Sioni dhiki kuandika wala kutamka kwa kinywa kipana kabisa bila ya chembe ya ukakasi kooni kuwa- muungano huu (Tanganyika na Zanzibar), ni kosa la kihistoria  kwa Zanzibar ambalo Sheikh Abeid Karume alilifanya.

Muugano wetu ni dubwasha lililokuwa mwazo wa  kuimeza Zanzibar na kuisotesha kimaendeleo, wale ambao unawanufaisha ndio wanaupigia kelele uwepo kama ulivyo kwa sababu wao unawajazia matumbo yao.

Leo Uingereza kuna kura ya maoni juu ya kubaki ama kujiondoka katika Umoja wa Ulaya, dalili zinaonesha kuwa wanaotaka Uingereza iendelee kubaki katika Muungano wa huo huenda wakashinda, japo kwa ushidi mdogo, ushindi huu unaweza kuwapa vinywa vipana wale wahafidhina wetu wa Muunganon huu ambao unaibana mbavu Zanzibar.

Kubaki Uingereza katika muungano wa Ulaya si kielelezo kuwa lazima na Zanzibar ibaki katika muungano na Tanganyika, wala sio mfano mzuri kwetu kuwa na Zanzibar nayo iendelee kuwemo hata kama inaminywa.

Lililo zuri halikataliwi, kwa vile Muungano wa Ulaya ni bora kwa Waingereza wengi basi matokeo yake yatakuwa ni kubaki katika Muungano huo na kama unawabinya matokeo ya kujiengua ndio utakayo yaona.

Kinachoogopwa kwetu sisi ni kuwa watawala wanajua wazi kuwa muungano wetu ni wa kikandamizi, hivyo hata ukiwauliza Wazanzibari kuwa munautaka ama la – wengi watataka kujiondoa. Ndilo wanaloogopa!

Kama watawala wa kwetu watazingatia kuhusu kura ya kuulizwa Waingereza juu ya Muungano wao na Ulaya- jawabu watakayo toa huenda isiwe ya msingi sana kwetu, kwa sababu matokeo yatatokana na mitazamo ya Waingereza wenyewe juu ya muungano huo na wao ndio watakaonufaika mwanzo.

Kwetu lililo la muhimu ni kurithi ile demokrasi ambayo huku  imekosekana, demokrasia ya kuwafanya wananchi kuwa ndio waamuzi wa mustakbali wao wenyewe.

Ile maana ya demokrasia kwa mujibu wa Abraham Lincon (rais wa zamani wa Marekani) inafanya kazi kwa wenzetu lakini kwetu imekosekana. Lincon alisema kuwa demorkasia ni serekali ya watu, imewekwa na watu na ipo kwa ajili ya watu .

Kwetu ni kinyume chake- kwa maana kuwa serekali iliyopo ipo tu kwa ajili ya matumbo ya wachache ni kama ajira tu wamejiajiri, na ndio ukakuta wengi  wa raia ni masikini kwa sababu serekali inanufaisha kundi dogo la watu.

Pia haijawekwa na watu kwani kilichofanyika ni mauza-uza ya kuiba na kupora haki za wengine, kisha wakajiweka madarakani, kama kawaida yao  wameanza kupora haki za wengine muda mrefu sio Octoba tu.

Halikadhaalika serekali iliyopo haipo kwa ajili ya watu – viongozi hujifikiria wao kabla ya watu wao, wananchi walitaka muungano wa mkataba mpaka leo hakuna lililokuwa , kilichofanyika ni serekali kutumia wafuasi wake (wabunge maalum) kutengua ambacho wananchi wanakihitaji.

Sipati wasi wasi wa kuangalia nyuma mara nisemapo maneno haya-“muungano kama utabaki kuendelea kuwa huu, ni kheri uvunjwe”, nasema hivyo kwa sauti kubwa kwa sababu hasara ya kuwepo kwake ni kubwa kuliko faida.

Faida za muungano huu ni sawa na kumshika mtu ukamcharaza bakora, mateke, ngumu, ukamtesa kisha akiwa hoi bin taabani – ukampa mia tano ukamwambia atafute panadoli ameze. Muungano unavyoitesa Zanzibar, faida yake ni kama vile kupewa mia tano baada ya kukumutwa vilivyo.

