Mambo yote yanayotengenezwa na binaadamu duniani yana uwezekano wa kuvunjwa. Imekuwa hivyo kwa sababu mwanaandamu ana mipaka katika kufikiri kwake na ana khiyari katika kuamua kwake. Kwa sababu mbili hizi, mwanaadamu anaweza kufikiri jambo kuwa ni zuri muda wote na hatimaye mambo yakabadilika na kubainika jambo hilo si zuri kwa muda wote.

Aidha, anaweza kuamua jambo kwa maslahi yake na ya binaadamu wenzake na hatimae ikabainika jambo lile halina maslahi tena kwake na wala kwa binaadamu wenzake. Na khulka hii kwa binaadamu katika kufikiri na kuamua kwake haiwakhusu tu raia wakawaida, bali inawakhusu hata viongozi wa kitaifa na kimataifa. Na haimkhusu binaadamu mmoja mmoja, bali inakhusu jamii kwa ujumla wake.

Leo tumeshuhudia Uingereza ikijitoa kwenye kitu kikubwa sana chenye matarajio makubwa sana katika dunia – kitu kinachoitwa Muungano wa Umoja wa Ulaya (EU). Hapana shaka Uingereza (raia na viongozi) si wapumbavu katika uamuzi wa mwanzo wa KUJIUNGA na Umoja huo, wala si wapumbavu katika uamuzi wa pili wa KUJITOA kwenye Umoja huo.

Sisi ni waumini kuwa wakati Waingereza walipoamua kujiunga na Umoja huo walikuwa wakiitakia mema nchi yao, na walipoamua kujitoa kwenye Umoja huo wamegundua kuwa mema wanayoitakia nchi yao hayawezi tena kupatikana ndani ya Umoja huo na kwa hivyo, tathmini yetu ni kuwa, maamuzi yote waliyoyafanya Waingereza – yale ya mwanzo na haya ya sasa YOTE ni maamuzi sahihi.

Suali la msingi tunalouliza: ni kwa nini Wazanzibari hawapati fursa ya kuulizwa kuhusu Muungano wakati Muungano umekuwa ukionekana una khasara zaidi kulikoni faida (kama zipo) kwa Wazanzibari?

Kwa Wazanzibari, kujitoa kwa Uingereza kwenye Muungano wa Umoja wa Ulaya ni darasa tosha iwapo tutakuwa ni wenye mazingatio. Muhimu zaidi kwenye tukio hili ni kujifunza haja na umuhimu wa mambo mawili: UELEWA wa Wananchi khasa kuhusu matkwa na madaraka yao ndani ya nchi yao, na UWAJIBIKAJI wa viongozi.

Kadhalika, ni muhimu zaidi kutambua ya kwamba umefika wakati tuamini kivitendo kuwa, msingi wa kila upande na watu wake kujiamulia mambo yao wenyewe, na uhuru wa kila taifa ndani na nje – ni sehemu ya shabaha za kidemokrasia; msingi ambao unatiliwa mkazo katika maandiko yote ya haki za binaadamu (right to self determination).

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Khalid Gwiji, ni mwanaharakati wa demokrasia na haki za binaadamu visiwani Zanzibar.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.