Hatimaye lile jungu lililokuwa likipikwa kwa mawiki kadhaa dhidi yangu, limeiva na kupakuliwa. Alkhamisi ya tarehe 23 Juni 2016, Idara ya Habari Maelezo hapa kisiwani Pemba iliniita na kunipoka kitambulisho changu cha uandishi wa habari, ambacho nilikuwa na haki ya kukitumia kwa muda wa miezi sita – kuanzia tarehe 29 Machi hadi 29 Septemba 2016. Sababu ya uamuzi huu sikupata kufahamishwa mara zote ambazo niliitwa na maofisa wa idara hii, licha ya kuwa mara zote hizo niliwaomba sana wanieleze nilichokosea.

Siandiki kulalamika hapa, maana sioni cha kulalamikia wala wa kumlalamikia. Naandika kuelezea tu kilichonitokezea kwa malengo mawili: moja, kuujulisha umma na dunia ili ujuwe upande wa hadithi hii na kisha wale watakaopendelea kufuatilia, basi watawauliza watu na mamlaka ambazo nitazitaja kwa majina humu, na pili kuithibitishia mamlaka ambayo imejaribu kuukata mkono wangu mmoja wa kupatia riziki kwa kuniziba mdomo, kuwa sauti yangu bado ni yangu mwenyewe, na hii itabakia hivyo milele na milele!

Mkasa wenyewe ulianzia wiki tatu zilizopita pale siku moja nilipotafutwa na RCO wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bwana Issa Juma, kupitia kwa mtu wa tatu, akitaka apatiwe nambari yangu ya simu. Kutokana na khofu aliyokuwa nayo mtu huyo, aliamua kumjibu Afande Issa kwamba hakuwa na nambari yangu. Badala yake akanipigia mwenyewe kunifahamisha jambo hilo. Nikamshukuru na kisha nikamuomba anipatie nambari ya RCO Afande Issa ili niweze kumpigia mwenyewe kujuwa shida yake kwangu.
Nilifanya hivyo, lakini katika hali ya kushangaza, Afande Issa akaruka kimanga kwa kunieleza kuwa si yeye aliyekuwa akinihitaji, “bali Mkuu wa Idara ya Habari kisiwani Pemba.” Nilimuuliza: “Kwa nini Mkuu wa Idara ya Habari anitafute kupitia kwako RCO?” Akajibu kwamba hafahamu. Pia nikamuuliza kwa nini yeye mwenyewe RCO atafute nambari yangu ya simu kupitia njia za vichochoroni, wakati kamanda wake wa mkoa, Mzee Hassan Nasir, anazo nambari zangu na mara kadhaa yeye RCO amenishuhudia nikiwa na kamanda huyo? Hakuwa na jibu zaidi ya kujibaraguza! Nikamwambia waziwazi kwa njia ya simu: “Nafahamu Bwana RCO kuna jungu munalipika dhidi yangu, lakini litajulikana tu! Na nambari yangu basi ni hiyo. Mpe huyo aliyeiomba!” Haingii akilini kuwa Ofisi ya Idara ya Habari ambayo ndiyo kama ofisi yangu nikiwa mwandishi wa habari iombe nambari ya simu kwa RCO wakati data zangu zote wanazo mezani pao.

Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, akiwa kwenye ofisi za Idara ya Habari Maelezo Pemba, alikoitwa kunyang'anywa kibali cha kufanyia kazi.
Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, akiwa kwenye ofisi za Idara ya Habari Maelezo Pemba, alikoitwa kunyang’anywa kibali cha kufanyia kazi.

