Natafakari tu, kuhusiana na hoja ya Mh.  Ally Kessy kuwa Wabunge kutoka Zanzibar wasishiriki shughuli za Bunge pale yanapozungumzwa mambo yasiyo ya Muungano kama vile kilimo, utalii, afya n.k ; ambayo amedai kuwa kimsingi ni mambo ya Tanganyika na Wabunge wa Zanzibar hayawahusu.

Kwanza nakubaliana na  mtazamo wake (kwa asilimia mia) kuwa Wabunge wa Zanzibar wasishiriki shughuli za Bunge yanapokuja mambo yaliyo nje ya Orodha ya Mambo ya  Muungano. Ukweli ni kuwa mambo yasiyo ya Muungano Wazanzibari hayawahusu asilani na kushiriki kuyajadili, kuyafanyia maamuzi na kuyatungia sheria SI haki wala haieandani na hata mantiki ya kawaida. Ukiwa Mbunge unatakiwa ujadili mambo yanayowahusu  wananchi wako na wewe mwenyewe, na pia huwezi kushiriki utungaji wa sheria kwa mambo ya wengine ambapo baadae sheria hio haikugusi wewe ulieshiriki kuitunga wala wananchi wako.

Zaidi ya hayo ni kuwa Tanganyika na Zanzibar ziliungana kupitia Orodha ya MAMBO YA MUUNGANO, nje ya mambo hayo kila upande una haki ya kujiamila mambo yake. Mambo ya Muungano yalianza 11 na sasa yamefikia 22.

Ukweli ulio bayana ni kuwa Muungano huu uliakisi Mambo ya aina tatu yaliyo tofauti kabisa. Aina ya kwanza, Mambo ya Muungano (ambayo haya yanawahusu pande zote mbili za Muungano na ndio MAMBO YA SHIRKA).

Aina ya pili,  Mambo ya Tanganyika (ambayo ni mambo ya upande wa Tanganyika tu ukiondoa yale  ya Muungano ) na aina ya tatu , Mambo ya Zanzibar (ambayo ni mambo ya upande wa Zanzibar tu ukiondoa yaliyo ya Muungano).

 

Kiinimacho cha kisiasa kilichotokea ni pale Mambo ya Muungano , ambayo ni mambo ya SHIRKA yalipochanganywa na Mambo ya Upande wa Tanganyika yakatiwa KAPU moja ikawa Mambo Mawili chini ya Serikali Moja na chini ya Bunge Moja.

Huo ndio msingi wa figisufigisu inayoukumba Muungano huu tokea kuasisiwa kwake miaka 52 iliyopita. Na ndio maana wapo wanaohoji ufasaha na udhamira wa Muungano kwa kitendo kile cha kuyamega mambo muhimu ya Nchi ya Zanzibar na kuyaondoa katika Milki na Mamlaka ya Zanzibar na kuyaingiza na kuyachanganya na mambo ya Nchi ya Tanganyika na Zanzibar ikawa haina uwezo wa kimaamuzi juu ya mambo hayo na kuwa milki na khatamu za kimaamuzi  juu ya  mambo yake hayo ziko kwa Nchi nyengine kupitia huo ulioitwa Muungano. Mambo ya Tanganyika na Mambo ya Muungano ambayo Zanzibar ni mshirika yamehodhiwa na Tanganyika kupitia inayoitwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanganyika haikumega chake chochote na kukiingiza.popote. Yaliyomegwa ni mambo ya Zanzibar nayo yakaingizwa katika Tumbo la Tanganyika ambayo nayo baada ya  kujiongezea Mamlaka ikajibadilisha jina na kuwa Tanzania. Kiinimacho cha mchana kweupe.

Lakini eneo ambalo bado nipo kwenye tafakuri kuona usahihi wake ni pale aliposema Wabunge wa Zanzibar ndio watoke Bungeni kupisha mijadala ya Mambo ya Tanganyika. Nadhani kwa vile lile ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania usahihi ni kwa Wabunge wa Tanganyika/Tanzania Bara kutoka wao katika Bunge la Muungano na kuunda Bunge lao makhsusi kwa shughuli zao za Tanganyika. Wasilete mambo yao ya Tanganyika kwenye Bunge la Muungano. Yawepo Mabunge matatu na Serikali Tatu kila Serikali/Bunge ishughulike na Mambo yake. Figisugisu Iwe Basi.

Tanbihi: Makala ya Awadh Ali Said

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.