Wakati leo dunia ya Kiislamu ikiwa imegawika baina ya wale walio ndani ya funga ya Ramadhaan na wale ambao bado wanakula, hatuna budi kuliangalia suala hili kwa jicho la kifikra kulingana na mazingira yaliouzunguka Uislamu na Waislamu hivi sasa. Hapa nitajikita zaidi katika mazingira ya Waislamu wa Afrika Mashariki ambako mwenyewe nipo, wa Ulaya, ambako wako baadhi ya jamaa zangu, na wale wa Mashariki ya Kati, kunakoangaliwa kuwa ndiko kuliko na kitovu cha dini hii.

Mnamo majira ya saa 4:00 asubuhi ya leo Jumatatu ya tarehe 6 Juni 2016, nilifanya mazungumzo na mjomba wangu ambaye anaishi Munich, Ujerumani. Katika mazungumzo yetu nilimuuliza iwapo yupo kwenye swaumu au laa, naye akanieleza kwamba Waislamu wanaoishi Ulaya wapo kwenye funga ya siku ya kwanza ya Ramadhaan, kwa kuwa mara nyingi wakaazi wa bara hilo hufata mwandamo wa mwezi wa kimataifa, yaani ule ambao huonekanwa mahali popote na kutolewa taarifa za kuonekanwa kwake.

ahmad
Na Ahmad Abu Farsi

Wakati nikijadiliana hili na mjomba wangu huyo – yeye akiwa Ujerumani, nami nikiwa Pemba – pembeni yangu kuna mama anaandaa sheli la kupwaza kikiwa kisabeho cha wanawe, ambao kwa wanavyoonekana ni wakubwa wa kuweza kufunga. Maana yake ni kuwa, kwa mama huyu na watoto wake – kama ilivyo kwa sehemu kubwa ya wakaazi wa kisiwa hiki – leo si siku ya kufunga. Picha hizi mbili kwa wakati mmoja – moja ya mjomba wangu aliye Ujerumani na ya pili hii ya mama aliye kando yangu hapa kisiwani Pemba – ndizo chanzo cha wazo la makala hii.

Mazungumzo baina yangu na mjomba wangu yananifanya nijihisi kwamba kuna kitu ambacho nakikosea juu ya suala la funga ya Ramadhaan. Mawazo yananijaa na kuanza kuyafasiri mazingira yaliyonizunguka, hasa kwenye suala la imani yangu ya Kiislamu. Hivyo naanza kwa kuwatazama walio karibu yangu na jinsi ufahamu wao wa masuala ya Kiislamu ulivyo. Nagundua kwamba mimi nina afadhali mara mbili ya wao! Kwamba kama hivyo ndivyo, haiwezekani kwa wenzangu hawa kuishibisha nafsi yangu yenye kiu kali ya kutaka kujua, kwa mfano, kwa nini Waislamu wa Afrika Mashariki tutofautiane na wale wa Ulaya na Mashariki ya Kati kwenye kuiendea funga ya Ramadhaan.

Imesadifu kwamba sio mbali kutoka mahali tulipoketi pana madrassa. Hata hivyo, ndani ya madrassa hiyo kuna wanafunzi pekee waliobobea kwenye ucheza, kwani Maalim wao hayupo muda huu. Ninapowauliza alipo, wanafunzi wananijibu kwamba yuko shamba anapanda visiki vya muhogo.

Hali ya madrassa na hawa watoto haiashirii uwezekano wa kupatikana kwa wasomi wa baadaye wa hii dini yetu tuipendayo. Mazingira ya madrassa ni mabaya na si salama kwa watoto wanyonge wasomao ndani yake. Imejaa vumbi kiasi cha watoto wasomao ndani yake kuwa weupe utadhani walikuwa wakigaragara kwenye chokaa! Madrassa ina sura zote za eneo ambalo watoto hubeba zaidi maradhi kuliko elimu iliyokusudiwa. Wengi wa wasomao humu wanasumbuliwa na tatizo la mafua na kuliwa na funza miguuni, maarufu kama vyepu!

