Kwa muda wa wiki kadhaa sasa eneo la Mtambwe limekuwa na shida ya usafiri kwa njia ya bahari. Eneo hili ni mashuhuri kwa shughuli zake za utumiaji wa vyombo vya baharini kama vile mashua na mitumbwi ambayo hutumiwa na wakaazi wengi wa huko kama njia rahisi na nafuu ya kuwafikisha kwenye miji mikubwa kama vile ya Wete na Chake Chake.

Hata hivyo, usafiri huu sasa umesitishwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), ambalo ni kama jeshi la wanamaji kwa Zanzibar, sambamba na mamlaka husika kuwapokonya madereva wa magari ya abiria ‘ruti’ za baina ya Mtambwe na maeneo mengine ya kisiwa cha Pemba.

Chanzo cha suintofahamu hii kinahusishwa na mgomo wa kijamii unaoendelea kisiwani Pemba baina ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao ni wengi, dhidi ya wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao ni wachache. Ukweli ni kuwa mgomo huo kwa sasa umeshika kasi na kuna mtafaruku mkubwa miongoni mwa wanajamii kiasi cha wengine kutoshirikiana kwa aina yoyote, wala kwa lolote. Kwamba si jambo la kushangaza kwa maiti mmoja kuwa na matanga mawili uwanja mmoja makhsusi kwa watu kulingana na itikadi za vyama vyao, yaani CCM lao na CUF!

Na Ahmad Abu Farsi
Na Ahmad Abu Farsi

Wenye mamlaka, kwa maana ya ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya, wanaona kuwa njia nyepesi ya kurejesha utangamano wa kijamii ni kuwalazimisha wafuasi wa CUF kuacha kuwagomea wafuasi wa CCM, tena kwa kutumia vyombo vya dola, vipigo, mabomu na mateso. Bahati mbaya, hali ya kisiasa na kijamii kisiwani Pemba haikubaliani na dawa hiyo inayotumiwa na watawala, na hivyo badala ya mgomo kupungua, ndio kwanza unaongezeka makali yake kila uchao.

Tukio kama la Mtambwe la kuzuwiwa kwa vyombo vya usafirishaji wa baharini, siiku ya Jumatano ya tarehe 1 Juni 2016 likaibukia kwenye kisiwa kidogo cha Kojani, ambako kikosi cha KMKM kilizishikilia kwa muda boti kadhaa ambazo hutumika kuvuushia watu kwenye eneo la Likoni na kuwapeleka Kojani au Kojani na kuwaleta Likoni.

Hata hivyo, kinyume na Mtambwe ambako wananchi waliwaachia tu kuchukuwa mashua zao, kwa Kojani hali ilikuwa tafauti. Wakaazi wa kisiwa hicho ni maarufu kote kwenye pwani ya Afrika Mashariki kwa ukarimu lakini pia ukakamavu wao. Mtafaruku uliozuka baada ya KMKM kutwaa boti zao kwa nguvu haukuwa mdogo. Ilifika mahala polisi wakaenda na kurusha mabomu ya machozi hewani kwa lengo la kudhibiti hali,  lakini haikuwa dawa ya kuwafanya Wakojani kutawanyika na kuacha mambo yawe kama ilivyo kwa Mtambwe, bali walisimama imara kudai vyombo vyao hadi wakafanikiwa kuvipata.

Pamoja na busara iliyotumika baina ya Wakojani na jeshi la Polisi kulifanya eneo hili kuendelea kuwa na amani baada ya boti hizi kurejeshwa kwa wenyewe, acha leo niseme neno la indhari kwa kikoso hiki cha KMKM. Nimejikusuru kwa hili kwa vile naelewa madhara yanayowakumba wanachi wengi kwa matendo haya ya KMKM ya kuzuwia vyombo vya usafiri wa majini kwenye eneo tete kama hili la kisiwa cha Pemba.

Hakuna uwezekano wa KMKM kudhibiti watu au kuwafanya wabadili misimamo yao, bali mchezo wanaoendelea nao sasa ni ule wa kumimina petroli kwenye moto na wasipokuwa makini unaweza kuwaripukia. Unaweza kuwaripukia na ni vyema wakaacha kutumika kisiasa na waendelee na jukumu lao la kulinda magendo kama yapo. Hili ni tatizo ambalo kama KMKM hawakuwa makini, kuna siku watajikuta wameingia kwenye mkondo mwingine wa kumwaga damu za raia wanyonge waliochoka madhila na unyanyasaji huu wanaoufanya dhidi yao.

