Siku kadhaa zilizopita, nimeona makala iliyoandikwa na sheikh maarufu wa Tanganyika, Bwana Mohammed Idd Mohammed, maarufu kama Abu Idd, ambayo ilichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi kupitia safu yake iitwayo Kalamu ya Abu Idd. Katika safu hio alijaribu kuishauri serikali kutomkalia kimya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kile alichokiita “kauli zake za kichochezi”.

Sheikh Mohammed Idd Mohammed, "Abu Idd"
Sheikh Mohammed Idd Mohammed, “Abu Idd”

Kabla ya kuingia kwenye mada yenyewe, ni muhimu kumjuwa huyu Sheikh Abu Idd ni nani. Binafsi nimemjua Sheikh Mohamed Idd tangu miaka ya ‘90 mara baada ya kukaribishwa na kupewa uimamu wa Msikiti wa Mnyamani uliopo Buguruni, jijini Dar es Salaam. Mnyamani ni mtaa maarufu kibiashara kutika eneo la Buguruni na Vingunguti nzima, nami ndio mtaa nilioishi muda mrefu zaidi katika maisha yangu kupita eneo jingine lolote.

Nakumbuka msikiti huu ulikuwa miongoni mwa misikiti iliyogubikwa na umangimeza katika wilaya ya Ilala. Uongozi wa msikiti ulijaa unyambi na matumizi mabaya ya rasilimali. Ilifika mahali michango kwa waumini ikawa kero kutokana na kutoonekana tija yake na hivyo kupelekea kuzuka masuali miongoni mwa waumini na hatimaye kuibuka makundi mawili yaliopingana waziwazi hadi kufikia mahali waumini kuswali jamaa mbili ndani ya msikiti mmoja.

Kutokana na kundi lililoasi dhidi ya uongozi wa msikiti huu, ambalo liliongozwa na Sheikh Rajab Sultan Kikopa na Sheikh Rajab Vuru (Allah Awarehemu wote wawili) na katibu wao, Sheikh Juma Ismail Kipenzi, kuwa na nguvu kubwa kwa kuungwa mkono na vijana, uongozi uliingiwa khofu kuwa huenda msikiti ungeliangukia mikononi mwa wanaharakati hao. Hivyo ili kusaka salama ya kubakia madarakani, uongozi huo dhaifu na uliogubikwa na ufisadi wa kutisha dhidi ya mali za waumini, ukamtafuta mtu wa kuwaokoa, na hapo ndipo Sheikh Mohamed Idd aliposhawishiwa na kukubali kuwa imamu wa Msikiti wa Mnyamani.

Hata hivyo, ujio wa Sheikh Mohamed Idd haukuwa wa kawaida wala wa kistaarabu. Aliingia kwenye uongozi kwa staili ya mabavu na kudhalilisha jamii fulani ya watu na ubaguzi dhidi ya waumini wenye msimamo tofauti na ule wa Baraza la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), ambalo yeye alikuwa mwanachama wake. Ni ujio huo ambao kwa mara ya kwanza uliibuwa misamiati iliyokuwa haikufahamika kwenye eneo hilo, kama vile kubandikwa jina la MAWAHABI wale wote waliokuwa wakipingana na uongozi wa msikiti. Ni ujio huo pia ulioibua ubaguzi mkubwa dhidi ya jamii ya Kipemba, huku pia ukipelekeya mali za Waislamu kuliwa kwa mgongo wake.

Nakumbuka miongoni mwa mambo yaliyozuwa maswali mengi wakati wa mwanzo mwanzo wa uongozi wa Sheikh Mohammed Idd ni waumini kukosa sauti za kuhoji kima kikubwa cha pesa zilizoliwa na uongozi kwenye ununuzi wa jengo moja lililokuwa mbele ya kibla cha msikiti kabla ya kujengwa kama ulivyo sasa. Kwa wengi wetu vijana, kuja kwa Sheikh Mohammed Idd hakukuwa na uhusiano hata mmoja na kuupeleka mbele Uislamu na Waislamu.

