Vuta picha kwamba uko usingizini ndani ya nyumba ambayo imeezekwa kwa makuti na tayari yana miaka kadhaa juu ya paa na, hivyo, yameshakauka na yameshaanza kupoteza uimara wake wa kuweza kuhimili mvua kubwa kama za Masika au Vuli. Makuti hayo yamebadilika na kuwa kama upukupuku kiasi cha kupoteza sura halisi ya kuti hadi kutoeleweka iwapo ni makuti ya mnazi au nyasi za ukoka.
Ghafla usiku wa saa  6:00, nyumba hii inaungua moto wakati wewe na watoto wako mumelala. Mungu anafanya rehma zake, unashituka kutoka usingizini na kukuta moto umepashanda juu na tayari mapaa ya nyumba ya makuti yaliyochoka yameanza kuteketea. Unaamka kutafuta nguo za kujistiri, kisha unatoka chumbani ulimokuwa na kwenda chumba kingine kwa lengo la kumuamsha mwenzi wako kwa vile mulilala vyumba tofauti. Hata hivyo, wakati ukimuamsha mwenzi wako, yeye anaamua kukukatalia kwamba huo sio moto, na anakutaka urudi chumbani ukalale. Wewe kwa juhudi kubwa unaendelea kumuamsha sambamba na kupaza sauti za “moto, moto, moto” ili mupate msaada toka kwa majirani.
Kweli, majirani wanatoka na kuja kukupa msaada wa kuzima moto ambao kweli ulikuwa unawaka juu ya paa la nyumba yako. Hata hivyo, wakati majirani wakifika kwenye nyumba yako, wanakuta tayari kuna mtu yuko juu ya paa la nyumba akiendelea na juhudi za kuuzima moto huo na tayari amefanikiwa kiasi kikubwa kuudhibiti. Vipi ameweza kufika juu ya paa refu la nyumba ya makuti na kufanikiwa kuudhibiti moto huo, hicho bado ni kitendawili na suali ambalo hadi leo hii wananchi wa Pembeni, Shengejuu, kisiwani Pemba bado wanajiuliza pasi na kupata jibu.
Nilifika nyumbani kwa Bwana Ali Hamad maarufu Ali Basha na kupata mkasa mzima wa nyumba yao kuungua moto huku wenyewe wakilinasibisha tukio hili na hujuma za kisiasa dhidi yao na hawakusita kwakueleza wasiwasi wao kwamba waliofanya hili ni wafuasi wa Chama Cha Wananchi – CUF. Bwana Ali na Mkewe bi Raya ni makada wa Chama Cha Mapinduzi-CCM na wasaidizi wa Sheha wa shehia ya Pembeni Shengejuu. Walinieleza kwa undani namna tukio hili lilivyo tokea lakini ingawa walitumia juhudi kubwa kulijengea taswira tukio hili kwamba lilifanywa maksudi dhidi yao na wapinzani wao wa kisiasa, nilishangaa pale waliponieleza kwamba majirani wote waliofika kuuzima moto huo walikuwa ni wafuasi wa CUF kwani eneo hilo wana CCM ni yeye na mkewe tu! Kwamba watu wabaya waliochoma nyumba hio moto ni wafuasi wa CUF halafu tena wabaya hao wakafanya uungwana kwa mbaya wao na wakampa msaada wa kila aina kuuzima moto huo!
 
Matukio yenye utata wa aina hii ni mengi mno kwenye kisiwa hiki cha Pemba. Binafsi nimeshuhudia matukio kadhaa likiwemo lile la uchomwaji wa shamba la mikarafuu kule Kwale kwenye milima ya Raha na Taifu Wete Pemba ambako pia mmiliki wa shamba hili bwana Ahmad Azzan na kada wa chama cha Mapinduzi hakusita kulinasibisha tukio hili na wapinzani wake wa CUF. Pia kwenye shamba hili kumejaa utata wa kimazingira kwani shamba hili liliungua baada yakufyekwa kwa amri ya Bwana Ahmad Azzan mwenyewe na siku mbili baadae likaunguzwa moto. Nilifika kwa bwana huyu saa 10 jioni siku ya pili lakini nilishangaa kwamba hadi muda huo hakuwa ameripoti tukio hili Polisi kwani hata nilipojaribu kumuuliza kamanda wa mkoa wa kaskazini Bwana Hasan Nasir hakuwa na taarifa za tukio hili ambalo lilitokea pua na mdomo na makao makuu yake huku Bwana Azzan mwenyewe akidai kwamba aliamua kupumzika na angekwenda kwa sheha na baadae polisi baada ya swala ya magharibi!
 
Pamoja na matukio haya, hivi karibuni kumeripotiwa matukio ya kukatwa mikarafuu na migomba huko wilaya ya mkoani kwenye vijiji vya Kiwani. Hata mara baada ya matukio haya mawili, kilichofuata na polisi kufika maeneo haya nakuanza kupiga mabomu ya machozi kinyume na matarajio ya wengi kwamba ungefanyika uchunguzi wa kisayansi na hatmaye wahusika wa kweli kufikishwa kwenye vyombo vya sheria lakini badala yake yanatengenezwa mazingira yakuwaingiza watu wasio husika kwenye dhiki hii ambayo pia inatoa taswira yakupangwa kwa malengo yakulikomoa kundi fulani la kisiasa!
 
Binafsi napata shaka juu ya ukweli wa matukio mengi yanayo tokea Pemba na kisha kunasibishwa na chama fulani. Napata mashaka kwavile matukio yote yaliotokea hutujaona wahusika wa kweli kukamatwa nakufikishwa kwenye vyombo vya kisheria na badala yake twashuhudia wakiangushiwa jumba bovu wanyonge wasio husika. Pengine umefika muda sasa wa Polisi kufanya kazi zake kisayansi na watuletee wahusika wa kweli hata kama ni hawa wajipigao wenyewe na kisha kuangua vilio! Nilimuuliza Bi Raya, jee paa refu kama hili, mwanao alitumia nyenzo gani usiku wa saa sita kuweza kupanda juu ya paa lenye moto? Hakutoa jibu na akabaki ana pwesa pwesa kama mdoli! Ni ngumu kuuzima moto wa makuti usiku wa saa sita kwa mazingira ya Pemba kwani muda huo ni usiku mkubwa mno au vinginevyo watu weshapanga unyambi wao wakujipiga wakilia! Twendeni na ipo siku tutafika!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.