia kelele za kuomba msaada kutoka kwa familia hiyo. Lakini pia walikuwa hawaamini kwamba nyumba ya Bwana Ali na Bi raya  ilichomwa na mtu kutoka nje ya nyumba yenyewe kwa chuki za kisiasa, bali wenyewe wenye nyumba ndio walioamua kuichoma nyumba yao “kwa hizo hizo chuki za kisiasa!”
“Sikiliza bwana muandishi, moto wa kuti hauzuiliki kirahisi vile, kaskazi hii.” Mmojawapo aliniambia na mwengine akaongeza kuwa: “hata kama Ali Basha angekuwa na faya (kikosi cha zimamoto), asingeweza kuudhibiti moto wa makuti makavu yaliochoka kama ya kwenye paa lake. Wasitutafutie balaa apa kijijini.” Jirani huyu aliniambia kuwa ni mmoja wa walioshiriki kuzima moto kwa maji ya ndoo!
Huo ni mkasa mmoja uliotokea kisiwani Pemba na ambao umekuwa moja ya sababu ya watu wa Pembeni na vitongoji vyake kuandamwa na makundi ya serikali na vyombo vya dola wakiadhibiwa kila mara kwa “kuchoma moto”.
Ukweli na uongo wa jambo hilo na mengine utakuja kunibainikia takribani mwezi mmoja baadaye na hapo, baada ya kutembelea maeneo ya Kisauni, Langoni, kisiwani Unguja, wiki iliyopita. Nilifika eneo hilo nikiwa nimeongozana na mwenzangu na nikapata bahati ya kuketi kwenye kijiwe kimoja jirani na msikiti mkubwa uliopo chini ya barabara. Kijiweni pale nilijumuika na vijana watatu ambao hapana shaka walikuwa ni wenyeji wa eneo lile. Kama ilivyo kawaida yetu vijana wa Kizanzibari, ilinichukuwa muda mdogo kuweza kuzoweana nao na ikawafanya wasiwe na khofu na hivyo kuzungumza kwa uhuru mpana na kujiamini pamoja nami.
Mambo yalikuja kuwa mazuri zaidi baina yetu, baada ya mimi kupokea simu kutoka kwa rafiki yangu niliyeishi naye kipindi kirefu katika jiji la Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo ya simu, ambayo yalisikika wazi na vijana wote niliokuwa nao kwenye kijiwe kile kutokana na sauti kubwa itokayo kwenye tablet yangu, rafiki yangu huyo alinitania kuhusu watu kulazwa saa moja kutokana na bakora za mazombi. Nikamueleza kwamba hayo hayafanyiki Unguja ambapo kwa wakati huo nilikuwepo, bali kisiwani Pemba ninakotokea. Akaendelea kwa kugusia suala la wana CCM kukatiwa miti kwenye mashamba yao pamoja vipando kama vile migomba na mihogo. Wakati rafiki yangu akizungumza nami, kijiwe kilikuwa kimya kusikiliza mazungumzo yetu na huku vijana wale kukishangaa kifaa nilichotumia kwa mawasiliano – tablet ambayo ni mzigo wenye upana unaokaribia futi moja!
Mara baada ya kumaliza mazungumzo ya simu, mmoja wa vijana wale akataka kujuwa bei ya mzigo huu wa tablet. Nikamtajia bei ambayo aliishangaa: “Hizo pesa zinatosha kununua kiwanja bro!” Akanishangaa.
Wakati utani baina yetu ukiendelea, nikagundua kuwa mmoja wa vijana wale (hapa nitamuita Bro X) alikuwa kimya akisikiliza tu mzaha wa wenzake bila kutia neno. Alibaki kusikiliza na kutabasamu ingawa ndani yake alionekana kujaa mazito yenye kuukereketa moyo wake. Udadisi wa kiuandishi ukaniongoza kumvuta kwenye anga zangu ili anifunulie moyo huo. Nikamtengezea mazingira ya kutapika kwa kujinafasi ili nifaidike. Na, naam, akajaa teletele na akaanza kufunuka.
Bro X alizizongowa picha mbaya za matukio ya udhalilishaji aliopata kuushiriki au kuushuhudia dhidi ya watu wa kisiwa cha Pemba wakifanyiwa kupitia vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Namna alivyokuwa akizungumza kwa uchungu nikagunduwa kuwa Bro X alikuwa amejawa na maudhi ambayo sasa amechoka kuyabeba kifuani na ameona bora ayatuwe kwa kuyatapika hadharani. Alitapika nami nikajipa muda wa kunuka matapishi yake! Nikaona hii ni fursa ya mimi na kila aumizwaye na unyama wa vikosi hivi ambao huwezeshwa kwa kila aina ya nyenzo na serikali ili vikomeshe vizuri wale wote walioinyima kura CCM!
