Kuweza kuifanya makala hii ifahamike kirahisi kwako, ni bora niielezee kwa mtiriko wa hadithi, kuanza tukio la mwanzo kabisa hadi la mwisho kabisa.

Wiki iliyopita nilipata simu kutoka kwa bwana mmoja aliyepata kunipeleka eneo la Likoni penye kivuuko kinachounganisha kisiwa kikubwa cha Pemba na kile kidogo cha Kojani.

llibidi nipelekwe eneo hili kwa kuwa usafiri wangu uliniharibikia. Nililazimika kwenda Likoni kuripoti tukio la kuzuwiwa kwa boti mbili zitumikazo na wakaazi wa kisiwa cha Kojani, ambao wengi wao hulazimika kutoka kwenye kisiwa hicho kila asubuhi na kuvuuka kuja eneo la Likoni na kisha kusambaa kwenye vijiji na miji mbali mbali ya mbali na karibu kwa kazi za kilimo au shughuli nyingine za kuendesha maisha yao sambamba na huduma nyingine kama vile za matibabu au elimu.

Na Ahmad Abu Farsi
Na Ahmad Abu Farsi

Nilifika Likoni majira ya saa tisa kasorobo mchana na bahati njema nikakuta boti hizo mbili zimeshaachiwa baada ya kuzuiliwa zaidi ya masaa sita na askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo (KMKM) kwa mujibu wa maelezo niliyopata kutoka kwa msemaji wa Wakojani ambaye aliteuliwa kufanya mahojiano nami.

Bwana huyo alinieleza adha waliyoipata kwa uamuzi huu wa KMKM kuzuwia vyombo hivi pekee wavitegemeavyo kwa kuwavuusha kwenda au kurudi kisiwani Kojani. Hata hivyo, mwisho wa maelezo yake akanieleza kwamba suluhu ilishapatikana baina yao na hatimaye kurejeshewa tena usafiri wao huo wa pekee.

Mara baada ya kupata maelezo hayo ya wakaazi hawa, nikalazimika kufunga tena safari hadi Makao Makuu ya KMKM, mjini Wete, ili kupata maelezo ya upande wa pili kama inavyotakiwa katika kazi yangu ya uandishi. Kwamba siruhusiki kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari katika jambo ambalo linahusisha pande nyingi na tata,  hadi niwe nimeikamilisha taarifa yangu kwa kumuhusisha kila mwenye kuhusika nayo. Kwa vile suala la Likoni lilihusisha wananchi na kikosi hiki cha KMKM, na nilishafika eneo la tukio na kupata maoni ya wananchi, sasa nikalazimika kwenda kwa KMKM pia.

Niliwasili ofisi za KMKM saa kumi kasorobo alaasiri na nikajitambulisha mapokezi, ambapo pamoja na kuwa na kitambulisho changu cha kazi shingoni mwangu, nilijitambulisha kwa askari wawili waliokuwa mapokezi nakuomba kukutana na msemaji wa kikosi chao, ambaye kwa bahati nzuri alikuwa bado yungali ofisini.

Mtu wa mapokezi alinikubalia ombi langu mara moja na akamfuata dada mmoja ambaye nadhani ndiye katibu muhtasi wa bosi wa KMKM. Naye bila kuchelewa alifika mapokezi kunisikiliza na kisha kufikisha taarifa za uwepo wangu na madhumuni yake kwa bosi mwenyewe. Bila kukawia, akarejea kuniambia kwamba bosi alikuwa amekubali kukutana na mimi ila kwa sharti la kuwacha kila kitu pale mapokezi. Hivyo nikakabidhisha kamera, tablet na simu yangu ya mkononi.

Nilipoingia ofisini mwa bosi, nikakutana na jopo la watu watatu ambao wote walibeba ishara za vyeo na ukubwa katika kikosi. Nilikaribishwa kwenye kochi na kisha kuanza kuulizwa masuali mfululizo na watu wale ambao waliongozwa na mkuu wao aliyeketi nakujaa kwenye kiti. Baada ya masuali kadhaa ambayo aliyaandika kwenye karatasi, nikawasilisha kwake ombi langu la kutaka kufanya mahojiano naye kuhusu kadhia ya boti kuzuiliwa kutoa huduma kwa wananchi wa Kojani. Hata hivyo, ombi langu lilikataliwa kwa maelezo kwamba hadi muda niko pale hakuwa na taarifa za kutosha kuweza kunipa. Kamanda huyu wa KMKM alijitambulisha kwangu kwa jina moja tu la Hussein.

