Wiki hii imekuwa wiki ya Micheweni. Imesadifu kwamba watu wawili dhaifu kuitwa na kuhojiwa na mamlaka za dola kwa muda na maeneo tofauti. Ambapo siku ya Jumatano ya tarehe 8 Juni 2016, Idara ya Habari Maelezo kisiwani Pemba ilimwita na kumuhoji kwa zaidi ya saa moja na nusu mwandishi wa makala hii katika ofisi za idara hio mjini Chake Chake, kwa upande wake Jeshi la Polisi lilimwita n akumuhoji zaidi ya masaa mawili Mwenyekiti wa wa Chama Wananchi (CUF) wa Wilaya ya Micheweni, Bwana Rashid Khalid, kwa kile kinachodaiwa “kutoa kauli za uchochezi.”

Hata hivyo, wakati Bwana Khalid alihojiwa kwa madai ya uchochezi, kwa mwandishi wa makala hii hapakuwepo na madai makhsusi wala mdai anayemlalamikia, jambo ambalo linazua masuali mengi vichwani mwa wadadisi wa mambo. Ingawa si jambo baya kwa vyombo vya sheria na vile vyenye dhamana ya mambo husika kuwaita wanaoonekana kuwa sehemu ya vyombo na dhamana hizo kwa mahojiano, kuna kila dalili kuwa matukio yote mawili ni muendelezo wa vitisho sambamba na kutengeneza mazingira ya kuwafungulia mashitaka.

Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris

Kwa upande wa mwandishi wa makala hii, kinachookena wazi ni kuwa pana mbinu pia za kumfungia kutofanya kazi zake, ambazo zimekuwa zikisikika kwenye vyombo vya habari vya kimataifa pamoja na mitandao mingine ndani na nje ya nchi. Huenda hilo halijawapendezesha wenye mamlaka kiasi cha wakubwa kushinikiza kudhibitiwa kwa mwandishi huyo, licha ya kutokuwepo kwa madai ya msingi dhidi yake.

Kadhia za wawili hawa zimekuja muda mchache baada ya Jeshi la Polisi kumuhoji kiongozi mkuu wa upinzani visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye wiki chache zilizopita alikuwa kisiwani Pemba kwenye ziara ya kuwashukuru wapigakura wa huko. Ikumbukwe kwamba kwa miongo kadhaa sasa, kisiwa cha Pemba kimekuwa ngome imara na isiyotetereka ya CUF kinachoongozwa na Maalim Seif. Tangu kurejeshwa tena kwa  mfumo wa vyama vingi katika miaka ya ‘90, haijawahi kutokea kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata kiti kwenye chaguzi zote ambazo chama cha CUF kiliamua kushiriki uchaguzi.

Mara baada ya kufutwa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, Pemba imekuwa miongoni mwa maeneo yenye fukuto kali la kisiasa kiasi cha utengamano wa kijamii kutoweka baina ya wafuasi wa vyama vyenye ushindani mkubwa vya CUF   na CCM. Tukio la kufutwa kwa uchaguzi ndio lililopelekea haya yanayojiri sasa ya watu kutozikana au kutopeana huduma kwenye maeneo mbalimbali ya kijamii, kama vile madukani au kwenye magari ya usafiri.

Tofauti na miaka mingine, fukuto la mwaka huu limekuwa kali zaidi kutokana na mbinu mpya itumiwayo na wanajamii walio wengi dhidi ya wachache, ambao wanaaminika kuwa wafuasi wa CCM. Mbinu mpya itumiwayo na wanachi wengi ni ile yakuuza bidhaa kwa wana CCM tu na sio kununua kutoka kwao, jambo ambalo limepelekea wana-CCM wengi kufunga biashara zao kwa kukosa wateja.

Hata hivyo, kuna hali ya mbinu hizi kubadilika na kuchukuwa hatua ya juu zaidi kutoka ile ya kutengwa na kususiwa maduka na magari tu, hadi sasa inaelekea kugomewa hata wale wachache ambao hutokezea kutoa huduma kwa mwana-CCM! Na hili linawaumiza watawala sana, inavyoonekana.

Kuna siku nilipata kushuhudia watu wakiisusia supu baada ya kada mmoja maarufu wa Wingwi Mapofu ajulikanaye kwa jina la Beden kukaa kwenye barza ya soko, mahala ambapo mwana CUF hupatumia kila asubuhi kuuza supu yake ya kuku. Nimeshuhudia pia bwana mwengine akikimbiwa na wateja baada ya barza yake ya kahawa kuhudumia wana-CCM na hivyo kupelekea barza hii kufa baada ya muuza kahawa huyu kuhamisha kijiwe chake kwa kuwakimbia wana CCM hao, ambao kwake wanapelekea afe njaa. Nimeshuhudia abiria kumi na nne wakiteremka gari baada ya mwana-CCM mmoja kuingia kwenye gari hiyo, jambo ambalo lilimlazimu kondakta kumteresha mtu huyo ili asipoteze abiria wake aliokwishatoka nao mbali.

