Septemba 16, 2001, siku tano tu baada ya shambulio la Septemba 11, 2001 kule Marekani, Mchungaji Jeremiah Wright, aliyewahi kuwa mchungaji wa raisi wa sasa wa Marekani, Barack Obama, alitoa hotuba iliyowakera wahafidhina wa nchi hiyo lakini iliyokuwa na ukweli.

Siku hiyo ya Jumapili, akiwa kanisani mwake, Mchungaji Wright alisema maneno haya: “Tuliipora nchi hii (Marekani) kwa ugaidi kutoka kwa makabila ya wazawa ya Sioux, Apache, Arikara, Comanche, Arapaho na Navajo. Tulifanya ugaidi! Tuliwachukua Waafrika kutoka katika nchi zao kutujengea nchi yetu kiurahisi, kuwafanya watumwa na kuwafanya waishi na hofu. Ni ugaidi. Tuliiripua jamii ya watu weusi Panama na kuuwa watoto wasio na silaha, watoto wachanga na mama wajawazito na akinababa  wachapakazi. Tuliiripua nyumba ya Qaddafi na kumuua mtoto wake, tuliiripua Iraq na kuuwa raia wasio na silaha waliokuwa wakijitafutia maisha.Tuliripua Hiroshima na Nagasaki kwa nyuklia,  wala hatukuwahi kupepesa jicho. Tumeunga mkono taifa la kigaidi (Israel) dhidi ya Wapalestina na Makaburu dhidi ya Waafrika Kusini weusi .Na sasa tunaumia kwa sababu mambo ambayo tumeyafanya nje ya nchi yetu yanaturudia wenyewe. America’s chickens are coming home to roost (Vifaranga vya Kimarekani vinarudi nyumbani kupumzika).”

Vifaranga vinarudi nyumbani kupumzika ni msemo unaomaanisha kuwa matendo mabaya, maovu na machafu uliyoyafanya nyuma yanakurudi na kuwa tatizo kwako baadaye.  

Mchungaji Wright alikuwa na maana kuwa mashambulio ya Septemba 11, yalikuwa ni matokeo ya unyama, na uovu ambao Mrekani imeufanya katika nchini nyingi, akitolea mfano, utumwa, mauaji ya watu weusi Panama, na mabomu ya nyuklia kule Japan. Na vifaranga vya Kimarekani viliporudi nyumbani, athari zake zilikuwa kubwa kupita kiasi.  Kila mtu aliona.

Ukweli usiofichika ni kuwa katika nchi yetu ya Zanzibar vifaranga navyo vinarudi nyumbani kupumzika. Sasa tunavuna matatizo kwa sababu ya dhulma ambayo imetendwa huko nyuma.

Wiki kadhaa nyuma, Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid, aliamuru kufungwa kwa maduka matatu ya rejareja na kusimamisha magari ya abiria kati ya Wete na Mtambwe kwa madai ya kutoa huduma kwa misingi ya ubaguzi wa kisiasa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wafanyabiashara hao wamelalamikiwa na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiwatuhumu kukataa kuwahudumia kutokana na itikadi zao za vyama.

Lazima tukiri kuwa kinachoendelea sasa Zanzibar, na hasa kisiwani Pemba, ni tatizo. Watu  wanabaguana katika misiba, sherehe, vyombo vya usafiri na biashara kwa misingi ya tofauti za vyama. Wananchi wamekuwa maadui wao kwa wao – wanasusiana harusi, mazishi, maduka na shughuli mbali mbali za kijamii ambazo hapo awali walikuwa wakizifanya pamoja.

Sasa, katika nchi mara nyingi uovu ukifanywa na serikali, ni raia wa kawaida ndio wanaoumia. Uchafu uliofanywa na CCM na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika uchaguzi uliopita ndio sasa unaowanaoteketeza raia wa kawaida kwa sababu wao ndio wamegeukiana kuwa maadui wao kwa wao kwa matatizo yaliyosababishwa na watawala.

Hivi karibuni nilipokea simu kutoka huko Pemba, nikielezwa kuwa upande wa kaskazini ya kisiwa hicho ndiko ambako hali imekuwa mbaya zaidi, kwani wana-CCM wanasusiwa hadi vyakula harusini. Ule muingiliano wa awali wa kijamii umepotea kabisa. Hata hivyo, tunapoliangalia suala hili, tusione tu kuwa haya yanayofanywa (ya kususiana na kugomeana) huenda yakawa sio sahihi, lakini lazima tungalie chanzo ama mzizi wake. Tujiulize: mbona huko nyuma hayakuweko? Kwa nini leo?