Huo ukawa mwisho wa mazungumzo yangu naye, lakini ukawa mwanzo wa kile kilichokuja kuhitimishwa wiki tatu baadaye. Baada ya RCO kuipata nambari yangu, nikapokea simu sasa kutoka Idara ya Habari kwenyewe, nami nikaitikia wito. Huko nikaelezwa kwamba kuna malalamiko. Nikawauliza walioniita, Bibi mmoja kwa jina la Jamila, malalamiko yenyewe hasa ni yapi na mlalamikaji hasa ni nani? Hakuna hata mmoja aliyeweza kunijibu. Baada ya kukosekana kile chenye kulalamikiwa, nikatakiwa kutotoa habari yoyote kwa muda wa wiki moja mpaka suala langu liwekwe sawa. Nikakubali. Hata hivyo, siku chache baadaye nikatakiwa kufika tena kwenye ofisi hizi na mara hii nikawekwa kikaoni chini ya Afisa Mdhamini aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Ali Nassor. Kwa mara nyingine tena, nilihoji kutaka kujua malalamiko yaliyopo dhidi yangu na yule mwenye kunilalamikia. Lakini kama kawaida, hapakuwa na malalamiko hayo wala mlalamikaji dhidi yangu! Hapa napo nikaombwa tena kutotoa habari yoyote hadi pale uongozi wa idara hii utakapokutana na mlalamikaji na kujuwa anachokilalamikia kwangu.

Katika kikao hiki kuna jambo ambalo kidogo lilinistua, nayo ii ile kauli ya Afisa Mdhamini, Bwana Ali Nassor, kwamba alikuwa amepanga kwenda Mjini Wete kukutana na RCO, Mkuu wa Mkoa na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huko, ili wamueleze hasa nini malalamiko yao kwangu! Hii inamaanisha kuwa hakimu anamfuata mlalamikaji nyumbani kwake ili amueleze jambo ambalo mimi mlalamikiwa nimemkosea, na sio mlalamikaji kumfata hakimu ofisini kwake kumpelekea malalamiko yake dhidi yangu, mlalamikiwa! Yaani mimi mlalamikiwa niliitwa pale Idara ya Habari Maelezo (mahakamani petu kwa muktadha huu) kuelezwa kwamba kuna malalamiko dhidi yangu (ambayo hayajuilikani hasa ni yapi) lakini mwenzangu mwenye kunilalamikia anafuatwa ofisini kwake na Afisa Mdhamini (hakimu) ili akaeleze kile nilichomkosea!
Jambo jengine la kushangaza ni kwamba hata kwenye vikao hivyo na maafisa wakubwa wa Idara ya Habari Maelezo, maafisa hao walinitaka nikabidhi rikodi za taarifa zangu ambazo nimekuwa nikituma kwenye vyombo vya habari. Kwamba mimi ambaye nalalamikiwa, ndiye ambaye natakiwa niwasilishe kile kinacholalamikiwa. Yaani mtuhumiwa apeleke kwa hakimu ushahidi ambao utamfanya atiwe hatiani na kisha ahukumiwe kwa ushahidi huo! Sikuwa na kosa lolote, niliamini, lakini kama walikuwa wanasaka kosa langu, lilikuwa jukumu lao kukusanya ushahidi wao dhidi yangu na sio kuwa mimi niwakusanyie ushahidi. Ndivyo nilivyowaambia.
Wakaazi wa kijiji cha Kiungoni, kaskazini Pemba, wakionesha magamba ya risasi zilizotumika wakati kijiji chao kilipovamiwa.
Wakaazi wa kijiji cha Kiungoni, kaskazini Pemba, wakionesha magamba ya risasi zilizotumika wakati kijiji chao kilipovamiwa.

Tangu hapo, nilishafahamu kitambo kuwa kusingekuwa na haki nitakayoipata kutoka kwa mahakama hii wala kwa hakimu huyu. Sikutendewa haki toka mwanzo hadi mwisho wa kadhia hii na kilichofanyika ni uhuni uliosimamiwa na Idara ya serikali dhidi yangu kwa kufuata mashinikizo ya wanasiasa waliopoteza muelekeo sahihi wa kisiasa. Ni uhuni mtupu kuanzia mwanzo hadi mwisho. Masikitiko yangu ni kwa Idara ya Habari, ambayo inatakiwa iongozwe na wanataaluma na weledi wa kazi zao, kujikubalisha kuwa wakala wa uhuni huu. Mwandishi wa habari hutazamia kuwa chombo hiki kinatakiwa angalau kujaribu kulinda hesihma na hadhi yake, kama hakiwezi kufanya hivyo kwa uhalisia. Lakini katika kesi yangu, hata kujaribu haikujaribu. Mathalani, wangeamua kunipoka kitambulisho changu hata kwa visingizio visivyokuwepo, lakini kwa njia sahihi za kuainisha visingizio hivyo kwa njia ya barua rasmi ambayo ingetowa ushahidi wa mimi kuikabidhi nyaraka hii kwao. Lakini kinyume chake wakaichukua kwa njia za kupoteza ushahidi na ili ionekane nilirejesha kibali hiki kwa khiyari yangu. Nilishangaa pale muhusika wa kadhia hii, Bwana Marzouk, ambaye alikuwa likizo Dar es Salaam lakini akaitwa rasmi kwa dharura ya kuja kuninyang’anya kipande changu, eti kwa kuwa yeyse ndiye aliyenipa – aliponitamkia wazi kwamba yeye hawezi kuandika barua ya kujifunga!

