Kamusi maarufu la lugha ya Kiingereza, Oxford, linalielezea tendo la kigaidi kama hivi ifuatavyo: the calculated use of violence (or the threat of violence) against civilians in order to attain goals that are political or religious or ideological in nature; this is done through intimidation or coercion or instilling fear. Tafsiri yake kwa Kiswahili ni kwamba tendo la kigaidi ni matumizi yaliyopangwa ya njia za fujo (au kitisho cha kutumia njia za fujo) dhidi ya raia kwa lengo la kufikia malengo ambayo ni ya kisiasa au kidini au ya kiikadi kwa dhati yake; na hili hufanyika kwa njia ya vitisho au matumizi ya nguvu au kupandikiza khofu. Hoja yangu ya leo ni kuwa watawala visiwani Zanzibar wanafanya ugaidi wa kidola dhidi ya wananchi wa visiwa hivi. Na kwa kuwa suala la usalama wa raia na mali zao na ulinzi kwa ujumla ni miongoni mwa mambo ya Muungano, hoja hii inawahusu pia watawala wakubwa, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitathibitisha.

Kuna siku nilibahatika kuketi kwenye baraza moja na wazee fulani hapa kisiwani Pemba, na ghafla akapita kijana mmoja kuja kuwasalimia wazee wale. Baada ya kumaliza maamkizi nao, hakukaa na akaondoka zake. Mmoja kati ya wazee wale akamuuliza mwenziwe: “Huyu mtoto wa sheha siku izi yuko wapi?”, akimaanisha yule kijana aliyekuja kuwaamkia. Mzee aliyeulizwa, akajibu: “Huyu si ndio ayo mazombi! Hayupo apa siku hizi. Yuko Unguja uko apita akiiba ng’ombengwa!” Nikatanabahi kuwa hapa ndipo vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) vilipofika na hivi ndivo raia waliokusudiwa kulindwa na vikosi hivi wanavyovitazama vikosi ambavyo eti viliundwa kuwalinda (kama ni kweli viliundwa kwa sababu hiyo)!

Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Mazungumzo baina ya wazee hawa yakanikumbusha hadithi ya kusikitisha aliyonieleza bwana mwengine, mara baada ya kusambaa kwa taarifa za kashfa ya ngono dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi. Bwana huyo alikuwa akielezea mkasa uliompata mkewe wakati akiwa mbioni kutafuta kazi ya ualimu.

Kwa mujibu wa bwana huyu, mkewe aliitwa ofisini kwa mheshimiwa huyu wakati akiwa bado ni mkuu wa mkoa. Hii ni baada ya huyu bwana kumueleza mmoja wa wafanyakazi wa kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa tatizo la mkewe kutopata kazi muda mrefu, baada ya kumaliza masomo yake ya ualimu. Ikasibu siku mke wa huyu bwana akatakiwa afike ofisini kwa mkuu huyu wa mkoa. Hata hivyo, alishangaa pale mama huyo, ambaye ni mwalimu aliyesomea fani hiyo, alipoulizwa yuko mrengo gani kisiasa! Suali hili aliulizwa akiwa amezungukwa na vigogo watatu ambao ni mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na mwingine yumkini kutoka usalama wa taifa. Pamoja na mama huyu kuwathibitishia vigogo wale kwamba naye ni wa chama chao, aliambiwa arudi nyumbani hadi atakapoitwa tena. Hapa kusudio ilikuwa wakuu kujipa muda kumchunguza mama yule kama kweli alikuwa wa chama chao na ilipobainika kwamba mama yule kwao kulikuwa na dalili za mrengo wa upinzani, hakuulizwa kala wala kalamu hadi muda bwana huyu ananisimulia!

Kama ilivyo kawaida kwa visiwa vyetu vya Unguja na Pemba, matukio ya ajabu yenye kuacha simanzi na vilio dhidi ya raia yamekuwa kama chai ya asubuhi au chakula cha mchana. Kwamba kama halikukufika asubuhi, basi mchana unalo na likikukosa mchana, jioni linawe. Haya ndio maisha ambayo raia wa visiwa hivi wanayoishi nayo kwa sasa. Kwamba kama ukisalimika kuchapwa mijeledi basi dume wako wa ng’ombe atapitiwa atiwe kwenye magari ya vikosi vya serikali na kupelekwa wanakotaka wao!