Niliwasili eneo hili muda ya saa 8:00 mchana na kukuta muafaka umeshafikiwa baina ya polisi na wakaazi hawa wa Kojani. Hata hivyo, nilipojaribu kumuhoji muwakilishi wa wananchi hawa alieleza kile kilichotokea na chanzo cha boti zao kuzuwiwa. Alieleza kwamba pamoja na eneo hili kuwa na vivuko kulingana na itikadi za kisiasa, walishangaa kuona asubuhi yake, boti ambazo hutumiwa na wapenzi na wanachama wa CUF zikiwa zimeshikiliwa na kikosi cha KMKM kwa maelekezo ya sheha, jambo ambalo wao wanalipinga na hawakubaliani nalo. Na matokeo ya uamuzi huu wa KMKM ukapelekea kina mama shupavu wa kisiwa hiki cha Kojani kuliteka na kulipeleka kusikojulikana boti ambalo hutumiwa na wanachama na wapenzi wa CCM!

https://soundcloud.com/mohammed-k-ghassani/wakaazi-wa-kojani-watunishiana

 

Hii mana yake nini na inatowa ishara gani? Kwangu hali hii ina maana moja kwamba watu wameshachoka na hawana tena uoga kwa vyombo vya ulinzi pamoja na silaha walizo nazo. Kwamba ikiwa mwanamke wa Kipemba amefikia mahala sasa anateka na kulipeleka mafichoni boti la kuvuushia, ieleweke kwamba mambo yameshabadilika na sasa kitu pekee ambacho kitatunusuru na kutuepusha na vurugu za kijamii baina yetu, ni busara pekee na wala si makeke ya kijeshi au ya kipolisi.

Kutokana na hili, nililazimika kufunga safari hadi makao makuu ya KMKM pale mjini Wete. Hata hivyo niliruhusiwa kuingia ofisini kwa mkuu wa KMKM nikiwa nimelazimishwa kusalimisha kamera, simu na tablet yangu eneo la mapokezi na sikuruhusiwa kufika ofisini kwa mkuu huyo nikiwa na vifaa hivyo kama vitendea kazi vyangu. Nilipojaribu kueleza na kujitambulisha na lengo la kuwa kwangu mahala pale, nilijibiwa na muhusika kwamba nitakabidhiwa vitu hivyo mara baada ya kukutana na mkuu na yeye kuridhia mahojiano na mimi!

Sikuwalaumu watendaji hawa wa chini kwani nilishagundua kwamba hule haukuwa uamuzi wao bali wa bosi wao ambaye alionekana ni mtu asiyependa kuongea na wanahabari. Inawezekana hii ni kutokana na kujijuwa kwamba anaendesha kazi zake kisiasa au kwa kufata mashinikizo ya kisiasa.

Nalisema hili kwani siamini kwamba mtu ambaye anafanya kazi zake kitaalamu angepata uthubutu wa kuzuwia vyombo vya kuvuushia watu kwenye eneo kama la Kojani. Tuelewe kwamba Kojani ni kisiwa, hivyo usafiri pekee wa kutoka na kuingia eneo hili ni huu wa mitumbwi na viboti. Sasa inakuaje mtu makini mwenye kutambua shida na mahitaji ya watu watumiao usafiri wa aina moja, akapata thubutu ya kushikilia usafiri wao kwa masaa kadhaa? Kweli mkuu huyu wa KMKM ambaye amejitambulisha kwangu kwa jina moja tu la Hussein, anafahamu kwamba miongoni mwa watu waishio kwenye kisiwa hiki wana shida na kadhia mbali mbali ambazo zinawalazimu kuvuuka kuja upande wa pili ili wakidhi shida zao? Anapataje ujasiri wa kuzuwia usafiri wao wa pekee wa njia ya bahari?

Kamanda Hussein alikataa kuongea na mimi kwa kisingizio cha kutokuwa na taarifa za eneo hilo kutoka kwa maofisa wa chini yake walio kwenye eneo hilo. Huu ni udhaifu mwingine wa kiuongozi na kiutendaji, kwamba watu wanateseka na kukosa huduma muhimu kwa maisha yao, halafu bado yeye anapata ujasiri wa kukaa kwenye kiti cha kuzunguka ndani ya ofisi yake?

Nimefanya kazi na watu makini kama Kamanda Hassan Nassir na Kamanda Mohamed Shekhan wa Jeshi la Polisi ambao, pamoja na mapungufu ya kibinadamu, wana busara na umakini wa hali ya juu katika utendaji wa majukumu yao kwetu wanahabari na jamii wanayoitumikia tofauti na Kamanda Hussein ambaye hata kutoa jina lake kwa mwanahabari ni jambo la kujifikiria!

Ni dhahiri KMKM imeamua kutumika kisiasa, lakini mambo yamebadilika na sasa kinamama ndio wamejifunga mkaja kupambana kwa ajili ya haki zao. Vita dhidi ya mwanamke aliyesimama upande wa haki ni vigumu kuvishinda!

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Farsi, ni  mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba. Anapatikana kwa nambari ya simu +255 774 581 264.

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.