Nilidhani hayo aliyoniambia yangebakia baina yangu na yeye, maana nilimuona kabisa kuwa ameelemewa na analazimika kufanya jambo la kitoto na kihuni kabisa, lakini nikashangaa tena pale alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani (Deutsche Welle) – ambayo ni moja ya redio nilizokuwa nikifanya nazo kazi – akidai kwamba nimerejesha kibali hiki kwa khiari yangu na wala sikulazimishwa kukirejesha! Kwamba mimi ni mjinga kiasi cha kurejesha kitambulisho ambacho ndio chanzo cha mimi kupata riziki ya kula na familia yangu! Ikumbukwe kwamba ni kitambulisho hiki ndio ambacho kiliniwezesha mimi kukusanya habari kwa mujibu wa sheria na kanuni za uandishi na kisha kuzisambaza kwa vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi na hivyo kuwa chanzo kimojawapo cha riziki zangu. Kukirejesha kunamaanisha kujinyima mwenyewe uwezo wa kufanya kazi hii ya uandishi na kama ni chanzo kimoja cha mkate wangu wa kila siku, mimi nitaishije?
Kwa ufupi, ni kuwa kiilichofanyika ni uhuni dhidi yangu, wenye lengo la kuninyamazisha kutokana na uamuzi wangu wa kuisemea jamii dhaifu iliyowekewa vizingiti vyote vya kutotakiwa madhila yake kusikika. Sijawahi kuvunja maadili, miko wala sheria za kazi hii niliyoikalia chuoni miaka minne kujifunza kwa uweledi mkubwa kabisa. Daima nilisimama kwenye misingi yake mikuu; yaani kuripoti ukweli mtupu, kuwapa nafasi wahusika wote wa ripoti yangu kusikika, kuchunguza kwa makini kila jambo kabla ya kulirusha hewani, kuzingatia maslahi mapana ya jamii na nchi yangu. Nawapa changamoto wale ambao wamechukuwa hatua hii dhidi yangu waoneshe kosa langu hasa ni lipi, zaidi ya kuwapa sauti wasiokuwa na sauti!
Kama nilivyotangulia awali kusema, mimi sijuti wala silalamiki kwa hili. Kinyume chake ni kuwa ni fahari yangu kusimama kwenye misingi ya taaluma yangu hata mbele ya vitisho vilivyopo mbele yangu. Leo nasimama tena kama mwanahabari niliyejikubalisha kueleza kila chembe ya ubaya wafanyiwao wanyonge wa mama yangu Zanzibar. Pamoja na juhudi za kunifumba mdomo, sauti yangu bado ninayo. Na nitaendelea kuitumia kwa njia nyengine isiyokuwa uandishi rasmi wa habari kupitia vyombo rasmi, ambavyo sheria inanitaka niwe na kibali ambacho nimeshapokonywa.
Namalizia kwa kuwasihi waandishi wenzangu wa habari na pia wanaharakati mbali mbali wakiwemo wa haki za binadamu, za wanawake na za watoto, waitupie jicho la huruma Zanzibar, na khasa kisiwani Pemba niliko mimi kwa sasa. Ndani ya kisiwa hiki kuna unyama mkubwa mno unaoendelea dhidi ya raia. Kuna matukio ya kinyama ambayo hayastahili binadamu kufanyiwa. Ndani ya kisiwa hiki, kuna makundi ya kiharamia ambayo huvishwa sare za kijeshi na kupewa silaha zitumikazo kuumiza raia wanyonge wasio na hatia.