Nawapa pole raia wenzangu waliokumbwa na mtihani wa mambo nilioeleza. Kama walivyotakiwa na waungwana wengine, nami nichukue fursa hii kuwasihi kuendelea kuwa na subra kwani mungu anaiona dhulma dhidi yao na wala hawana chakupoteza. Waelewe kwamba hakuna akipatacho dhalimu isipokuwa khasara nakudhalilika. Hapati dhalimu isipokuwa tabu hapa duniani na mbele twendako na tusikokuwa na ubavu wakukwepa kwenda.

Jumatatu ya wiki hii ilianza kwa staili ya aina yake. Mapema asubuhi nilipokea simu toka kwa bwana mmoja akiomba msaada wangu. Aliomba msaada huo baada ya mkwamo aliokwamishwa na walinzi wenye jukumu la kuzuwia magendo maarufu kama KMKM. Mapema Jumatatu hii vikosi hivi vilifunga barabara ielekeayo kwenye mahkama ya Wete. Barabara hii imepita kwenye ofisi zao, ingawa si mali yao na hivyo wakaamua kuweka vizuwizi ili raia wenye shida mbalimbali kwenye mahkama hii washindwe kufika.

Hata hivyo, uzuwiaji huu ulifanywa dhidi ya watu fulani tu, ambao hawakutakiwa kufika kwenye eneo hili la mahkama na wengine waliruhusiwa kujinafasi na kujivinjari wakiwa ndani ya eneo hili ambalo wengine hawakuruhusiwa kukanyaga ingawa wana haki hio na sababu ya kufanya hivyo. Miongoni mwa walioruhusiwa kuingia mahkamani pale ni wale wote waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma za kuchoma moto mashamba ya makada wa Chama Cha Mapinduzi hapa kisiwani Pemba. Watuhumiwa hawa walifikishwa mahkamani pale wakiwa kwenye mikono ya polisi ambao ndio pekee wenye dhamana kikatiba kukamata na kufikisha mahkamani kila mwenye kustahili kufanyiwa hivyo. Hata hivyo, ufikishwaji wa raia wenzetu haukuwa wa kawaida, kwani kilichoshuhudiwa baadaye ni ukiukwaji mkubwa wa haki za raia ambazo wamepewa kisheria na kikatiba. Ndugu wa watuhumiwa walizuwiwa kutokaribia eneo la mahkama na muda mfupi baadaye wakashuhudiwa watuhumiwa wale wakipelekwa rumande baada ya dhamana zao kufungwa!

Kuna taarifa kwamba watu hawa wametakiwa kukaa huko kwa wiki mbili kabla ya kuletwa tena mahkamani. Mtu anaweza kujiuliza maswali mengi kwa hatua hii. Inakuwaje watu wafungiwe dhamana kwa tuhuma za kufikirika? Ni kufikirika kwani wengi twaamini watendaji wa kweli wa matukio haya hawaguswi na badala yake kinachotumika ni ujanja wenye lengo la kuwakomoa watu fulani kisiasa, khasa wenye mrengo wa upinzani na ambao ndio walengwa wakuu.

Mara kadhaa nimelizungumza hili, ingawa halizingatiwi na wenye dhamana ya usalama wa raia. Najua halizingatiwi kwa vile jeshi letu la polisi limeamua kufanya kazi zake kama kitengo fulani cha kulinda Chama Tawala, ambacho kimekataliwa na raia walio wengi. Nimeeleza na leo naeleza tena kwamba iwapo polisi itawahoji kisayansi wale wenye kudai kuharibiwa mashamba au vipando vyao, itawajua watendaji wa kweli wa matukio haya na sio hawa wa kusingiziwa, ambao leo limetolewa shinikizo la wao kufungiwa dhamana ili wengine waogope kuikosoa na kuikataa serikali wasiyoiamini. Lakini ataogopaje wakati si wao watendaji wa hujuma hizo? Kwa nini watu wasingiziwe na kisha wanyimwe haki yao ya dhamana!?

Kuna bwana ambaye usiku wa Jumamosi wiki iliyopita alivamiwa nyumbani kwake kijiji cha Kiungoni mkoa wa Kaskazini Pemba. Huyu anaitwa Omar Ismail. Omar alifuatwa usiku wa saa saba, ambapo kutokana na hali tete ya usalama na watu kupigwa nyakati za usiku na vikosi vya serikali, alikataa kufungua milango na ndipo vikosi vikaingia kazini kuvunja milango kisha kuondoka naye pamoja na ng’ombe wake dume! Alichukuliwa hadi viwanja vya Mnazi Mmoja, mjini Wete, ambako alipigwa na kuumizwa vibaya. Kwa mujibu wa wakaazi wa jirani na viwanja hivyo, Omar alisikika akisema “wananiuwa, wananiuwa” na baadaye akawa hasikiki tena baada ya kuzirai kwa kipigo. Baada ya kazi hii ya kumtuuga kadiri walivyoweza kumalizika, walimfikisha Kituo cha Polisi cha Wete akiwa mahututi, na kumbwaga hapo, ambapo asubuhi ya siku iliyofuata alikimbizwa hospitalini Wete kwa matibabu ya dharura.