Sehemu kubwa ya waliomo kwenye madrassa hii ni watoto wadogo na wale wasiozidi miaka 14. Hapa ndio kusema idadi kubwa ya mabarobaro wa kuanzia miaka 15 na kuendelea wapo maporini wakipiga tanu au kokote kwengine wakijitafutia chochote cha kujikimu kimaisha. Yaani hawa hawapo madrassa wala skuli, bali maporini!

Tukubali kuwa suala la elimu kwetu limekuwa mtihani usio msahihishaji. Wengi huacha skuli na madrassa wakiingia kipindi cha baleghe, yaani mara baada ya kumaliza darasa la saba au kufikia umri wa miaka 15. Hapa kundi kubwa hudharau suala la elimu na kuseleleya kwenye mambo ya kutafuta zaidi pesa na si elimu tena. Pesa yenyewe si kwamba ipo ya kuwafanya hasa watatuwe matatizo ya maisha yao na ya familia zao.

Kizazi cha aina hii mara nyingi huishia kwenye kufata mkumbo na hivyo kujikuta kwenye utumwa wa kifikra. Hakisimami chenyewe, bali kila jambo huendewa katika hali ya kuiga kama afanyavyo fulani! Ni hawa ambao hutumbukia kwenye wigo wa kuvaa suruali chini ya makalio kama msanii fulani au hunyoa kiduku kama nyota fulani wa mpira. Hawa, hata wakielemea kwenye dini, basi nako huwa ni yale yale ya kufuata mkumbo. Wavae vikanzu vifupi na kufuga ndevu kama ustadhi fulani, lakini kichwani hawana maarifa yoyote ya dini hiyo.

Wakati hawa ndio walipaswa kuandaliwa kuwa maulamaa wa kutoa fatwa mbalimbali za masuala ya kidini hapo baadaye, leo wengi wamekimbia madrassa na sasa muda mwingi huutumia kuzurura maporini wakiwa na kundi kubwa la mbwa, eti wawinja! Ni hawa ambao walipaswa kuandaliwa kesho waje wawe madktari, lakini leo hawako mashuleni na sasa wanashinda maporini kukwapua mazao na kuiba kuku wa watu!

Hawa ndio leo wanaofuata ama mwandamo wa pao au wa nje ya pao, lakini si kwa elimu waliyonayo, bali  kwa ufuasi na ushabiki. Madrassa na skuli hazikuwajenga chochote cha aina hiyo, kwa wale wanaobakia, ingawa kama nilivyosema hapo kabla, wengi huwa hawasalii humo. Hamuna mazingira ya kuwaweka.

Siyaandiki haya kwa furaha, bali nimejaa simanzi isiyo na wa kuliondoa. Moyo wangu umejaa huzuni kuiona jamii ikiwa kwenye mazingira haya katika ulimwengu ambao unahitaji zaidi matumizi ya akili na sio miguvu ya misuli. Moyo unaniuma kuona nguvu kazi ambayo kama ingeandaliwa vizuri ingeliweza kuleta tija siku za usoni, ikiishia kwenye ukwezi na kupiga tanu za mkaa! Hawa ni watoto wetu. Hawa ndio mustakbali wa taifa letu.

Hakuna jamii iliyojaaliwa watu wake wote kuwa vilaza. Bali tatizo hili huandaliwa na wenye dhamana za kuongoza watu. Suala la elimu ni suala la mkakati ambao ukipangiliwa huneemesha wengi na ukikosewa ukaangamiza wengi. Kosa kubwa ambalo watawala wamelifanya kwa jamii, ni kudharau kwao madrassa na kuziona kama ni mahali pa kuwarundika watoto tu kwa mazoea ili tuambiwe kuwa tumewapeleka watoto wetu chuoni kusoma Qur’an na Maulidi.

Hivi sivyo. Kwenye jamii kama yetu ambayo ina 100% ya Waislamu, madrassa zingewekewa utaratibu sawa na ule uliowekwa kwenye maskuli. Tulitegemea watu muhimu kama waalimu wa madrassa nao wangelipwa kwa kazi yao iliyotukuka ya kuwaelimisha watoto tangu waanzapo kuitamka herufi ALIFU!