Njooni mujionee na muwasikie wenyewe watu wanaokumbwa na hayo. Ni binaadamu kama nyinyi, ni watu kama mimi. Njooni mumuone na kumsikia mtoto Ali Said mwenye umri wa miaka 13. Huyu ni mkaazi wa kijiji cha Kiungoni, mkoa wa kaskazini Pemba, ambaye amejikuta kwenye hali tata ambayo hakuwahi kuwa nayo kwa umri wake wote. Vikosi vyenye silaha vilikivamia kijiji chao nyakati za usiku na kuanza kufyatua risasi na mabomu chini ya nyumba yao. Watu wakakimbilia maporini usiku huo na mtoto huyu akajikuta akiwa amezingirwa akiwa pekee ndani ya nyumba yao. Kutokana na msituko alioupata, hivi sasa Ali ana tatizo la kutokwa na mkojo bila kuzuwia. Nilimshuhudia kwa macho yangu mtoto huyu akipitwa na mikojo huku baba na mama yake wakiwa hawajui nini wafanye kutokana na umaskini mkubwa uliowazonga. Ali anahitaji kusaidiwa ili kuokoa maisha yake.
Njooni mumuone Bwana Othman Hemed, mkaazi wa kijiji cha Wingwi. Bwana huyu ni mgonjwa mwenye kusumbuliwa na ugonjwa wa kisukari pamoja na presha. Hali yake ya afya si madhubuti na inatoa ishara zote za mtu ambaye ameshazidiwa na ugonjwa na sasa anahisabu siku zake za kuishi. Akiwa njiani kutoka dukani ambako alienda kununua dawa za maumivu, kundi la askari wenye silaha maarufu kama Mazombi, walimvamia na kumpiga marugu hadi akapoteza fahamu. Alistuka akiwa ndani huku amezungukwa na kundi la watu waliokuwa wakimpepea na huku akiwa na maumivu makali ya mgongo baada ya kupigwa na kitu kizito mgongoni. Othman alifikishwa hospitali ya Micheweni kwa msaada wa ndugu zake.
Njooni mumuone Bi Fatma Juma, mkaazi wa kijiji cha Kinazini wilaya ya Micheweni. Usiku wa kuamkia Jumatatu ya tarehe 20 Juni 2016, alivamiwa na watu wenye silaha nyumbani kwao Kinazini akiwa na mtoto wake mdogo, ambaye alikuwa ametoka kumuasha barazani alipokuwa amelala mtoto huyo. Dada huyu alitandikwa na watu hao kwa kitu alichokiita mkia wa taa au waya na kuumizwa vibaya kwenye jicho lake la kulia na ziwa lake la kushoto! Bi Fatuma ni miongoni mwa raia niliowahoji wakiwa hospitali ya Micheweni ambako walipelekwa kwa matibabu.
Njooni basi muzisikilize familia za watu wanaokamatwa ovyo ovyo na kufikishwa mahakamani na kisha kupelekwa rumande katika mazingira ya kukomolewa. Hali hii huwakumba zaidi wale wenye kutuhumiwa kuchoma mashamba au kuharibu vipando vya makada wa CCM.
Njooni muwaone wazee wa kijiji cha Kiungoni, ambao walipata kuwasilisha maganda ya risasi Makao Makuu ya Polisi ya Mkoa wa Kaskazini Pemba kama ushahidi wa kuthibitisha uovu waliofanyiwa ikiwemo kuibiwa pesa taslimu milioni kadhaa baada ya maduka yao kuvamiwa na askari wa vikosi vya SMZ. Nilibahatika kufika kijijini hapo na kukutana na wazee hao. Walinipokea kwa kunisuta huku wakinionesha maganda ya risasi kumi na mbili waliofanikiwa kuyaokota baada ya watu wenye silaha kuvamia kijijini hapo wakapiga risasi na kisha kuanza kupiga watu na kuiba vitu kadhaa zikiwemo pesa taslimu, baiskeli na televisheni. Wazee hawa wamefungua kesi polisi na kupewa RB, lakini usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 26 Juni 2016, mmoja wao ajuilikanaye kwa jina la Bwana Omar Ismail Hemed alivamiwa usiku wa saa nane nyumbani  kwake, nyumba ikavunjwa na yeye akachukuliwa hadi Uwanja wa Mnazi Mmoja, Wete, ambako alipigwa mijeledi hadi akarufai, na wakati naandia makala hii yuko mikononi mwa polisi ile ile ambayo alikwenda kuwapa maganda ya risasi wiki moja nyuma, huku polisi ikikataa kumtoa, kumtibu wala hata kusema wanamshikilia kwa kosa gani.
