Sikumbuki mwezi wala tarehe, lakini mwaka ni 1985. Naukumbuka mwaka huo kwa kuwa nilikuwa darasa la tatu katika skuli yangu ya Pandani. Kinachonifanya niukumbuke mwaka ni hilo darasa lenyewe nililokuwa nikisoma. Chumba chetu kilikuwa upande wa kushoto wa ofisi ya Mwalimu Mkuu, Maalim Nassor Hemed Khamis (Allah amrehemu), na kutokea chumba hicho tuliweza tunaweza kuiona kwa tabu nyumba ya Bi Moza Shkeli, mama yake Daud, ambayo ilikuwa umbali wa kama viwanja viwili vya mpira.

Jina la Daud halikuwa maarufu kwenye eneo letu wakati huo, lakini Daud mwenyewe alikuwa akijuilikana na kila mtoto wa marika yangu. Nadhani sababu zilikuwa ni mbili: moja ni kuwa alikuwa akitaniwa sana kwa ile hadithi iliyokuwemo kwenye kitabu cha Darasa la Tatu inayoanza na sentensi “Daudi ni kama wewe, lakini yeye ni mcheshi na mchangamfu…”. Sababu ya pili, nadhani, ni kwa kuwa nyumba yao ilikuwa ikipokea ugeni wa mtu tuliyemuona kuwa mkubwa na kiongozi wa juu wa nchi wakati huo, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hadi sasa ninachofahamu (lakini sina hakika) ni kuwa Bi Moza alikuwa urafiki wa kifamilia na familia ya Maalim Seif na mara kadhaa familia ya Maalim Seif ilikuja kumtembelea. Bibi huyu alikuwa na mtoto mmoja mgonjwa wa ndani, ambaye alikuwa hawezi kusema wala kutembea peke yake, na muda mwingi alipaswa kukaa nyumbani kumuangalia.

Siku ninayoizungumzia hapa ni moja kati ya siku ambazo msafara wa Maalim Seif uliwasili nyumbani kwa Bi Moza, nyakati za jioni karibu na muda wa kengele kupigwa ya kumaliza masomo. Kipindi cha mwisho kama hiki kilikuwa ni cha kuimba nyimbo darasani.

“Kengele lialia
Saa zimefikafika
Ama leo tumbo laniuma
Siwezi kwenda kusoma!”

Lakini tuliposikia tu magari yamesimama kwa Bi Moza, sote tukaacha kuimba. Nani atataka kuimba wakati huko nje kuna jambo linaloshughulisha macho na nyoyo? Sijui kwa nini, lakini ni kama kwamba tulikuwa tunajuwa na mapema kuwa leo ungelikuja ule ugeni pale. Ghafla nyumba ya Bi Moza ikawa imezungukwa na maaskari, mlango wa mbele na wa nyuma, wengine wakisambaa umbali hadi karibu usawa wa njia ya kuingilia ofisini kwa Mwalimu Mkuu. Maalim Seif, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alikuwa amewasili.

Kama ulivyo, udadisi wa kitoto hutaka kujuwa na kuona kila jambo. Lakini badala ya kutulia kila mmoja aone kwa utaratibu, wengine tukaanza kuparamia ukuta ili tuwe warefu zaidi. Mara Mwalimu Mkuu, Maalim Nassor, akatoka na kijibakora chake kifupi akaja darasani kwetu. Mikwaju ya kuondokea ikatupata wengine. Na haitoshi. Wanafunzi wote tukaambiwa kengele ya kuondoka ikilia, tupitie njia ya Kwa Juma Faiz na sio Midorianini, ambako tungeweza kuona japo yale magari na kupita chini ya maaskari.

Siku hiyo nilirudi nyumbani na unyonge. Unyonge wenyewe haukutokana na zile bakora za kuagia alizotupiga Maalim Nassor kwa kuweka kwetu fujo. Kwa sisi wengine, ambao utundu ulikuwa mtindo wetu wa maisha, bakora kama hizo halikuwa jambo kubwa. Unyonge wangu ulitokana na kushindwa kupita karibu na nyumba ya Bi Moza nikaona magari na maaskari waliokuja kwenye msafara wa Maalim Seif. Baya zaidi ni kuwa tulitegeshea njia nzima kuwa msafara huo ungelirejea kwa njia ya Mzambarau Takao, lakini bahati mbaya kwetu msafara ulirejea kwa njia ya Mzambarauni Kwa Kyarimu.