Niliondoka ofisi za KMKM nikiwa na masuali mengi zaidi kuliko niliyokuwa nimekwenda nayo. Inakuaje watu wamezuwiliwa usafiri wao kwa zaidi ya masaa sita na kikosi chake – tena usafiri pekee mkubwa – naye anakosa taarifa za kilichojiri? Je, KMKM inaendeshwa bila mkufu wa kamandi za kijeshi, kama vilivyo vikosi vyengine vya usalama?

Maswali mengine yalikuwa yanahusiana na mzozo wenyewe, hasa kulingana na hii hali ya ukisiwa. Kwamba huwezi kufika kisiwa kikuu cha Pemba kutoka Kojani kama hujavuuka kwa boti. Kutokana na udogo na muundo wake, wakaazi wengi wa kisiwa cha Kojani wanaishi wakitegemea mahitaji yao kutoka nje ya kisiwa hicho kidogo. Haishangazi miongoni mwao wakawemo wazee, watoto na wagonjwa, ambao bila kuwafikisha hospitali kama za Wete au Chake, hakuna utatuzi mwingine. Jee, ni sawa kuzuwia usafiri wa kuingia eneo kama hili kwa zaidi ya masaa sita?

Lakini ni sawa pia kukumbusha kuwa sababu ya kuzuiliwa kwa usafiri huo ilitokana na siasa. Kote kisiwani Pemba na visiwa vyake vidogo vidogo vinavyokizunguka, kunaendelea hivi sasa mgomo wa kijamii dhidi ya wafuasi wachache wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao wanashukiwa kuwasababishia majirani zao madhila na mateso kutoka vyombo vya dola na serikali kwa ujumla. Tayari wakaazi wa Mtambwe wako kwenye kipindi kama hiki cha kuzuiliwa vyombo vyao vya usafiri wa pwani na magari ya abiria kufutiwa leseni zao, kwa kile ambacho watawala wanaamini ni njia ya kuwalipizia kisasi kwa kushiriki mgomo huo.

Wakati nikiwa nimezama mtandaoni siku iliofuata, ghafla nikapigiwa simu na Bwana Mwinyi. Huyu ndiye yule dereva aliyenipeleka Likoni na baadaye makao makuu ya KMKM. Mwinyi alinieleza kwamba alipigiwa simu na RCO akitaka apatiwe namba zangu za simu. Hata hivyo, Mwinyi alipatwa na khofu kulingana na mambo yalivyo kwenye kisiwa hiki, ambako watu wanaonekana wazi kupoteza imani kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Baina yao sasa hapana tena kutazamana kwa jicho la wema bali la chuki iliyopitiliza. Hili limechangiwa sana na jinsi vyombo vyenyewe vilivyojikubalisha kuwa watumishi wa wanasiasa badala ya kuwa watumishi wa jamii yote bila kujali itikadi au misimamo ya kivyama. Kama kuna kosa baya ambalo vyombo vyetu vimelifanya, ni hili; kwani limewaweka mbali mno na mioyo ya watawaliwa, ingawa linawafurahisha watawala.

Mwinyi hakumpa namba yangu RCO huyo, bali mimi ndiye niliyemtaka anipe namba yake, kwani sikuwa na sababu ya kumkwepa wakati sina baya lolote nikumbukalo kulitenda au kumfanyia mtu. Kwa mujibu wa kazi yangu, ninapaswa kuwa karibu mno na polisi kwani matukio mengi huhitaji maelezo kutoka kwao. Sasa iwapo nitajiweka mbali nao, nitawezaje kufanya kazi yangu? Hapana siwezi kuwakwepa au kuwaogopa, kwani uoga si kitu ambacho muandishi anapaswa kuwa nacho.

Baada ya kumaliza mambo yangu, nikamtafuta RCO, lengo kutaka kujua, nini alihitaji kutoka kwangu kiasi cha kutafuta namba yangu kupitia watu mbalimbali, wakati kamanda wake wa Mkoa wa Kaskazini, Mzee Hassan Nasir, alikuwa na namba yangu? Alipokea simu na nikajitambulisha kwake na kutaka kujua hitajio lake kwangu. Hata hivyo, RCO alikataa kwamba si yeye anayenitafuta, bali Mkuu wa Idara ya Habari na Maelezo kisiwani Pemba. Nikaamuuliza: “Inakuaje mkuu wa idara ya habari atafute namba yangu kupitia kwako Bwana RCO?” Akajibu hajui. Nikacheka kisha nikamwambia: “Sawa ila kuna jungu linapikwa na mwisho wakee tutauona!”