Mikasa kama hii iko kote kisiwani Pemba. Kuanzia Nanguji na Kisiwapanza kusini mwa kisiwa hadi Mtambwe na Wingwi upande kaskazini ya kisiwa. Vyombo vya dola vinavyodai kuwasaka wahalifu na kulinda doria ili eti mikarafuu na migomba isiharibiwe, ndivyo vinavyopita kijiji kwa kijiji, mtaa kwa mtaa kudhalilisha na kuumiza wanyonge bila sababu.
Mimi nimekuja na ninaishi maisha yangu yote kwenye kisiwa hiki hivi sasa. Nilijuwa kwamba kuna hatari nyingi zilizo mbele yangu kulingana na kazi yangu hii ya uandishi wa habari katika eneo kama hili, ambalo lina wakaazi wengi waliokataa kuutii utawala uliopo madarakani, na ambao kwa hakika ni watu wangu.
Nilijiona nina wajibu kwa jamii yangu, maana kiuandishi wa habari, kisiwa hiki ni kama eneo lililofungwa kwa walimwengu wasilione. Dola haitaki kabisa yale ambayo yanatendeka dhidi ya watu yajuilikane. Waandishi wengi walioko huku ni wale wanaofanyia kazi kwenye vyombo vya watawala na wengine hata kuwa sehemu ya mfumo wa utawala wenyewe. Niliyajuwa hayo tangu nilipohamishia rasmi makaazi yangu kwenye kisiwa nilichozaliwa, baada ya kuishi nje yake kwa zaidi ya miaka 25. Lakini nilijikubalisha kuwa sauti ya jamii isiyo sauti pamoja na madhila mengi inayoizunguka jamii hii – madhila ambayo yana mkono na baraka za wazi za watawala.
Nilijuwa kwamba upo uwezekano wa asilimia mia moja ya mimi kufumbwa mdomo kwa namna yoyote ile, maana hilo si jambo geni si kisiwani Pemba tu, bali Jamhuri nzima ya Muungano wa Tanzania. Tunayakumbuka ya Daudi Mwangosi, tunayakumbuka ya Jenerali Ulimwengu, tunayakumbuka ya Absalom Kibanda, tunayakumbuka ya Said Kubenea, tunayakumbuka ya Marehemu Ali Nabwa, tunayakumbuka ya Salma Said. Ndiyo kazi yetu hii tuliyoichagua ilivyo. Roho yako inakuwa mikononi mwa watawala na au wale wenye nguvu ambao wanaguswa vibaya nayo.
Nilijuwa kuwa chochote kinaweza kunitokezea; aidha kwa njia kama hii ya kupokwa kibali cha kufanyia kazi zangu au hata kufanyiwa hujuma nyingine dhidi yangu au familia yangu. Nilijuwa kwamba upo pia uwezekano wa mimi kukamatwa na kufunguliwa mashtaka bandia kama wafanyiwavo Wazanzibari wengine wengi kwenye kisiwa hiki cha Pemba. Nilijuwa kwamba mawakala wa watawala hawatoniacha niionyeshe dunia dhulma wanayoifanya kwa raia dhaifu kwa madai ya kuimarisha ulinzi na usalama. Lakini pia nilijuwa kuwa hata nikizibwa mdomo, bado nitabakia na sauti yangu na hii itaendelea kusema siku zote.
TANBIHI: Makala ya Ahmad Abu Faris, mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba, ambaye Idara ya Habari Maelezo kisiwani humo imemnyang’anya kibali chake cha kufanyia kazi. Anapatikana kwa simu nambari +255 774 581 264. 

One thought on “SMZ, mumeniziba mdomo, lakini hamuwezi kuichukuwa sauti yangu”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.