Usiku wa siku hiyo kabla ya kulala, nikamuambia baba. “Nataka kuwa kama Seif”. Baba akacheka mpaka mbavu akawa haziwezi. Nilikuwa nimedhani kuwa sentensi yangu ilikuwa imetoka bila kutazamiwa, lakini kumbe mama alikuwa amemuhadithia yaliyokuwa yamenitokea jioni yake kule skuli, baada ya kuniona na alama ya bakora matakoni na nikamueleza nilipoipatia.

“Mbona wanicheka?” Kwa wasiojuwa, baba yangu alinizaa mimi nikiwa mtoto wake wa pili na wa mwisho, yeye akiwa tayari ana miaka 55. Kwa hivyo, kwake nilikuwa mjukuu, na mara nyingi mawasiliano yetu yalikuwa yakielekea kwenye babu na mjukuu kuliko baba na mwana, ingawa nikivuuka mpaka kidogo tu, alikuwa ananiweka sawa kwa mikwaju.

“Basi kuwa!” Lilikuwa ndilo jibu lake baada ya kesho kumalizika. Hakuuliza nataka kuwa Seif yupi, yumkini kwa kuwa Seif aliyekuwa kwenye hadithi aliyopewa na mama siku hiyo alikuwa ni mmoja tu na, kwa hivyo, hapakuwa na cha kuuliza. Lakini aliponiuliza kwa nini nataka kuwa kama Seif, jibu langu lilizidi kumpasua mbavu.

“Nikija hapa nyumbani, maaskari nyumba nzima mpaka kule dukani kwa Msabaha, watu wote hapa watetemeka. Mote humu.”

Masikini, mdogo kama nilivyokuwa, picha ya Seif ambaye nilitaka kuwa kama yeye ilikuwa ni Seif kiongozi mkubwa, mwenye kusindikizwa na maaskari wenye bunduki na magari. Labda kwa utoto wangu ninaweza kusameheka, maana kama nilivyokuja kujuwa baadaye, nguvu hasa ya Maalim Seif haikuwamo kabisa kwenye zile nilizoona kuwa ni alama za nguvu. Pengine nilikuwa mdogo mno kuweza kumfahamu Maalim Seif huyo, lakini ukweli alikuwa karibu yangu sana. Hadithi za uwezo na nguvu zake zilikuwa zinasimuliwa kwenye vibaraza na vikao vya mitengoni. Hapana shaka, nyingi zilikuwa zimeongezwa chumvi kidogo, lakini kwa mtoto mdogo ni shida kutenganisha.

Kilichokuwa muhimu ni kuwa hata wakati huo nikiwa mdogo, tayari Maalim Seif alishakuwa alama ya nguvu ambayo nadhani sikuwa peke yangu niliyeijuwa, kuihisi na kuihusudu. Nguvu hii ikisafirishwa kwa matukio na simulizi za mikasa, hasa ile ya kupimana nguvu kati yake, Maalim Seif, na Mwalimu Julius Nyerere. Nikukumbushe kuwa hata katika utoto huo, tayari nilishajengwa kumjua Mwalimu Nyerere kama kiongozi asiye na nia njema kwa Zanzibar. Nakumbuka kulikuwa na hadithi iliyosema kuwa Maalim Seif alikuwa akimuangalia Mwalimu Nyerere usoni kisha Mwalimu Nyerere akainamisha uso wake, kisha Mwalimu Nyerere akamualika Maalim Seif akamtembelee mama yake Butiama, naye Maalim Seif akamuambia angelikwenda baada ya yeye Nyerere kurudi kumuona mama yake, Maalim Seif, Mtambwe.

Turudi kwenye hadithi yetu. Ikatokezea mwaka huo huo wa 1985, dada yangu Fatma akaolewa, na ikasadifu kuwa mume aliyemuoa ni mtoto wa kaka yake Bi Aweina Sanani, yaani mke wa Maalim Seif. Kwa hivyo, wakati Fatma alipojifungua mtoto wake wa kwanza mwaka 1986, Bi Aweina akaja nyumbani kwetu kumjulia hali mzazi, tena naye akiwa na mtoto wa mikononi. Nakumbuka akiitwa Sharifa.