Nakumbuka ni ujio ambao ulipelekea wengine kuhojiwa polisi kwa madai ya kuanzisha fujo msikitini na wengi wa waliohojiwa walikuwa vijana wenye asili ya Kizanzibari. Imesadifu hivyo kwa vile mtaa huu ni mtaa wa biashara na, hivyo, wengi wa waumini walikuwa ni Wazanzibari kutokana na wengi wao kuwa hapo kibiashara na kuwa wachangiaji wakubwa wa msikiti huo. Hawa walikuwa wanahoji inapokwendea michango yao.

Sio tu kuwa kuingia kwake kwenye uongozi wa msikiti huu kulifanikisha ile haja ya kufichwa madhambi ya wazee waliomuweka madarakani, bali pia ulimpa yeye Sheikh Mohammed Idd nafasi ya kujitengenezea kundi kubwa la wafuasi, hasa miongoni mwa wazee wahafidhina na makada wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na, hivyo, akafanikiwa kujijenga hadi uongozi wa juu wa chama hicho tawala na serikali.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Mohammed Idd ni miongoni mwa masheikh wa Tanganyika waliojikubalisha kutumika dhidi ya wapinzani enzi zile CCM ikiwa chini ya ukatibu mkuu wa Yussuf Makamba. Tulikuwa tunaambiwa kuwa alikuwa mmoja wa waliokuwa wameahidiwa umufti wa BAKWATA, jambo lililozuwa msuguano mkali baina yake na Sheikh wa sasa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum Mussa.

Ndiyo maana wala sishangai kusoma makala yake leo kwenye gazeti la Mwananchi akitoa kauli kama hii dhidi ya Maalim Seif, maana yeye yu miongoni mwa watu waliojikubalisha – tangu awali – kutumia dini kupeleka mbele maslahi yao na ya chama chao. Huyu hayupo msikitini kwa lengo la kuupeleka mbele Uislamu, bali ni aina fulani ya wapigadebe wa CCM wanaoutumia mgongo wa dini kujinufaisha binafsi.

Haiyumkini kwa kiongozi ajiitaye wa Kiislamu kutoa kauli za kujipendekeza kwa watawala, badala ya kusimamia haki na misingi ya ukweli. Tulitaraji kama ni mkweli angeangalia chanzo cha kauli za Maalim Seif na wala sio athari za kauli zake. Tulidhani angeutazama na kuutolea kauli uchaguzi wa Oktoba 25 uliofutwa kwa misingi ya kukibeba chama tawala na ule haramu wa Machi 20 ambao umesimika upya mizizi ya fitna na hasama kwa Waislamu wa visiwani, kwa kuyavunja kabisa Maridhiano  na Umoja wa Kitaifa.

Nilidhani Sheikh Mohammed Idd wetu angekuwa muumini wa kweli kwa kuwaeleza watawala waliokataliwa jinsi ilivyo vibaya kutenda dhulma dhidi ya wanyonge. Nilitarajia angekuwa wa kwanza kupaza sauti kama wafanyavyo masheikh makini na wasomi kama Maalim Ally Basaleh wa Masjid Idrissa.

Sijawahi kumsikia akikemea mateso wanayopatishwa Waislamu wanyonge wa Zanzibar na watawala wao, ambao katika Ramadhaan ya mwaka jana, walifika pahala pa kupigwa risasi, kubakiwa watoto wao na hata kushambuliwa majumbani mwao na makundi yaliyopewa jina la Mazombi, ambayo yanaratibiwa na CCM na vyombo vya dola. Alikaa kimya!

Leo hii anapokuja kuzungumzia umuhimu wa umoja baina ya Waislamu wa Zanzibar, kwa kumtuhumu Maalim Seif kuwa ni mgawanyaji watu, mtu anapaswa kujiuliza mengi kumuhusu. Lakini maswali hayo utajiuliza tu, ikiwa humjui hasa Sheikh Mohammed Idd na tabia yake halisi. Ukishamjuwa, hatakushangaza.

Tanbihi: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, ni mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba. Anapatikana kwa simu namba +255 774 581 264 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.