Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ya mwaka 1975-76 inaseama “vikosi vya usalama vya Argentina vilianza kutumia kile kiitwacho makundi ya mauaji (death squads) mwishoni mwa mwaka 1973.

Mfano wa vikosi hivyo ni Alianza Anticomunista Argentina,  ambacho kwa mujibu wa Amnesty International kilisababisha vifo vya takribani watu 1,500, huku zaidi ya  9,000  wakitoweka katika mazingira ya kutatamisha na wengine wengi kubakwa na kuuawa kwa siri.

Makundi ya mauaji ni nini? Haya ni makundi yenye silaha ambayo hufanya  mauaji, kuteka, kupoteza watu katika njia za kutatanisha, kutia hofu raia kwa kuwapiga na kuharibu mali zao, na yote huyafanya kwa lengo kisiasa wakiwa chini ya serekali.

Baadhi ya nchi ambazo bado zinatumia vikundi vya mauaji ni kama Colombia, Iraq, Sudan, Marekani (nje ya nchi hiyo), Syria na kwa nchi za hapa karibu yetu imo Kenya kwenye orodha ya mataifa yanayotumia vikundi vya mauaji. Pia zipo nchi za Congo na Burundi.

Nimeanza na historia hiyo kwa sababu hoja yangu ni yaliyotokea Zanzibar kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 25 na kisha ule wa marudio wa Machi 20 yana uhusiano wa uwepo wa makundi hayo.

Mazombi wakiwa kwenye gari ya Kikosi cha KMKM Nam. 155 maeneo ya Kilimani, mjini Unguja, Februari 2016.
Mazombi wakiwa kwenye gari ya Kikosi cha KMKM Nam. 155 maeneo ya Kilimani, mjini Unguja, Februari 2016.

Katika ripoti ya Chama cha Wananchi (CUF) iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Nassor Ahmed Mazrui mbele ya waandishi wa habari tarehe 22 Mei mwaka huu, kuna mtiririko wa vitendo kadhaa vya uvunjifu wa haki za binaadamu visiwani Zanzibar kwa mwaka 2015/2016.

Sehemu ya ripoti hiyo inaelezea: “Kuibuka kwa makundi ya maharamia ambao wananchi wamekuwa wakiwaita MAZOMBI ambao hufunika nyuso zao na huku wakibeba silaha za moto na silaha za kienyeji na wakiwa ndani ya gari zenye namba za Vikosi Maalum vya SMZ ambao wamekuwa wakipiga, kuwaibia mali zao, kuwajeruhi na hata kuwakata sehemu za miili yao wananchi wasio na hatia katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba”.

Alkhamisi ya tarehe 4 Febuari mwaka huu, watu waliofunika nyuso zao wakiwa na silaha za jadi na moto, walipita katika  maeneo ya Kilimani mjini Zanzibar, wakiwa katika gari lenye namba za usajili KM 155.

KM ni kifupi cha KMKM- Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Ufupi ni kuwa ni gari la kikosi cha serikali kinacholinda rasilimali za Zanzibar kupitia ardhini na nchi kavu.

Mchana kweupe, Alkhamisi hiyo wafunika nyuso hao walionekana  wakipita huku na kule na hadi kufika jioni walikuwa tayari wameshaharibu mali na kujeruhi watu kadhaa.

Vitendo kama hivi viliendelea kuanzia uandikishaji wapigakura katikati ya 2015 hadi siku kadhaa baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20. Muda wote huo, wananchi walikuwa wakilalamika, vyama vya siasa vya upinzani vilikuwa vikilalamika, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilikuwa vikiripoti, lakini Jeshi la Polisi, serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa ama wakikanusha kuwepo kwa makundi yanayofanya vitendo hivyo, au wakitishia kuwachukulia hatua wale wanaolalamika na kuripoti.

Masuali ya kujiuliza ni kwanini Mazombi hao walizuka katika kipindi cha uchaguzi kisha wakapotea uchaguzi ulipoisha? Kwanini Mazombi walibeba silaha za moto ambazo zinamilikiwa tu na vikosi vya serikali? Kwa nini Mazombi walitumia gari zenye namba za usajili kutoka katika vikosi vya serikali? Kwa nini wafiche sura? Kama ni kundi la linalojitegemea kwa nini wasitoe madai yoyote kama yanavyofanya makundi mengine?

Tuweke katika mizani ya akili masuali niliyouliza na tuyajibu kwa pamoja ili tuone jawabu ya mwisho itakuwa ni ipi. Si busara kuacha hali hii itokee kisha tukaridhika kuwa imepotea bila ya kujua sababu ya kwa nini inatokea na kujirudia.

Ikumbukwe kuwa makundi mfano wa haya yalikuwepo baina ya mwaka 1995 na 2000 na wananchi wakayapa jina la Melodi, kisha baina ya 2001 na 2005 yakapewa jina la Janjawidi. Kwa hivyo, mtiririko wa matukio kwenye historia ya karibuni visiwani Zanzibar unaonesha kuwa makundi ya kiharamia yanayofanya uhalifu wa kisiasa huwapo na hujirejea kuwapo kila baada ya muda.