Hali hii ni tofauti sana na wenzetu. Wao suala la dini wamelipa umuhimu mkubwa kiasi cha wachache miongoni mwetu kwenda kujifunza kwao. Hawa suala la elimu ya dini wamelithamini na kulipa umuhimu mkubwa kama ambavyo twashuhudia wakizalisha maulamaa wakubwa ambao wengine tumetoka nao jamii moja.

Dk. Ibrahim Ali Hamad, almaaruf Ibrahim Ghullam, huyu ni kijana wa Kipemba ambaye kama tungekuwa na utaratibu mzuri wa kuthamini elimu ya dini, basi angekuwa bobezi wa masuala ya dini akiwa mdogo mno. Dk. Ghullam ni miongoni mwa waliopata fursa za kwenda kusoma nchi za Kiarabu na sasa ni daktari wa falsafa katika masuala ya dini ya Kiislamu na Katibu wa Baraza la Ulamaa Tanzania. Je, sisi, kama Waislamu wa kizazi na kizazi, tumeshindwa kuzalisha watu wa aina hii hapa kwetu?

Suala la kuandama kwa mwezi limekuwa na utata mkubwa miongoni mwetu. Hii inamaanisha kwamba wapo walao mchana wa mwezi wa Ramadhaan, huku wakijiona wako sawa, kwani suala la mwezi kuandama nje ya mipaka yao wao haliwahusu! Hapa kwangu pananipa utata wa kifikra kila mwaka iingiapo Ramadhaan. Zaidi huwa nawaza kama haiwezekani mtoto kuzaliwa mara mbili baada ya kukaa tumboni miezi tisa, je itawezekana vipi mwezi ambao ni mmoja duniani uandame mara mbili baada ya kukamilisha mzunguko wake wa siku 28 au 29?

Kwa vyovyote, wapo walao mchana wa Ramadhaan na suala hili linahitaji mjadala wa haraka wa wanazuoni wetu wenye kuaminika kwa elimu zao na sio umaarufu wao. Waitwe maulamaa waliobobea kwenye masuala ya mzunguko wa mwezi na vituo vyake ili watowe maamuzi ya kuishikimanisha dunia ya Kiislamu na sio hii ilioparaganyika! Waitwe waweke misingi mipya ya umoja duniani kama tunavyoamrishwa na Muumba wetu. Wakaye wajadili miparaganyiko hii ambayo haina tija kwetu zaidi ya kuleta farka. Kwamba tumefikia mahala sasa kuna mwezi wa watu waliopewa jina la mwezi wa VIKANZU (Ansar Sunna) na ule wa waitwao VITOJO (wanaosubiri kutangaziwa na kadhi wa Zanzibar). Najuwa hawa wameitwa VITOJO kutokana na maulamaa wanaosimamia suala la mwezi Zanzibar kunasibishwa na Chama Tawala, CCM!

Tukumbuke suala la dini kwetu limepewa umuhimu mdogo ukiacha kusali na kufunga. Sisi kuuona kwetu mwezi ni mpaka tukae juu ya mlima kweupeni tuutafute, ilihali wenzetu wana wizara za kusimamia suala la mwezi na nyenzo za kuutafuta popote ulipo. Wenzetu hawautafuti mwezi mwandamo kwa kukaa juu ya mlima, bali hupeleka vyombo angani kuutafuta! Wameunda mamlaka huru zenye kujiweza kwa kila aina kwa manufaa ya Waislamu. Wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuratibu na kusimamia mambo mbalimbali yahusuyo Uislamu. Hawapo pale kutekeleza amri za wakubwa wa dola, bali amri za Uislamu.

Wenzetu wamejenga taasisi ambazo leo zimekuwa na tija kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Na hapa ndipo chimbuko la sisi kukimbilia kwao pindi tunapohitaji kuujuwa vyema Uislamu wetu. Ni hawa walioanzisha na kufadhili vyuo mbalimbali ambavyo tumeshindwa kuvitumia vyema kwa maslahi ya Waislamu wa nchi hii. Ni hawa walioijenga na kuifadhili Tunguu University, Chuo cha Kiisilamu Kiuyu, na vingine vingi ambavyo vimekuwa chanzo cha sisi kujidai bila kutumia elimu inayopatikana ndani yao.