Ukiyatafakari hayo na ukayatafakari maneno ya Mchungaji Wright, utapata jawabu kuwa vifaranga vya Kizanzibari navyo sasa vinarudi nyumbani kupumzika. Zanzibar inavuna matatizo ambayo yamesababishwa na uovu na ukosefu wa haki ambao CCM na SMZ wameufanya kipindi cha uchaguzi.

Wafuasi wa CUF wanaamini kuwa haki yao imeporwa, wamenyang’anywa tangu huko nyuma na Oktoba iliyopita unyang’anyi uliendelea, historia na muendelezo wa vipigo, mauaji, ubakaji, mazombi, utesaji na idhilali nyingi.

Uovu huo umezalisha chuki kati ya wafuasi wa CUF na CCM, kama vile ambavyo uovu ambao Marekani imeufanya katika mataifa mengine kisha ukazalisha tatizo la  Septemba 11. Hicho ndio kinachotokea sasa Pemba.

SMZ na CCM waelewe kuwa uovu siku zote utabaki kuwa ni vifaranga ambavyo vitarudi tu nyumbani kupumzika – kwamba uovu huzaa uovu, ugaidi huzaa ugaidi, ubaguzi huzaa ubaguzi, ukosefu wa haki huzaa matatizo kama haya tunayoyashuhudia.

Mnamo tarehe 27 Januari, 2016, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akihutubia Umoja huo alisema: “Vijana wa Kipalestina wamekosa matumaini. Wanakasirishwa na sera za kikandamizi za kupora ardhi zao na kuzikalia kimabavu. Wamechanganyikiwa na vikwazo vya kila siku katika maisha yao. Wanaangalia jinsi Israel inavyozikalia  kwa mabavu ardhi zao ikiwemo Jerusalem Mashariki, wanapanua na kupanua. Wanapoteza imani kwa kutoiyona ndoto yao ya kuwa huru, kuwa na mipaka na kuliona taifa huru la Palestina, linasonga mbele”.

Ban alizungumza mengi. Mazungumzo yake yalifuatia na matukio ya uchomaji visu ambayo Wapalestina wanatuhumiwa kuyafanya dhidi ya Waisrael. Sitaki kusema kuwa hili la kuchomana visu ni sahihi. La hasha! Lakini nataka kusema kuwa msingi wa tatizo sio kuchoma kisu, bali ni dhulma ambayo Israel inaifanya dhidi ya Wapalesitina, ikwa ni pamoja na kuchukua ardhi zao kwa nguvu, kuwafunga watoto wadogo magerezani, ukandamizaji na mauaji.

Wapalestina wamekata tamaa, wamechanganyikiwa wakiamini kuwa kuchoma visu ndio suluhisho kama vile ambayo Pemba wamekata tamaa na dhulma za CCM wakiamini kuwa kuwasusia ndugu zao harusi, matanga, maduka na magari ndilo suluhisho. Kwa ukweli si suluhisho la tatizo la msingi lililopo, lakini pia si tatizo lenyewe. Ni matokeo tu ya tatizo, ambalo ni dhulma za wazi dhidi yao. Siku zote itazaa matatizo, kinachozaliwa sio msingi wa tatizo, ila kile kinachosababisha haya mataitzo yatokee ndicho tatizo kubwa.

Kinachotoke Pemba ni mavuno ya dhulma, ubabe, unyang’anyi, wizi wa haki, ubakaji wa demokrasia. Vifaranga tayari vimerudi nyumbani kupumzika. Sasa tutaona mengi yakiwa ni matokeo ya uovu wa SMZ na CCM. Kama kuna watu wanataka kweli suluhisho la yanayotokea Pemba, warudi kwanza kwenye chanzo chake. Rudisheni haki, wacheni dhuluma!

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Rashid Abdallah, mwanafunzi wa Stahahada ya Mawasiliano ya Umma wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro.

2 thoughts on “Vifaranga vya Zanzibar vyarudi nyumbani kupumzika”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.