Matendo wanayoyafanya ni yale yale na athari yanayowacha ni ile ile, isipokuwa tu wananchi huwa wanayabadilisha majina yao – kutoka Melodi wa miaka ya ‘90 hadi Janjawidi wa miaka ya 2000, kutoka Janjawidi hadi Mazombi wa 2015 na 2016.

Hivi sasa, kila siku tunapokea taarifa za kuvamiwa kwa vijiji kadhaa kisiwani Pemba nyakati za usiku, lakini uvamizi wa sasa haufanywi na Mazombi, bali na jeshi la kawaida la polisi, ambao hupiga risasi za moto hewani, humwaga mabomu ya machozi, huku pia kukiwa na ripoti za kuibiwa kwa mali za raia wakati wa matukio hayo. Kisingizio ni mgomo wa kijamii unaoendelea kisiwani humo, ambapo wananchi walio wengi na wafuasi wa CUF wanawagomea walio wachache, wafuasi wa CCM. Kwa hivyo, polisi inatumika kuwatia adabu wagomaji kwa staili hiyo.

Si jambo la kushangaza hata kidogo kuwa hadi sasa jeshi hilo hilo la polisi halijawahi kumshika hata Zombi mmoja, japo kwa tuhuma tu za yale yaliyotendwa nao, na hata walipokuwa wakiulizwa, maafisa wa jeshi hilo walijibu kuwa ama hawapo au ni “wahuni na hao wanaolalamika kukutwa na maafa ya mazombi huenda nao ni wahuni wenzao”.

Mambo ya kujiuliza, vipi wahuni wanaweza kutumia gari la KMKM-Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo? Vipi wahuni wanaweza kutumia silaha za moto na kuhatarisha amani ya nchi, kisha serekali ikiulizwa inatoa jawabu rahisi la wahuni?

Ukisikia mwandishi fulani katekwa, redio imevamiwa usiku na kuharibiwa, vikundi hivi vya siri huwa ndio wanatekeleza haya kwa niaba ya serikali, yanafanywa kisiasa kuziba midomo waandishi na vyombo vya habari vyenye mrengo usiokuwa wa kiserikali.

Kitu kimoja kipo wazi. Makundi haya – yaite jina lolote utakaloyaita – huwa yanazuka kipindi cha uchaguzi na hupotea baada ya vumbi la uchaguzi kutulia. Hii inatupa jawabu kuwa makundi haya ni siasa chafu. Yanaundwa na kutumiliwa kisiasa!

Ikiwa Mazombi wanatumia gari zenye usajili wa vikosi vya SMZ, ni wazi kuwa serikali ndio inaowatumia Mazombi kwa sababu za kisiasa.

Ikiwa Mazombi wanatumia silaha za moto ambazo hakuna makundi ya watu wanaomiliki Zanzibar isipokuwa vikosi vya serikali, ni dhahiri kuwa serikali ya Zanzibar iko nyuma ya mchezo huu wote.

Ikiwa hawatoi madai yoyote ya wazi, ni wazi kuwa wanachokifanya ni kutia watu hofu katika kipindi cha uchaguzi, maana hicho hasa huwa ndicho wanachotumwa.

Kwa hivyo, kwa kuwa tunaweza kupata hitimisho la aina moja kwa masuali yetu – kuwa Mazombi ni vijana wanaotumiwa na serikali kwa sababu za kisiasa, basi tunaweza pia kuongeza hitimisho letu kwa kusema kuwa Mazombi nao ni mfano wa makundi vya mauaji (death squads), ambayo serekali nyingi duniani huyatumia kwa sababu zao za kisiasa.

Lakini suala la kuwa Mazombi wanatumika na SMZ si la muhimu tena sana,  kwani kila mtu analijua hilo sasa, ushahidi wa picha, macho ya watu na hata miti kama ingekuwa na uwezo wa kusema ingelishuhudia hilo.

Labda la  kushukuru ni kuwa, kwa sababu moja au nyengine, Mazombi hawakufanikiwa kufanya mauaji ya kutisha kama wale wa Alianza Anticomunista wa Argentina, lakini walipiga, walitia hofu raia, waliharibu mali na kujeruhi vibaya mno na yapo matukio mengine ya kushangaza ambayo si ajabu kuamini kuwa wao ndio watekelezaji.

Matukio ya nyumba za watu kuchomwa moto, maskani za vyama vya kisiasa Unguja na Pemba, vyombo vya habari kuvamiwa na waandishi kutekwa, vipigo na majeraha wanayopewa raia wa kawaida, napigia mstari kwamba hii ni kazi ambayo watu waliandaliwa kuifanya kwa sababu za kisiasa.

Lilo la muhimu kwa sasa ni kuwa wananchi waelewe na ulimwengu mzima ufahamu kuwa Mazombi ni mfano wa “death squads” kama ambavyo mataifa mengine yanatumia makundi hayo kwa faida za kisiasa, lakini la muhimu kuliko yote ni kuelewa kuwa utakapokaribia uchaguzi mwengine wowote ujao,  Mazombi watarudi tena.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Rashid Abdallah, mwanafunzi wa stashahada ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro.

One thought on “Mazombi ya Zanzibar ni mfano wa ‘death squads’”

  1. kwanini hatujibu mapigo ikiwa hadi magari wanayotumia tunayajua tuwachewoga tufute kaulu ya mapinduzi daima

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.