Licha ya Naibu Spika, Dkt. Tulia Akson, spika kuwatishia wabunge wa upinzani, ambao wamekuwa na kawaida ya kujisajili na baadaye kutoka kila siku ambayo bunge linaongozwa na yeye, inaonesha dhahiri kwamba wabunge hao hawapo bungeni kwa kufuata posho pekee.

Leo tarehe 14 Juni 2016, wabunge hao wamedhihirisha tena kwamba kwao posho sio kitu cha msingi, kwani waliendelea na hatua yao ya kutoka bungeni mara baada ya Dkt. Tulia alipoingia na kukalia kiti cha uspika kwa ajili ya kuendesha bunge hilo.

Ikumbukwe kwamba wabunge hao wanapingana na mwenendo ambao naibu huyo wa spika analiendesha bunge hilo, wakimshutumu kwa ubabe, uonevu na kutoheshimu kanuni na taratibu za uendeshaji bung. Ikumbukwe pia, kwamba wiki moja iliyopita Dkt. Tulia alitoa maamuzi kwamba wabunge wote watakaotoka bungeni bila ya shughuli za maalum, basi wasingelipwa posho kwa kipindi chote ambacho hawapo katika vikao vya bunge.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Dkt. Tulia alisema kutokana na wabunge wengi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kulalamika na kuomba mwongozo wa spika juu ya wabunge wanaotoka nje baaada ya kujisajili, alikuwa amelipitia suala hilo na hatimaye kuja na hitimisho kuwa wabunge hao hawatapokea posho zao kwa kipindi chote ambacho hawakuhudhuria vikao.

“Uamuzi huu nimeufikia baada ya kupitia maamuzi mbalimbali yaliyotolewa na bunge juu ya wabunge ambao walikuwa wanaondoka bila kuchangia mjadala, ambapo tarehe 08 Aprili 2008 wabunge wa chama cha CUF walitoka bungeni na kususia shughuli zilizokuwa zimepangwa na kiti kilitoa uamuzi wa kutowalipa posho kwa siku zote watakazokuwa nje” Alisema Tulia.

Vitendo vyote viwili vinavyofanywa na pande zote mbili si viashiria vyema vya ustawi wa taifa na demokrasia. Pamoja na kwamba utamaduni wa wabunge kutoka bungeni pale inapofikia kutokubaliana na jambo fulani, ni kitendo kinachokubalika katika nchi zinazofuata mfumo wa demokrasia, kwa kuwa ni ishara ya kujisafisha kutokana na kinachotendeka wanachoamini si sahihi, lakini ni picha mbaya kwa jumuiya zinazosimamia mfumo huo na hata kwa raia wa ndani ya nchi.

Lakini pia si picha nzuri kwa naibu spika na bunge kwa ujumla hasa katika ulimwengu huu unaoamini katika majadiliano na maridhiano, ambazo ni miongoni mwa kazi za bunge na naibu spika. Hivyo, Dk. Tulia ana dhima ya kuliunganisha bunge na sio kukubali mgawanyiko.

Nianachokiona mbele ya macho yangu ni msitu wa kiza uliofungwa vyema kwa kamba za ‘Mkunguzi’ na chini yake kukiwa na miba mikali ya kifaurongo, kwani leo ni siku ya 11 tangu wapinzani waanze hatua yao hii. Naibu Spika na Wabunge hao wamewakosesha uwakilishi mamilioni ya Watanzania nchini, huku pande zote zikitunisha misuli kutokubali kushindwa.

Upande wa uongozi wa bunge unaonekana kukomaa zaidi kwa kuwa wangeweza kumtumia Spika Job Ndugai au wenyeviti wa bunge hilo kukalia kiti, wakati wakitatua tofauti hii, endapo kuna nia njema. Lakini hadi leo hii, Mheshimiwa Ndugai hajakalia kiti kwa siku hizo zaidi ya 10, wakati kabla ya sarakasi hizi haijawahi kutokea. Tuliwahi kuambiwa yuko matibabuni. Ukweli wa hilo unahitaji kuthibitishwa.

Najiuliza kwa nini pande mbili hizi zisikae kutafakari hali hii kushauriana na kukubaliana na kupatana badala ya kuendeleza uadui, uhasama na kutishana?

Ikiwa hawaoni suluhisho la tatizo hilo wao wenyewe, basi kipo chombo cha usulihishi na utatuzi wa migogoro ya kisiasa. Bunge ni sehemu ya siasa kwa kuwa ili uwe mbunge lazima utoke katika cham kimojawapo cha siasa, hivyo Baraza la Vyama vya Siasa liombe kuingilia kati mgogoro huu na kuutafutia usuluhishi.

Endapo hali hii ikiendelea kupuuzwa, basi taifa linazidi kupasuka na baadaye kutawayjika.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.