Bro X akaeleza namna walivyokuwa wakichukuliwa usiku mkubwa kutoka kwenye makambi yao hadi kwenye mashamba wakiwa na mapanga, mashoka na majisu kwa kazi ya kuharibu miti na vipando kwenye mashamba ya wana-CCM. Akaeleza kwamba haya hufanyika usiku mkubwa chini ya maelekezo na wana-CCM wenyewe, ambao baadaye huibukia polisi kupeleka mashtaka kwamba wameharibiwa mashamba yao. “Wenyewe wenye mashamba wanakuwepo na kazi yao kubwa huwa ni kutuonesha mipaka ya mashamba yao ili tusiharibu mashamba ya wengine wasiokuwa wana CCM!”
Bro X, ambaye sasa nilishafahamu kuwa naye ni katika hao mazombi, alikwenda mbali hadi kueleza idadi ya matukio waliyofanya likiwemo shamba la mtu aliyewahi kushika nyadhifa kubwa serikalini na lile tukio la karibuni katika mkoa wa Kusini Pemba, ambako mwenye shamba aliahidi kukusanya waganga wa Pemba nzima kusoma halbadiri, endapo wahusika wasingejitokeza ndani ya siku kumi na nne! Hivi ninapoandika umeshakaribia mwezi na hakuna ajuwaye ikiwa bwana huyo anao uthubutu kweli wa kusoma halbadiri.
Maelezo ya kijana huyu alieajiriwa kwenye kikosi cha serikali yalinifariji na kunituwa zigo la fikra nyingi lililotamalaki kwenye kichwa changu – zigo la masuali ambayo mara nyingi hujiuliza pasi kupata majibu yake. Maelezo yake yalitosha kunishibisha na kuimaliza kabisa kiu yangu ya kutaka kujua mbinu halisi zitumikazo kuhujumu mashamba na wale watekelezaji wa hujuma hizo. Huyu alimaliza kiu yangu na nikamuhisi kama samaki shujaa ambaye ana mengi ya kusema lakini mdomo wake umejaa maji. Lakini nikamuhisi pia kuwa naye amejihisi kama amelitua zigo kubwa kutoka kifuani pake na ninaamini kuwa usiku huo alilala usingizi mnono, kwa kujuwa kuwa mimi aliyenisimulia ni mwandishi na nitayasimulia maneno yake kwa ulimwengu.
Hatua ya SMZ kunipoka kibali cha uandishi kimepelekea nijuane na mwanahabari mmoja ambaye ni muajiriwa wa serikali. Mwanahabari huyu alinieleza jinsi wao kama waandishi wa habari wasivyoweza kuitetea jamii ambayo watawala wameigeuza kama gunia la mazowezi kwa vikosi vyao vya ulinzi. Akanionesha namna walivozibwa midomo kwa kitisho cha ajira ya shilingi 150,000  walipwayo kila mwezi. Ni huyu aliyenisimulia kadhia ya mauwaji ya mwaka 2001 wakati huo Amiri Jeshi Mkuu akiwa Benjamin Mkapa. Alinieleza namna watu walivyomiminiwa risasi kwa makumi akishuhudia kwa macho yake “utadhani popo”, kwa maneno yake.
Kubwa na baya ambalo bwana huyu linamuuma ni ile hali ya yeye kushindwa kuyaandika haya kwa kulinda kibarua chake. Hapa bwana huyu akanisimulia mkasa wa kutisha wa namna walivyolazimishwa na watawala wa Zanzibar kuandika kisichokuwepo kwa lengo la kuficha kilichopo. Alinisimulia mkasa wa bibi mmoja kada wa CCM namna siku moja alivyoropoka maneno baada ya kushawishiwa akubali nyumba yake ichomwe kisha apatiwe fidia na inayoitwa “Kamati ya Maafa” ya chama chake. Katika hali ya kutojuwa, bibi anaeleza kwamba yeye alikubali nyumba yake ichomwe kwa vile kamati ilimuahidi kumuezekea makuti mengine mapya na kuikarabati nyumba yake, kwani tayari mapaa na makuti yake yalishaliwa na mchwa!