Nilijuwa kazi ndiyo ilikuwa imeanza hiyo na chochote kinaweza kutokea dhidi yangu kuanzia sasa. Niliwaza hili kulingana na mazingira yalioizunguka tasnia ya habari hapa Zanzibar. Kwamba watu hutenda yao halafu hawataki dunia iambiwe yale watendayo. Lakini kwa nini waogope?

Siku iliyofata, nikapokea simu nyengine. Safari hii ilikuwa ni sauti ya mwanamke, ambaye alijitambulisha kwangu kama Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Pemba. Lazima niseme kuwa yeye, kinyume na wenzake wengine ambao hadi hapo nilikuwa nimeshawasiliana nao, alikuwa mpole na alitumia busara kubwa kuniingia. Hili lilinifurahisha kwani nilizihisi hekima zake. Kubwa alitaka kujua nilipo kwa muda ule na mwisho akataka nifike ofisini kwake kwani alikuwa na mazungumzo nami. Hapa nikataka anigusie kidogo kiini cha mazungumzo yetu, ila kwa vile huyu ni mwandishi kama mimi, akawa anajaribu kucheza na saikolojia yangu. Nikaahidi kufika leo Jumatano ya tarehe 8 Juni 2016, saa 4:00 asubuhi. Na kweli nikafika muda na saa kama nilivyoahidi.

Nilifika ofisi za Idara Habari Maelezo na kukutana na jopo jengine la watu wanne, ambao wote ni wafanyakazi wa idara hii hapa Pemba. Kubwa ambalo nimeitiwa ni malalamiko dhidi yangu ambayo ya idara hii imepokea. Nikauliza nani mlalamikaji? Nikaambiwa hajuilikani. Nikauliza malalamiko hayo yanahusu nini hasa makhsusi? Nacho pia hakikuwa kikijuilikana. Nikapigwa na butwaa. Yaani hata hawa watendaji wa idara yachabari pia hawamjui mlalamikaji na kile kinacholalamikiwa dhidi yangu mimi mwandishi wa habari mwenzao, na bado wananiita kujadili hilo!

Badala yake, Kaimu Mkurugenzi akataka nimpe rekodi za kazi ambazo nimeripoti kwenye vyombo vya habari. Mantiki ya dai hili ilinipa wakati mgumu kidogo, kwa vile mimi kama mlalamikiwa sikupaswa kudaiwa rekodi za taarifa zangu, ikiwa ndio kiini cha malalamiko kilipo. Ushahidi huo wa malalamiko dhidi yangu ulipaswa kutolewa na yule mlalamikaji kama ushahidi dhidi yangu!

Nimelisoma tukio la leo kama vile hakimu kupelekewa kesi, halafu akadai uthibitisho wa ushahidi  kwa mtuhumiwa! Kwamba Idara ya Habari inanitaka niwapatie uthibitisho kwa malalamiko ambayo hayapo na mlalamikaji asiyekuwepo! Lilikuwa tukio kubwa kwangu.

Hata hivyo, baada ya kukosa majibu kwa masuali yangu, jopo likataka nirejeshe kitambulisho ambacho nilipatiwa na idara hii kama ruhusa ya kufanya kazi zangu za uandishi kwenye mipaka ya Zanzibar. Uamuzi huu niliuridhia hapo hapo, ila kwa sharti moja tu – la kupatiwa kwa njia ya tamko la kusimamishwa kufanya kazi za kiuandishi sambamba na nakala ya malalamiko ya mlalamikaji ili yaiwe kama marejeo ya kuniwezesha kupigania haki yangu kisheria.

Hili nalo limeshindikana, kwani hakuna malalamiko wala mlalamikaji hadi sasa. Mkutano wangu umepangwa siku nyengine wiki ijayo.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, anaishi kisiwani Pemba na anapatikana kwa simu nambari +255 774 581 264.

 

One thought on “Mtawala anapoamua kufunga banda na farasi keshatoka”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.