Ni miezi imepita tangu kufanyika kwa kile kiitwacho “Uchaguzi Mkuu wa Marudio” wa Machi 20 baada ya ule wa awali wa Oktoba 25 “kufutwa” na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Ingawa hatua hizo zote mbili – yaani kufutwa na kurejewa kwa uchaguzi wa Zanzibar – zilipigwa vikali na waangalizi wote wa ndani na wa kimataifa, wakiwemo wa Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola, vyama vya upinzani zaidi ya sita kati ya vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo kikiwemo chama kikuu cha upinzani – Chama cha Wananchi (CUF) – ambacho inasemekana ndicho kilichoelekea kupata ushindi wa uchaguzi huo wa Oktoba 25, bado zilitendeka.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Lakini pamoja na kutendeka kwake na hatimaye kuapishwa kwa waliosemekana kushinda kwenye uchaguzi wa Machi 20, CUF pamoja na mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, wamekuwa wakiendelea na hatua ya kuusaka ushindi wao ulioyeyuka mikononi mwa Jecha kwa kitendo chake kinachoelezwa kwamba ni kinyume na sheria na hakikufuata utaratibu wa uchaguzi.

Nimekuwa nikijiuliza, nadhani na wengi wanajiuliza, ni kipi kinachompa matumaini Maalim Seif kwamba ataipata haki ya kuiongoza Zanzibar kama anavyoidai? Najiuliza hivi kutokana na kauli za kuwahakikishia wananchi kila wakati anapokutana nao kwamba ataipata haki hiyo kwa njia za amani bila ya kumwagika hata tone moja la damu, huku mpinzani wake, Dk. Ali Mohammed Shein, akimtunishia msuli kwamba yeye (Maalim Seif) hana uwezo wa kumng’oa madarakani.

Haikuwa hadi tarehe 13 Juni 2016, ndipo nilipoanza kulipata jawabu la swali langu. Maalim Seif, ambaye hadi naandika makala hii yuko ziarani nchini Marekani, siku hiyo alihudhuria mkutano uliondaliwa na Taasisi ya “Center for Strategic and International Studies” (CSIS) ya nchi hiyo, ambapo katika mkutano huo alielezea mwenendo mzima wa hali ya uchaguzi ulivyokwenda na matokeo yake baada ya uchaguzi.

Kualikwa katika kikao na taasisi hiyo kuna ishara nyingi na kubwa kwenye siasa za mapambano kwa viongozi wa Kiafrika ambao wamepitia uzoefu kama huu alioupitia Maalim Seif. Rais wa sasa wa Ivory Coast, Alassane Outtara, baada ya kuaminika kushinda uchaguzi wa mwaka 2010 na ambao rais wa wakati huo, Laurent Gbagbo, alikataa kuachia madaraka na kusababisha mauaji na mateso ya maelfu ya raia wa Ivory Coast, alikuwa akialikwa kuhudhuria mikutano kama hii.

Bahati mbaya, Ouattara hakuweza kuhudhuria moja kwa moja kwa kuwa maafisa wa kiusalama na waliokuwa watiifu kwa Rais Gbagbo walipogundua ana mpango wa kuondoka nchini ili kuhudhuria mkutano huo, walimueka kizuizini katika hoteli moja mjini Abidjan.

Pamoja na kizuzi hicho, lakini Ouattara aliweza kushiriki kwa njia ya simu kama ilivyoelezwa na John Hamre, rais wa CSIS, katika mkutano mwengine kama huo ulioandaliwa tena kwa ajili ya Oauttara miezi sita baada ya kuapishwa kuwa rais wa nchi hiyo kwa msaada wa jumuiya za kimataifa ikiwemo CSIC nasSerikali ya Ufaransa.

Kwa mantiki hiyo, hatua hizi anazozichukuwa Maalim Seif pamoja na jumuiya za kimataifa kama CSIS na nyenginezo, mimi nauona kuwa ndio mlango aliopitia Rais Ouattara kumrejeshea ushindi wake wa urais ulioporwa na Gbagbo na, hivyo, unaweza kuwa sawa kwa Maalim Seif.

Huenda pia alipoishia Gbagbo sasa, ambaye anasubiri mashitaka dhidi yake akiwa kwenye mikono ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague, ndipo atakapoishia yule anayejisifia kwa kuwa na vifaru, bunduki na mizinga. Wakati utaamua!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.