Wakati nikijiandaa kufika hospitalini pale kumuangalia majeruhi huyo, nikapokea taarifa kwa njia ya simu kwamba amesomewa mashtaka yake akiwa kitandani na pamoja na hali aliyokuwa nayo, amefungiwa dhamana na ametakiwa kwenda rumande kwa wiki mbili. Kosa la Omar alilosomewa na ambalo ni kubwa kiasi cha yeye kufungiwa dhamana, ni lile la kumzomea Sheha wa Pandani, Bwana Said Hamad Shehe, mwenyeji wa Kiungoni, kijiji chake Omar.

Pengine wengi hawajuwi lakini kutokana na kipigo ambacho Omar alikipata wakati akiwa kwenye mikono ya vikosi hivi, hivi sasa anakojowa damu; na kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya wakati akiwa rumande, ilibidi asafirishwe kwenda kufanyiwa vipimo vya uhakika kisiwani Unguja. Kuna wasiwasi mkubwa kuwa amepata madhara makubwa yaliyotokana na kipigo cha kupitiliza alichopigwa kiasi ch akuzirai akiwa mikononi mwa wale waliomchukuwa nyumbani kwake usiku huo.

Kwa mujibu wa mashuda, Omar alichukuliwa nyumbani kwake usiku huo pamoja na ng’ombe wake dume ambaye alipakizwa naye kwenye gari aina ya Defender ya vikosi hivyo. Sasa wakati tunaelezwa kwamba kosa lililopelekea akamatwe na kupigwa ni lile la kumzomea sheha, mtu anajiuliza na yule ng’ombe wake dume aliyechukuliwa pamoja naye alimzomea nani hadi naye achukuliwe?! Huu tuupe jina gani kama si ugaidi wa dola kwa raia zake?

Nikiwa nimeketi kuandika makala hii, ghafla napokea simu ikinijulisha kwamba kuna wananchi wengine saba ambao Jumatano ya leo ya tarehe 29 Juni 2016 wamefikishwa mahkamani huko Konde wilaya ya Micheweni. Wakaazi hao wa kijiji cha Tumbe wilaya ya Micheweni, nao pia dhamana zao zimefungwa na wakapelekwa rumande wiki mbili. Kwamba hawa nao watakuwa mbali na familia zao hadi tarehe 13 Julai 2016.

Wakati wenye serikali yao wakifurahia sikukuu ya Idd na watoto wao kwa biriani na mapilau ya kukata na shoka na kujivinjari kwenye magari ya kifahari maeneo ya hadhi yao, watoto wa wanyonge hawa watatia mdomoni watachokipata huku fikra zao zikiwa na huzuni ya kutenganishwa na wazee wao ambao kwa maksudi wanakomolewa na wenye nchi kwa sababu tu ya msimamo wao wa kisiasa!

Huku hayo yakiendelea, unamsikia Naibu Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Salum Msangi, akiwatishia wanasheria wanaojitokeza kuwatetea watu wanaokamatwa na vyombo vinavyoitwa vya dola, wanaoteswa mikononi mwao, na wanaodhulumiwa haki zao, eti na wao hao wanasheria watakamatwa na kupelekwa ndani, kisha “wakateteane huko huko” na watuhumiwa wanaowatetea.

Hii ni dhulma mbaya sana ambayo hakuna binadamu mwenye chembe ya utu ataacha kuikemea. Huu ni ubaya ambao wafanyao lazima waelezwe na wakitaka waelewe kwamba ipo siku utakuja kuwatafuna. Hata kama twazibwa midomo ili tusiseme, bado tutapaza sauti kusema kwamba huu ni ugaidi wa dola kwa raia zake.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, ni mwandishi wa habari kwa taaluma, ambaye katika siku za karibuni mamlaka visiwani Zanzibar zimemnyang’anya kibali cha kufanyia kazi zake za uandishi. Anaishi kisiwani Pemba na anapatikana kwa simu nambari +255 774 581 264.

 

 

One thought on “Huu ni ugaidi wa dola dhidi ya raia”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.