Hivyo taswira ya mgomo na fukuto hili ni zito na ngumu kudhibitika. Ni ngumu kwa vile haya ni maamuzi ya umma ambao unaamini kutotendewa haki na watawala na sasa wameamua kuonesha nguvu na hisia zao kwa watawala hao kwa njia hii ya kinyonge sana lakini yenye mchomo mkali. Je, vifaru na makombora vitafua dafu kwenye mazingira kama haya?

Binafsi siamini kwamba utatuzi wa sintofahamu hii utapatikana kwa njia za mabavu ya kutishiana vifaru au mizinga. Au utapatikana kwa njia ya kufunga midomo ya waandishi wa habari au kuwaita na kuwahoji viongozi wa kisiasa kwenye vituo vya polisi. Siamini kwamba dola ina ubavu wa kushindana na raia zake, halafu iwe mshindi. Siamini hilo!

Pengine watawala wameamua kutumia kodi zetu nyingi kwa kuimarisha vikosi vyao vya ulinzi, badala ya huduma nyingine muhimu za kijamii. Nalisema hili kwa sababu naona jinsi magari ya kijeshi yapishanavyo ili kuonyesha raia namna vikosi vyetu vilivokuwa imara, lakini haya yanafanyika wakati kwenye mahospitali yote ya kisiwani Pemba hakupatikani tena hata Panadol. Serikali inaonesha namna ilivyo imara kupitia vikosi, lakini ikishindwa kuonyesha uimara wake kwenye huduma za kijamii kama vile elimu, afya, uvuvi, kilimo na maeneo mengine. Kuna haja gani ya kuonyesha uimara wa kijeshi, wakati watu hawapati huduma muhimu kama vile maji na badala yake biashara zote zimefungwa kutokana na mripuko wa kipindupindu!?

Pengine viongozi wetu wanautazama uimara wao kupitia vikosi kwa vile, pengine, ndivyo vilivyowaweka kwenye madaraka. Lakini wengine fikra zetu hazikulala huko na hatuna imani wala matumaini kwamba nchi itaweza kusonga mbele kwa utawalaji wa aina hii. Hatuamini kwa vile wapo waliopata kuwa na majeshi na vikosi imara sambamba na viwanda vikubwa vya kutengeneza silaha hizo, lakini umma ulipowakataa, walisalimu amri na wengine kufa magerezani. Kwa hapa Afrika rejeeni kwa makaburu. Je, tunalo jeshi na vikosi imara kupita vile vya P.W. Botha wa Afrika ya Kusini, Hosni Mubarak wa Misri na Muammar Gaddafi wa Libya?

Tumekuwa watu wa ajabu tunaoongozwa na hasadi za roho badala ya utu. Siamini kwamba watawala wangepata tena uthubutu wa kuirejesha Zanzibar kwenye shimo lenye mamba ambalo tulishatoka. Siamini kama wale vinara wa haya wamefikiri vizuri. Tulishatoka kwenye ujinga huu na nchi ilishaanza kusonga mbele, lakini leo wameturudisha tena kwa ulafi tu wa madaraka na vyeo! Ili iweje?

Hivi hawaoni madhila wanayoyapata watu kwa kukosa huduma za msingi? Hawaoni wanyonge wanavyoteseka kwa kukosa madawa, huku wakiwa hawana vipato vya kuyanunua? Hivi Dk. Ali Mohammed Shein hawaoni maskini wa Unguja na Pemba wanavyohangaika na vitoto ambavyo vinakaribia kuwafia migongoni mwao kwa maradhi na njaa?

Akili yangu ishavurugika kwani naandika haya huku machozi yakinitoka na sasa najihisi si miye tena. Ila fanyeni mufanyavyo, vifaru na mizinga havitowafanya muogopwe na umma ambao umeshapoteza imani nanyi na hii ya kuita watu na kuwahoji au hata kuwatia magerezani haitowasaidia, bali huku ni sawa na kulitia panga cherehe ili likate zaidi.

Madhila mumewadhili wengi, kufunga mumefunga wengi na kutesa kila mtu ana kovu lenu ndani ya moyo wake, lakini je, mumewaweza au bado ni mwiba mkali uchomao nafsi zenu!?

Maalim Seif hana hata kisu cha chane, lakini ana umma unaompenda na kumkubali. Hamutomuweza sio kwa vifaru na mizinga bali hata kwa B52. Acheni kuudhikisha umma ambao hauna shida nanyi na uliwathibitishia hilo Oktoba 25. Munayoufanyia sasa ni fedheha zaidi kwenu!

Tanbihi: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, ni mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba na anapatikana kwa simu nambari +255 774 581 264.

 

One thought on “Mwenye mizinga na mwenye umma, nani hasa mwenye nguvu?”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.