Siku hiyo nikatamani kumuuliza Bi Aweina yote niliyokuwa nikisikia (au nikiyadhania kichwani mwangu tu) kuhusu mumewe. Sikuwa nimesahau kuwa nilitaka kuwa kama mumewe. Nikawa siondoki kizingitini kwenye mlango wa chumba cha mzazi. Lakini wapi. Siku nzima ikapita nikijiimania na kushika hiki mara kile. Nikashikwa na haya za kitoto.

Siku nyingi baadaye, maisha yalikuja kunikutanisha uso kwa uso na Maalim Seif, katika mazingira ya kinyumbani, nikiwa barobaro mzima lakini mgonjwa mikononi mwa familia ya Bwana Hamad Rashid Mohammed, Mikocheni, Dar es Salaam, ambayo ikishughulikia matibabu yangu ya kuanguka mkarafuu mwaka 1993. “Huyu ni nani?” Maalim Seif alimuuliza mwenyeji wake, Bwana Hamad Rashid, usiku mmoja alipokuwa amekuja kuitembelea familia hiyo. “Ni kijana wa Sheikh Ali Said, yupo hapa kwa matibabu. Anatibiwa na Dokta Sharif.” Huyu Dokta Sharif ni mtoto wa kaka yake, Maalim Seif, Bwana Ismail Sharif, na alikuwa mtaalamu wa mifupa katika Hospitali ya Muhimbili. Sheik Ali ni kaka yangu, Ali Said Omar, anayeishi Sharjah na ambaye alikuwa rafiki wa wote hao na alinikabidhisha kwa Bwana Hamad ili anisaidie kupatiwa matibabu. Miongoni mwa hadithi zangu nilizokuwa nasimulia nyumbani Pemba baada ya kutoka matibabu, ilikuwa ni hiyo ya usiku huo kumuona na kumpa mkono Maalim Seif.

Siku nyengine nyingi zikapita tena na mengi yakajiri hapo katikati yake, mengine yakiingia na mengine yakitoka kwenye maisha ya mwanzo wa ujana, likiwemo la kuondokewa na baba yangu, mwaka 1995. Nadhani hata zile ndoto za kitoto za kutaka kuwa kama Maalim Seif nazo zikawa zimeyeyuka na maisha. Kisha ukaja Muafaka wa I mwaka 1999, nami nikawa tayari ni mpigapicha wa kujitegemea. Siku yenyewe ya Muafaka nilipata fursa ya kuingia jengo la Baraza la Wawakilishi mchana wake na usiku wake nikawa miongoni mwa waliohudhuria chakula ya Ikulu.

Kule Baraza la Wawakilishi, Maalim Seif alikuwa amevaa kanzu, koti na kofia, akiwa amekaa benchi moja na Mzee Shaaban Khamis Mloo. Nikawapiga picha. Akaniangalia sana kama ananikumbuka (au nikadhani kuwa ananiangalia na ananikumbuka). Usiku wake pia, nikampiga picha akiwa na Dk. Salim Ahmed Salim (wakati huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika), Jakaya Kikwete (akiwa Waziri wa Mambo ya Nje) na ile picha maarufu ya yeye na Dk. Salmin Amour wakikumbatiana, ambayo asubuhi yake ilikuwa sehemu ya picha za magazeti nikiwa nimeiuza kwa bwana mmoja anaitwa Charles aliyekuja.

Tangu siku hiyo, nikajijuwa kuwa mimi napenda kumpiga picha Maalim Seif. Napenda kuichukuwa taswira yake na kuihifadhi. Je, ile ya kuwa nataka kuwa kama yeye ilikuwa na maana hii? Maisha ya kikazi yalikuja kunikutanisha tena kwa ukaribu na Maalim Seif miaka mitano baadaye. Na muda wote nikawa nafanya kile nikipendacho zaidi nafsini mwangu – kuichukuwa taswira yake. Hapa ninapoandika, nadhani nina kama picha 1,000 ambazo nimempiga Maalim Seif kwenye maeneo tafauti ndani ya Tanzania, baina ya mwaka 1999 na 2015. Nadhani umbali huu ndivyo ninavyoweza kuwa kama yeye, umbali wa kumuhifadhia taswira yake. Lakini sio kwenye ile taswira ya awali ya nguvu na alama ya nguvu halisi ambayo utotoni nilikuwa  nayo.

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.