Suala la mwezi limegubikwa na utata mwingi, lakini haiyumkini Ulaya wafunge leo Ramadhaan, halafu sisi ambao tuko kwenye ukanda mmoja na Mashariki ya Kati, tuendelee kula mabale ya masheli mchana kwa kisingizio kwamba kwetu haujaonekana. Je, itawezekana mwezi mmoja uandame jana Mashariki ya Kati na leo uandame Afrika Mashariki? Au muandamo ni mmoja tu, isipokuwa kukubali kwetu kutangaziwa mwezi na “vitojo” ndio kosa letu litufanyalo tule mchana?

2 thoughts on “Waislamu wa Zanzibar twapaswa kujiangalia ndani yetu”

 1. Sheikh Ahmad, umeanza vyema unemalizia vibaya. Umeanza kwa kutoonesha unapoegemea ktk suala hili lenye ikhtilafu. Sikuona umuhimu kwako kulizungumzia suala la kidini kwa njia ya makala ya kisiasa. Lakini kwa sababu uligusia mambo ya kijamii kama elimu kwa vijana na ujenzi wa jamii bora ya baadae nilifurahia kuona unakonipeleka. Kadri nilivyokufata ktk safari yako nikagundua kwamba kumbe nawe umetatizwa na kuvutiwa na “vikanzu” kama mwenyewe ulivyowaita. Mas-ala haya wala si kwamba hayajibiwi, hayajadiliwi, au hayatolewi fatwa na hoja. La hasha! Maswali haya yana tatizo moja, watu hutia ushabiki. Na pia huchukua akili zao na uelewa wao mdogo wa hata mfumo wa dunia kisha wakajidai kuhoji fatwa za kidini. Basi hata hujiulizi kwa nn ulaya wanafata saudia? Kwa nini ulaya hawatazami muindamo wao? Mimi nchi nilipo nafinga madaa 20 na nusu. Ndani ya hii nchi hii hii kaskazini mwake hakutuji jua yaani kuna jua full time. Hawa je watafungaje? Badala ya kuwakejeli wafuatao “vitojo” ukadhani haiingii akilini nadhani ilikuwa busara ungebaki pale ulipotoa wito mambo haya yajadiliwe kwa kina, and of course, yamejadiliwa sana kiasi kwamba sasa kuhusu ramadhan ukitaka kujichanganya ujichanganye mwenyewe tu.

  Hata ulamaa maarufu duniani wameulizwa wakiwemo masheikh wakuu wa Saudia wa sasa na wale wa zamani kuhsu kufata mwezi wa kimataifa (au mwezi wa Saudia). Nao pamoja na kukiri kuwepo mvutano huo, wote wametoa rai ya kufata muindamo ktk nchi yako. Hata mwaka jana alifika sheikh mwenye kutegemewa kielimu na kukaribishwa na Sheikh Kishki. Akaulizwa akasema pia kwamba tufate muindamo wetu. Kiukweli ni kwamba ukiachilia mbali ulaya ambako misimu na hali zao za hewa pamoja na kutokuwepo kwa mamlaka za kiislam za kuthibitisha muindamo wa mwezi wao hufata Saudia kwa vile calender yake hupatikana kirahisi. Kwengineko kote hawafati bali hufata muindamo wao. Mashuhuri sana ya nchi zinazofata muindamo wake bila kutetereka ni Oman, pia na wengineo.

  Kiufupi nikukosoe jambo. Huko unakokudharua “kuangalia mwezi kwa kukaa juu ya kilima” ndiko mtume s.a.w alivyotuamrisha. Hakusema uchunguzeni mwezi kwa darubini. Na ndani ya Saudia taasisi nyingi za kiislam zinapinga jambo hili la kuweka calenda na kuuchunguza mwezi kwa vifaa. Ni izushi huu (bidaa). Kilichoelewa ni kuuangalia mwezi (kwa macho) na msipouona mkamilishe 30, yaani pakifanya wingu msiuone. Hakuna sharti la kutumia microscope. Kama Makka na Sham zishatofautiana kufunga kwa muindamo, washangaaje Afrika mashariki na mashariki ya kati. Mwisho kabisa. Sasa hivi Saudia wana nyakati zenye kutofautiana nasi za swala. Naambiwa kwamba sasa hivi takriban sisi Tanzania twaswali Isha wao ndio Maghrib yaingia. Ukitaka kujua kihusu haya mambo usiyaongee katika makala za kisiasa na kijamii, kayasome, jielimishe na uwaelimishe wengine. Wahka wako upewe majibu uridhike uifate dini yako kiusahihi. Ukiandika uwe unaeleza elimu yako sio mashaka yako.