Kauli hii ikamfanya kiongozi wa kamati amzuwie bibi huyo kuendelea kubwabwaja, huku akimtaka muandishi yule asiyaandike maneno yale kwenye habari yake. Kiongozi wa kamati alisingizia kuwa “uzee ndio uliomfanya bibi aropokwe!” Na kweli mwandishi huyu akashindwa kuandika kama alivyoeleza bibi yule, si kwa utashi wake bali kunusuru kibarua chake kwani yeye na ajira hii ya serikali, ni mithili ya mfungwa asiye  na haki ya kuchagua gereza! Huyu naye nilimuona ni samaki mwingine ambaye anashindwa kusema kutokana na mdomo wake kujaa maji!
Nilisimuliwa mkasa mwengine na bwana mmoja anayeishi na kufanya kazi kwenye kambi moja ya jeshi huko katika kijiji cha Ole mkoa wa Kusini Pemba. Huyu anipa kituko alichokishuhudia yeye na wenzake kwenye kijiji kiitwacho Kikunguni maeneo ya Chake Chake. Mwanajeshi huyu alinieleza namna siku moja usiku wakati yeye na wenzake watatu wakiwa wameketi kupata mambo yao kwenye vichaka nje kidogo ya kambi yao, ghafla wakamuona mzee mmoja katoka ndani na kuanza kuichoma moto nyumba yake. Mara baada ya moto ule kupamba, mzee yule akaanza kupiga mayowe kuomba msaada kutoka kwa majirani, huku akilia: Ma_CUF washanichomea nyumba yangu wee!”
Kauli hii iliwastua wanajeshi hawa na ikawalazimu siku ya pili wamrudie mzee yule. Walimueleza namna walivyoushuhudia mchezo wake toka mwanzo hadi mwisho, kisha waakampa indhari kwamba kama alifanya lile ili kujipatia fidia kutoka kwa kamati ya maafa ya chama chao, hawana tatizo naye, lakini kama alifanya lile kwa lengo la kuwaumizisha raia wenzake, hilo wasingelifumbia macho.
Kelele za watu kufanyiwa dhuluma zimetapakaa kila mahali Unguja na Pemba. Jamii imejaa simanzi, chuki na visasi vya wazi dhidi ya watawala waliowakataa. Hili limepelekea ndani ya chama cha watawala hao kuundwa makundi ya kuidhalilisha jamii hii ambayo imewakataa katakata na sasa inawinwa na kulazimishwa kwa mtutu wa bunduki na silaha nyingine! Nalisema hili baada ya bwana mmoja kada wa chama hicho kunidokolea yanayoendelea ndani ya chama chao. Kwamba kweli ndani ya chama hicho kumeundwa kamati maalumu iitwayo kamati ya maafa. Kazi ya kamati hii ni kupanga na kuratibu hujuma. Kwamba wale makada ambao hukubali kujihujumu kwa kujichomea moto au kujikatia miti kwenye mashamba, hulipwa. Hili mara nyingi hufanyika na ndio sababu ya kila mmoja wetu kushangaa namna hujuma hizi zinavyotokea. Kwamba mara zote hushuhudia nyumba zikiwaka moto lakini viathirikavyo ni vitambara vibovu, huku ndani mukiwa hamna watu!
Haya yanaumiza ingawa yanatowa ishara ya chama kilichochoka. CCM imechoka na sasa inapaswa kupumzishwa kwa amani ili jamii ya Wazanzibari ibaki salama. Nalisema hili kwani pamoja na kelele tupigazo kuhusu hujuma wafanyiwazo raia, chama hiki kipo kimya utadhani hakipo na badala yake tunawasikia waitwao wapinzani pekee. Niseme basi, kwa muktadha huu kwamba hawa si wapinzani bali wenye haki zote za kuitawala Zanzibar, ingawa munalazimisha kwa vifaru na mabunduki! Mulianza mbali na sasa mumevamia kwenye kuwafumba midomo waandishi kwa kuwaundia mashtaka yasiyo kichwa wala miguu! Kwa hapa Zanzibar, mulianza na Jabir Idrissa kisha ikaja zamu ya kutekwa nyara Salma na leo mumechukua kibali cha Ahmad mukiamini kwamba mutafanikiwa. Hapana musijidanganye. Hakuna mafanikio katika hili.
Kwangu tukio hili limenizidisha ari na kunichonga makali. Kwangu tukio hili ni ishara ya wazi na uthibitisho wa utawala unaokaribia kusambaratika kwa kukosa ridhaa ya umma, ambao kutokana na umma huo kuukataa utawala, leo twashuhudia wenye mitutu wakipita mitaani wakiiba ng’ombe na kuvamia maduka na kuiba na sio tena kulinda raia na mali zao, bali sasa ni kuumiza raia na kuwaibia mali zao!
Tanbihi: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, anapatikana kwa simu nambari 0774581264

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.