Hivi karibuni Mbunge wa Nkasi bwana Ally Kessy aliwaeleza wabunge wa Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla;  waache kug’ang’ania kupata nusu kwa nusu kila kitu na bara,  kwa kuwa wao (Zanzibar) ni 4% na wanastahili kupata 4%, kwenye kila kitu na sio nusu kwa nusu.

Anayoyasema Ally Kessi kuwa,  Zanzibar haipaswi kupata nusu, twende kama hivyo atakavyo yey kuwa si lazima Zanzibar kupata nusu kwa nusu kwa vile  ni ndogo kuliko Tanganyika, lakini suali la msingi ni kuwa; hiyo 4% ambayo ilikubaliwa, Zanzibar inapata kama itakiwavyo?

Katika kipindi cha Mkasi kinachooneshwa na East Africa Television, mwezi Febuari 2015 alipokuwa akihojiwa Mbunge wa Singida Mashariki –Chadema Mh Tundu Lissu anasema;“kuna sheria inasema katika kila fedha inayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano waTanzania – Zanzibar inahitajika kupata 4.5%”.

Tundu Lissu anaendelea kwa kusema;“katika moja ya kazi niliyoifanya na kupenda kuifanya ni kuibua uongo huo, kwani kwa miaka yote hii hatujawapa Zanzibar hata hiyo shillingi 4 kwa kila shilingi mia tunayopata, tunawapunja, tunawanyonya”.

Muungano wa namna hii ambao hata mulilokubaliana halitekelezwi, ndio ambao hauna maana na inahitajika watu waulizwe haraka ikiwa wanautaka ua laa, ili hizi duhlma za kunyonyana na kuibiana kwa jina la Muungano ziondoke.

Muungano ambao unazingatia haki za kila upande kile ambacho pande mbili wamekubaliana ndio kifanyike kwa mujibu wa makubalino hayo, hapo kusingekuwa na tatizo na  kama kura ingeitishwa ya kuulizwa Watanzania ikiwa wanautaka au la,  basi viongozi wa Kihafidhina wangekuwa na uhakika mkubwa wa kuwa muungano utaendelea kudumu kwa sababu haubinyi sehemu moja.

Muungano ulianza na mambo dazeni moja tu kisha yakaongezwa kinyemela mpaka yakafika dazeni tatu na ushei, huu ndio muungano ambao watu wanapaswa kuulizwa wanautaka au laa, kama wakiukubali ni shauri yao.

Wiki chache zilizopita Mbunge wa jimbo la Kijito Upele-CCM, Shamsi Vuai Nahodha alikuwa akilalama bungeni, anasema; “tumezungumza kwa muda mrefu suala la kugawana mapato kati  ya Serekali ya Mapinduzi Zanzibar na Serekali ya Muungano, ndugu zangu wale tunaoipenda Tanzania na Zanzibar naomba suala hili lifike mwisho limaze, amani ya Tanzania inategemea sana mustakbali wa uchumi wa zanzibar”.

Kikubwa alichokuwa akikilalamikia Nahodha ndicho kama kile alichokisema Tundu Lissu, kuwa hiyo 4% Zanzibar haipewi, hayo mapato ambayo yamekubaliwa kugawanwa – Zanzibar haipewi.

Mpaka ukimuona Muhafidhina kama Nahodha analalamika kuwa makubaliano ya Muungano hayatekelezwi, ujue kuwa Zanzibar imeshaumia sana. Yeye ana maslahi yake na Muungano, hadi analalamika tafsiri yake ni kuwa kiwango cha unyonyaji kimefikia katika hatua kubwa.

Muungano wa namna hii ndio ambao watu wanapaswa kuulizwa ikiwa wanautaka, wakiukubali ni hiyari yao. Hatuwezi kuwa na Muungano wa kinyonyaji kiasi hiki, kisha  unaowanufaisha ni wachache na wanataka udumu kwa maslahi yao lakini wengi – wachini unawaumiza.

Tanbihi: Makala hii imeandikwa na Rashid Abdullah, mwanafunzi wa stashahada ya uandishi wa habari wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.