  Mbali na hayo, makala yako imezungumza.mengi kuhsu jamii yetu ambayo twapaswa kuyatafakari kwa maendeleo ya nchi yetu.

 2. Na niongezee kidogo juu ya suala lako kuhsu umoja wa kiislam. Watu wengi wenye kushabikia muindamo wa kimataifa, na kiukweli sio muindamo wa kimataifa ni muindamo wa Saudia. Maana muindamo wa kimataifa ni kufunga kutokana na taarifa ya mwezi hata uonekane china. Lakini Saudia wao hawafati mwezi ukionekana kwengineko duniani. Uzumbukuku huu tunao sie tu huku kwetu. Jambo la mwezi kufunga pamoja au kutangulia kundi flani halihusiani na suala la umoja wa kiislam. Bwana Mtume s.a.w alipouzungumzia mwezi akasema pakifanya wingu mkawa hamuuoni basi mtimize 30, hakutueleza kwamba jitihada zifanyike kuusaka kwengineko duniani. Na ukumbuke kwamba uislam unandeshwa na sheria na tartibu zivukazo maendeleo ya wakati ambazo haziathiriki kwa kuwepo au kutokuwepo maendeleo ya sayansi na teknolojia. Enzi za Mtume s.a.w na baada ya kuondoka kwaje kwa karne nyingi hakukuwa na runinga, satelite, simu, wala namna ya kujua kichaendelea nchi au mji wa jirani isipokuwa kwa kumtuma mjumbe kwa farasi au ngamia na kurudisha majibu. Hii inaanshiria wazi kwamba walioambiwa pakifanya kiwingu mkawa hamuooni timizeni 30 ni jamii husika sio wingu dunia nzima.

  Kwa maana hiyo Mtume s.a.w alijua kuwa mahala tofauti huweza kuwa na utofauti wa muindamo. Lakini alipolizungumzia hili la swaumu hakututahadharisha kwamba tufunge pamoja dunia nzima maana ndio umoja wa kiislam, la hasha! Bali kilichosahihi ni kwamba ibada za swala na funga ziliegemezwa ktk nyakati za jua na muindamo wa mwezi. Msingi huu ni msingi madhubuti usihitaji satelite, darubini wala maendeleo ya sayansi na utabiri. Vipi leo tuutie uislam ugumu. Vipi leo tuutafsiri umoja wa kiislam kwa njia hii wakati yapo mambo muhimu kifalsafa ambayo ndiyo yanazungumzwa katika jambo linalohusu “umoja wa kiislam”. Yote hii ni fatwa akili ambayo twapaswa kuepukana nayo.

  Ni lazima tukaelewa ikhtilafu zilizopo ktk jambo hili, kisha kutokana na uzito wake mtu binafsi akajiridhisha kwa hoja ili afate fatwa inayomshawishi. Funga usimkejeli mwenzako, usimdharau wala usione kapitiwa na wakati au hajui. Kadri elimu inapokuwa ndipo utaheshimu tofauti za kimawazo, na kadri elimu inapokuwa ndipo utajithibitisha kuwa hujui na moyo wako utapata hekma na busara hutawaona wengine hawajui au hawajatafakari kama unavyoweza kutafakari wewe. Utapoanza kuyajadili mambo ukaona kama watu hufuata kibubusa kumbe ni hisia zako tu, bali kumbe watu wanaonekana wanafata kimazoea misingi iliyojengwa kielimu na kihoja thabiti. Hapa sipo mahala pake, niishie hapa. Wassalaam.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.